NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, February 26, 2009

TUSIJE TUKAJISAHAU TUKASAHAU KUSAHAU

Umeshawahi kusahau mahali ulipoweka funguo zako? Pesa je? Au kama ulifanikiwa kumkwepa konda wa daladala na hivyo ukasafiri bure jana? Bado unalikumbuka jina la mpenzi wako wa kwanza?

Wataalamu wanasema kwamba kusahau ni jambo la kawaida na si mara zote ni dalili za moja kwa moja za magonjwa kama Dementia au Azheimer. Kutokana na habari nyingi ambazo ubongo inabidi uzitunze, wataalamu wamegundua kwamba, mbali na kujipumzisha wakati ukiwa umelala (ingawa bado ubongo wako huendelea kufanya kazi kuhakikisha kwamba moyo unapiga, unapumua n.k.) ubongo inabidi ujisafishe kwa kuziondoa na wakati mwingine kuzifuta kabisa habari ambazo wenyewe unadhani kwamba si za muhimu.

Hata hivyo inakubidi uanze kuwa na wasiwasi kama ukianza kusahau jina la mkeo/mmeo, mahali ulikoficha mabilioni ya fedha zako za ufisadi na kama jana ulipata kinywaji ama la!. Hizi zaweza kuwa dalili za magonjwa kama Dementia au Azheimer. Na kama umesahau kama unapumua ama la (japo umo katika shangingi lako tena lenye viyoyozi), basi yawezekana kabisa ikawa tayari umeshakoma kuishi ingawa bado UPO. Na siku nyingine ukimsahau mtu hebu jaribu kujiuliza, YEYE ANAKUKUMBUKA?

Kwa mazoezi mbalimbali ya ubongo bofya hapa. Lakini kabla ya yote, tusije tukajisahau tukasau kusahau!

HABARI KUU YA GAZETI INAPO"FYATULIWA"

Ni gazeti la Sani Februari 25-27, 2009. Pengine ni katika kukurukakara na mikikimikiki ya kuwahisha udaku mitaani...

Friday, February 20, 2009

WATANZANIA: NI NINI KIMETUFIKISHA HAPA???

Hebu tazama hizi picha za kutisha kwa KUBONYEZA HAPA. Ni nini kimetufikisha hapa? Zile falsafa za upendo, undugu na umoja alizotuachia Mwalimu Nyerere ziko wapi? Kama taifa, tunaelekea wapi? Leo ni maalbino, kesho itakuwa zamu ya nani? Je, huu ni mwanzo wa mwisho wa Tanzania iliyokuwa inasifika kwa amani na upendo? Tukiweza kuzigundua sababu hasa ambazo zimetufikisha hapa, ndiyo tutaweza kupata suluhisho la kudumu la tatizo hili. Hili ni tatizo la kila Mtanzania na Watanzania wote tukiamua kulimaliza tunaweza tena mara moja (tusiitegemee serikali). Hebu na tupambane na kuhakikisha kwamba tunaitokomeza hii kansa kabla haijagoma kutibika!

Monday, February 16, 2009

HATIMAYE SERIKALI YAUKOROMEA "UANDISHI UCHWARA" WA HABARI

Kutokana na kufumuka kwa magazeti ya udaku (ambayo yanaweza kuandika udaku wa aina yo yote kumhusu ye yote, po pote na bila kujali cho chote), serikali hatimaye imeonyesha kukerwa na hali hiyo duni ya kiwango cha uandishi wa habari nchini (aka uandishi uchwara). Sijui itachukua hatua gani. Je, utitiri huu wa magazeti ya udaku, ni uhuru wa habari uliopindukia kimo? Hata hivyo ni lazima tukiri kwamba magazeti haya ya udaku yanapendwa sana po pote duniani na ndiyo yanauzika zaidi kuliko magazeti makini ya uchambuzi (Uingereza na Marekani ni mifano mizuri). Kwa vile tumeukubali (au tuseme imetulazimu tuukubali) utandawazi, mimi nadhani magazeti haya yanayoandika habari hizi za uzushi zisizo na kichwa wala miguu hayaepukiki. Utandawazi ni zimwi tena lisilotujua. Swali ambalo tunatakiwa kujiuliza ni hili: Ati, zimwi lisilotujua laweza kutula lisitumalize?

Kwa maoni mengine kuhusu suala hili, mtembelee mzee wa changamoto kwa kubofya hapa

"Uandishi uchwara" kutoka gazeti la Tanzania Daima la Februari 13, 2009 (hisani ya kennedy blogu)













Kutoka gazeti la udaku la Kiu la Februari 13-15, 2009 (hisani ya kennedy blogu)

Wednesday, February 11, 2009

LOJIKI YA KIZAZI CHA DOT COM

Haya ni maongezi ya kweli ambayo niliyashuhudia hivi karibuni. Wazungumzaji walikuwa ni wapenzi matineja - wote Waafrika. Binti ni Mchaga kutoka Moshi na mvulana anatoka Cameroon ingawa wote sasa wanaishi Marekani. Kilichonishangaza ni kwamba vijana hawa hawajui kabisa na wala hawajawahi kuona mnyama aitwaye mbuzi. Pengine hili si jambo la kushangaza kwa vijana wetu wa dot com. Kilichonishangaza ni hii lojiki katika mazungumzo yao (tazama hapa chini):

Binti: A goat is a lamb. And a lamb is like a sheep
Mvulana: A sheep, therefore, is a female lamb.

Lojiki hii ilinichanganya kidogo. Lakini hawa ni vijana wa kisasa ambao pengine ukiwauliza kuhusu chakula alichokula Britney Spears mwezi uliopita watakueleza kila kitu tena kwa kina. Kazi ipo!

Tuesday, February 10, 2009

TUNAELEKEA WAPI???

Kama tutawanyima watoto wa masikini (ambao ndio wengi) nafasi ya kujipatia elimu ya juu, tutakuwa tumewazika katika kaburi la kudumu la umasikini na kutoendelea; na utafika wakati Tanzania itaelemewa na uzito wa matabaka haya tunayojitahidi kuyajenga na kuyaimarisha. Mungu ibariki Tanzania!

Monday, February 9, 2009

WAMAREKANI WANAPOMIMINIKA KWA "WAGANGA WA KIENYEJI"

  • Hali ya uchumi hapa Marekani ni mbaya. Watu wengi wamepoteza kazi zao, kazi hazipatikani na karibu kila jimbo lina matatizo ya fedha. Shule na vyuo vikuu vya umma vinapunguza wafanyakazi na kwa ujumla hali si ya kutia moyo. Katika msukosuko huu wa kiuchumi, watu hawawaamini tena wataalamu na washauri wao wa mambo ya fedha na badala yake wanamiminika kwa waganga wa kienyeji (a.k.a. watabiri au wapiga ramli) kuangalia bahati zao na mwelekeo wa mambo yao ya kifedha. Bei ya waganga hawa wa kienyeji wa Marekani ni ghali na inaweza kuwa kati ya dola 75 na dola 1,000 kwa saa moja – shilingi za Tanzania 75,000/ mpaka 1,000,000 kwa saa moja! Lakini watu hawajali bei hizi ghali na wanamiminika huko na biashara ya utabiri na upiga ramli ni kati ya biashara chache zinazotia fora katika kipindi hiki kigumu cha kiuchumi. Kinachoshangaza ni kwamba wengi wa watu wanaokimbilia kwa hawa waganga wa kienyeji ni wasomi na wenye (au waliokuwa na) kazi nzuri. Soma makala kutoka katika gazeti la New York Times hapa.
  • Niliposoma makala haya kutoka gazeti la New York times na kutazama habari na maoni ya wanasaikolojia katika televisheni jana kuhusu jambo hili, nilijaribu kulinganisha na suala la waganga wa kienyeji huko nyumbani ambao wameshapigwa marufuku kufanya kazi zao kutokana na sakata la mauaji ya maalbino. Tunajua kwamba Marekani ni taifa lililoendelea na lenye watu wengi ambao wamesoma. Kupamba moto kwa biashara ya utabiri na upigaji ramli katika kipindi hiki cha shida za kiuchumi kunatufundisha au kunatuambia nini? Pengine tunapaswa kujiuliza maswali ya msingi: Nani wanakwenda kwa waganga wa kienyeji? Kwa nini wanafanya hivyo? Ni kwa nini watu hawa wanakuwa tayari kutoa cho chote wanachoambiwa (mf. viungo vya maalbino, ngozi za binadamu, shilingi 1,000,000 kwa saa moja n.k.) na waganga hawa? Nini kifanyike? Japo inaweza kuwa ni hatua muhimu, mimi siamini kama kuamka tu siku moja na kupiga marufuku shughuli za waganga wa kienyeji kama serikali ilivyofanya bila kujibu baadhi ya maswali hapo juu ni suluhisho la kudumu la tatizo hili. Tukumbuke kwamba kitu kinapokatazwa huwa adimu na mara nyingi hadhi yake hupanda. Tusije kushangaa kuona kwamba hatua hii ya kuwapiga marufuku waganga wa kienyeji inawanufaisha na kuwaongezea hadhi zaidi badala ya kuwatokomeza (au lengo lolote ambalo marufuku ya serikali inakusudia kulitimiza).
  • Pata mtazamo mwingine wa suala hili kutoka katika gazeti la KIU (Februari 9-12). Hili ni gazeti la udaku na usitegemee kupata uchambuzi wa kina.
 

Thursday, February 5, 2009

NI KWELI WAAFRIKA HATUNA ROHO YA UDADISI, KUJITOA MUHANGA NA UGUNDUZI?

Majuzi juzi hapa nilikuwa naangalia Comedy Central na mwanakomedia/mkomedia/mchekeshaji? mmoja mweusi alinichekesha sana aliposema kwamba yeye anafikiri kwamba wazungu ni watu wa ajabu. Aliwauliza watazamaji wake kwamba mtu mzima na akili zako timamu unawezaje kuacha kazi yako nzuri na kujitolea kwenda kuishi katika misitu ya Indonesia eti kusaidia kuokoa jamii ya nyani inayokaribia kuangamia? Aliendelea kusimulia kwamba bosi wake (mzungu) ndiye alikuwa amefanya hivyo na kwake yeye jambo hili haliingii akilini kabisa.

Maneno ya huyu mwanakomedia yalinikumbusha swali ambalo mama yangu mzazi aliniuliza alipokuja kunitembelea hapa Marekani. "Hawa wazungu wana nchi nzuri namna hii, kuna simenti kila mahali, hakuna vumbi, maduka yamejaa, umeme haukatiki, kuna raha za kila aina, mahospitali mazuri, kwa nini wanaacha nchi kama hii na kuja kukaa vijijini"? Hapa alikuwa anamwongelea padri mmoja aliyekuja tangu zamani na kujenga kimisheni chake cha Kikatoliki katika kijiji kimojawapo kule Bariadi, Shinyanga.

Nilipofikiria vizuri nilianza kuwafikiria wasafiri, wafanyabiashara na "wagunduzi" wa Kizungu kutoka Ulaya waliomiminika Afrika enzi zile - akina Vasco da Gama, David Livingstone, Carl Peters, Mungo Park na wengineo. Japo wengi wao walikuwa wametumwa na nchi zao, wengi wao hawakujua walikokuwa wanakwenda na kama wangerudi salama lakini walikuwa tayari kujitoa mhanga. Kutokana na juhudi na "ugunduzi" wao, ndiyo maana Ulaya, na hasa Uingereza, iliweza kuitawala dunia nzima. Kwa wazungu, roho hii ya kukabili yasiyojulikana na kujaribu yasiyowezekana ndiyo mtaji wao mkubwa kabisa - mtaji ambao umewafanya waweze kuendelea - hata kama ni kwa kuwanyonya na kuwatumikisha watu wengine. Kwa mzungu kufa huku akijaribu kupanda mlima Everest, akipambana na mawimbi makubwa baharini au akijaribu kuruka kwa ndege yake aliyojitengenezea mwenyewe gerejini mwake si jambo la ajabu. Udadisi, udadisi, udadisi...Lakini sisi je?

Je, roho hii ya udadisi, kujitoa mhanga na ugunduzi sisi watu weusi hatuna? Kama jibu ni ndiyo, ni kwa nini? Nawaza tu. (By the way, sikuweza kumpa mama jibu la kuridhisha. Pengine nitapata jibu la maana katika mjadala huu.)

Hebu tujikumbushe jinsi hawa jamaa walivyotutawala hapa chini:

video

Msikilize pia Noam Chomsky - mwanaisimu bingwa na mchambuzi makini wa mambo ya kisiasa akitoa maoni yake kuhusu ukoloni kupitia jicho la mgogoro wa Uganda.

video

Wednesday, February 4, 2009

ASANTE YETU KWA MASHUJAA WETU

Nimesoma habari ya kufariki kwa koplo Sostines kwa masikitiko (tazama hapo chini). Polisi shujaa kama huyu alipaswa kukimbizwa Afrika Kusini kwa matibabu ya kiwango cha juu zaidi kama ilivyo kawaida kwa viongozi wakuu wa serikali na wabunge. Bila kujali kama angepona au la, huu ungekuwa mfano bora zaidi kwa vijana mashujaa kama huyu na ungesaidia kuwapandisha morali. Wangeona kwamba ushujaa wao unathaminiwa na kwamba serikali yao iko tayari kuingia gharama kubwa kuwashughulikia wanapoumia wakiwa kazini. Mungu amlaze Marehemu Koplo Sostines mahali pema peponi.

===============================

POLISI SHUJAA ALIYEPAMBANA NA MAJAMBAZI AFARIKI DUNIA


2009-02-04 17:08:06
Na Sharon Sauwa, Polisi Kati


Askari Polisi mwenye namba F 8681, Koplo Sostines, yule afande shujaa ambaye akishirikiana na mwenzake, walifanikisha kuokoa shilingi milioni 56 katika tukio la ujambazi lililotokea hivi karibuni pale Manzese Darajani Jijini Dar es Salaam, amefariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata katika mapambano hayo.


Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema shujaa huyo alifariki juzi saa 8:00 mchana katika Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa (MOI), alipokuwa amelazwa tangu Januari 21 mwaka huu.


Amesema mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kupelekwa Bunda mkoani Mara kwa mazishi ambapo mipango ya mazishi.


``Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ndiye aliyesimamia taratibu za mazishi akishirikiana na ndugu wa marehemu,`` amesema Kamanda Kova.


Ameongeza kuwa askari huyo atazikwa kwa heshima za hali ya juu kutokana na kitendo chake alichokifanya cha kuhakikisha maisha na mali za watu zinakuwa salama.


Aidha Kamanda Kova amesema kitendo cha ushujaa alichokifanya askari huyo cha kukubali kupoteza maisha yake kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine na mali zao, ni kielelezo cha uwajibikaji wa jeshi hilo hasa kwa kanda yake.


``Tupo tayari kupoteza maisha ili kulinda maisha na mali za Watanzania na tukio hili ni kielelezo cha uwajibikaji wa jeshi hili kwa Watanzania hasa kwa kanda maalum ya Dar es Salaam,`` akasema Kamanda Kova na kuwaomba wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na watu wanaofanya uhalifu.


Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilimtunuku cheo cha Ukoplo askari huyo na mwenzake mwenye namba F 8407 Koplo Lazaro.


Katika tukio hilo, dereva wa kampuni ya Mount Meru Filling Station, Omary Single alipoteza maisha baada ya kupigwa risasi katika majibizano ya kurushiana risasi kati ya polisi na majambazi waliokuwa wakitaka kupora zaidi ya Sh. milioni 56 zilizokuwa zikipelekwa benki ya Standard Chartered.


SOURCE: Alasiri


Tuesday, February 3, 2009

MAGAZETI YA TANZANIA NA ....

Hii ni habari kuu (front page) ya gazeti la KIU la Februari 2-5, 2009. Mimi sikujua kama raisi Bush naye alikuwa anagombea uenyekiti wa chama cha Republican. Kazi ipo...(Picha za gazeti kutoka blogu ya Kennedy Kimaro)

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO