NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, September 30, 2009

ATI, WATOTO WA KIMAREKANI WANA AKILI KULIKO WATOTO WA KIAFRIKA?

Mwaka huu nimejitolea kufundisha wanafunzi wa darasa la tatu katika shule moja ya msingi (darasa la kwanza mpaka darasa la tano). Niliamua kufanya hivi ili niweze, mbali na mambo mengine, kujifunza na kuuelewa vizuri mfumo wa elimu wa hawa wenzetu "walioendelea" na kusema kweli nimeona, nimejifunza na kushangazwa na mengi.

(1) Shule zao nyingi zina karibu vitu vyote vya muhimu ambavyo vinawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo. Kuna maabara nzuri, chumba cha kompyuta na vitu vingine muhimu.

(2) Elimu yao inamakinikia zaidi vitendo na wanafunzi wanasisitizwa sana kufanya majaribio yao wenyewe ama wakiwa shuleni au nyumbani wakisaidiwa na wazazi wao. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba wanafunzi hujifunza vizuri zaidi wanaposhirikishwa kivitendo katika kujifunza. Elimu ya kukariri kwa kweli imeshapitwa na wakati na haimsaidii mtoto kujifunza hadi kufikia upeo wake kiakili.

Nimeshangazwa na ukweli kwamba mtoto wa darasa la pili wa Kimarekani anaweza kukueleza vizuri kabisa na kwa kutumia maneno yake mwenyewe mfumo mzima wa maji (hydrological cycle) pamoja na dhana mbalimbali za msingi katika sayansi kama usumakishaji (magnetism), umeme, nguvu ya uvutano (gravity), mwendo (motion), ukinzani (friction), mfumo wa sayari (planetary system), sauti, sifa za mada (properties of matter), hali ya hewa na majira, nishati (energy) pamoja na dhana nyinginezo. Ni kutokana na ukweli huu kwamba nilianza kujiuliza kama wanafunzi hawa wana akili zaidi kuliko wanafunzi wa nyumbani. Nilikumbuka pia utafiti mmoja ambao ulilinganisha watoto wa Ulaya na wa Afrika. Utafiti huo ulionyesha kwamba watoto wa Afrika wako "slow" wakilinganishwa na wenzao wa Ulaya. Kwa nini?

Mbali na matatizo mengi yanayoukumba mfumo wetu wa elimu (ambayo mengi ni ya kujitakia tu), tatizo kubwa kabisa kwa maoni yangu ni lugha ya kufundishia. Ni ukweli wa kisayansi kwamba elimu ya kweli inawezekana tu pale mtoto anapofundishwa katika lugha anayoifahamu vizuri. Ili mtoto aweze kukomaa na kufikia kilele chake cha kiakili ni lazima afundishwe kwa lugha yake mwenyewe. Cha ajabu ni kwamba mtoto wa Kiafrika, kinyume na mtoto wa Kichina anayefundishwa kwa lugha yake ya mama, kinyume na mtoto wa Kijapani anayesomeshwa kwa lugha yake ya kwanza, kinyume na mtoto wa Kithailand anayefundishwa kwa lugha yake ya mama, kinyume na....mtoto wa Kiafrika yeye anafundishwa katika lugha ambayo HAIELEWI, lugha ambayo haifundishwi vizuri na hata wafundishaji wenyewe hawaimudu vizuri. Matokeo yake elimu inakosa maana na inageuka kuwa zoezi la kukariri tu - hata kwa dhana zilizoko katika mazingira yake mwenyewe kama hii ya "hydrological cycle", mmomonyoko wa udongo, mito n.k. Ati, kukariri "Newton's Laws of Motion" kikasuku kweli ni elimu?

Bila mabadiliko ya kweli katika mfumo mzima wa elimu mimi naamini kwamba Afrika tutaendelea kuwa washangiliaji tu katika mchezo wa kisiasa, kitamaduni na kiuchumi unaochezwa hapa duniani. Mbaya zaidi hata "wasomi" wachache tunaowapata kupitia mfumo wetu huu wa kukaririshana kikasuku hasa katika nyanja za utabibu na uhandisi wanakimbia kwenda nje na hakuna anayejali.

Watoto wote wako sawa na dai la kijumla kwamba eti watoto wa Ulaya/Kizungu/Kimarekani wana akili kuliko watoto wa Kiafrika halina ukweli wo wote wa kisayansi. Kama watoto wa Ulaya/Kizungu/Kimarekani wanaonekana kuwa "sharp" ni kwa sababu elimu yao iko makini zaidi na wanayo bahati ya kufundishwa katika lugha yao wenyewe. Kwa bahati mbaya sana mtoto wa Kiafrika hana bahati hiyo!

Monday, September 28, 2009

HIKI CHOO KIMENIKUMBUSHA MBALI SANA - FUNZO KWA WATUNGA SERA

Kwa wale ambao mmekulia mijini pengine hamjawahi kutumia choo kama hiki. Lakini kwa wale waliokulia mijini, choo kama hiki ni cha kawaida sana na mpaka leo ukienda vijijini vyoo vya aina hii bado utaviona!

Nakumbuka katikati ya miaka ya 80 kulikuwa na kipindupindu kijijini kwetu na serikali iliamru kila familia kuchimba choo pamoja na kuchemsha maji ya kunywa. Kila siku ungewaona vijana wa mgambo wakizunguka kila kaya kukagua kama kulikuwa na choo na kama maji ya kunywa yalikuwa yanachemshwa.

Ambacho wanamgambo hawa hawakukijua ni kwamba watu walitii amri ya serikali na kuchimba vyoo lakini walikuwa hawavitumii, na walikuwa wanachemsha maji ya kunywa na kuyaweka katika mtungi mkubwa sana kwa ajili ya kuwaonyesha wanamgambo hawa wakija lakini maji haya walikuwa hawayanywi. Wakati ule sikuelewa ni kwa nini wakati kweli kipindupindu kilikuwepo na kilikuwa kinaua watu.

Baadaye niligundua kwamba kulikuwa na tatizo: watu walikuwa hawaamini kwamba kipindupindu kilikuwa kinasababishwa na kunywa maji machafu bali ushirikina. Eti watu walikuwa wanarogana na kusingizia kipindupindu. Kwa mantiki hii, watu hawakuona sababu ya kunywa maji yaliyochemshwa (ambayo walidai hayana ladha nzuri kama yale ambayo hayakuchemshwa) na kutumia vyoo (ambavyo walidai vinanuka sana) wakati wanajua kwamba haisaidii cho chote katika kuzuia kipindupindu.

Serikali nayo kwa upande wake haikuchukua hatua yo yote kuwaelewesha watu kwa kina kuhusu visababishi, kinga na tiba ya kipindupindu. Yenyewe iliweka amri tu ya kuchimba vyoo na kuchemsha maji ya kunywa ikidhani kwamba watu hawa wa kijijini "wasiofahamu" cho chote wangetenda kama walivyoambiwa. Mpaka leo, sera nyingi (hata ziwe nzuri namna gani) zinashindwa kwa sababu zimepandikizwa tu kwa walengwa wake - hasa walengwa hao wakiwa ni watu wa kijijini ambao inasadikiwa na kuaminika kwamba ni watu ambao wanastahili kuambiwa na kuelekezwa nini cha kufanya. Sera nyingi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali zingepata mafanikio mno kama zingejipa muda wa kuwaelewa walengwa wake - zikajibidisha sana kujumuisha maoni, maarifa na uzoefu wao katika uandaaji na upangaji wa sera hizo. Bila kufanya hivi, tutaendelea kucheza katika mduara usio na fundo huku tukiwalaumu watu wa kijijini kuwa ni "wajinga", wasio na elimu, wasiostaarabika, wasiosaidika wakati ukiangalia na kuchunguza vyema - pengine watunga sera, "wasomi" na mabingwa wa kuelekeza ndiyo wajinga!

Picha ni kutoka kwa Mjengwa

Saturday, September 26, 2009

NI LAZIMA TUKOJOE "VICHOCHORONI"?

Mwanafunzi mmoja mzungu aliyekuwa anafanya utafiti kule Tanga, Mbeya na Dar es Salaam alinieleza kushangazwa kwake na tabia ya wanaume kukojoa hovyo hovyo mijini. Swali hilo lilinikumbusha Mtanzania mmoja ambaye alipigwa faini kali pamoja na kupewa adhabu ya kuokota takataka mabarabarani baada ya kubambwa laivu akikojoa katika sehemu ya maegesho ya magari kule jijini Los Angeles. Mtanzania huyu alishangaa zaidi kwamba tabia yake hii ya kukojoa hovyo kidogo imletee matatizo alipokwenda kwenye usaili kwa ajili ya kupatiwa "Green Card". Aliulizwa kama alikuwa amewahi kukojoa tena hadharani. Baada ya miaka saba - bado rekodi zilikuweko kwamba alikuwa amewahi kukojoa hadharani (public urination, indecent exposure)!

Ati, ni kwa nini tunapenda kukojoa mabarabarani na vichochoroni? Ni ukosefu wa vyoo vya umma na miundombinu wezeshi (kama mitaro mizuri, madampo, magari ya kuzoa taka n.k) au ni tabia yetu ya kupenda "uchafu"? Ni kweli kwamba sisi tunapenda "uchafu"?

Huyu mwanafunzi mzungu aliniambia kwamba vikojozi wote wa umma aliowaona walikuwa wanaume na kamwe hakuwahi kuona mwanamke akikojoa barabarani. Nilimpa maoni yangu kuhusu suala hili na kumtaka asifikie majumuisho (generalizations) ya haraka haraka kama mababu zake walivyofanya walipotia guu Afrika kwa mara ya kwanza wakiwa na Biblia zao mikononi huku wakidai kwamba walikuwa wamekuja "kutustaarabisha"

Hawa jamaa hapo juu wamenifurahisha jinsi walivyoamua "kukilinda" kijiwe chao na hili tangazo. Wasiwasi wangu ni kwamba sidhani kama hili tangazo litasaidia cho chote!

Friday, September 25, 2009

PESA ZAKO ZINANUKA - NA BEN R. MTOBWA

Pesa Zako Zinanuka ni Riwaya nzuri sana iliyoandikwa na Marehemu Ben R. Mtobwa na kuchapishwa na Heko Publishers mwaka 1984. Niliisoma nikiwa Mlimani lakini nilipoziona picha za hawa "waheshimiwa" nikaikumbuka riwaya hiyo. Itabidi niitafute niisome upya. Mwisho wa "waheshimiwa" hawa sijui utakuwaje. Ngoja tusubiri tuone lakini ni wazi kwamba mabilioni yao yananuka. What a legacy!











Thursday, September 24, 2009

ATI MABINTI - NI LAZIMA MUOLEWE?

  • Katika jamii nyingi za Kiafrika wanawake walitegemewa kuolewa mara tu walipovunja ungo. Binti ambaye alibakia kuwa nyumbani bila kuolewa alionwa kama mwenye matatizo na kwa kawaida halikuwa jambo jema. Hata mwanamke angekuwa amesoma vipi, hata kama angekuwa na kazi nzuri au uwezo mkubwa wa kiuchumi kiasi cha kuweza kuendesha maisha yake bila kumtegemea mwanaume, bado jamii ilimtegemea aolewe. Kule Usukumani wanawake wa aina hii walikuwa wakiitwa 'bagidatolwa' - wasiooleka!
    • Katika gazeti la USA Today la leo kulikuwa na makala iliyokuwa, mbali na mambo mengine, inaonyesha jinsi ambavyo idadi ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 na kuendelea ambao hawajawahi/hawataki kuolewa imekuwa ikingezeka hapa Marekani. Kwa mfano makala hiyo imebainisha kwamba mwaka 2006 asilimia 27.3 ya wanawake wote hapa Marekani walikuwa hawajaolewa na hawategemei kuolewa. Mwaka 2008 idadi hiyo ilikuwa imefikia zaidi ya asilimia 28.1%. Wanawake wengi wanasema kwamba hawaoni sababu ya kuolewa. Naamini kwamba katika nchi nyingi za Ulaya na kule Skandinavia kwa dada Yasinta, mambo ni yale yale.
    • Kwa vile hizi ni zama za utandawazi - ambapo tunaiga kila kitu cha wazungu, sitashangaa kama jambo hili tutaliiga pia. Hata hivyo nadhani kwamba pengine uigaji wetu hapa utachukua muda kwani nimeambiwa kwamba sasa kuoza mtoto pale Dar es salaam imegeuka kuwa ni nafasi ya wazazi kujionyesha uwezo wao wa kifedha kuanzia kitchen party, send off party (sijui kama hizi ni tofauti) na hatimaye harusi yenyewe. Wazazi wanatumia mamilioni ya shilingi katika shughuli hizi za kuoza watoto wao na pengine kila binti atapenda siku moja kushiriki katika umeremetaji huu wa kitambo na kuwafurahisha wazazi wake. Naamini pia kwamba jamii bado inaiona ndoa kama taasisi muhimu katika ujenzi na utangamano wa jamii. Swali hasa ambalo ningependa kuwauliza wanawake ni hili: Je, kuolewa ni lazima? Kwa nini?
    • Ati, jamii ya leo inamtazamaje mwanamke ambaye ameamua kukaa peke yake bila kuolewa?
    Hebu tumsikilize Daudi Kabaka na wimbo wake Mashuhuri wa Msichana Mwenye Sura Nzuri.

    KABURI LA WILLIAM SHAKESPEARE LINAHITAJI MATENGENEZO - LA SHAABAN ROBERT JE?

    (1) Paa la kanisa alimozikwa William Shakespeare - yule mwandishi mashuhuri katika fasihi ya Kiingereza (kule Stratford-upon-Avon) limeoza na linahitaji matengenezo yatakayogharimu dola 80,000 za Kimarekani. Matengenezo hayo yanategemewa kuanza mara moja!













    (2) Hapa chini ni kaburi la Shaaban Robert - yule mwandishi bora kabisa katika fasihi ya Kiswahili. Kwa nini William Shakespeare aenziwe vile na Waingereza na sisi tumfanyie hivi Shaaban Robert wetu? Mwamko wetu wa kitamaduni uko wapi? Makaburi ya akina Chifu Mkwawa, Kinjeketile, Mtemi Mirambo na mashujaa wetu wengine tunayatunzaje kwa ajili ya vizazi vijavyo? Hata hili nalo mpaka tupate wafadhili? Kwa uchambuzi wa kina kidogo kuhusu suala hili gonga hapa.

    Wednesday, September 23, 2009

    WAMAREKANI NA SERA YAO YA MICHEZO - MFANO KUTOKA CHUO KIKUU CHA FLORIDA

    Jumamosi ya wiki jana (tarehe 19/9/2009) kulikuwa na mechi ya "mpira wa miguu" wa Kimarekani kati ya Chuo Kikuu cha Florida na Chuo Kikuu cha Tennessee. Mechi hiyo iliyochezewa hapa Chuo Kikuu cha Florida ilihudhuriwa na watazamaji wapatao laki moja (100,000) hivi. Kwa kawaida kunapokuwa na mechi za mpira wa miguu wa Kimarekani (ambao huchezwa kwa kutumia mikono) familia nzima husafiri hata umbali wa maili 500 kuja kushuhudia mpambano. Hii huambatana na kupika vyakula, kuchoma nyama na kunywa bia. Mwaka huu kuna msisimko wa aina yake kwani Chuo Kikuu cha Florida ndicho kilichukua ubingwa mwaka 2006, mwaka 2008 na mwaka huu timu yake inasemekana ndiyo timu bora kabisa hapa Marekani (gonga hapa). Inawezekanaje mechi ya chuo kikuu ihudhuriwe na watazamaji 100,000?

    Wamarekani wana sera nzuri sana ya michezo. Kwao wachezaji huanza kuandaliwa mapema wakiwa katika shule za mwanzo mwanzo kabisa na mtoto anapofika High School tayari kipaji chake kinakuwa kimeshajulikana. Makocha wa vyuo vikuu wanakwenda kusaka wachezaji kutoka katika High School hizi. Makocha wa timu mbalimbali zinazoshiriki ligi za mashirika ya michezo kama National Basketball Association (NBA) na National Football League (NFL) nao huenda kutafuta wachezaji kutoka vyuo vikuu mbalimbali. Ni pale tu mchezaji anapokuwa na kipaji cha pekee (kama Kobe Bryant wa Los Angeles Lakers au Lebron James wa Clevelend Cavaliers) ndiyo anaweza kuruka ngazi ya chuo kikuu na kwenda moja kwa moja katika NBA. Sijui kama kwenye NFL inawezekana kuruka hatua ya kucheza katika chuo kikuu. Kwa hali hiyo wachezaji wao wote wanakuwa angalau wamepita chuo kikuu na wameanza kuandaliwa tangu wakiwa watoto. Hii inawawezesha kucheza michezo yao kisayansi na kuimudu kwa kipeo cha hali ya juu sana.

    Hivi karibuni tumekuwa na Hashim Thabeet ambaye amefanikiwa kuingia NBA baada ya kupitia Chuo Kikuu cha Connecticut. Kama vile ambavyo Mzee wa Changamoto alihoji baada ya kukerwa na mapokezi makubwa aliyopatiwa Hashim (ikiwemo kukaribishwa Ikulu), Tanzania ilimfanyia nini ili kukikuza kipaji chake kabla hajaenda Marekani? Ni wazi kwamba tunao akina Thabeet wengi tu lakini je tunawaandaje? Tunasubiri kimiujizaujiza tu wacheze soka la mchangani halafu waibukie Yanga au Simba, wavume kwa miaka miwili mitatu hivi halafu wanafifia na kusahaulika. Wachezaji wa aina hii hata wakienda nje, inawawia vigumu kukubalika katika kiwango cha kimataifa kwani, mbali na matatizo ya tofauti za kitamaduni ikiwemo lugha, bado wanakuwa hawana zile "basics" za mchezo kama taaluma ya kisayansi. Vipaji vyao vinakuwa bado havijanolewa sawasawa. Kumbuka kwamba sisi bado tunategemea "mafundi" na "wazee" wa timu katika michezo.

    Naamini kwamba tukiwa na sera nzuri ya michezo tunaweza kuwa na wachezaji wazuri wenye viwango vya kimataifa, wachezaji ambao mbali na kujipatia ajira bora kabisa, wataweza kutusaidia katika kulitangaza jina la nchi yetu na kuwa mfano bora kwa vijana wetu.

    RAIS KIKWETE ALIPOONGEA NA WANANCHI KUPITIA RUNINGA

    Rais Kikwete alipofanya mahojiano na vituo kadhaa vya televisheni vya Marekani ikiwemo CNN, baadhi ya "wasomi" walidai kwamba alitoa majibu ambayo hayakuridhisha - majibu ambayo hayakuwa na data. Hata hivyo alipoongea na wananchi wake tarehe 9/9/2009 kupitia kwenye runinga ya taifa alitoa majibu mazuri (yenye data) ambayo yaliwafurahisha hata wapinzani. Rais alijibu maswali ya wananchi vizuri kiasi kwamba watu wengine walifikiri pengine maswali hayo yalikuwa yameandaliwa.

    Ingawa pengine kulaumu na kulalamika ni rahisi zaidi, si vibaya tukimsifia rais pale anapofanya jambo zuri - na bila kujali sababu hasa iliyomfanya achukue hatua hii hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, mimi naamini kabisa kwamba hili lilikuwa ni jambo zuri. Ninamuomba rais aendelee kuongea na wananchi mara kwa mara na ajaribu sana kuzitatua kero zao kwa vitendo. Hii itazidi kuwapa imani wananchi juu ya kiongozi wao - kwamba yupo na anawajali. Mungu ibariki Tanzania!

    Tuesday, September 22, 2009

    KUMEKUCHA: KAMALA LUTANISIBWA LUTABASIBWA KUMVAA DR. KAMALA BUNGENI

    Kutoka kwa Mjengwa. Pichani ni mwenzetu Kamala Lutatinisibwa nyuma yake kushoto ni Mbunge Ole Sendeka wa Simanjiro, mahali ni kijiwe cha Royal Chef, Lumumba. Taarifa zilizonifikia ni kuwa Kamala Lutatinisibwa keshokutwa alhamisi atakuwa ni miongoni mwa wabunge wa upinzani kwenye Bunge la Vijana litakalofanyika pale Ukumbi wa Karimjee Dar. Niliongea nae kwa simu jana na amenihakikishia kuwa kati ya mambo atakayoyavalia njuga ' atamvaa' Mbunge na Waziri wa Afrika Mashariki Dr. Deodoros Kamala ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo lake. Bila shaka ni kuhusiana na suala la Muungano wa nchi za Afrika Mashariki na nafasi ya Vijana wa Tanzania kwenye soko la ajira. Je, safari ya mwenzetu Kamala Lutatinisibwa kwenda 'Bunge la Kweli Kweli' imeanza?!

    Kamala Lutanisibwa Lutabasibwa - Kweli kumekucha! Nakutakia kila la heri, na kama alivyosema Mjengwa basi huu uwe ndiyo mwanzo wa kumwangusha Dr. Kamala ili uingie kwenye 'Bunge la Kweli Kweli". Hili likitokea nitategemea kwamba utaendelea kublogu na kwamba hutatugeuka na kutupa mgongo kama ilivyo kawaida kwa wale wanaofanikiwa kukifikia kilele!

    SERA YA ELIMU AU SERA YA LUGHA? - NA PROFESA CHARLES BWENGE

    Hapa chini ni makala nzuri ya Profesa Charles Bwenge kuhusiana na sera mpya ya lugha ya kufundishia katika shule za Tanzania, sera ambayo imetilia mkazo Kiingereza kutumiwa kama lugha ya kufundishia kuanzia darasa la kwanza. Makala hii ilichapwa katika gazeti la Kwanza Jamii la tarehe 15/9/2009.

    Sera ya Elimu au Sera ya Lugha?

    Na Profesa Charles Bwenge

    NI ukweli usiopingika kwamba lugha ndio nyenzo kuu ya kufundishia na kujifunzia. Walimu hutumia lugha kufundisha kile walichokusudia na wanafunzi hupata maarifa wanayotafuta kwa kusikiliza kinachosemwa na mwalimu au kusoma kilichoandikwa vitabuni au mitandaoni. Maktaba huhifadhi vitabu. Kitabu hakiwezi kuwa kitabu kama hakuna lugha. Kwa hivyo, huwa ni vigumu kuweka kando suala la elimu unapozungumzia au kuunda sera ya elimu. Pamoja na hayo, ukweli unabaki pale pale kuwa lugha sio elimu. Unaweza kuwa na sera ya lugha bila kuihusisha na elimu. Kwa mfano hapa kwetu tuna wizara ya elimu lakini si wizara ya lugha. Hii ina maana, elimu ni kitu kipana zaidi ya lugha. Lugha ni nyezo, bila shaka nyenzo muhimu katika mchakato wa kuelimisha na kujielimisha au kuelimishana.

    Kwa bahati mbaya, uhusiano huu kati ya elimu na lugha haueleweki vizuri kwa watu wote. Kutoeleweka kwake vizuri katika jamii yetu kumepelekea watu wengi kujenga fikira potofu kwamba kiwango fulani cha ujuzi wa lugha fulani ni kielelezo cha kiwango fulani cha elimu. Kutokana na mtazamo na historia ya ukoloni ambapo kila kilichokuwa cha asili ya Ulaya ndicho kielelezo cha ‘ustaraabu’ na kila kilichokuwa cha asili ya Afrika ni kielelezo cha ‘ushenzi’, tulifanywa kujichukia na kuchukia vitu vyenye asili ya Afrika na kuenzi vitu vya wazungu. Lugha ilikuwa na inaendelea kuwa mojawapo ya ‘kasumba’ hii.

    Waingereza walipotutawala walikuja na lugha yao ya Kiingereza na kuifanya kuwa lugha yenye hadhi ya juu kuliko lugha zote zilizokuwa zikizungumzwa hapa kwetu. Ilifanywa kuwa lugha ya kufundishia hususan katika elimu ya kati na ya juu. Na kwa vile lengo halikuwa kuwapatia watu wote elimu hiyo, wale wachache waliobahatika kuipata ndio wakawa pia wanaomudu Kiingereza. Zaidi ya hapo, elimu yenyewe ilikuwa ni kuwawezesha wakoloni kutawala na kuchuma bila shida.

    Kuanzia wakati huo kiwango cha kumudu Kiingereza kikawa ndio kipimo cha kiwango cha elimu. Kwa Mtanzania, kila anayemudu Kiingereza , au ambaye mayai yanapanda chambilecho vijana wa mitaani, basi huyo ameelimika. Asiyejua Kiingereza huyo hana kitu! Sio tu kwamba tumefikia ambapo Mmarekani ambaye hajaenda hata shule lakini anazungumza Kiingereza kwa sababu ni lugha yake mama anaweza kuja hapa akapewa umeneja wa Tanesco kwa vile ‘amesoma sana’, bali pia kila tunapokuwa na mjadala wa kuhusu sera ya elimu tunaishia kujadili lugha tu kana kwamba lugha ni sawasawa na elimu.

    Mjadala juu ya elimu na lugha nchini mwetu umekuwepo tokea tupate uhuru na unaendelea kuwepo. Lakini kila unapoibuka, tunajikuta tunajadili tu ni lugha ipi kati ya Kiswahili na Kiingereza inafaa kufundishia kiwango kipi cha elimu.

    Mjadala wa lugha umekuwepo kwa sababu lugha hizi mbili ambazo ninaweza kuziita lugha dada zimekuwepo na sisi wenyewe kuendelea kuzishindanisha kwa sababu zisizokuwa za msingi. Wiki ya jana gazeti la The Guardian toleo la mtandaoni la tarehe 9 Septemba 2009 limeripoti kuwa katika pendekezo la sera mpya ya elimu serikali inasisitiza umuhimu wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi. Na sababu za msisitizo huu ni kwamba matumizi ya Kiingereza yameongezeka kutokana na utandawazi. Kama habari hii ni kweli, basi utandawazi umegeuka kuwa utandumazi, yaani unatudumaza.

    Tumerejea pale pale, kiwango cha elimu kinapimwa kwa kiwango cha Kiingereza. Wataalamu wa masuala ya elimu wa hapa kwetu na kwingineko walikwishaweka wazi suala la matumizi ya lugha na kiwango cha elimu. Wanafunzi wanapofundishwa au kujifunza kwa kutumia lugha ya ‘kienyeji ‘ ni rahisi kujenga ubunifu na ugunduzi kuliko wanapotumia lugha ya ‘kigeni’. Ushahidi juu ya hoja hii uko wazi. Nchi zote zinazoitwa ‘nchi zilizoendelea (kiviwanda na kiteknolojia)’ na hivyo ndio nchi tajiri zote zinatumia lugha zao za kienyeji katika elimu kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu. Kwa mfano, zile nchi za G8 na lugha zao za kienyeji katika mabano: Marekani, Uingereza na Canada(Kiingereza), Japan (Kijapani), Ufaransa (Kifaransa), Italia (Kiitaliano), Ujerumani (Kijerumani), na Urusi (Kirusi). Nchi zinazoibukia kwa kasi kama China inatumia Kichina. Kwao wanapofikiria kuboresha viwango vya elimu hawapotezi muda kujadili lugha ipi, bali wanajadili mbinu na mazingira ya kuongeza ubunifu na ugunduzi.

    Hata hivyo, kwa zile nchi ambazo Kiingereza si lugha yao ya kienyeji zinatambua, kama nasi tunavyotambua, kuwa Kiingereza ni lugha iliyotokea kujipambanua kama lugha ya mawasiliano mapana duniani kote. Hili halipingiki. Na mintaarafu utambuzi huo, wamejumuisha mikakati mizuri katika sera ya elimu ya kufundisha Kiingereza katika viwango vya ubora kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu.

    Kiingereza kinavundishwa kwa nguvu zote. Kwa mfano, ukiwakutanisha vijana wawili waliomaliza madarasa kumi na mawili mmoja kutoka Japan na mwingine kutoka Tanzania (tena ambaye amepitia akademi), Mjapani zaidi ya huo ‘uchawi ‘ wa koampyuta alio nao ambao aliupata kupitia Kijapani atakuwa anaongea Kiingereza safi tena chenye lafudhi kama ya wenyeji! Ni kwa nini? Kwa sababu sera yao ya elimu ni kuelimisha jamii na papo hapo bila kusahau kuwa hawaishi kisiwani – lugha ya dunia inafundishwa vizuri.

    Sisi kwa sera zetu mbovu za elimu tunakosa vyote viwili – ubunifu na ugunduzi ni zero na hiyo lugha ya watu tunayong’ang’ania kiasi cha kutaka iwe ya kufundishia nayo ni zero. Wajibu wa Wizara ya elimu ni kupanga sera itakayowezesha wanajamii kupata elimu bora, elimu inayojenga ubunifu, utundu, na ugunduzi katika kila afanyacho binadamu. Si wajibu wa Wizara ya elimu kuwa wakala wa kupalilia kasumba ya kibeberu kwamba kufundishia kwa Kiingereza ndio kutafanya Watanzania wawe watandawazi. Mimi nilifikiri tumeishapita mitego hiyo ya kijinga. Lugha yetu ya kienyeji, Kiswahili, tunayo na inafaa kabisa kufundishia elimu ya kiwango cho chote kama tungeamua hata leo hii. Kwa kutumia Kiswahili tutawezesha vijana kuelimika. Katika sera yetu ya elimu bora hatutathubutu kuacha Kiingereza nje. Tutafanya kama Wajapani na Wachina wanavyofanya, yaani kuwa na mikakati mathubuti ya kufundisha Kiingereza kama lugha ya Kigeni.

    Mtu anaposema tutumie Kiingereza kama lugha ya kufundishia, anataka kutwambia kwetu hapa Kiingereza ni kama lugha ya kienyeji ambavyo ukweli ni kwamba ni lugha ya kigeni na itaendelea kuwa lugha ya kigeni. Kamwe huwezi kutumia lugha ya kigeni kufundishia na ukatarajia kupata watu walioelimika. Hata kama ungekuwa na walimu wanaoimudu lugha hiyo ya kigeni wa kuweza kufundisha shule zote za msingi, kwa mfano, hutaishia kudumaza uwezo wa vijana wa kubuni na kugundua. Mathalani, watoto wa vijijini na hata wa mijini katika familia nyingi watakwenda darasani na kufundishwa kila kitu katika hicho kimombo, lakini wakiwa njiani kurejea majumbani na wakiisharejea dunia yote iliyowazunguka wanaiona, wanaisikia, wanainusa, na hata kuihisi katika Kiswahili.

    Hali kama hii itawadumaza zaidi kuliko hata hiyo bora elimu inayotolewa kwa sasa kwa kutumia Kiswahili. Mwalimu Nyerere alipobuni ‘elimu ya kujitegemea’ kama nyenzo ya kujenga uchumi wa kijamaa na kujitegemea hili alikuwa ameliona na ndio maana ilikubaliwa kuwa Kiswahili ndio ilikuwa lugha muafaka ya kutolea elimu hiyo. Elimu ya kujitegemea ilikuwa na maana pana na ya ndani kuliko baadhi ya watendaji wake walivyoitafsiri. Kiini chake ilikuwa ni kujenga ubunifu na ugunduzi ili taifa hili hatimaye liweze kufikia kujitegemea. Nani asiyependa kujitegemea. Mabepari waliipiga rungu hiyo Sera ya elimu ya kujitegemea pamoja na mzazi wake, itikadi ya ujamaa na kujitegemea - na leo hii sio tu kwamba tunajivunia kuwa mabingwa wa dunia wa kuomba misaada, bali pia tunaona ni haki yetu kusaidiwa na tunapanga hata hizo chembe ndogo tulizokuwa tunazipata kutokana na kutumia lugha yetu nazo zitoweke.

    Kwa kupendekeza kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika mfumo wote wa elimu ni fikira potofu na ni sawa na kuangalia puani, yaani leo tu na kusahau kesho na kesho kutwa.
    Kiswahili kilikuwepo kabla ya mkoloni aliyetuletea Kiingereza, na kiliendelea kuwepo hata baada ya mkoloni kuondoka na kurithiwa na mkoloni mamboleo, na kimeendelea kuwepo hata baada ya ukoloni mamboleo kukabidhi mwenge kwa utandawazi. Kwa mantiki hiyo, hata utandawazi wakati wake utafika na utapisha itikadi nyingine ambayo hatujui kama itakuja na Kiingereza au Kichina.
    Lakini ukweli ni kwamba Kiswahili kitaendelea kuwepo. Kitaendelea kuwepo kwa sababu ni lugha ya kienyeji. Na kwa hoja hii, kama tunafanya uamuzi wa busara na unaoangalia mbele katika vizazi vijavyo, Kiswahili ndio lugha inayofaa kufundishia kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu. Na lugha yo yote ya kigeni ambayo inakuwa imeshika hatamu ya zama husika ifundishwe vizuri sana katika ngazi zote za elimu.

    Kwa zama za leo Kiingereza ndio kimeshika hatamu na hatuna budi kukifundisha vizuri sana. Tushughulikie sera ya elimu itakayotoa elimu bora na ninaamini kuwa ubunifu na ugunduzi miongoni mwa vijana wetu utabakia ndoto tu kama tutaendelea na huu ung’ang’anizi wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Tusikubali utandawazi kutudumaza.

    JINSI YA KUWAKAMATA MATAPELI WA NIGERIA - NA CHRIS HANSEN

    Chris Hansen ni mwandishi wa habari za kiuchunguzi na mtangazaji wa kipindi cha Dateline NBC hapa Marekani. Katika mfululizo huu anaonyesha jinsi matapeli wa Nigeria wanavyofanya utapeli wao. Unaweza kuona ubunifu wa matapeli hawa kwa kubonyeza hapa. Nashangaa mpaka leo hii watu wengi bado wanatapeliwa kwa njia hii. Kwa hapa Marekani inasemekana wazee waliostaafu ndiyo hasa wanatumbukia katika mtego huu wa Wanigeria. Ni kazi kwelikweli!











    Wednesday, September 16, 2009

    HIZI TAKWIMU ZA ELIMU MBONA ZINAKATISHA TAMAA???

    Mwaka 2007 - wanafunzi wanaofikia milioni nane (8,000,000) walikuwa wameandikishwa (wanasoma) katika shule za msingi (darasa la 1 - 7).

    Lakini....

    Mwaka huo huo (2007), ni wanafunzi milioni moja na elfu ishirini na mia tano na kumi (1,020,510) tu ndio walikuwa wameandikishwa (wanasoma) katika shule za sekondari (kidato cha 1 - 6)

    Kuna anayejua/anayejali wanakoenda hawa karibia milioni saba (7,000,000) ambao hawaonekani katika shule za sekondari? Na kati ya hawa milioni moja ambao wamebahatika kufika sekondari, ni wangapi wanafika hadi chuo kikuu? Nilikuwa sijui kama bado tuko nyuma namna hii katika suala zima la elimu. Kwa data mbalimbali za elimu Tanzania, tembelea hapa.

    Friday, September 11, 2009

    HATIMAYE KIINGEREZA KUTUMIWA KAMA LUGHA YA KUFUNDISHIA KUANZIA SHULE ZA MSINGI

    Mnaionaje sera hii mpya ya elimu Tanzania?
    • Kiingereza kianze kutumiwa kama lugha ya kufundishia kuanzia shule za msingi. Kiswahili kifundishwe kama somo.
    • Shule za binafsi ziruhusiwe mapema kuanza kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia na baadaye shule za umma/serikali zitafuata.
    • Soma makala hapa chini kutoka gazeti la "The Guardian" la jana.
    =======================================
    English set to be a medium of instruction in primary schools

    By Erick Kabendera

    The Guardian, 10th September 2009

    • Use of Kiswahili will be consolidated and that of English expanded
    The proposed new education policy has highlighted the importance of using English language as a medium of instruction in primary schools in the country, ‘The Guardian’ has authoritatively learnt.

    A draft of the policy, whose copy was obtained by this newspaper this week from impeccable sources, also indicates that the government has given the green light to a section of private primary schools to use English as a medium of instruction due to requests from parents who favoured their children to be taught in English instead of Kiswahili.

    The government notes in the report that the use of English had increased due to globalisation, thus necessitating making it a medium of instruction in primary schools in future.

    However, the policy points to the heated debate in the country on whether English or Kiswahili be used as a language of instructions at primary school level.

    “So there is need to consolidate the use of Kiswahili and expand the use of English as a medium of instruction in primary schools,” reads the policy in part.

    It maintains that the languages of instruction would be both English and Kiswahili, but that English would only be used as a medium of instruction in private schools and taught as a subject in most of the public primary schools.

    Kiswahili became the medium of instruction at primary schools shortly after independence while English is taught as a subject and used as a medium of instruction in secondary and tertiary education.

    However, proponents of Kiswahili as a medium of instruction argue that using English as a medium of instruction would lead to giving the language more emphasis at the expense of Kiswahili.

    This school of thought wants Kiswahili to become a medium of instruction from primary school to higher learning institutions.

    The policy will be submitted to the Cabinet for approval in two months time before the final draft is relayed to the Parliamentary Social Services Committee for review, after which the Attorney General will prepare a bill from the national policy on education to amend the 1978 National Education Act.

    The proposed policy will replace the current Education and Training Policy which has been in use since 1995.

    The general secretary of Tanzania Association of Managers and Owners of Non Governmental Schools and Colleges (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya welcomed the proposed policy, but said it was unjust for the policy to recommend the use of Kiswahili and English as mediums of instruction at primary school level but limit secondary schools to using English alone.

    Nkonya said non-government schools had advised the government to endorse a system which would allow students to use one language as a medium of instruction from pre-school to tertiary level.

    “We will make the problem worse if students who are taught in Kiswahili at primary level abruptly switch to English as a medium of instruction in secondary school. The decision will weaken the students’ creativity and their ability to learn new concepts.

    “We want the two languages as mediums of instruction to be introduced at the secondary school level so that students may decide which way to go. A student who learned in Kiswahili in primary school should be given a choice to continue learning in the same language until he or she finishes the university,” said Nkonya.

    Following failure to include such provision in the draft policy, Nkonya vowed that non-government schools through their coalition would make sure the provision is included before the policy is endorsed by the ministry of education.

    Elizabeth Missokia, the Executive Director of Hakielimu, an educational NGO said in a telephone interview this week that NGOs dedicated to education would meet at the end of next week under the Tanzania Education Network (TenMet), a national network of more than 200 members to discuss the proposed policy and give their recommendations.

    She said Hakielimu does not favour any of the languages being used as a medium of instruction but said there was need to distinguish between a language of instruction and language of communication.

    The country needed English as a language of communication but Tanzanians needed to ask themselves if there were enough competent teachers to teach English as a medium of instruction or as a subject, she said.

    “Teachers need to master the language they are using to teach. The quality of education is going down in Tanzania and Africa in general so we need to redefine and reflect what we want to achieve otherwise we will never get anywhere,” said Missokia.

    Tanzanians always developed the best policies, but Missokia reckoned that the problem was the implementation of such policies, saying the education policy needed to put special emphasis on improving quality of education and teachers’ welfare rather than focusing on infrastructure development.

    “It is important we start enrolling students who score division one and two into teachers’ colleges instead of those with division four…” she said.

    According to the draft policy, English will remain the medium of instruction at secondary school level, but a research that was conducted by Martha Qorro, a senior lecturer in languages and linguistics at the University of Dar es Salaam titled: “Does Language of Instruction Affect Quality of Education?” says teachers and students at all education levels are able to debate and discuss and ask and answer questions and therefore generate knowledge when they understand the language of instruction.

    “In Tanzania the language of instruction factor has been ignored for a long time and this has had a negative impact on the quality of education…..insisting on using English as the language of instruction in Tanzanian secondary schools and institutions of higher learning does more harm than good towards the provision of quality education as well as language teaching,” she concludes in her research.

    WANASAYANSI - SEMENYA NI "HERMAPHRODITE"

    • Aliposhinda mashindano ya riadha mwezi jana kwa kishindo wengi waliingiwa na wasiwasi kwamba pengine hakuwa msichana na wakataka afanyiwe uchunguzi wa kitaalamu.












    • Halafu akatokea katika gazeti akiwa amejirembua kwelikweli. Mwanamke ni kujiremba ati!












    • Sasa watalaamu wamethibitisha kwamba "binti" huyu wa Afrika Kusini ana viungo vya uzazi vya kike na vya kiume, na viungo vyake vya kiume ndivyo "vinavyotawala". Kwa habari zaidi soma hapa.
    • Kwa hali hiyo "binti" huyu hatapoteza medali zake ingawa shirikisho la riadha linafikiria kutunuku medali nyingine ya dhahabu kwa mshindi wa nafasi ya pili Janeth Jepkosgei kutoka Kenya.
    • Mimi nasubiri mashindano yajayo nione shirikisho la riadha duniani litafanya nini - litamruhusu Semenya ashiriki mashindano ya wanawake au wanaume? Au atapigwa marufuku kabisa?
    • Wengi wanasema kwamba pengine ataombwa afanyiwe upasuaji wa kuondoa viungo vya kiume na kama akikataa basi atapigwa marufuku kushiriki mashindano yo yote.

    Thursday, September 10, 2009

    HATIMAYE IMEKUWA - WAJAWAZITO RUKSA MTIHANI DARASA LA SABA

    Hii ni hatua muhimu katika harakati za kujikomboa kwa wanawake wa Tanzania. Juhudi ziimarishwe zaidi kuwadhibiti wanaowapa mimba mabinti hawa (mf. adhabu kali). Tunasonga mbele!

    Picha kutoka kwa Mjengwa (Gazeti la Sauti ya Watu Tanzania, 9/9/200). Kwa habari kamili soma hapa.

    Wednesday, September 9, 2009

    HOTUBA YA RAISI KWA WANAFUNZI WA TAIFA LAKE INAPOSUSIWA

    Jana rais Obama aliwahutubia wanafunzi wote wa Marekani. Katika hotuba hiyo, Obama aliwaasa wanafunzi hao kufanya kazi kwa bidii, kutimiza wajibu wao na kutenda kile kinachopaswa kutendwa. Hotuba hiyo hata hivyo ilikuwa inapingwa vikali na wazazi wahafidhina ambao walikuwa wanadai kwamba Obama angeitumia nafasi hiyo kupiga propaganda zake za kisoshalisti (tazama hapa). Kwa hali hiyo kuna shule ambazo hazikuruhusu hotuba hiyo kutangazwa, na wazazi wengine waliwachukua watoto wao kutoka shuleni ili wasilishwe mawazo ya kisoshalisti na rais wao. Isikilize hotuba hiyo hapa chini, pamoja na hoja za wahafidhina.






    Friday, September 4, 2009

    UJUMBE WA IJUMAA: HATA KAMA UNA NGUVU NAMNA GANI, LAZIMA KUNA MTU MWENYE NGUVU ZAIDI YAKO

    (1) MIKE TYSON ALIYEKUWA AKIOGOPWA SANA....


    (2) NA GEORGE FOREMAN ALIYEKUWA NA NGUVU ZA SIMBA...

    • Kumbuka, hata wewe, pamoja na nguvu na akili zako zote, lazima kuna mtu anayekuzidi nguvu pamoja NA AKILI. Be humble!!!

    Thursday, September 3, 2009

    ASKOFU KAKOBE "AONYA" KUHUSU UPOLE WA JK NA HATARI ZAKE

    Madhehebu ya dini (mf. Wakatoliki na Waislamu) kuibuka na kutoa "nyaraka/miongozo" ya kisiasa kwa waumini wao ni sawa? Je, hali hii ikiachiwa haiwezi kweli siku moja 'kufufua" hisia za udini miongoni mwa Watanzania na kuweza kuleta shari? Mbona kiongozi wa nchi amekaa kimya kuhusu suala hili muhimu? Askofu Kakobe anasema kwamba JK ni mpole mno na upole wake unaweza kuwa hatari kwa taifa. Sijui kama hii ni kweli. Unaweza pia kutazama hapa na hapa kuhusu masuala yanayohusiana na hili.

    Kakobe: Upole wa JK hatari
    Asema viongozi wa dini ndio chanzo cha ufisadi
    Chanzo: Tanzania Daima, 3/9/2009

    ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, amesema ameshtushwa na ukimya wa Rais Jakaya Kikwete kushindwa kukemea nyaraka zinazotolewa na madhehebu ya dini, hali ambayo inaweza kusababisha machafuko kama haitadhibitiwa.

    Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Askofu Kakobe alisema tamko la Rais Kikwete lina uzito kuliko kiongozi yeyote nchini.

    Alimtaka Rais Kikwete asikae kimya, kwani kufanya hivyo kutaonekana kama ni kutaka kumfurahisha kila mtu.

    Alisema kama hali hiyo ikiendelea, inaweza kuligawa taifa ambalo limekuwa na misingi ya amani, umoja na utulivu tangu wakati wa Mwalimu Nyerere.

    “Rais Kikwete anapaswa kutoa tamko juu ya viongozi wa dini, ambao sasa wanatoa nyaraka mbalimbali… tunaamini kauli yake itakuwa nzito kuliko kiongozi yeyote,” alisema Askofu Kakobe.

    Alisema Rais Kikwete ni mpole, lakini anapaswa kuonyesha ujasiri wake ili taifa lisipoteze amani iliyojengeka muda mrefu isitoweke.

    Akionekana dhahiri kutoridhishwa na nyaraka hizo za kidini, alisema umefika wakati uhuru wa kutoa maoni utumiwe kwa mipaka, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa maoni yanayotolewa hayasababishi kwa namna yoyote ile taifa kugawanyika.

    Alisema moja ya jukumu kubwa la viongozi wa dini, ni kuilinda serikali kwa manufaa ya Watanzania wote na si kwa manufaa ya dini fulani.

    “Mtu kama anataka kutoa maoni yake atoe kama yeye na si kushirikisha dhehebu zima, na aangalie kitu gani anachozungumza si kama walivyofanya Wakatoliki na Waislamu kwa kusema kuwa ‘huu ni waraka wa Wakirsto’ na ‘huu ni muongozo wa Waislamu’,” alisema Askofu Kakobe.

    Sababu kubwa ya viongozi wa madhehebu ya dini kutoa waraka na mwongozo, ni kuwataka wafuasi wa dini hizo na Watanzania kwa ujumla kuchagua viongozi wanaofaa.

    Alisema viongozi wa dini hawatakiwi kutoa waraka unaohusu siasa na kuwahimiza waumini wao kuchagua viongozi wa dini zao kwani katika uchaguzi mkuu wa mwakani watatakiwa kuchagua viongozi wa serikali na wala si wa dini.

    “Kiongozi akienda kuomba kura, haendi kama muumini wa dhehebu fulani, bali anaenda kama mfuasi wa chama fulani. Sijawahi kusikia mbunge wa dini fulani, ila ni mbunge wa Watanzania wote. Kinachotuunganisha ni Utanzania si dini wala ukabila,” alisema Askofu Kakobe.

    Alisema nyaraka zilizotolewa na Wakristu na Waislamu, zimejaa maneno ya kichochezi ambayo yanatumika kama miongozo kwa waumini wa dini hizo na Watanzania kwa ujumla.

    “Waislamu walipozindua waraka wao, walisema; ‘Wakatoliki wamemwaga ugali na sisi tunamwaga mboga. Kama Wakatoliki wangezingatia ushauri huenda tusingefika huku sisi Waislamu’. Kauli hizi ni za hatari, zinaweza kuleta vita,” alisema Kakobe.

    Kuhusu waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki, Askofu Kakobe alisema hali hii inaonyesha mpasuko kwani kila dhehebu linataka mfuasi achague kiongozi kutoka kwenye dini husika.

    Akitoa mfano wa maneno yanayoashiria mpasuko katika waraka wa Kanisa Katoliki, Kakobe alinukuu kifungu kinachosema; “wagombea wanavyotawaliwa na dini yao ni muhimu kuwadhibiti kwa lengo la kuwasaidia kuanzia ngazi za vijiji hadi taifa kwa jumuia za kanisa ili tunu za Kikirsto zionekane katika sera na uongozi.”

    Katika hatua nyingine, Kakobe alikemea kauli iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati wa mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Antony Mayalla, kwamba wanasiasa hawana haki ya kuwafundisha viongozi wa dini kama walivyofanya mara baada ya kanisa hilo kutoa waraka wake.

    Alisema, Pengo alionyesha jeuri na utovu mkubwa wa nidhamu kwa kiongozi wa nchi, kwa kutoa kauli hiyo mbele ya Rais Jakaya Kikwete.

    “Nikemee vikali tamko la kiongozi mmoja wa dini aliyesema ‘wanasiasa wasitufundishe’. Kauli ile aliitoa mbele ya rais, ule ulikuwa ni utovu wa nidhamu. Ilionyesha jinsi alivyo jeuri na asivyotaka kushaurika. Sisi kama viongozi wa dini, tunapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani na utulivu,” alisema Kakobe huku akiepuka kutaja jina la Pengo ingawa baadaye alijisahau na kumtaja.

    Alisema kawaida waraka hutolewa na viongozi wa vyama vya siasa wakati wa kampeni kwa ajili ya kujinadi mbele ya wananchi.

    “Dini inapotoa waraka, inamaanisha inataka kushika madaraka kama vyama vya siasa… wote tunaamini kwamba dini inafanya kazi kama ilivyosajiliwa,” alisema Askofu Kakobe.

    “Unajua kama DECI ilisajiliwa na kufanya shughuli zake, lakini ilivyogundulika kwenda kinyume cha sheria, ilifungiwa na kushuhudia inafikishwa mahakamani. Hivyo dini hizi zinapaswa kufunguliwa mashitaka kwa kwenda kunyume na usajili,” alisema Askofu Kakobe.

    Alisema anawashangaa viongozi wa dini na watu wanaoshabikia waraka huo wa Kanisa Katoliki, kwamba unapinga viongozi mafisadi wasichaguliwe, ilhali chanzo kikuu cha kuwepo kwa mafisadi ni viongozi wa dini kushindwa kuwajibika na kuwaelimisha waumini wao hadi wakajiingiza kwenye ufisadi.

    “Mafisadi wana dini na wamelelewa katika dini hizi hizi, sasa iweje wao wawasemee mafisadi? Ina maana wamekuwa wazembe katika kukemea na kujenga maadili. Kwa hiyo wao ndio wanaotengeneza mafisadi,” alisema Askofu Kakobe.

    Aliwataka wananchi kutoshabikia nyaraka zinazotolewa na viongozi wa dini na waziogope kama ukoma kwani vita ikitokea, hakuna fidia watakayopata wananchi kama walivyopata wahanga wa matukio ya milipuko ya mabomu Mbagala.

    Alishauri viongozi wa madhehebu ya dini, wanasiasa na viongozi wa kiserikali wakutane na kujadili mustakabali wa umoja na amani ya taifa, ikiwa ni pamoja na athari za dini au dhehebu kutoa waraka unaowaandaa wananchi kwa ajili ya chaguzi za kisiasa.

    NI KWELI OBAMA ANAJARIBU KUMFUFUA KARL MARX KULE MAREKANI?











    • Obama anapigwa vita vikali sana na wahafidhina wa chama cha Republican; na mapendekezo yake ya kuubadilisha mfumo wa bima ya afya ili kumwezesha kila Mmarekani kupata tiba anapougua yamewasha moto mkali wa upinzani. Tayari ameshapachikwa jina la mkomunisti.
    • Wakati mabishano haya yakiendelea deni la taifa linazidi kukua, vita kule Afghanistan (ambavyo sasa ameanza kulaumiwa kwa kuviendeleza) haviendi vizuri, majimbo hayana pesa za kutosha, hali ya maisha ya Wamarekani (waliozoea raha ajabu) inazidi kuporomoka...... Hali hii inawafurahisha sana wahafidhina kwani wanafikiri kwamba pengine wataweza kumwangusha katika uchaguzi wa mwaka 2012 na kuwa rais aliyeshindwa. Tangu hapo siasa ni mchezo mbaya ati!


    Wednesday, September 2, 2009

    WASUKUMA HIVI NDIVYO TUNAVYOHESABU - SOLO, BILI, YATU...










    Kikwenu mnahesabuje? Picha imetoka kwa dada Florah Lauwo

    UTAFITI: UNENE FUTUFUTU WA KUPINDUKIA (EXTREME OBESITY) UNAWEZA KUPUNGUZA MIAKA 12 KATIKA MAISHA YAKO

    Wiki mbili zilizopita nilibandika hapa matokeo ya utafiti ulioonyesha kwamba watu weusi ndiyo wanaongoza kwa unene hapa Marekani (tazama hapa). Nilijaribu kuoanisha matokeo ya utafiti huo na ukweli kwamba watu weusi ndiyo wanaongoza kwa kufa mapema pia. Sasa utafiti mpya unaonyesha kwamba unene futufutu wa kupindukia (extreme obesity) kwa wastani unapunguza miaka 12 katika maisha ya mtu. Zaidi ya asilimia 6 ya watu wote hapa Marekani ni wanene futufutu kupindukia. Baadhi ya mambo ya muhimu katika utafiti huu mpya ni:
    • Matatizo yanayosababishwa na unene yamewasababisha Wamarekani kupoteza miaka karibu milioni 95 katika jumla yao ya miaka ya kuishi. Kuhusu gharama, kwa mwaka 2008 walitumia dola bilioni 147 (US $ 147,000,000,000) kutibu magonjwa yanayosababishwa au kuhusiana na unene.
    • Uvutaji wa sigara ni hatari sana. Tineja wa kizungu mwenye miaka 18 asiyevuta sigara anaweza kutegemea kuishi miaka 81. Kama ni mnene futufutu kupindukia na anavuta sigara basi ategemee kuishi miaka 60 tu. Hii ni tofauti ya miaka 21.
    • Wanaume na wazungu ndiyo huathirika zaidi na unene kuliko wanawake na watu weusi hali kadhalika.
    • Unene wa kawaida haupunguzi miaka ya kuishi. Kwa habari zaidi juu ya utafiti huu soma hapa.
    Vipimo hivi vya unene vinapimwa kwa kutegemea Body Mass Index (BMI). Kuwa mnene futufutu kupindukia (extreme obese) ni lazima uwe na BMI ambayo ni 40 au zaidi. Soma hapa na hapa ambapo pia utaweza kukokotoa BMI yako. Tusisahau kwamba tofauti za kitamaduni, mazingira na mfumo wa maisha bila shaka vinaweza kuathiri matokeo ya utafiti kama huu.

    Msikilize Oprah hapa akiongelea suala la unene (futufutu wa kupindukia) na misukosuko yake.

    JIANDIKISHE HAPA

    Enter your email address:

    Delivered by FeedBurner

    BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO