NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, December 15, 2009

VIONGOZI WETU WANAPOZABWA VIBAO

 • Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi alipozabwa kibao, Watanzania wengi tulilalamika sana na kusema kwamba kitendo hicho kilikuwa hakiendani na maadili yetu kama jamii iliyosimikwa katika misingi ya upendo, heshima, amani na mshikamano. Ndiyo maana watu hawakuridhika na adhabu aliyopewa mzabaji huyo (mwaka mmoja jela) na wakataka apewe adhabu kali zaidi ili liwe fundisho.
 • Wapo pia ambao walilaumu mfumo mzima wa ulinzi wa viongozi. Walihoji kwamba inakuwaje rais mstaafu mzima azabwe kibao tena mbele ya halaiki? Ingekuwaje kama huyo mzabaji angekuwa na silaha nyingine kali?
 • Nimekikumbuka kisa hiki baada ya waziri mkuu wa Italia, bilionea mtanashati Silvio Berlusconi kutandikwa ngumi jana na kung'olewa meno mawili, kupasuliwa mdomo pamoja na uso wake kutapakaa damu. Picha zilizopatikana zinamwonyesha bilionea huyo mwenye mbwembwe akiweweseka mithili ya bondia aliyeelemewa katika shindano (tazama video ya Youtube hapa chini).
 • Katika kisa cha rais Mwinyi baadhi ya watu (ma-anonymous) katika blogu mbalimbali walionekana kutoshtushwa sana na kitendo hicho na wakakiona kama matokeo ya kukua kwa matabaka katika jamii. Dai kuu kutoka kundi hili la watoa maoni ni kwamba watu wamesikinika mno na wamefikia hatua ya kukata tamaa, na pengine vitendo kama hivi ni dalili tu za volkeno ya kitabaka inayofukuta mumo kwa mumo. Sina uhakika kama dai hili lina mashiko yo yote.
 • Katika blogu mbalimbali, watu wengi pia wamefurahishwa na kitendo cha Berlusconi kung'olewa meno mawili na kupasuliwa mdomo wakidai kwamba bilionea huyo ni mtu asiyejali, ni mzinzi sana na anapendelea operesheni za kujitengeneza sura. Wanadai kwamba kama bilionea, haelewi hali halisi ya maisha ya Mwitalia wa kawaida.
 • Kisa hiki kinaweza pia kutufanya tujiulize swali hili: Je, viongozi wetu (wote) kweli wanajua hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida (masikini anayeishi kule kijijini) au nao wamegeuka kuwa MaBerlusconi?
 • Hebu basi viongozi wetu wasisubiri mpaka kuzabwa vibao ndiyo wakumbuke jukumu lao la msingi - kuboresha maisha ya umma uliowaweka madarakani. Ni maisha bora kwa kila Mtanzania ati!

5 comments:

 1. Prof. fanya marekebisho kidogo hapo umeandika wasifu sivyo...

  ReplyDelete
 2. Asante dada Subi - nimerekebisha. Sijui kwa nini nilikosea na kusema kuwa Silvio Berlusconi ni waziri mkuu wa Uhispania...Kazi kwelikweli.

  ReplyDelete
 3. Asante kushukuru Prof.
  Kukosea kawaida yetu binadamu, ndiyo uandishi tena.

  ReplyDelete
 4. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!December 16, 2009 at 7:54 AM

  ati wanaowapiga viongozi ni vichaa? alombonda Mwinyi alipelekwa huko Mirembe, na huyu swahiba wa 'baluskonyi' nae ati kichaa.

  yawezekana vichaa wanaweza kutenda jambo 'jema?' Kuna kausemi kuwa ati mchonga (mzee wa mwitongo - R.I.P) aliwahi kusema kuwa atakayemuua ni kichaa, je kuna kaukweli ndani yake kufanya jambo lisilowezekana?

  na alomdunga papa yohani paolo II risasi naye alikuwa kichaa?

  duh! orodha inaweza kuwa ndefu lakini tafakuri yako Mzee Masangu inafikirisha saaana!

  ReplyDelete
 5. Ng'wanambiti - huwezi jua. Pengine tutakombolewa na VICHAA!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU