NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, August 31, 2009

KWA NINI NI LAZIMA TUULIZE "KWA NINI?" - FUNZO KUTOKA KWA SIR ISAAC NEWTON



Bado unazikumbuka Newton's Laws of Motion? Inasemekana chimbuko lake ni utundu wa Sir Isaac Newton wa kuuliza "kwa nini?" Inasimuliwa kwamba siku moja alikuwa amejipumzisha karibu na bustani alipoona tunda likidondoka kutoka mtini. Jambo hili lilimtatanisha na alianza kujiuliza: kwa nini tunda limedondoka chini badala ya kwenda juu au wimawima na kuangukia sehemu nyingine? Kwa nini chini?

Inasemekana pia kwamba leo hii mambo mengi yanakwenda mbagombago kwa sababu badala ya kuuliza "kwa nini?" tumebadilika na kuwa watu wa "ndiyo". Hata mfumo wetu wa elimu kwa kiasi kikubwa hauwapi nafasi ya kuuliza "kwa nini" akina Isaac Newton wetu. Matokeo yake vyuo vyetu vimegeuka kuwa viwanda vya kufyatua watu wasiohoji mambo - mabingwa wa kukariri na kusema "ndiyo" tena kwa HERUFI KUBWA ZENYE MSISITIZO uliojaa mwangwi wenye ombwe.

Matokeo ya jumla ya mtindo huu tindifu ni jamii ya kikondoo, jamii isiyosaili mambo, jamii isiyouliza "kwa nini?", jamii ambayo (kama kondoo) iko tayari kuifuata sauti tamu ya mchungaji laghai kuelekea machinjioni. Lini tutaanza kuwauliza "wachungaji" wetu "kwa nini?". Kwa nini hawajatufikisha kwenye nchi ya ahadi waliyotuahidi, nchi inayotiririka maziwa na asali? Kwa nini bado tunazunguka jangwani - bila maji, bila malisho, bila kivuli, bila matumaini? Kwa nini inaonekana kama vile wanakotupeleka ndiko siko? Kwa nini?

OBAMA NA NIKOLAS SARKOZY HAPA VIPI???

Hebu utupie tena jicho utafiti huu (hapa). Halafu Watupie jicho mzee mzima Obama na mwenzake Nicolas Sarkozy (Rais wa Ufaransa) katika hii picha. Picha hii "imetamuishwa" au ni picha ya kweli?

Picha imetoka kwa Kamala.

Sunday, August 30, 2009

MATUMIZI YA KISUKUMA KATIKA NYIMBO ZA MTOTO WA DANDU (COOL JAMES)

Ulimwengu unakumbuka miaka saba (na siku tatu) tangu James Maligisa Dandu a.k.a Mtoto wa Dandu a.k.a Cool James a.k.a Ng'wanamalia a.k.a CJ Massive a.k.a Ng'wanawapelana a.k.a Nzokaihenge aage dunia kwa ajali ya gari tarehe 27/8/2002 (tazama hapa). Sikupata bahati ya kumwona lakini yeye pamoja na Saida Kalori na Mr Ebbo pengine ndiyo waimbaji wa kizazi kipya ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kuzitukuza lugha zao za mama katika nyimbo zao - na hivyo kutupilia mbali ile dhana kwamba kizazi cha dot.com hakiwezi kuguswa na nyimbo zenye ladha ya kikabila. Mtoto wa Dandu japo hakuimba katika Kisukuma moja kwa moja, hapa na pale hakuisahau lugha yake ya mama iliyomkuza na kumlea kule Mwanza (Kisukuma). Hapa ni baadhi ya mifano tu ya matumizi ya Kisukuma katika nyimbo za mwanamuziki huyu mashuhuri aliyeondoka akiwa bado mchanga.

Jina lake mara nyingi alipenda kujiita Nzokaihenge yaani nyoka mwenye makengeza (nyoka makengeza). Alikuwa akijiita pia Ng'wanawapelana yaani Mtoto mwenye hasira. Alipenda pia kujiita Ng'wanamalia - mtoto wa Maria. Hii inaonyesha kwamba pengine jina la mama yake ni Maria (Wasukuma hawana sauti " r" na hivyo mara nyingi huitamka kama "l" - kinyume na Wakurya)

Korasi mashuhuri inayosikika katika nyimbo zake nyingi inasema hivi:

Ng'wanamalia
Kolobelaga lukumo lwane.
Jaga Ng'wigulya.
Jaga Ubagisha shikamoo abakolobela ng'weli...

Tafsiri

Mtoto wa Maria
Umashuhuri wangu acha uenee sehemu zote
Uende juu zaidi
Uende ukiwasalimia shikamoo waliokwishasonga mbele

Kwingineko mara kwa mara anasikika akisema:

Nabiza wa galama.
Nulunagaja gubugeni nadiko gwigashiji gogo mpagi sumbi lya nghana

Nimeshakuwa mtu wa thamani (heshima)
Hata nikienda ugenini siwezi kukalia gogo
Inabidi nipewe kiti kizuri cha kukalia

Inavyoonekana pia alikuwa ni mtu wa kutoa shukrani. Katika baadhi ya nyimbo zake anaonekana akimsifia na kumshukuru Jumanne Kishimba - tajiri mkubwa kule Mwanza na mmiliki wa duka kubwa la Imalaseko Supamaketi jijini Dar es salaam. Anasema hivi:

Jumanne Kishimba
Mlinamoyo gwape giti buluba

Tafsiri

Jumanne Kishimba
Mna roho nyeupe mithili ya pamba

Huu ni mfano wa kuigwa. Hebu fikiria kama wanamuziki wengi wa kizazi kipya wangeiga mfano wa Saida Karoli, Mr Ebbo na Mtoto wa Dandu, wakaimba nyimbo katika lugha zao za mama (Saida Karoli - Kihaya) au kuingiza vipengele vya lugha zao za mama katika nyimbo zao kama Mtoto wa Dandu (Kisukuma) na Mr Ebbo (Kimasai). Hatua hii ingesaidia sana kukikumbusha kizazi hiki cha dot com kwamba lugha zao za mama zipo, zina hadhi kama lugha nyingine yo yote na zina manufaa ya kimatumizi hata katika ulimwengu huu wa kisasa. Kwa hivyo dhana ya kwamba lugha hizi ni za kizamani, zimeshapitwa na wakati na hakuna sababu ya kujifunza au kuzizungumza tena haina ukweli wo wote. Ingefurahisha kama nini kama wanamuziki hawa wangetimiza wajibu huu wa kitamaduni na kuziunga mkono lugha zetu za asili katika wakati huu zinapopita katika mikikimikiki ya kudharauliwa na kuonwa kwamba hazifai tena.

Mungu aendelee kumpumzisha salama Mtoto wa Dandu/Cool James/Ng'wanamalia/Ng'wanawapelana/Nzokaihenge/CJ Massive.

Muziki wake kwa hakika utadumu!

Nyimbo zake mbili hizi hapa:

(1) MPENZI


(2) SINA MAKOSA

Saturday, August 29, 2009

WAMAREKANI WANAVYOHANGAIKA NA OBAMA WAO

Picha inajieleza yenyewe. Unaweza pia kutazama hapa na hapa.






Friday, August 28, 2009

UTAFITI: KUTAHIRIWA HAKUWASAIDII MASHOGA KUTOAMBUKIZWA VIRUSI VYA UKIMWI

Ingawa tohara ya wanaume imethibitishwa kuwa njia mojawapo muhimu katika kupambana na maambukizi ya gonjwa la UKIMWI miongoni mwa wanaume wanaofanya mapenzi ya kawaida na wanawake, utafiti uliofanywa na Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (Center for Disease Control and Prevention - CDC) cha Marekani umeonyesha kwamba tohara haisaidii cho chote katika kuzuia maambukizi ya UKIMWI kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao yaani mashoga. Mbali na mambo mengine, utafiti umeonyesha kwamba:
  • Maambukizi ya UKIMWI kwa wanaume wa Kimarekani wanaofanya mapenzi ya kawaida na wanawake yamebakia kuwa ya kiwango cha chini (pengine) kutokana na ukweli kwamba karibu asilimia 80 ya wanaume wote hapa Marekani tayari wameshatahiriwa. Pamoja na asilimia hii kubwa ya tohara CDC imesema kwamba itaendelea kuwahimiza wazazi kuwatahiri watoto wao wa kiume wanapozaliwa.
  • Zaidi ya nusu ya maambukizi mapya ya UKIMWI kila mwaka hapa Marekani yanatokea miongoni mwa mashoga ingawa mashoga ni asilimia 4 tu ya wanaume wote.
Utafiti huo ulihusisha wanaume 4,900 waliokuwa wakifanya mapenzi na wapenzi wao mashoga ambao tayari walikuwa wameshaambukizwa virusi vya UKIMWI. Matokeo yake yalionyesha kwamba hakukuwa na tofauti yo yote katika maambukizi. Mashoga waliotahiriwa na wale ambao hawakutahiriwa waliambukizwa virusi vya UKIMWI kwa kiwango kile kile kinachofanana.

Kutokana na utafiti huu serikali ya Marekani ikishirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema kwamba itaendelea kuhimiza tohara kwa wanaume wa marika yote katika nchi za Kiafrika kama njia muhimu ya kupambana na maambukizi ya gonjwa hatari la UKIMWI. Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa.

Thursday, August 27, 2009

ATI, TANZANIA IMEANZA KUTUMBUKIA KATIKA UDINI?

Nimeiona hii katuni ya Musa Ngarango kutoka katika blogu ya Mjengwa na ikanikumbusha mambo kadhaa. Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kupambana na udini pamoja na ukabila kwani aliamini kwamba kama vitu hivi viwili vingeachiwa vingeweza kuhatarisha mustakabali na umoja wa taifa. Na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa (Msikilize hapa kuanzia dakika ya 9:06).

Kutokana na ule waraka wa maaskofu wa kanisa katoliki, waislamu nao inasemekana wametoa waraka wao (soma hapa). Hali hii inawafanya watu wengi waanze kujiuliza kama Tanzania imeanza kutumbukia katika tatizo la udini - jambo ambalo linaweza kuwa la hatari kama tulivyoshuhudia katika sehemu mbalimbali duniani. Ni lazima tuwe waangalifu sana na jambo hili ili tusije tukajuta baadaye. Cha kushangaza ni kwamba serikali imekaa kimya na inavyoonekana ni kama vile imemwachia Komredi Kingunge Ngombare Mwiru ashughulike na suala hili. Ngoja tuone atasema nini kuhusu huu waraka wa Waislamu!

HUYU MHUBIRI KANIFURAHISHA SANA

Hebu msikilize Mtume Onesmo N. Ndegi wa Living Water Center Makuti Kawe Dar es salaam (ni sekunde 42 tu). Mimi sina cha kuongeza.

Wednesday, August 26, 2009

HATA WEWE NI "CELEBRITY" TENA WA KWELI JAPO HUJUI

Binadamu sie, kwa vile hatujui tunachokijua kuhusu tukijuacho kwamba kinaweza kutupa furaha na ridhiko katika maisha yetu, watu wengi huvutiwa na watu wanaoitwa "ma-celebrity". Ndiyo maana udaku juu ya maisha ya watu hawa ni biashara ya mabilioni ya dola kila mwaka. Tunataka kujua "ma-celebrity" wetu jana walikula nini, walivaa nini, walikwenda wapi, walikuwa na nani, walionekanaje na kwa nini.

  • Tunafikiri kwamba maisha yao ya "u-celebrity" yameremetayo daima pengine ndiyo yanaakisi kiwango halisia cha mafanikio, ridhiko na furaha ya kweli ambayo tunaweza kuipata katika maisha yetu. Ndiyo maana tunashangaa sana tunaposikia kwamba wengi wa "ma-celebrity" hawa hawana furaha na ridhiko katika maisha yao na wengi wanaishi maisha ya ukaburi - kwa nje wanaonekana wamepambika na kumeremeta ajabu lakini kwa ndani wamejaa mafunza na uozo wa upweke, kutoridhika, madawa, ulevi na shida.
  • Orodha ya ma-celebrity waliojihitimishia maisha yao na kutuachia maswali lukuki juu ya maisha-mng'aro waliyoishi ni ndefu. Imethibitishwa, kwa mfano, kwamba Michael Jackson, pamoja na kumeremeta kwake kule, aliyahitimisha maisha yake katika lindi la madawa makali, upweke wa ajabu na maisha ya kukata tamaa (soma hapa).
  • Kwa vile hatujui tunachokijua kuhusu tukijuacho kwamba kinaweza kutupa furaha na ridhiko katika maisha yetu, "u-celebrity" wa kweli kwangu mimi ni kuwa na familia yenye furaha, familia inayopendana na kujaliana (kama hiyo katika picha)
  • Ninapotoka kazini nikiwa nimechoka na kuvikuta vibinti vyangu virembo vimalaika vya Mungu vikinisubiri kwa hamu tucheze, tukimbizane, tufanye "homework" pamoja, tusimuliane hadithi (zikiwemo za Kisukuma), tule ugali na kusali pamoja - kwangu mimi huu ndio "u-celebrity" wa kweli, "u-celebrity" unaozidi hata ule wa kuandamwa na mapaparazi barabarani wakiwa wamesheheni vimwekamweka. Huu ndio "u-celebrity" unipao ridhiko la kweli na furaha nono mno katika moyo wangu.
  • Naamini kwamba hata wewe ni "celebrity" wa kweli hapo nyumbani kwako japo hujui! Na kama bado hujawa, basi nakuomba sana uwe. Haigharimu cho chote!

Tuesday, August 25, 2009

UTAFITI: KUENDESHA GARI HUKU UKITUMA UJUMBE KWENYE SIMU (TEXTING) NI HATARI ZAIDI KULIKO KUENDESHA UKIWA UMELEWA POMBE AU BANGI

Utafiti uliofanywa na "The Transport Research Laboratory" nchini Uingereza umeonyesha kwamba madereva wanaotuma ujumbe huku wakiendesha wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ajali kuliko wenzao waliokunywa pombe kiasi au kuvuta bangi. Madereva hawa ni wale wenye umri kati ya miaka 17-24 (matineja). Kwa mfano utafiti umeonyesha kwamba:

(1) Utayarifu wa madereva hawa kuepuka ajali ulipungua kwa asilimia 35 ikilinganishwa na asilimia 12 kwa waliokuwa wamekunywa pombe kiasi na asilimia 21 kwa wavuta bangi.

(2) Madereva waliokuwa wakituma au kusoma ujumbe katika simu zao walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kutangatanga kutoka sehemu moja ya barabara kwenda nyingine na uwezo wao wa kudhibiti usukani ulipungua kwa asilimia 91 ikilingalishwa na wenzao wanaoendesha bila kutumia simu. Wavuta bangi, kwa upande mwingine, uwezo wao wa kudhibiti usukani ulipungua kwa asilimia 35.

(3) Madereva hawa pia walikuwa na taabu ya kuacha nafasi inayotakiwa kati yao na magari yaliyo mbele yao. Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa.

Tatizo hili ni kubwa hasa hapa ninapoishi kwani ni kamji kadogo na kuna wanafunzi wapatao 50,000 hivi na mara kwa mara utawaona wengine wakituma na kusoma ujumbe kwenye simu zao na wengine wamelala au wanasinzia huku wakiendesha.

Kama na wewe mdau una tabia hii ya kutuma na kusoma ujumbe kwenye simu yako wakati unaendesha, fikiria mara mbilimbili kabla ya kufanya hivyo. Ajali nyingi sana (za magari, treni, mabasi n.k.) zimetokea hapa Marekani na zimethibitishwa kwamba zilisababishwa na utumaji na usomaji wa ujumbe kwenye simu kwa madereva waliohusika. Kwa mfano tazama hapa (Onyo: Kuna picha za kutisha. Usitazame kama hujiwezi). Hiyo text message bila shaka inaweza kusubiri mpaka utakapofika nyumbani!

Monday, August 24, 2009

MHESHIMIWA DR. HARRISON MWAKYEMBE: WANAIGERIA WANATUMIA JINA LAKO KUFANYIA UTAPELI

Nimepata hii email na nikafurahi kuona kwamba Mheshimiwa Mbunge Dr. Harrison Mwakyembe kaniandikia (kuandikiwa na Mheshimiwa mbunge si jambo rahisi ati!). Basi nilipoifungua nikakuta kumbe ni wale matapeli wa Nigeria. Kazi kwelikweli!
================================================

Your friend, DR. HARRISON MWAKYEMBE (drharrison209@yahoo.com) has sent you this information from Yahoo! (Email address has not been verified.)

Personal message:
ATM INTERNATIONAL CREDIT SETTLEMENT
OFFICE OF THE DIRECTOR OF OPERATION
OFFICE OF THE PRESIDENCY

ATTENTION HONORABLE BENEFICIARY

THIS IS TO OFFICIALLY NOTIFY YOU THAT WE HAVE VERIFIED YOUR CONTRACT INHERITANCE FILE AND FOUND OUT THAT WHY YOU HAVE NOT RECEIVED YOUR PAYMENT IS BECAUSE YOU HAVE NOT FULFILLED THE OBLIGATIONS GIVEN TO YOU IN RESPECT OF YOUR CONTRACT/INHERITANCE PAYMENT.


SECONDLY, WE HAVE BEEN INFORMED THAT YOU ARE STILL DEALING WITH THE NONE OFFICIALS IN THE BANK,ALL YOUR ATTEMPT TO SECURE THE RELEASE OF THE FUND TO YOU.WE WISH TO ADVISE YOU THAT SUCH AN ILLEGAL ACT LIKE THIS HAVE TO STOP IF YOU WISH TO RECEIVE YOUR PAYMENT SINCE WE HAVE DECIDED TO BRING A SOLUTION TO YOUR PROBLEM. RIGHT NOW WE HAVE ARRANGED YOUR PAYMENT THROUGH OUR SWIFT CARD PAYMENT CENTER ASIA PACIFIC, THAT IS THE LATEST INSTRUCTION FROM MR. PRESIDENT,UMARU MUSA YAR'ADUA (GCFR) PRESIDENT FEDERAL REPUBLIC OF NIGERIA AND FEDERAL MINISTRY OF FINANCE.


THIS CARD CENTER WILL SEND YOU AN ATM CARD WHICH YOU WILL USE TO WITHDRAW YOUR MONEY IN ANY ATM MACHINE IN ANY PART OF THE WORLD,BUT THE MAXIMUM IS ONE THOUSAND FIVE HUNDRED DOLLARS PER DAY, SO IF YOU LIKE TO RECIEVE YOUR FUND THIS WAY PLEASE LET US KNOW BY CONTACTING THE CARD PAYMENT CENTER AND ALSO SEND THE FOLLOWING INFORMATION TO HIM IN ORDER TO PROCEED IMMEDIATELY:


1. FULL NAME
2. PHONE AND FAX NUMBER
3. ADDRESS WERE YOU WANT THEM TO SEND
THE ATM CARD TO(P.O BOX NOT ACCEPTABLE)
4. YOUR AGE AND CURRENT OCCUPATION
5. A COPY OF YOUR IDENTIFICATION

HOWEVER, KINDLY FIND BELOW THE CONTACT PERSON:
MR, HENRY ONYEMEM
DIRECTOR, ATM PAYMENT
DEPARTMENT
EMAIL: paymentcode.atm128@gmail.com

THE ATM CARD PAYMENT CENTER HAS BEEN MANDATED TO ISSUE OUT ($8,300,000.00 USD) AS PART PAYMENT FOR THIS FISCAL YEAR 2009. ALSO FOR YOUR
INFORMATION, YOU HAVE TO STOP ANY FURTHER COMMUNICATION WITH ANY OTHER PERSON(S)OR OFFICE(s) TO AVOID ANY HITCHES IN RECEIVING YOUR ATM PAYMENT.

FOR ORAL DISCUSSION, I CAN BE REACHED ON OR EMAIL ME BACK AS SOON AS YOU
RECEIVE THIS IMPORTANT MESSAGE FOR FURTHER DIRECTION AND ALSO UPDATE ME ON ANY DEVELOPMENT FROM THE ABOVE MENTIONED OFFICE.

HAVE IN MIND THAT BECAUSE OF IMPOSTORS, WE HEREBY ISSUED YOU OUR CODE OF CONDUCT, WHICH IS (ATM-128) SO YOU HAVE TO INDICATE THIS CODE WHEN CONTACTING THE CARD CENTER BY USING IT AS YOUR SUBJECT.

BEST REGARDS,

HON. DR. HARRISON MWAKYEMBE (TANZANIAN LEGAL & FINANCIAL EXPERT)
CHIEF AUDITOR TO THE PRESIDENT
FEDERAL REPUBLIC OF NIGERIA

ATI, HATUWEZI KUJADILI JAMBO BILA KUTUKANANA

Katika mada ya utafiti yenye kichwa "Utafiti: Watu Weusi Ndiyo Wanaongoza kwa Unene" kulizuka mjadala mkali sana kati ya mdau mmoja anayeitwa Aika M na Ma-anonymous kadhaa. Msimamo wa Aika ni kwamba yeye hapendi watu weusi kwa sababu ni wavivu, wachafu, wasiojituma, waliolaaniwa, wenye magonjwa, na kila mahali wanapowekwa ni lazima mambo yaharibike - iwe ni Afrika, Marekani, Australia, Karibeani na kwingineko. Aika yeye hataki mwanaume mweusi na anatafuta mwanaume mzungu amuoe na kumpeleka Ulaya; na akishaenda huko basi hatatia mguu wake Afrika tena!

Msimamo huu wa Aika uliwasha moto vibaya sana na ma-anony kadhaa walimwandama kweli kweli. Hata hivyo ukitazama vizuri ni watu wachache ambao walichangia mjadala huu kwa kutoa hoja (mf. tazama michango ya watu ambao si ma-anonyous). Mjadala haukukawia kugeuka na kuwa mashindano ya kutukanana. Jambo hili lilinisikitisha kwani nimeshawahi kulilalamikia sana katika ile makala yangu ya "Ati, Ze Utamu Imetufundisha Nini?" Ati, ni kwa nini hatuwezi kujadili jambo bila kutukanana?

Hapa chini ni maoni ya kina kuhusu sababu zinazosababisha tabia hii kutoka kwa mdau makini wa blogu hii. Yeye anaamini watu wengi hawawezi kujenga hoja katika mijadala kwa sababu ya mfumo wetu wa elimu ambao unawawezesha vijana wetu kukariri tu; pamoja na usasa/utandawazi. Vijana wanashinda katika kompyuta wakiangalia mitandao ya ngono na mambo ya udaku basi. Hawana haja na mambo ya muhimu yanayotokea duniani na kwa hivyo welewa wao kwa ujumla unakuwa mdogo. Soma hoja zake hapa chini uone kama unakubaliana naye.
===========================================
Habari,

Kwakweli inasikitisha kuona watu wanageuza blogu ya CHAKULA (na nyingine pia) kuwa ni uwanja wa kutua frustration zao. Mi nafikiri lengo la kuwa na blogu ni kushea ideas, uzoefu na mengine mengi educative.

Naogopa hata kuweka haya mawazo kwenye blogu yako maana naweza kutupiwa makombora mazito utafikiri Ze Utamu vile. Unajua hapa nyumbani huwa kuna kipindi kinarushwa na ITV kinachowakutanisha wa somi wa vyuo vikuu vya baadhi ya nchi za Afrika.

Huwa ninakipenda sana na kukifuatilia kipindi hicho, cha ajabu ni kwamba vyuo vyetu vya Tanzania huwa tunashindwa vibaya sana. Nilichogundua ni kwamba tatizo si lugha isipokuwa ni kwamba hatuna UFAHAMU wa kutosha wa dunia jinsi inavyokwenda. Mfumo wa elimu yetu ni mbaya sana. Tunasoma kwa ajili ya kujibu mitihani, baada ya mtihani kila kitu tumesahau. Sawa huo unaweza kuwa ndo mfumo ambao ni mbaya kweli, lakini baada ya kumaliza elimu tulitakiwa kuwa na utamaduni wa kusoma na kujua ulimwengu unavyokwenda na kupata maarifa mbalimbali, lakini si hivyo. Watu wape magezi ya udaku nani kafumaniwa, sijui sasa fulani ana mimba fulani ana VIRUSI. Mambo yasiyo kichwa wala miguu ambayo hata ukiyasikia au usiposikia hayana maendeleo yoyote. Sasa ikiwa fikra zetu ni mbovu kiasi hicho sijui tutafiti vipi kwenye huu ulimwengu wa sasa.

Huwa ninaumia moyo sana nikiona hata waandishi wetu hawafurukuti kwenye mashindano ya waandishi wa habari yanayotolewa na CNN ingawa mara mbili tatu tumeshinda lakini si kama wenzetu.

Hata ukitembelea blogu nyingi utaona. Weka jambo ambalo linataka uchangiaji wa kisomi kama kuna mtu atachangia lakini weka suala la NGONO basi mada itakuwa ni motomoto Kila mtu atataka kuchangia.. Kwanini? Blogu inageuzwa kilabu cha pombe.

Watu wanatoa mawazo yao ya ajabu sana. Sawa kuna uhuru wa kutoa maoni lakini mbona watu wana-abuse? Maana ya kwenda shule inakuwa hata hakuna. Kama umekwenda shule basi toa hoja za kisomi. Watu kama akina Aika na baadhi ya akina ANONY(s) (nimewataja with all due respect) naona kama wanatumia uhuru wao wa maoni vibaya. Kuwa na uhuru wa kutoa mawazo si kutukana watu, hakuna haja ya kuonesha watu ULOFA wako. Kubishana just for the sake of it ni mbaya sana, ni kweli mtu unaweza kuwa na mawazo au msimamo wako tofauti na watu wengine, lakini baada ya kusikia wengine wanasemaje juu ya jambo fulani, badala ya kuwaponda watu hao just kubali yaishe maana inawezekana kubishana juu ya jambo la kipuuzi mwaka mzima. Kama nilivyogusia si lazima umuoneshe mtu ulofa wako, unaweza kuwa na mawazo yako ambayo watu wengine hawaafikiani nayo basi kaa kimya.

Kwenye blogu mbalimbali ilikuwa ni sehemu ya waungwana kukutana kujifunza, kubadilishana mawazo na uzoefu na mambo mengine kama hayo. Zamani pia watu walifikiri kwenye internet ni sehemu ya kuangalia ngono tu, kumbe ni the largest library ever. Naomba nikupe experience yangu moja. Nilikuwa na mdogo wangu anasoma IFM, alikuwa na shida ya pesa tulikakubaliana nimplelekee chuoni. Sikumkuta chumbani kwake lakini akanieleza kwamba alikuwa kompyuta room. Nilipoingia, guess what chamber kulikuwa na kompyuta 20 ama zaidi. Kulikuwa na wanafunzi na kila mmoja alikuwa kwenye mtandao wa ngono isipokuwa mdogo wangu (wote walikuwa ni wavulana) na yeye bila shaka alibadili tu kwa kuwa alijua nilikuwa nakwenda. Niliona aibu kwani kwa mila zetu za kiafrika ni nadra sana kukuta kaka na dada eti wanaangalia ngono. Nilijifariji kwamba angalau yeye hakuwa akiangalia ngono. Na asingeweza kuwaambia eti wenzie wabadili websites walizokuwa wanaangalia kwa kuwa SISTA ANAKUJA.

Lakini msikate tamaa endeleeni kupika na kutulisha chakula kitamu envetually tutabadilika for the better. Kwa kweli tuna safari ndefu. Elimu inahitajika ambayo itatukomboa.

Saturday, August 22, 2009

VYUO VIKUU BORA VYA MAREKANI HIVI HAPA

Kila mwaka gazeti/shirika la U.S News and World Report huchapisha orodha ya vyuo vikuu bora hapa Marekani. Baadhi ya vigezo vinavyotumika katika kuandaa orodha hii ni pamoja na upatikanaji wa mahitaji muhimu (waalimu, vifaa n.k), idadi ya wanafunzi wanaoomba kujiunga na wale wanaopokelewa, idadi ya wanafunzi wanaohitimu pamoja, maoni kutoka kwa marais wa vyuo n.k. (tazama hapa). Kwa mwaka huu chuo nilichosoma shahada za uzamili (M.A) na uzamifu (PhD) katika Isimu (Linguistics) kati ya mwaka 1997 - 2003 kimeshika namba mbili kwa ubora kati ya vyuo vya umma. Hiki si kingine bali ni Chuo Kikuu cha California, Los Angeles - University of California, Los Angeles (UCLA). Chuo hiki kimezungukwa na Hollywood, Beverly Hills na Bell Air; na maisha hapa ni ghali sana. Ni chuo bora kabisa katika nyanja nyingi zikiwezo Isimu, Udaktari, Biashara na fani nyinginezo. Kumi na tano bora ya vyuo vikuu vya Marekani mwaka huu imekaa ifuatavyo:

(I) VYUO VYA UMMA

1. University of California Berkeley
2. University of California Los Angeles (UCLA)
2. University of Virginia
4. University of Michigan
5. University of North Carolina, Chapel Hill
6. William and Mary (Virginia)
7. Georgia Tech
7. University of California, San Diego
9. University of Illinois, Urbana Champaign
10. University of Wisconsin, Madison
11. University of California, Davis
11. University of California, Santa Barbara
11. University of Washington
14. University of California, Irvine
15. Penn State
15. University of Florida (chuo ninachofundisha sasa)

Kwa orodha kamili ya vyuo ya umma tazama hapa.

II. Ukijumlisha na VYUO BINAFSI, kumi bora imekaa ifuatavyo:

1. Harvard University
1. Princeton University
2. Yale University
4. California Institute of Technology
4. Massachusetts Institute of Technology (MIT)
4. Stanford
4. University of Pennyslvania
8. Columbia University
8. University of Chicago
10. Duke

Kwa orodha kamili ya vyuo vyote (umma na binafsi) tazama hapa.

Nyumbani kumeibuka vyuo vikuu vingi sana kwa miaka ya karibuni. Kama tukivipanga kwa ubora sijui itakuwaje. Mlimani naamini kitachukua nambari wani...na vitakavyofuatia hapa wala sina fununu lakini pengine Mzumbe....

Friday, August 21, 2009

UTAFITI: TALAKA INAWEZA KUKULETEA MATATIZO SUGU YA KIAFYA

Ingawa tafiti mbalimbali tayari zimeshaonyesha kwamba watu waliooa au kuolewa (wanandoa) wanaishi maisha yenye afya nzuri zaidi kuliko makapera (Mzee wa Changamoto na Dada Koero mnasikia?), wanasayansi walikuwa bado hawajajua kinachotokea kiafya ndoa inapovunjika.

Utafiti mpya unaonyesha kwamba wanandoa wanapokuwa makapera tena ama kupitia talaka au kifo, mbali na kupata misukosuko ya kimihemko (emotions), mara nyingi afya zao pia huporomoka. Mporomoko huu wa afya huwa ni wa kudumu hata kama wakioa/wakiolewa tena baadaye. Ili nisirudie kila kitu katika utafiti huu, hapa chini ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyotajwa.

  • Kiafya inaonekana ni bora kutooa kabisa kuliko kuoa na kuacha ama kuachika. Watu wa makamo ambao hawakuwahi kuoa wana matatizo sugu ya kiafya machache kuliko wale waliooa na baadaye kutalikiana au kufiwa na wapenzi wao.
  • Kwa ujumla wanandoa waliotalikiana au waliofiwa na wapenzi wao wana matatizo sugu ya kiafya (mf. kisukari na saratani/kansa) mengi zaidi kwa asilimia 20 kuliko wenzao ambao hawajatalikiana au kufiwa na wenzi wao.
  • Japo kuoa/kuolewa tena kulionekana kuboresha afya, utafiti umeonyesha kwamba wanandoa waliorudia ukapela ama kupitia talaka au ujane, kamwe hawarudii afya walizokuwa nazo kabla ya ndoa zao kuvunjika. Watu ambao ndoa zao zilivunjika halafu wakaoa/wakaolewa tena walikuwa na matatizo sugu ya kiafya mengi zaidi kwa asilimia 12 kuliko wenzao ambao ndoa zao hazikuwahi kuvunjika. Kwa habari zaidi juu ya utafiti huu soma hapa.

Kama kawaida utafiti huu umefanyika kwa wazungu ambako kiutamaduni ni tofauti sana na nyumbani. Kwa mfano, ningependa kujua kama talaka ina madhara yo yote kiafya kwa mwanaume mwenye wake zaidi ya mmoja au mwenye nyumba ndogo. Nyumbani pia nadhani kwamba wanawake ndiyo wanaathirika zaidi na talaka kwani wao ndiyo hutakiwa kubeba visulupwete vyao na kuondoka. Huku Marekani mara nyingi mwanaume ndiye anafungasha virago vyake na kuwaachia mama (na watoto) nyumba.

  • Mwathirika mkuu wa talaka, kwa maoni yangu, ni watoto!
  • Inasemekana India ndiyo ina idadi ndogo kabisa ya talaka wakati Sweden ndiyo inaongoza (Dada Yasinta upo?) ikifuatiwa na Marekani. Tazama hapa.

Wednesday, August 19, 2009

MWALIMU NYERERE ALIPOUNGURUMA CHIMWAGA (1995) NA KUTUPATIA BENJAMIN MKAPA. ALIKUWA SAHIHI?

Ni katika hotuba hii ambayo Mwalimu aliitoa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM waliokuwa wamekutana katika ukumbi wa Chimwaga kule Dodoma mwaka 1995 kuchagua mgombea wa urais ambapo kimsingi alianza na hatimaye alifanikiwa kumtengenezea Mheshimiwa Benjamin Mkapa njia ya kuwa rais. Mwalimu alitaja sifa nne kuu za kiongozi aliyekuwa akimtaka: (1) Kiongozi ambaye angeweza kupambana na rushwa (2) Aliyekuwa anafahamu kwamba nchi ya Tanzania bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao bado ni masikini, kiongozi ambaye angepambana na (3) Udini pamoja na (4) Ukabila (Sikiliza sifa hizi kuanzia dakika ya 9:06). Mwalimu aliamini kwamba kiongozi mwenye sifa hizi kamwe asingeweza kutoka nje ya CCM, ambamo pia aliamini kwamba kulikuwa na kansa ya uongozi mbovu. Tazama baadhi ya kauli zake hapa.

Baada ya kuisikiliza tena hotuba yake hii (ambayo nimeitoa kwa Dada Subi a.k.a Nukta 77) naamini kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na nia njema kutuchagulia Mkapa; na aliamini kabisa kwamba Mkapa ndiye alikuwa kiongozi safi kati ya wagombea wote wa urais wa wakati ule. Kutokana na tunayojua (au tunayofikiri tunajua) sasa kuhusu baadhi ya wagombea wale, Mwalimu alikuwa sahihi kutuchagulia Mkapa? Mimi nadhani kwamba Mwalimu alikuwa sahihi kwani sioni mgombea mwingine wa wakati ule ambaye "angejaribu" kama alivyojaribu Mkapa.

Tuesday, August 18, 2009

MNAIONA "PARADOKSI" KATIKA PICHA HII?

Nafikiri lengo la mtengenezaji wa picha hii inayokera (ambaye naamini ni mzungu au Mwafrika anayetafuta misaada kwa wazungu) ni kuonyesha, mbali na mambo mengine, kwamba wakati sehemu nyingine duniani wanapambana na unene, Afrika pamoja na utajiri wake wote, yenyewe bado watu wake wengi wana utapiamlo na wengine wanakufa kwa njaa.

Kama utafiti niliourejerea Ijumaa ya wiki jana ulivyoonyesha, sababu kubwa iliyotajwa kuwa chanzo cha unene ukiwemo ule wa futufutu (obesity) nchini Marekani ni umasikini. Swali la ki-paradoksi ni kwamba, inakuwaje sababu ile ile moja (umasikini) isababishe utapiamlo na kufa kwa njaa Afrika (ambayo ni tajiri sana) na unene (wa futufutu) Marekani na Ulaya?

Monday, August 17, 2009

HATA ADOLF HITLER ALIJUA

Adolf Hitler (1889-1945), yule dikteta hatari aliyetaka kuitawala dunia nzima, alijua kwamba nguvu na mamlaka yake yalitegemea "ujinga" na kutofikiri kwa umma. Alisema hivi:

"What luck for rulers that men do not think"

Rais George W. Bush (II) yeye alisema hivi:

“You can fool some of the people all the time, and those are the ones you want to concentrate on.”

Ni mambo mangapi ambayo wanasiasa, viongozi na "watawala" wasingeweza kuyafanya kama wangekuwa wanatawala umma unaofikiri? Nchi kama yetu na Afrika kwa ujumla ingekuwa wapi kama umma wake ungekuwa umeamka?

Mwanamapinduzi Che Guevara alisema "I am not a liberator. Liberators do not exist. The people liberate themselves." Dawa ya ufisadi, uonevu, rushwa na matatizo mengine mengi yanayotukabili ni umma ulioamka. Na watawala wetu wanajua hivyo.

Friday, August 14, 2009

UTAFITI: WATU WEUSI NDIYO WANAONGOZA KWA UNENE

Utafiti uliofanywa na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Centers for Disease Control and Prevention) vya Marekani unaonyesha kwamba watu weusi ndiyo wanaongoza kwa unene wa futufutu (obesity) hapa Marekani. Utafiti huo umeonyesha kwamba karibia asilimia 36 ya watu weusi ni wanene futufutu ikilinganishwa na asilimia 24 tu kwa wazungu. Hii ni hatari kwa sababu unene huu wa futufutu ndiyo kisababishi kikubwa cha magonjwa kama kisukari (diabetes), magonjwa ya moyo, kiharusi, shinikizo la damu na baadhi ya saratani. Hii pengine inaweza kueleza ni kwa nini watu weusi ndiyo wanaongoza kwa kufa mapema hapa Marekani.

Sababu kubwa iliyotajwa katika utafiti huu ni umasikini. Watu weusi ndiyo masikini zaidi na kwa hivyo hawana pesa za kujinunulia vyakula vizuri visivyonenepesha (kama mbogamboga), bima za afya na pesa za kujiunga na vilabu vya kufanyia mazoezi (gyms).

Sababu zingine ni za kitamaduni. Imetajwa kwa mfano kwamba katika utamaduni wa watu weusi unene (ukiwemo huu wa futufutu) hauonwi kama ni tatizo na kwa hivyo watu hawaoni sababu za kujibidisha kupunguza uzito wao. Mambo ya kuitana Big Dady (jibaba), Big Mama (jimama) na hata tabia ya watu weusi kupenda wanawake wanene ni sababu za kitamaduni zinazochangia ufutufutu kwa watu weusi.

Wanawake weusi ndiyo wanaongoza zaidi katika unene huu wa futufutu wakifuatiwa na wanaume na halafu watoto. Jimbo la Maine ndilo linaongoza kwa kuwa na watu weusi futufutu wengi zaidi (asilimia 45). Kwa habari zaidi soma hapa.

Niliposoma utafiti huu nilifikiri mambo mawili. Kwanza, kwa nini unene huku ni dalili ya umasikini wakati sisi kule nyumbani ni (ilikuwa) dalili ya utajiri? Pili, kwa nini watu weusi ndiyo wanaongoza kwa umasikini hapa Marekani? Nani alaumiwe kwa tatizo hili?

"I AM THE GREATEST!" - MUHAMMAD ALI

Mchezo wangu mimi ni masumbwi na hakuna mwingine kama mwenyewe "The Greatest!" - ndani na nje ya ulingo.

Thursday, August 13, 2009

MWALIMU NYERERE NA OMBWE LA UONGOZI TANZANIA

Katika kipindi cha pili cha uongozi wa awamu ya pili, Mwalimu Nyerere aliamini kwamba kulikuwa na ombwe (vacuum) la uongozi katika chama na serikali ya CCM. Na kwa vile hulka (nature) inayo tabia ya kutovumilia ombwe, Mwalimu aliamini kwamba ombwe hilo la uongozi ama lingezibwa na chama cha upinzani (japo hakuona chama kizuri hata kimoja) au CCM iliyojirekebisha. Alisema yafuatayo:

"Waingereza wana msemo: "Nature abhors a vacuum", "hulka huchukia ombwe". Hata siasa huchukia ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo, au upo kwa maslahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo; hauwezi kuachwa wazi hivi hivi. Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, una tabia ya kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni tofauti na hulka ya siasa ya watu wengine; kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu" (Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Zimbabwe Publishing House 1993:52)

Ati, CCM imeshajirekebisha na kuziba ombwe hilo la uongozi chamani na serikalini mwake? Kama bado, wapinzani wana nafasi yo yote ya kuliziba katika uchaguzi wa mwaka kesho? Wapinzani wenyewe, wanao uwezo wa kuweka uongozi imara usiotetereka na wenye kuweka maslahi ya wananchi mbele? Kwa maneno mengine, kuna chama cha upinzani makini ambacho kinaweza kuchukua nafasi ya CCM, na kuleta mabadiliko yatakayolinufaisha taifa?

MASHINDANO YA UREMBO YAZIDI KUPAMBA MOTO TANZANIA - SASA KUNA MISS TOTOZ!

Haya unaambiwa ni mashindano ya Miss Totoz Temeke (2009). Ina maana kuna Miss Totoz Ilala, Kinondoni, na wilaya zingine Tanzania au yanafanyika kitaifa? Picha na post nzima nimevidokoa kutoka blogu ya Father Kidevu (samahani Father Kidevu). Ni kazi kwelikweli!

Miss Totoz 2009, Fatuma Issa

Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, Dully Sykys, akiimba na watoto, wakati wa kutumbuiza onyesho la Miss Totoz Temeke 2009.

Miss Totoz Tmk 2009, Fatuma Issa(kati) akiwa na mshindi wa pili Jane Anthonyn na mshindi wa tatu Yunis Anthon wakati wa onyesho.

Mbunge wa Viti Maalum Al-Shymaa Kwegiar akiwa na washiriki wa Miss Totoz katika ukumbi wa Equator Grill Dar es Salam jana (10/8/2009)

Habari kamili kuhusu mashindano haya hatimaye nimezipata kutoka kwa Michuzi Jr

Fatuma Issa (7) ameibuka kidedea katika shindano la kumpata Malkia wa Watoto, Miss Totoz Temeke 2009 katika Ukumbi wa Equator Grill baada ya kuwashinda warembo wenzake 11 katika shindano lililokuwa gumu na la aina yake wakati majaji Mariam Chaheli, Jowalipokuwa wakichuja nafasi ili kumpata mrembo wa Ukweli kwa Watoto wa Wilaya ya Temeke.

Shindano hilo ambalo lengo lake ni kukuza na kuendeleza Sanaa kuanzia ngazi za chini lilikuwa na mvuto na msisimko mkubwa kutokana na watoto kuchuana vikali kila mmoja akiitaji kuibuka na ushindi na kuweka rekodi ya kwanza katika maisha yake katika shindano hilo, warembo waliobahatika kupanda jukwaani ni pamoja na Janey Anthony, Fatuma Issa, Zaituni Hassan, Neema Ally, Ester Frenk, Ashura Omary,Mariam Karama,Nasra Ally, Yunis Anthony, Angela Silayu,Happy Peter, na Eda Damian.

Aidha warembo waliobahatika kuingia katika hatua ya tano bora ni pamoja na Fatuma Issa, Jane Anthony, Yunis Anthony, Mariam Karim, na Ashura Omary,ambapo nafasi ya pili ilichukuliwa na Jane Anthony, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Yunis Anthony, Mgeni Rasmi katika Onyesho hilo la Miss Totoz alikuwa ni Mh. Mbunge wa kuteuliwa viti Maalum, Al-Shymaa Kwegiar, ambaye aliwapongeza waandaaji wa shindano hilo kampuni ya Jacqueline Intertaiment kuwa yana nia njema ya kuwapata washiriki wa masuala ya Urembo kwa miaka ijayo.

"shindano hili kusema kweli ni la kipekee, ukiwatazama watoto unagundua kuwa pia wanaitaji kupatiwa mafunzo haya ikiwa mapema ili ifikapo wakati wa mshiriki anakuwa apati tabu na pia anakuwa ana tena aibu kama tunavyowashuhudia baadhi ya washiriki wanashindwa hata kujielezea, kujibu swali hata kama siyo gumu, ukweli wengi wao wanakuwa na aibu, hivyo watoto wakianza kufunzwa angali wadogo bila shaka siku zijazo tutakuwa na washiriki wengi wa Urembo"alisema Al-Shymaa

Naye mratibu wa mashindano hayo kwa watoto Jacqueline Magayane alisema kuwa baada ya kupata watoto warembo wa Temeke sasa ni zamu ya ilala na kisha Kinondoni ambako warembo wa Miss Totoz watano kila Mkoa wa Kipolis watashindana kupata mshindi mmoja wa jiji la Dar es Salaam mapema mwaka huu, "kwa kweli ndiyo kwanza tunaanza kuweka changamoto kwa watoto wetu, kwani tunao warembo wengi sana watoto ambao wakipatiwa maelekezo wakiwa na umri mdogo watakuwa katika mazingira ya kutambua vipaji vyao na hivyo kuzidi kuviendeleza, kwa hiyo hadi sasa nimepata warembo wa Temeke watano na sasa watapatikana wengine wa wilaya zote na kisha watashindana ili kupata wa Jiji letu.

kikubwa ninawaomba watu mbalimbali kujitokeza kusaidia kufanikisha shindano hili ambalo ni changamoto kwa watoto wetu, ili pia waweze kujitambua umuhimu wao juu ya masuala ya Urembo wakiwa bado wadogo kama ilivyom katika masuala mengine kama mpira wa miguu, na kikapu watoto wanaanza kuelimishwa wakiwa wadogo na hivyo kukua wakijua namna ya kuvitumia Vipaji vyao"alisema Jack

Mshindi wa kwanza katika shindano hilo alizawadiwa TV na Cheni, wa pili na wa tatu Radio na Cheni wa nne na tano walipatiwa cheni kila mmoja, sambamba na washiriki wote kupatiwa vifaa vya shule ikiwamo vitabu, peni, na madaftari ambavyo vyote vilikabidhiwa na mgeni Rasmi Mh. Mbunge Viti Maalum, Al-Shymaa Kwegiar.

Wednesday, August 12, 2009

NIMETUMIWA HOMEWORK YANGU YA PHYSICS YA KIDATO CHA NNE (KAHORORO SEC, MWAKA 1988)

Mdau Ephraim amenitumia homework yangu ya Fizikia niliyofanya nikiwa kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Kahororo. Yeye alisoma Kahororo baadaye kidogo na aliikuta homework hiyo ikiwa bado ingaliko. Mwalimu wangu wa Fizikia - Christian Agricola - alikuwa anapenda sana mwandiko wangu kiasi kwamba alikuwa ananipa madaftari ya bure mara kwa mara kama zawadi ingawa uwezo wangu katika somo hilo ulikuwa ni wa hivi hivi tu!

Kama unavyoweza kudhani, homework hii imenikumbusha mambo mengi sana, kwani baadhi ya misimamo yangu kuhusu maisha ilifinyangwa katika kipindi hiki - uvumilivu, kutokata tamaa, kufanya kazi kwa bidii, kusamehe, kujizuia na mengineyo.

Ijapokuwa nilikuwa napenda masomo ya sayansi (hasa Bayolojia kiasi cha kushika namba moja katika mtihani wa Mock mkoa wa Kagera), kusema kweli nilikuwa sipendi kukariri tu vitu nisivyovijua katika Fizikia na Kemia. Na japo mpaka leo ninaweza kukutajia Newton's Laws of Motion, elementi 21 za mwanzo katika Jedwali Radidi la Elementi (Periodic Table of the Elements) na mengineyo, mambo mengi kwangu yalikuwa kama usiku wa giza na tulikariri tu kwa lengo la kufaulu mitihani. Ndiyo maana ulipofika wakati wa kuchagua "combination" nilimwasi mwalimu wangu wa Bayolojia (Mwl. Kabyemela) aliyenisisitiza sana kuchagua PCB (Physics, Chemistry na Biology) kama combination yangu ya kwanza. Alipoondoka nilirudi kwa mwalimu wa taaluma na kujaza fomu zile upya safari hii nikichagua HGK (History, Geography na Kiswahili) kama chaguo langu la kwanza. Nilitaka kusoma vitu ambavyo nilikuwa navifahamu - vitu ambavyo sikuhitaji kujifunza kipurure (rote learning) na Historia, Jiografia na Kiswahili yalikuwa ni masomo ambayo yalinipatia nafasi hiyo, kwanza Sengerema High School na baadaye Mlimani.

Mpaka leo siujutii uamuzi huu ambao niliufanya wakati ule nikiwa bado kijana mdogo ninayejitafuta mimi mwenyewe na nafasi yangu hapa duniani. Maisha yetu ni mafupi sana hapa duniani na hakuna jambo la muhimu kama kufanya kile ukipendacho na ambacho kinakupa ridhiko moyoni mwako ali mradi hakiwadhuru wengine na wewe mwenyewe.

Katika jitihada zangu za kuipa "uhai" sayansi machoni mwa vijana wetu, nimeamua kuanzisha mfululizo uitwao "Wajue Vingunge wa Sayansi". Hizi zitakuwa ni makala zilizoandikwa kwa lugha ya kawaida na mimi mwenyewe katika blogu hii juu ya maisha ya wanasayansi mashuhuri na mchango wao katika sayansi. Makala hizo zitakuwa zinatoka hapa kila siku ya Jumatatu. Lengo langu la baadaye ni kuzikusanya makala hizi, kuzihariri na kisha kuzichapicha kama kitabu - kitabu ambacho naamini kitawasaidia vijana wetu kuwasona mabingwa wa sayansi wanaowasoma mashuleni (akina Pythagoras, Archimedes, Isack Newton, Ivan Pavlov, Ohm, Faraday, Hertz, Galileo Galilei na wengineo) na kuwaona kama watu wa kawaida tu ambao, pamoja na kuwa na vipaji, mafanikio yao hasa yalitokana na kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa. Nitafurahi sana mkiniunga mkono kwa kuwafikishia habari vijana wetu walioko mashuleni kule nyumbani!

Tuesday, August 11, 2009

KWA NINI TUSIWE NA REGINALD MENGI HALL PALE MLIMANI?

Hivi karibuni idara ya Lugha za Kiafrika na Kiasia hapa chuoni ilihamia katika jengo jipya linaloitwa Pugh Hall. Pugh mwenyewe ni milionea ambaye alisoma hapa miaka ya 60. Alisoma darasa moja na Bill Graham ambaye alikuwa gavana wa jimbo la Florida, seneta na baadaye mgombea wa uraisi kupitia chama cha Democrat.

Miaka mitatu hivi iliyopita Pugh alitoa pesa (zaidi ya dola milioni 15 ) na akaamua kujenga hilo jengo hapo chini. Ndanimwe kuna Bill Graham Center ambayo inajikita hasa katika kuwaanda vijana wanaotaka kufanya kazi za umma (public service), Idara ya Lugha za Kiafrika na Kiasia (kuwafunza Wamarekani lugha, fasihi na tamaduni zingine) pamoja na Programu ya Historia Simulizi ya Samuel Proctor (ndiyo, wenzetu wana programu za kutunza historia yao!). Ni jengo la kisasa kabisa lenye kila kifaa cha kisasa cha kiteknolojia.

Kwa vile tunaiga, mbona na sisi tusiige tabia ya hawa mamilionea? Ati, mbona tusiwe na Reginald Mengi Hall pale Mlimani? Kuna ubaya gani tukiwa na Rostam Aziz Hall? Edward Lowassa Hall? Andrew Chenge Hall? ...Hii itapunguza shida ya malazi kwa wasomi katika vyuo vyetu. Natumaini serikali haitashindwa kuunga mkono juhudi kama hizi kwa kuchangia pesa zaidi kukamilisha majengo haya yatakayojengwa na mamilionea wetu watakaoamua kuliachia urithi wa kudumu taifa lao lililowatajirisha!

UTAFITI: KUNYONYESHA HUZUIA KANSA YA MATITI KWA ASILIMIA 25 - 60

Mbali na ukweli kwamba kunyonyesha ndiyo chanzo cha lishe bora kabisa kwa mtoto, wanasayansi sasa wanadai kwamba kunyonyesha pia kunaweza kupunguza uwezekano wa mama kupata kansa ya matiti kwa asilimia 25 hadi 60.

Hizi ni habari njema kwa akina mama wa Afrika ambao kimsingi huchukulia kunyonyesha kama mojawapo ya wajibu wao baada ya kupata mtoto. Pengine hii inaweza kuwa ndiyo sababu iliyofanya saratani ya matiti isijidhihirishe sana Afrika.

Wasiwasi wangu ni juu ya kizazi kipya ambacho kinaiga mambo ya Kimagharibi kwa pupa. Nimeshasikia kwamba mabinti wengi sasa hawana hamu tena ya kunyonyesha vichanga vyao wakichelea kuharibu matiti na miili yao. Ukijumlisha na vitu vingine vinavyoingia Afrika vikiwemo vyakula vilivyolimwa "kisayansi", madawa na mabadiliko mazima ya mfumo wetu wa maisha, sitashangaa kama kansa itafumuka na kuwa ugonjwa wa kawaida tu muda si mrefu ujao. Hili likitokea, atakayefaidika bila shaka ni makampuni ya madawa ya nchi za Kimagharibi - na naamini kwamba hiki ndicho wanachotaka. Tuweni waangalifu na tuache mambo ya kuiga vitu kiholela bila kuelewa hasa kiini chake.

Kwa habari zaidi soma hapa. Kwa faida zingine za kunyonyesha soma hii makala ya Kiswahili.


Friday, August 7, 2009

UTAFITI: WANAUME HUTUMIA MWAKA MZIMA WA MAISHA YAO WAKIKODOLEA MACHO WANAWAKE

Nimesoma juu ya utafiti huu ukanichekesha. Watafiti sasa wanasema kwamba kwa wastani mwanamme hutumia dakika 43 kila siku akibung'alia wanawake tofauti tofauti wanaokaribia 10. Hii ni sawa na kutumia mwaka mzima wa maisha yake (tukihesabu kuanzia miaka 18 mpaka miaka 50) akitazama wanawake. Sehemu kubwa ambazo watu hupenda kufanyia shughuli hii ni katika maduka makubwa, katika baa, nightclubs na pengine tunaweza kuongeza barabarani (inasemekana baadhi ya ajali hutokea kwa sababu madereva wa kiume hawaangalii wanakokwenda bali wamekaza macho kwingineko kuangalia wanawake wanaotembea barabarani).

Wanawake nao pia wamo. Kwa wastani wao hutumia dakika 20 kuwacheki wanaume tofauti wanaofikia 6 kila siku. Hii ni sawa na miezi sita ya maisha yao ya kati ya miaka 18 na 50.

Umbo la mwanamke ndiyo sababu kubwa inayowafanya wanaume kumkodolea macho mwanamke wakati macho ya mwanamme ndiyo huwavutia zaidi wanawake. Tukumbuke hata hivyo kwamba utafiti huu ulifanywa kwa wazungu na ukifanywa kwetu pengine utaibua sababu na takwimu tofauti. Kwa habari zaidi soma hapa.

Kuna anayebisha kuhusu jambo hili la kutazamana?

MBUNGE KWENDA JELA ZAIDI YA MIAKA 20 KWA KULA RUSHWA

Huyu jamaa pichani anaitwa William Jefferson na alikuwa Congressman (mbunge?) kutoka jimbo la Lousiana (Marekani) kwa vipindi tisa mfululizo. Jana alikutwa na hatia katika makosa 11 (yakiwemo rushwa na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu) kati ya makosa 16 aliyokuwa akishtakiwa. Kosa mama lilikuwa ni kula rushwa ifikiayo kiasi cha dola za Kimarekani 400,000. Mwaka 2005 mashushushu wa FBI walimwekea mtego na akanasa: alipigwa picha za video akipokea rushwa ya dola 100,000 (pesa zenye namba maalumu kutoka FBI) kutoka kwa mwanamke mfanyabiashara aliyejifanya kuwa alikuwa anahitaji kupatiwa dili nzuri za kufanya biashara Afrika, jambo ambalo Jefferson alidai kuwa angeweza kumtekelezea. Baadaye mashushushu wa FBI walipovamia nyumba yake walikuta dola 90,000 zimefichwa katika friza. Atahukumiwa rasmi tarehe 30/10/2009 na anategemewa kwenda jela kati ya miaka 20 na 150. Kwa habari zaidi soma hapa na hapa.

Sisi pia tunao vigogo mbalimbali wanaokabiliwa na kesi za rushwa na ufisadi mahakamani (Mf. Daniel Yona, Basil Mramba, Liumba na wengineo). Kesi hizi zitamalizika lini? Kweli kuna uwezekano wo wote kwa watuhumiwa hawa ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kuliingizia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi kuweza kukutwa na hatia na hatimaye kwenda jela? Tetesi zilizoenea ni kwamba pengine kesi za vigogo hawa zitaendelea kuunguruma mahakamani kwa muda tu na uchaguzi ukishapita mwakani basi wataachiwa huru kwa ama mafaili yao kupotea au kushinda kesi kutokana na ukosefu wa vielelezo. Halafu bado unaambiwa eti sheria ni kama msumeno unaokereza kotekote bila kujali tabaka la mtu!

Thursday, August 6, 2009

SIASA ZA (KIBAGUZI) MAREKANI: OBAMA HAKUZALIWA MAREKANI, URAIS WAKE NI BATILI

Vuguvugu na uvumi kwamba rais Barack Obama hakuzaliwa Marekani na hivyo, kulingana na katiba, hawezi kuwa rais wa Marekani vinazidi kupamba moto. Juzijuzi hapa mwanajeshi mmoja aitwaye Stefan Cook alikaidi amri ya kwenda vitani Afghanistan akidai kwamba hawezi kwenda kupigana chini ya Amiri Jeshi Mkuu haramu ambaye si Mmarekani kwa kuzaliwa. Wahafidhina wengine kutoka chama cha Republican wakiwemo Rush Limbaugh (mtangazaji mashuhuri wa redio ya Kihafidhina wa chama cha Republican) na Lou Dobbs (mtangazaji wa CNN) wameendelea kudai kwamba Obama alizaliwa Mombasa Kenya na hivyo si Mmarekani kwa kuzaliwa; na kuiweka nchi katika uongozi wa mtu ambaye si Mmarekani kwa kuzaliwa ni jambo la hatari. Pamoja na jimbo la Hawaii alikozaliwa Obama kutoa uthibitisho mara mbili kwamba ni kweli raisi huyo alizaliwa jimboni humo, vuguvugu hili linazidi kupamba moto. Cheti cha kuzaliwa kinachoonyesha kwamba Obama alizaliwa Mombasa Kenya kimethibitishwa kwamba kilikuwa kimeghushiwa (tazama hapa na hapa)

Wachambuzi wengine wanaliona vuguvugu hili kuwa ni juhudi za makundi ya kibaguzi ambayo mpaka leo hayajaamini kama kweli mtu mweusi ndiye rais na yanafanya kila liwezekanalo ili kumwondoa madarakani, au kumfanya ashindwe kama rais. Ni makundi haya haya ambayo yametajwa kuwa yanahusika na ule uvumi ulioenezwa sana kwamba Obama alikuwa/ni shoga (tazama hapa). Mabadiliko yatakuja polepole ingawa bado safari ni ndefu kwani fikra za ubwana za wazungu za karne nyingi za kumwona mtu mweusi kama mtumwa na binadamu wa daraja la pili hazitatokomea hivi hivi. Cha ajabu ni kwamba hata weusi wenyewe tumeaminishwa hivyo na tumeikubali hadhi yetu ya kitwana (mfano, tazama hapa).

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO