NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, December 10, 2009

WANAFUNZI SIKILIZENI - MSIDHARAU SOMO LA HISABATI - HALIEPUKIKI!!!

 • Hebu tazama jamaa hapa chini alivyokokotoa mahesabu haya. Bila kuambiwa faida hasa ya ukokotoaji huu, wanafunzi wengi huliona somo la hisabati kama lisilo na maana wala faida. Somo hili muhimu pia huwa halifundishwi vizuri na pengine ndiyo somo linaloongoza kwa kuchukiwa na wanafunzi - na lina walimu wakali sana! Unawakumbuka walimu wako wa Hisabati?

 • Albert Einstein - pengine mwanasayansi mashuhuri kuliko wote - aliwahi kusema kwamba hisabati ndiyo lugha pekee inayoweza kueleza kila kitu.
 • Plato - anayetambuliwa na wengi kama baba wa Falsafa na mtu wa kwanza kufungua chuo alichokiita akademi - aliweka tangazo hili katika mlango wa kuingilia akademi yake" Let no one ignorant of geometry enter" Kwa hivyo kama wewe ulikuwa hujui/hupendi hisabati kamwe usingeweza kutia guu katika akademi ya Plato.
 • Pamoja na ukweli kwamba hisabati si somo rahisi (kama kuna somo rahisi!) mimi nadhani pia kwamba wanafunzi hawaambiwi hasa umuhimu wa somo hili katika karibu kila kitu ambacho watafanya baadaye; na mara nyingi ufundishaji wake ni shaghalabaghala tu. Mwalimu anakuja darasani, anatoa mifano miwili mitatu halafu anaanza kuuliza maswali. Ukikosea unaambulia viboko.

 • Mimi pia sikuona sababu ya kukazana kukokotoa mahesabu bila kujua hasa faida yake ni nini. Nilipoanza masomo yangu ya shahada za uzamili na uzamifu pale UCLA ndipo moto uliponiwakia. Pale nilitakiwa kuchukua madarasa ya "Mathematical Linguistics" na "Computational Linguistics". Madarasa haya - ambayo ni ya muhimu sana na wahitimu wake kusakwa na makampuni mbalimbali ya simu, michezo ya video, Google na mengineyo - yanataka ujuzi wa hali ya juu wa misingi ya hisabati na lojiki. Pamoja na ukali wao wote, niliwakumbuka walimu wangu wa Hisabati.

 • Ukweli ni kwamba hesabu haziepukiki na wanafunzi wetu inabidi waambiwe hivyo. Hata kama wakizikimbia leo, kuna uwezekano mkubwa kwamba watakutana nazo huko mbele.

8 comments:

 1. Sasa kaka Matondo, hiyo hesabu ya pili kwenye picha namba moja, kapita kooote huko halafu akaishia na jibu ni 0. Ah, yaani kazi yooote hiyo majibu 0. Sasa taabu yote ya nini kwa nini hakusema tangu mwanzo tu 0 kama huyo jamaa wa pili aliyeonesha x ilipo?
  just kidding)
  Good stuff!

  ReplyDelete
 2. Nimependa post yako. Mimi hesabu niliipenda, ila kuna kipindi nilikosa walimu wazuri, na miundimbinu ya kutafuta mwenyewe haikuwezekana. Sasa nafanya mamambo ya sayanzi ya sanaa, lakini pia huko hesabu ipo na inasaidia sana.

  ReplyDelete
 3. hoja ni ya msingi lakini hesabu hailipi hapa bongo,ni heri ukawa mwanamaigizo,mcheza ngoma,mwimbaji wa kwaya,au mwanasihasa yaweza kukutoa nawe ukaonekana,la sivyo utaiishia kuwa na mfadhaiko wa akili mwisho unachanganyikiwa,manake hapa bongo walimu wenyewe totaly confused,sas hao wanafunzi watafunzwa na nani?
  acha tu taifa liwe la wasanii

  ReplyDelete
 4. hesabu? nilikuwa naziogopa hata kutamka tu. lakini of late nimekuja kuelewa kuwa 'mase' ni mchezo mzuri sana na rahisi pia ukizipenda. nilifanikiwa kuzikwepa sekondary lakini ile nanusa tu mlimani mwaka 2000 nikakutana na 'AS 101 Methods of Social Research' la dk lymo. mfundishaji dk sichone. hapo ndio ngoma inogile. dk sichone anafundisha statistics utadhani
  anafundisha engineering class. nikajifaragua nikatokamo. lakini ilihitaji nguvu za ziada (za kuzingatia, sio 'migi')

  prof contact za makene nimeziweka pale pale ulipoziulizia.

  ReplyDelete
 5. kuna wanaoishi kwa hesabu bila kujua kama kuna somo la hesabu

  ReplyDelete
 6. Hesabu ni miongoni masomo mepesi, lakini ile dhana kwamba hesabu ni ngumu ndio sababu inapelekea wanafunzi wakaliogopa somo hilo. Nafikiri inabidi tuwashajiishe zaidi wanafunzi wetu tangu chekechea kuzipenda hesabu, na pia walimu wachaguliwe wenye roho nzuri na wanaoweza vyema kulifundisha somo hilo na kulifanya lipendwe na wanafunzi.

  ReplyDelete
 7. Shally medical corner. "Hesabu ni miongoni masomo mepesi" Are you sure? What makes a subject be jepesi? I am perplexed!

  ReplyDelete
 8. Dada Subi - ndiyo maana kuna umuhimu wa kusisitiza tena na tena umuhimu wa hesabu - vinginevyo itaonekana kama ni kupotezeana muda tu. Uhangaike vile halafu jibu eti ni ziro. Then what? Vinginevyo mtu waweza kukata tamaa na kuishia kufumbua mafumbo ya Sudoku kama lengo ni kunoa ubongo!

  Reggy - ni kweli - hata kwenye Social Sciences bwana hesabu zipo na kusema kweli haziepukiki. Ndiyo maana Mwalimu Mwaipopo pamoja na kuziogopa/kutozipenda kama mimi, mwishowe alikumbana nazo ana kwa ana pale Mlimani.

  Kamala - kama kawaida yako unafikirisha. Naamini hawa wanaoishi kwa hesabu bila kujua kama kuna somo la hesabu watalijua tu somo hili siku watakapokumbana nalo darasani, na kutakiwa kuchora grafu au kutafuta mzingo wa duara kwa kutumia ile kanuni ya "pai pi skweadi" Unaikumbuka?

  Shally's Med Corner - kama vile Malulumalu hata mimi sikubali kama hesabu ni somo rahisi. Na sijui kama kuna somo rahisi. Tunamaanisha nini tunaposema somo rahisi? Wengi huamini kwamba hesabu ni somo gumu kumbe kwa wapenzi na wenye "kipaji" cha hesabu kama nyinyi mnaliona kuwa jepesi. Wengine watakwambia Kiswahili ni somo rahisi - pamoja na ukweli kwamba wanafunzi wengi hufeli somo hili katika mitihani yao ya kidato cha nne. Hitimisho: HAKUNA somo rahisi!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU