NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, March 31, 2009

MFALME MSWATI III

Hii nimeiiba kutoka kwa FATHER KIDEVU. Hawa ni wakuu wa nchi wanachama wa SADC walipokuwa katika mkutano nchini Swaziland hivi karibuni. Mstari wa mbele toka kushoto ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Mfalme Mswati III wa Swaziland, Rais wa Afrika Kusini na Mwenyekiti wa SADC, Khaglema Montlante, Rais Joseph Kabila wa Congo DRC na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji. Mstari wa nyuma toka kushoto, Waziri Mkuu wa Lesotho Phakalitha Mosisili , Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika na Rais wa Zambia Rupia Banda.

Kilichonivutia ni huyu Mfalme Mswati III. Mbali na kulaumiwa sana kwa utamaduni wake wa kuoa vibikra vipya kila mwaka, na kuishi maisha ya kifahari kupindukia huku wananchi wa nchi yake ndogo wakihangaika katika umasikini, huwa ninavutiwa naye kwa jinsi anavyoonekana kusimama kidete kupigania utamaduni wake (ambao bila shaka ndiyo unamwezesha kuweza kuendelea kutawala na kunyakua hivyo vibikra vipya kila mwaka). Inapendeza kama nini kwa mfano katika picha hii kuona wenzake wameulamba kwa suti kali za bei mbaya lakini yeye amevaa mavazi yake ya jadi. Ingependeza zaidi kama mavazi haya "simple" yangeendana na maisha yake halisi anayoishi. Yote kwa yote - hata kwa hili dogo - anastahili "sifa" Na huwa ninakerwa na makelele ya watu kutoka nje hasa Ulaya wanaodai kwamba wakati wa kuwa na wafalme umeshapita wakati wenyewe bado wana malkia...

Monday, March 30, 2009

MAZINGIRA YASIYO SALAMA KIAFYA YAKO WAPI?

Nimetatanishwa na dai kuu katika picha hii. Mazingira yasiyo salama kiafya yako wapi katika picha hii? Hivi si ndivyo chakula kinavyoandaliwa huko vijijini ambako zaidi ya robo tatu ya Watanzania wanaishi? Hebu tufanye lojiki ya kitoto kidogo hapa chini.

(1) Chakula hiki kinapikwa katika mazingira yasiyo salama kiafya
(2) Zaidi ya robo tatu ya Watanzania hupika chakula katika mazingira kama haya
(3) Kwa hivyo zaidi ya robo tatu ya Watanzania hupika chakula katika mazingira yasiyo salama kiafya.

Na hili ni jambo la KUTISHA!!!

Nyongeza: Shuleni enzi zile wapishi walikuwa wakipika ugali na ndizi (za kutosha zaidi ya wanafunzi 600) kwa kutumia kuni huku majasho pamoja na KAMASI vikidondokea humo humo kwenye ugali na ndizi zetu. Ukiongeza na maharage yaliyooza basi we acha tu. Wengine walinenepeana, wengine walikondeana lakini hakuna aliyeugua.

Saturday, March 28, 2009

MKIONA NIKO KIMYA MJUE KWAMBA NIMEKWENDA KUPAMBANA NA "MZEE WA VIJISENTI" KUWANIA UBUNGE WA BARIADI MAGHARIBI

Hebu tazama huu ulaji. Yaani hata nimekosa la kusema. Mzee wa Vijisenti kaa chonjo naja! Natania tu kwani sina mabilioni ya kwenda kuwahonga wapiga kura (picha kwa hisani ya Kennedy)

Wednesday, March 25, 2009

JE, WATADUMU KATIKA NURU?

Nimevutiwa na ari na shauku ya kujisomea inayoonyeshwa na watoto hawa pichani. Wanaonekana kuwa na kiu ya elimu na wako tayari kujifunza. Huu ndio wakati ambao akili zao changa dadisi ziko tayari kufinyangwa, kuelekezwa, kulishwa na kuongezewa kile walichonacho tayari ili hatimaye waweze kufikia upeo wao na kuwa vile wanavyotakiwa kuwa. Mfumo wetu wa elimu unahakikishaje kwamba udadisi, ari na shauku ya watoto hawa kujifunza haukinzwi na wala kukunguwazwa? Je, watoto hawa watadumu katika nuru ya kupenda kujisomea? Inajulikana kwamba Watanzania ni watu ambao hatuna utamaduni wa kupenda kujisomea na waandishi wengi wameshalalamika sana kuhusu vitabu vyao kukosa wasomaji. Ni wakati gani ambapo tabia ya kupenda kusoma vitabu hudorora na hatimaye kufa kabisa? Na kama hatujisomei, sisi ni taifa ambalo tumo nuruni au gizani?

Samahani kwa maswali mengi lakini haya ni maswala ambayo huwa yananikera na kunikereketa sana.

Sunday, March 22, 2009

TAMADUNI ZINAPOGONGANA

  • Nilishangazwa na mshtuko walioupata wanafunzi wa Kimarekani baada ya kuwaonyesha picha hii ya keki ya arusi ya Kichaga. Wengine mpaka ilibidi watoke nje ya darasa kwenda "kujikusanya" na wengine walisema huu ulikuwa ni unyama wa kupindukia. Niliwaambia kwamba hata wao walikuwa na vipengele vingi tu katika utamaduni wao ambavyo vingeweza kuwatia kichefuchefu Waafrika. Niliwakumbusha kwamba kumbe hata wao hawakuwa na tofauti na babu zao wa Ulaya waliokuja katika bara letu na kuita karibu kila kitu kuwa kilikuwa cha kishenzi. Sijui mshenzi alikuwa nani - yule mgeni mjinga asiyeelewa utamaduni wa mwenyeji na hataki kujifunza au mwenyeji anayeyajua vizuri mazingira yake na kujivunia utamaduni wake uliomkuza na kumlea? Niliwaambia hawa wanafunzi kwamba tabia yao hii ya kutotaka kujifunza na kutokuwa na uvumilivu na tamaduni zingine ndiyo imewaletea matatizo katika vita vyao vya Iraq na Afghanistan - ambako walidhani kwamba silaha zao kali za kutisha na mabilioni ya dola yangeweza kushinda utashi na utaifa wa watu. Mwisho wa darasa walikuwa wamesuuzika na wale wenye mtazamo mpana waliahidi kuziangalia tamaduni zingine kwa heshima na jicho jumuishi.
  • Hata hivyo ni lazima nikiri hapa kwamba hawa jamaa waliokuja "kutustaarabisha" walifanya kazi nzuri mno ya "kutustaarabisha" kifikra na kutushenzisha; na kutufanya tuamini kwamba utamaduni wetu ulikuwa wa kishenzi. Ndiyo maana leo hii tunaiga kila kitu cha kigeni na kudharau vya kwetu. Ndiyo maana baada ya miaka zaidi ya hamsini ya uhuru bado tunafundishana "mlima Kilimanjaro uligunduliwa na ...." Chanzo cha mto Nile kiligunduliwa na..." Nitaandika kwa kirefu juu ya mada hii katika makala itakayotoka katika gazeti jipya la Jamii Kwanza. Tumalizie na maneno ya Steve Biko - yule mwanaharakati shujaa wa Afrika Kusini asiyetetereka aliyeuawa kikatili na makaburu..."the most potent weapon of the oppressor is the mind of the oppressed"

Friday, March 13, 2009

PICHA HIZI ZINAKUKUMBUSHA NINI?

Hasa kwa vijana mliokulia vijijini au mnaoyafahamu vizuri mazingira ya vijijini, picha hizi zinaleta kumbukumbu gani? Mimi zimenikumbusha mbali sana kwani huu ndio ulikuwa wakati wetu enzi zile tukiwa vijana (kama asemavyo mwanafalsafa Simon Kitururu) wa kuwa kwenye fani. Sasa ninapoziangalia picha hizi kidogo nashangaa. Kwa nini wavulana (ambao pengine ndio wenye nguvu zaidi) hatukujitolea/hawajitolei hata siku moja kumsaidia binti kubeba hiyo ndoo ya maji ili aweze kusikiliza hoja kwa makini na raha?

Sunday, March 8, 2009

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI - NAMUENZI MAMA

Ndio wanaojidamka saa 10 alfajiri kwenda kutafuta maji ya kunywa. Ndio wanaotembea maili nyingi kwenda kutafuta kuni. Ndio wanaofanya kazi mashambani kutwa ingawa mara nyingi hawafaidi wakizalishacho. Ndio mhimili na nguzo kuu ya familia na malezi. Ndio.....NI AKINA MAMA....

Katika kusherehekea sikukuu ya wanawake duniani leo napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza mama yangu mzazi Eunice Longh'we Mgema Dindai pamoja na akina mama wote duniani. Mama - wewe ni shujaa wangu nambari wani. Baada ya kuondokewa na mumeo mpendwa tukiwa bado wachanga hukukata tamaa bali ulitulea vyema na kuhakikisha kwamba tunasoma - ukilima pamba kila mwaka ili tupate karo ya shule. Hatuna cha kukulipa mama mbali na kusema tu asante kwa kujitoa muhanga kwako - leo hii sisi na wajukuu zako tunayo maisha yenye ridhiko na matumaini. Mungu akubariki sana na daima utabakia kuwa shujaa wetu!!!

Tunaungana na Boyz II Men katika wimbo wao wa A Song to Mama katika kukushukuru na kukutakia maisha marefu na yenye afya - wewe pamoja na wanawake wote duniani. Bila nyinyi pamoja na umakinifu wenu katika malezi ya watoto sidhani kama tungekuwa na jamii. ASANTENI SANA!!!

video

Thursday, March 5, 2009

WANAHISABATI WA KESHO...

Nakumbuka enzi zile nikisoma darasa la kwanza pale Shule ya Msingi Sima (Bariadi), tulikuwa tunatumia vijiti. Mimi nilikuwa na vijiti 100 nilivyokuwa nimevichonga kwa ustadi mkubwa sana. Ijapokuwa nilikwenda darasa la kwanza nikiwa tayari najua kusoma, kuandika na kuhesabu (kujumlisha, kugawa n.k.) ilikuwa bado lazima kuwa na vijiti. Japo mabinti zangu hapa wao wanajifunza haya mambo kwa kutumia picha na michezo ya kufurahisha katika kompyuta, vijiti na vifuniko vya soda hivi vinaonyesha ubunifu wetu wa kutumia kile tulichonacho katika mazingira yetu na kukifanya kile tunachojifunza kionekane chetu na chenye maana zaidi. Ubunifu huu hata hivyo hufifia mapema mtoto anapoanza kwenda madarasa ya juu ambako mkazo huwa katika kukariri zaidi na elimu huwa tena haihusiani kabisa na mazingira yanayomzunguka. Kwa mfano, kuna anayejua ni kwa nini tulikuwa tunakariri Jedwali Radidi la Elementi (Periodic Table of Elements)? Je, elementi hizo hazipo katika mazingira yetu? Elimu yetu masikini - mtu unakariri (au unadesa), unaandika ulichokariri katika mtihani, unapata A - unasonga mbele (hata kama hufahamu cho chote). Halafu kesho unapewa kazi unaboronga watu wanaanza kulalamika. Nani wa kulaumiwa?

Tuesday, March 3, 2009

MATUNDA YA KIASILI NA MAISHA YA KUMBUKONI

Picha hii kutoka kwa Mjengwa imenikumbusha mbali sana. Enzi zile tukichunga ng'ombe Unyantuzu Bariadi tulizoea kula hayo matunda meusi madogomadogo ambayo kwa Kisukuma (Kinyantuzu) yanaitwa Nhobo. Yakiiva yanapasuka na inabidi uwe na meno imara kuyatafuna hasa pale mwanzoni. Ukishavuka hii hatua ya mwanzo basi yanakulainikia mdomoni na kutoa utomvu mweupe mzito mtamu unaonatanata. Unatafuna mpaka unahakikisha kwamba utomvu huo umeisha. Unatema makapi yanayobakia, unachukua tunda jingine na kuanza upya. Asante sana Bwana Mjengwa kwa picha hii ambayo imenipa taswira nzuri sana ya maisha yale 'simple', matulivu na yenye ridhiko tuliyoishi enzi zile tukiwa watoto.

Sunday, March 1, 2009

KUTOKA MAKABAILA MPAKA MAFISADI - TUMEPIGA HATUA?

Naona Profesa Ndumilakuwili yuko kwenye profesheni yake hapa. Anamnyemnelea jamaa ambaye amenona na moja kwa moja anachukulia kwamba pengine ni fisadi.

Enzi zile watu wenye "afya" (ambayo kwa sababu zisizoeleweka inaashiriwa na unene au kitambi) walikuwa wanaitwa makabaila, mabepari na makupe. Inaonekana sasa ukiwa na "afya" a.ka. mnene mwenye kitambi basi wewe ni fisadi. Je, wenye vitambi vya gongo na dengerua je?

Tumetoka makabaila, tukaingia wahujumu uchumi enzi za Moringe Sokoinne na sasa tumeingia mafisadi. Tumepiga hatua, tuko pale pale tumesimama tisti au tunarudi nyuma? Tutabadili majina mpaka lini?

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO