NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, December 28, 2009

UPUMBAVU WA BINADAMU HUU HAPA (USITAZAME VIDEO HII KAMA UNAKEREKA KIRAHISI - dk 2:22)

 • Akilinganishwa na wanyama wengine binadamu ni kiumbe dhaifu sana. Hana meno wala makucha makali kama ya simba, hana mbio kama za duma (cheetah), ngozi ngumu kama ya tembo, harufu chefuzi kama ya fungo, ujanja wa kujificha peupe ili kuwakwepa maadui kama wa kinyonga wala nguvu za kifaru.
 • Pamoja na udhaifu wake huu, uwezo wake wa kufikiri umemwezesha kuzikwaa ngazi za mfumo tata wa kiikolojia hadi kufikia kileleni kabisa. Leo hii binadamu ndiye anayetawala viumbe wengine – uwezo ambao wengine wanaamini kwamba alipewa na Mungu siku ile Mungu alipokamilisha kazi yake ya kuiumba dunia na vyote vilivyomo.
 • Kinachoshangaza hata hivyo ni ukweli kwamba binadamu anautumia vibaya uwezo wake kama mtawala wa viumbe vyote - bila kujali kama uwezo huu ni zawadi aliyopewa na Mungu au kama ni matokeo ya mamilioni ya miaka ya mapambano yake dhidi ya mazingira yanayomzunguka.
 • Wakati wanyama wengine wanaua wanyama wengine kwa lengo la kujipatia chakula au kujikinga wenyewe wasigeuzwe chakula, inasemekana binadamu ndiye kiumbe pekee anayeua wanyama wengine kwa nia ya kujifurahisha tu. Kwa mfano, binadamu anaua wanyama wengine ili tu ajipatie pembe, kwato, meno au ngozi ili akapambe chumbani kwake au kujiwekea kumbukumbu.

 • Tamaa hii ya kujifurahisha imemfanya binadamu kujaribu kuwafuga au kuwakusanya wanyama mbalimbali katika maeneo maalumu (zoo). Ukitembelea maeneo haya utawakuta simba, twiga, tembo, “tiger” na wanyama wengine wakiwa wamekata tamaa kutokana na maisha ya kitumwa wanayoishi. Hiki ndicho nilichokiona, kwa mfano, kule San Francisco na Honolulu - madume ya simba kutoka Afrika yaliyokata tamaa na ambayo yanashinda siku nzima usiku na mchana yakiwa yamefungiwa katika vibanda au vieneo vidogo vilivyozungushiwa seng’enge, nondo au ukuta mrefu.

 • Katika video hapa chini (tafadhali usiiangalie kama unakerekeka kirahisi), ni “tiger” ambaye alicharuka, akamjeruhi mmoja wa waangalizi wake kwa kuung’oa kabisa mkono wake wa kushoto na hapa anaonekana anajipatia mlo wake bila wasiwasi. Sijui tukio hili lilitokea wapi na lugha inayozungumzwa hapa siifahamu. Kwangu mimi, hata hivyo, hili ni fundisho kwa binadamu ambaye amevuka mipaka na kuutumia vibaya uwezo wake kama mtawala wa viumbe vingine. Kwa nini umfuge mnyama hatari kama “tiger?”
 • Katika kuhitimisha tashtiti na upumbavu huu wa binadamu, naamini kwamba “tiger” huyu aliuawa, pengine kwa kupigwa risasi. Mtu unaweza kujiuliza, aliuawa kwa kufanya kosa gani? Kwa kuwa “tiger”?
 • Tuwe waangalifu na kujua mipaka yetu kama binadamu, walimu, viongozi, wanafunzi, waume, wake, n.k. Vinginevyo itakuwa ni kama walivyosema waswahili “akili nyingi………" Au “majuto ni……”

2 comments:

 1. Halafu kama haitoshi Binadamu bado wanaendelea kuzalisha mpaka hawa Liger[Baba ni lion , mama Tiger], na Tigon kitu ambacho hata sikielewi ni kwanini ukizingatia matatizo yote yajitokezao katika hawa wanyama binadamu wawabunio ambao nature hairuhusu .

  Nakubaliana kabisa na ulivyosema kuwa tuwe na mipaka kwa maana .....

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU