Wanablogu wenzangu, nilikuwa nimebanwa na pilikapilika za kubeba maboksi kwa wiki moja na ushee hivi. Sasa nimesharudi na kama kawaida tuendelezeni mapambano ya kuipigania jamii.
==================================================================
Inavyoonekana sasa kila kona ni mashindano ya urembo. Juzijuzi hapa nilisoma katika magazeti kwamba kulikuwa na mashindano ya kumtafuta Miss Maswa - wilaya moja katika Mkoa wangu wa Shinyanga. Halafu tena nikasoma kuhusu mashindano ya kumtafuta Miss. Malampaka - kakitongoji kamoja kule kule Shinyanga. Na karibu kila siku ukisoma gazeti ni lazima utakutana na aina fulani ya mashindano ya urembo mpaka haya mashindano Miss Landmine kutoka Angola.
Kwangu mimi naona kuna ruwaza (pattern) fulani hapa. Kwa kawaida sisi tunayo tabia ya kuiga vitu hata kuwazidi hao tunaojaribu kuwaiga, na hili si jambo la kufurahisha. Na katika haya mashindano ya urembo nadhani tunafanya vivyo hivyo - tena kwa kutumia vigezo vile vile vya hao mabwana wetu wenye utamaduni wenye hadhi. Tukiendelea hivi nadhani mwishowe tutakuwa na Miss Tarafa, Miss Kata, Miss Kijiji na hata Miss familia. Sijui tunaelekea wapi. Wakati mwingine hata nawasikitikia hawa dada zetu wanaojikondesha ili waweze kushiriki haya mashindano ya "urembo".
Mambo yamebadilika kwa kasi sana kwani juzijuzi tu hapa wembamba kwa Mwafrika ulikuwa ni dalili ya matatizo ya kiafya na watu walipendelea mwenzi aliyetakata. Na kutokana na mazingira ya kufanya kazi sana, wenzi hawa waliotakata hata hawakuwa na matatizo ya kiafya mengi kama saratani, kiharusi na shinikizo la damu - magonjwa ambayo sasa yanaenea kwa kasi bila kujali kama mtu amejikondesha ama la. Kwa ujumla utandawazi unavuruga kila nyanja ya maisha yetu. Sijui tunaelekea wapi.







