NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, October 31, 2009

MGENI WANGU KARIBU NYUMBANI, LAKINI.....

Eti, utajisikiaje ukitembelea familia yenye mkeka wenye maandishi kama haya mlangoni?

Friday, October 30, 2009

UKIWA ROMA FANYA KAMA........

Ni Madame Secretary Hillary Clinton huyu akiwa Pakistan janaNINA WASIWASI NA SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA

Lengo letu ni zuri sana. Kila kata iwe na shule yake ya sekondari. Lakini tumejiandaaje? Kuna walimu wa kutosha katika shule hizi? Kuna vitabu? Kuna maabara? Mazingira kwa ujumla yakoje? Watoto kweli wanapata elimu kama inavyotakiwa? Picha hii ya mama mpishi wa shule imenitatanisha!

Thursday, October 29, 2009

KICHEKO NI TIBA - KUTOKA WAVUTI.COM

Matani kutoka Kenya kutoka tovuti mpya ya Wavuti.com (zamani nukta77.blogspot.com). Kama unavyoweza kuona kuna Ki-sheng hapa na pale; na sarufi na hasa upatanisho wa kisarufi na ngeli za majina zimeparaganyika (mf. ukikunywa maziwa inafika...). Nawapenda Wakenya kwa sababu wao hawatilii maanani sana mambo kama haya ya usanifu wa lugha kama tunavyofanya sisi Watanzania. Nimeandika makala yenye kurasa 25 inayoitwa "Kiswahili Sanifu au Kiswahili cha Tanzania?: Matatizo ya Usanifishaji katika Kiswahili Sanifu" Ikichapishwa nitawapa "link" hapa kwa wanaopenda haya mambo ya lugha. Watanzania - tunayo haki ya kudai kwamba Kiswahili chetu ndicho sanifu kabisa na kile cha Wakenya na hata kile cha Demokrasia ya Kongo (ambacho wenyewe wanadai kwamba ni sanifu pia) si sanifu?
*************************************************************************

1. Ati wee ni m-black mpaka ukiingia kwa dinga (gari), dirisha zinakuwa tinted!

2. Kwenu kuchafu mpaka mende zinatema mate, ati ‘THU’ hii hao (HOUSE) ni noma.

3. Vile wewe mfupi, ukipigwa picha ya passport inatokea full.

4. Kwenu nyi wakristu hata dogi zenu zikiona mwizi anaiba, zinawaambia “wee iba tu Mungu anakuona.”

5. Ati hao (house) yenu ina gate lakini hakuna fence.

6. We’ ni mshort mpaka ukikalia kwa pavement (sakafuni) miguu ina hang kwa hewa.

7. We mjinga mpaka uli-fail blood test.

8. Wewe ni mblack mpaka mosquito ikitaka kukuuma lazima itumie torch.

9. We ni mrefu mpaka ukikunywa maziwa inafika kwa tumbo ikiwa mala (MGANDO/MTINDI).

10. Wewe ni mweusi ukikanyanga makaa unawacha footprint za black kwa makaa.

11. Nyanyako (bibi yako) mzee mpaka chawa za nywele yake hutembea na bakora.

12. Ati nyinyi ni wengi nyumbani kwenu yaani buda (baba) yenu hajui majina mpaka huwaaddress kama wananchi. (KAMA RAISI ANAPOTOA HOTUBA)

13. TV yenyu ni Ndogo lazima ufunge jicho moja ndio uone picha.

14. Wewe mblack mpaka unasweat soot.

15. Wewe mnono mpaka ukivaa yellow watoto wanafikiria ni schoolbus.

16. Manzii (mpenzi) wako ni m ugly mpaka alikataliwa ku act horror (movie ya kutisha) Hollywood.

17. Nyumba yenyu ni ndogo mpaka lazima utoke nje kuchange mind.

18. Kwenyu nyinyi ni wengi mpaka kwa hao (house) kuna round-about.

19. Kwenyu nyinyi ni wadaft (WAJINGA) mpaka kupata driving license ilibidi mpelekwe boarding school.

20. Nywele za watoto wenyu ni ngumu mpaka mnazitumianga kama steel wool.

21. Mko wengi kwa hao (house) mpaka kuna rush hours na kukinyesha kunakuwa na jam.

22. Wewe ni mshort mpaka ukishuka kutoka kwa zile vitanda double decker lazima utumie parachute.

23. Ati TV yenu ni ndogo hadi wasee wa news huanza kwa kusema ...ati munatuona jamani?

24. Sistaako ni ugly mpaka monkey ikampatia ndizi.

25. We mblack mpaka ukikutana na mzungu afternoon anakushow good evening?

26. Ngombe yenu mzee mpaka inatoanga yogurt.

27. Kwenu kumekauka mpaka ngombe yenu hutoa milk powder.

28. Wee ni mzee mpaka ukiumwa na mosquito zinatema mate

29. Paka yenu noma mpaka iki shika panya inaitisha chumvi, fork na pilipili.

30. Kwenu nyinyi ni wengi mpaka mkipigwa family photo wengine wanatokea kama wame hang (ning’inia) kwa frame.

31. TV yenu ndogo mpaka wasee wa News (watangazaji wa habari) wamepiga magoti.

32. We mrefu mpaka ukianza kuvaa underwear mbichi by the time ifike kwa magoti imekauka.

33. Nyumba yenu ni chafu mpaka cockroach huvaa slippers (malapa).

34. Budako (baba yako) ni fala, alienda ku-buy ngombe akaona ikikojoa akasema, sitaki hiyo, imetoboka

RIPOTI YA USAWA WA KIJINSIA DUNIANI - TANZANIA TUNARUDI NYUMA?

Ripoti mpya inayoonyesha usawa wa kijinsia duniani imetoka na nchi za Skandinavia bado zinaongoza (#1-Iceland, #2-Finland, #3-Norway, #4-Sweden). Kwa Afrika, Afrika Kusini (nafasi ya 6) na Lesotho (nafasi ya 10) ndizo nchi pekee za Kiafrika zilizomo katika kumi bora. Kwa Afrika Mashariki Uganda ndiyo inaongoza (nafasi ya 40), Tanzania imeshika nafasi ya 73 wakati Kenya ni ya 98. Marekani - ambako wanawake bado "wanabaguliwa" hasa katika suala la usawa wa mishahara, ajira, pamoja na mambo mengine - imeshika nafasi ya 31. Nchi ya mwisho ni Yemen (#134) ikifuatiwa na Chad (#133) na Pakistan (#132).

Baadhi ya vigezo muhimu vilivyozingatiwa katika uandaaji wa ripoti hii ni pamoja na usawa katika ushiriki wa shughuli za kiuchumi, usawa katika upatikanaji wa elimu ya viwango vyote, usawa katika upatikanaji wa huduma za afya na usawa katika ushiriki wa masuala ya kisiasa. Unaweza kuisoma ripoti kamili hapa na orodha ya nchi zote inapatikana hapa. Tovuti ya World Economic Forum ambayo huchapisha ripoti hii inapatikana hapa.

Jambo la kushangaza ni kwamba ripoti hii inaonyesha kwamba Tanzania inarudi nyuma katika juhudi zake za kuleta usawa wa kijinsia. Mwaka 2006 ilichukua nafasi ya 24, mwaka 2007 (nafasi ya 34), mwaka 2008 (nafasi ya 38) na mwaka huu (nafasi ya 73). Hii ni kweli?

Hapa chini ni Saadia Zahidi - mmojawapo wa waandaji wa ripoti hii akielezea jinsi walivyoweza kuiandaa.Swali: Nchi za Skandinavia pia ndizo zinaongoza kwa kuwa na talaka nyingi duniani. Je, kuna uhusiano kati ya usawa wa kijinsia na kiwango cha talaka au pengine hii imetokea kibahati tu?

Wednesday, October 28, 2009

ATI, MWAKA 2012 NDIYO UTAKUWA "MWISHO WA DUNIA"?

Kituo cha runinga cha History Channel cha hapa Marekani kimeanzisha kipindi kipya kiitwacho Nostradamus-effect. Nostradamus alikuwa mtabiri maarufu wa Kifaransa ambaye wataalamu wengi wa mambo ya utabiri wanadai kwamba alitabiri kwa usahihi kabisa, mbali na mambo mengine, kuzuka kwa Alexander the Great, Adolf Hitler, mashambulizi ya Septemba 11 na hata urais wa Obama. Kwa habari zaidi kuhusu kipindi hiki tembelea hapa.

Katika kipindi cha Nostradamus-effect cha wiki jana wataalamu mbalimbali wa Anthropolojia, Fizikia, Historia, Haidrofizikia na taaluma mbalimbali walijadili kwa kina utabiri maarufu wa Nostradamus kwamba dunia itagharikishwa kwa maji na moto ifikapo mwaka 2012. Walitaja kwamba pengine hili si jambo la kushangaza sana ukizingatia kuyeyuka kwa kasi kwa barafu kunakotokea sasa katika pembe ya kaskazini ya dunia. Athari za tukio hili hazifahamiki na binadamu anaonekana hajali. Wengine walisema kwamba mabomu machache tu ya Atomiki yakiripuka (ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya) basi dunia nzima inaweza kugharikishwa na mawingu ya miali hatari kabisa ya atomiki.

Jambo la kushangaza ni kwamba hata kalenda ya Wamaya (ambao himaya yao kubwa na yenye nguvu na maendeleo ya juu ya kisayansi na kiteknolojia iliangamia kutokana na sababu ambazo hazijulikani mpaka leo) inatabiri kwamba dunia itafikia mwisho wake mwaka 2012. Inaaminika kwamba Wamaya (Mayans) walikuwa na uwezo mkubwa wa utabiri na kalenda yao imeonyeshwa kwamba iliweza kutabiri kwa usahihi matukio mbalimbali yakiwemo kupatwa kwa jua, miripuko mikubwa ya volkeno, vita n.k. Cha ajabu ni kwamba hawakuweza kutabiri kuangamia kwa dola lao wenyewe.


Sijui kama wasiwasi huu ni wa kweli au ni yale yale ya Y2K (mnakumbuka?). Lakini ukiwasikiliza vizuri wanasayansi hawa, karibu wote wanakubaliana kwamba dunia itakumbwa na misukosuko ya kimazingira ambayo itasababishwa hasa na mabadiliko ya haraka ya hali ya hewa na mambo mengineyo ingawa hawajui misukosuko hii itatokea lini. Kuna haja ya kuwa wasiwasi?

Tuesday, October 27, 2009

RUSHWA WAKATI WA UCHAGUZI: NI KOSA LA WAGOMBEA AU WAPIGA KURA?

Tumefika mahali sasa – pengine kutokana na umasikini uliokithiri na ukosefu wa elimu-elimishi – wapiga kura wengi sasa wanafikiri kwamba rushwa wakati wa uchaguzi ni HAKI YAO. Ni ukweli ulio wazi kwamba bila kutoa rushwa huwezi kuukwaa udiwani na hasa ubunge. Nilikuwa nyumbani wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na kimsingi nilichokiona hakikuwa “demokrasia” bali mashindano ya kutoa rushwa – kuanzia magunia ya chumvi, sukari, mabati, kanga, vitenge, baisikeli na wajanja waliweza kupata mpaka pikipiki, mitaji ya kufanyia biashara na hata kujengewa nyumba kabisa. Mzee wa vijisenti alikujulikana kwa kufanya iliyokuwa inaitwa “kufuru”. Ni kwa sababu hii sikushangaa sana niliposikia kwamba alikuwa akiandamwa na kashfa mbalimbali za ufisadi. Mabilioni ya shilingi aliyokuwa akiyamwaga wakati wa “kufuru” zake inabidi yalipwe kwani hakuna cha bure hapa duniani.


Basi kama hivi ndivyo, tumlaumu nani katika hili sakata la rushwa wakati wa uchaguzi? Tumlaumu mgombea ubunge ambaye anajua kwamba bila rushwa hatachaguliwa hata kama awe na sera nzuri namna gani, au mpiga kura ambaye hatoi kura yake bila kupewa sukari? Nini suluhisho la mduara huu usio na fundo? Hii kweli ni demokrasia?

Saturday, October 24, 2009

NYIMBO ZA KISUKUMA/KINYAMWEZI HIZI HAPAUTAFITI: UBAGUZI (WA RANGI) HUANZIA UTOTONI

  • Watoto wenye umri wa miezi sita tu huanza kubagua.
  • Hata sisi weusi tunawabagua wenye rangi tofauti.
  • Inavyoonekana kila mtu ni mbaguzi.
  • Cha kushangaza ni kwamba, sisi weusi pia tunabaguana sisi kwa sisi.
  • Soma makala hapa.

Friday, October 23, 2009

JK HAPA UMEGONGA POINTI!

Kutoka gazeti la Tazama la Jumanne Oktoba 20, 2009 via Mjengwa.

WANASAIKOLOJIA: MASHOGA NA WASAGAJI HAWAWEZI KUBADILIKA AU KUBADILISHWA

Chama cha Wanasaikolojia wa Wamarakeni kimetoa tamko kikiwaonya wanasaikolojia na wafanyakazi wanaojishughulisha na afya ya akili kuacha mara moja kuwaambia wateja wao mashoga na wasagaji kwamba eti wanaweza kubadilika na kuachana kabisa na tabia hiyo. Wanasaikolojia hao wamepinga kwa kina “reparative therapy” – aina ya tiba ya kisaikolojia inayopendekezwa na kikundi kidogo cha wanasaikolojia (ambao wanaungwa mkono na wahafidhina wa Kikristo) ambao wanaamini kwamba mashoga na wasagaji wanaweza kubadilika/kubadilishwa. Kutokana na utafiti ambao wamefanya, wanasaikolojia hawa wanadai kwamba mashoga na wasagaji wakilazimishwa kubadilika wanaweza kutumbukia katika msongo wa mawazo na hata kuamua kujiua.


Dini imetajwa kuwa ndiyo chanzo kikuu cha mashoga na wasagaji kutaka kuachana na mtindo huo wa maisha ambao unapingwa sana na makanisa mengi ya kikristo. Badala ya kuwalazimisha kuachana kabisa na tabia hiyo wanasaikolojia wanapendekeza kwamba ni bora mashoga na wasagaji washauriwe kuishi maisha ya kutofanya mapenzi kabisa au kuhamia makanisa ambayo hayakatazi tabia hiyo.


Ushauri huu wa wanasaikolojia umepingwa vikali sana na Exodus International - mkusanyiko wa makanisa ya kilokole ambayo yanaamini kwamba nguvu za Yesu zinaweza kuvunja “minyororo” ya ushoga na usagaji. Raisi wa shirika hilo aitwaye Alan Chambers mwenyewe ni shahidi mzuri kwani nguvu za Yesu zilimfanya yeye mwenyewe azishinde tamaa zisizotakiwa za kufanya mapenzi ya jinsia moja alizokuwa nazo.


Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba pamoja na athari za kimazingira, pengine ushoga na usagaji ni tabia ambayo mtu anazaliwa nayo hivyo haiwezi kubadilishwa kirahisi. Wengine wanakwenda mbali hadi kudai kwamba tabia hii itazamwe kama ugonjwa na ianze kutafutiwa tiba kama magonjwa mengine ya kawaida. Watu wa utambuzi mnasemaje kuhusu suala hili na ubadilishaji wa tabia kwa ujumla?


Kwa habari zaidi gonga hapa na unaweza kusoma maoni ya wasomaji. Ted Haggard anayerejerewa mara kwa mara na watoa maoni alikuwa ni mchungaji wa kilokole mashuhuri sana hapa Marekani na ndiye alikuwa kiongozi wa chama chao cha kitaifa kijulikanacho kama "National Association of Evangelicals". Alivuliwa madaraka yote Novemba 2006 baada ya kubainika kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na malaya mmoja wa kiume!

Thursday, October 22, 2009

KUCHEKA NI TIBA

HEBU TUKIRUHUSU KIZAZI KINACHOMALIZA MUDA WAKE KITUFUNDISHE KABLA HAKIJATOWEKA

Niliiona picha hii katika blogu ya Mjengwa na ikanikumbusha mama yangu mzazi. Ingawa yeye ni mzee sana lakini bado analima kishamba chake kidogo, anakwenda kutafuta kuni, kuchota maji kwenye kindoo chake, kuosha vyombo na kufanya kazi zingine kama kawaida. Ukimwambia akae apumzike basi mtagombana vibaya sana. Kipindi fulani nilijaribu kumleta Dar es salaam eti apumzike lakini haikuwezekana. Nilipomuuliza ni kwa nini alikuwa hataki kukaa mjini ambako kuna kitu jibu lake lilinishangaza. “Maisha gani haya ya kukaa tu bila kufanya kazi?

Jibu hili kidogo lilinishangaza kwani huyu ni mwanamke ambaye tangu nipate ufahamu wa kuelewa mambo sijawahi kumwona amepitisha siku bila kufanya kazi isipokuwa pengine akiwa mgonjwa – tena mgonjwa wa kweli kweli. Nilijaribu kutaka anieleze kulikuwa na ubaya gani kupumzika kidogo Dar es salaam baada ya miaka yote ile ya kufanya kazi. Jibu lake kwa swali hili lilinishangaza zaidi. Alidai kwamba akiacha kufanya kazi basi atakufa na sikujua kama alikuwa anatania ama la!

Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara pengine ndiyo jambo la muhimu kuliko yote katika kulinda afya zetu pamoja na kuishi maisha marefu. Magonjwa mengi ya hatari kama vile magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu, aina fulani za saratani na mengineyo yanachangiwa sana na maisha ya deko ambayo hatimaye huishia katika unene usiotakiwa. Nilishangaa kugundua kwamba mwanamke huyu mzee ambaye hakupata “bahati” ya kuingia katika darasa la kizungu na kusoma vitabu alikuwa analifahamu jambo hili vyema. Tulikubaliana na ilibidi “raha za mjini” nilizokuwa najaribu kumpa pale Dar es salaam nimpelekee kule kule kijijini kwake.

Mwaka 2001 alikuja huku Marekani kutembea na nilimpeleka kwa daktari kufanyiwa uchunguzi. Nilishangaa daktari alipowaita wenzake kuja kuona matokeo ya baadhi ya vipimo. Alituambia kwamba alikuwa hajawahi kuona mtu mzee namna ile ambaye alikuwa salama vile. Walipomuuliza alikuwa anakula chakula gani aliwajibu bila kusita “bugali”. Niliwafafanulia ugali ni nini na walishangaa kugundua kwamba ni wanga “carbohydrates” ambazo hapa Marekani kila mtaalamu wa lishe atakwambia usile. Ambacho hawakujua hawa madaktari ni kwamba huyu mwanamke mzee alikuwa anafanya kazi zaidi ya masaa matano kila siku tangu akiwa mtoto mdogo mpaka sasa. Tena chakula anachokula ni cha asili kabisa na hakina aina yo yote ya kemikali! Na kijijini kwetu kuna ajuza wengi ambao ni wazee zaidi kuliko mama na wako salama – hakuna dementia, hakuna Azheimer, hakuna saratani, hakuna kuvunjika mifupa hovyo hovyo, hakuna……

Je, kizazi cha sasa kinachoshinda kikitazama televisheni kitaweza kweli kuishi miaka mingi (bila magonjwa) kama kizazi hiki kinachomaliza muda wake? Kizazi cha sasa kinachokula vyakula vilivyobadilishwa na kujazwa kemikali na homoni za kila aina kitaweza kusafiri safari ndefu ya maisha kama hiki kinachomaliza muda wake? Hebu kizazi kipya na kijifunze yaliyo mema kutoka kizazi hiki kinachoaga kungaliko na muda bado.

Tuesday, October 20, 2009

MWALIMU NYERERE NA JANGWA LAKE LA KIITIKADI

Makala haya yametoka katika gazeti la Kwanza Jamii la leo - 20/10/2009

Mwalimu Nyerere na Jangwa Lake la Kiitikadi


(Ati, ni Nani Hasa Alikuwa Mfuasi wa Itikadi ya Mwalimu?)


Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima


Katika diwani ya Karibu Ndani (Euphrase Kezilahabi, DUP, 1988:27) kuna shairi liitwalo “Azimio”. Beti chache za shairi hilo zinasema hivi:


Azimio sasa ni

Mabaki ya chakula

Kwenye sharubu za bepari

Kalamu inayovuja

Katika mfuko wa mwanafunzi

Vumbi zito

Baada ya ng’ombe kupita

Kilichosalia sasa

Ni punje za ulezi

Zilizosambazwa jangwani

Na mpandaji kipofu


Hivi ndivyo Kezilahabi – ajulikanaye pia kama Shaaban Robert wa Pili – alivyoliona Azimio la Arusha mwaka 1988. Nimelikumbuka shairi hili wakati nikitafakari Historia ya nchi yangu Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo nchi hii nzuri inaadhimisha miaka 10 tangu muasisi wake atoweke hapa duniani. Ni kweli Mwalimu alisambaza ulezi wake wa Ujamaa na Kujitegemea jangwani? Kama ni kweli, ina maana Mwalimu hakuwa na mfuasi wa kweli hata mmoja katika genge lake la Makomredi waliokuwa wakiimba ahadi za usawa wa binadamu? Ni nani hasa alikuwa mfuasi wa kweli wa itikadi kombozi za Mwalimu Nyerere? Ni Komredi Kingunge Ngombare Mwiru? Ni Edward Moringe Sokoinne? Ni Dr. Salim Ahmed Salim? Ni Rais Benjamin William Mkapa? Ni Mfaume Rashid Kawawa (Simba wa Vita)? Ni Rais Ali Hassan Mwinyi? Ni Jaji Sinde Warioba? Ni Oscar Kambona? Ni John Samwel Malechela? Ni Bibi Titi Mohamed? Ni Edward Lowasa? Ni Nani?


Msukumo hasa wa kuandika makala hii fupi niliupata kutokana na visa vifananavyo vilivyotokea kwangu mwenyewe na dada Subi Sabato wa nukta77.blogspot.com. Katika kuadhimisha miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Nyerere niliweka mkusanyiko wa video 17 za Mwalimu Nyerere katika blogu yangu (matondo.blogspot.com). Subi Sabato pia alifanya hivyo hivyo katika blogu yake. Haukupita muda mrefu nilipata barua kutoka kwa watu waliokuwa wakijiita watumishi wa serikali wakinitaka niziondoe video za Mwalimu Nyerere katika blogu yangu mara moja kwani eti sikuwa na hati miliki na kwa hivyo nilikuwa navunja sheria. Waliendelea kunitisha kwamba nisipofanya hivyo basi sheria kali zingechukuliwa dhidi yangu. Subi Sabato naye alipata vitisho kama hivyo. Jambo hili lilinishangaza sana na nilijiuliza maswali mengi ambayo mpaka leo sijapata majibu na ndiyo maana naandika makala hii. Ina maana kuna mtu anamiliki hotuba za Mwalimu Nyerere? Niliwauliza watishaji wangu wanieleze aliko mmiliki wa hati miliki wa hotuba hizi ili niweze kuwasiliana naye lakini mpaka leo sijapata jibu. Mimi nilikuwa ninadhani kwamba hotuba za Mwalimu ni hazina ya taifa na Watanzania wote tuna haki ya kuzisikiliza bila kutishwa na mtu. Nilichukulia mfano wa hapa Marekani ambapo sheria za hati miliki ni kali sana lakini hotuba nyingi za marais wao ziko mtandaoni na ukienda katika maktaba za maraisi hao utaweza kuzisikiliza bure. Ni hazina ya taifa lao. Ni mali ya wote. Ni kumbukumbu ya historia ya nchi yao. Hotuba hizi hazimilikiwi na mtu! Hata hotuba nyingi za Rais Obama tayari zipo mtandaoni! Kuna tovuti nyingi zenye hotuba hizi na mojawapo nzuri ni hii hapa.


Mpaka nitakapopata ufafanuzi wa kina kuhusu ni nani hasa mmiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere, ninashawishika kuamini kwamba kuna kundi la watu ambao wanakerwa, kutishwa na kukoseshwa amani na hotuba za Mwalimu kwani wamegeuka kuwa wasaliti. Hawa inawezekana walikuwa ni watu wa karibu sana kwa Mwalimu na walijifanya kuwa “ardhi yenye rutuba” kwa mawazo na itikadi zake kumbe kwa ndani walikuwa ni “majangwa” tu yasiyootesha wala kustawisha cho chote. Ni mbwa mwitu waliokuwa wamevaa mavazi bandia ya “ukomredi” huku wakiimba na kudumisha “fikra sahihi za Mwalimu” kikasuku tu huku kimatendo wakiwa wamekakawana jangwani. Na baada ya Mwalimu kuondoka sasa wanajaribu kila wawezalo kufanya mawazo yake kombozi yasiwafikie Watanzania huku wakitumaini kwamba kwa njia hii hatimaye pengine Mwalimu ataweza kusahaulika.


Katika hotuba zake nyingi unaweza kumsikia Mwalimu akikemea rushwa na ufisadi; na utulivu wake wa akili, falsafa komavu na uwezo wa kuona mbali, kuonya na kutabiri mambo unaonekana waziwazi. Anasema waziwazi kabisa kwamba rushwa ikiachwa iendelee itaweza siku moja kuutikisa “msingi” wa nyumba (Tanzania). Mwalimu, pamoja na mapungufu yake yote, alitambua kwamba rushwa na utajiri wa kupindukia wa watu wachache kwa upande mmoja, na umasikini na uhohehahe wa asilimia 100 kwa walio wengi kwa upande mwingine siku moja utaitikisa Tanzania kwani ipo siku hawa wasio na kitu watachoka na kusema “liwalo na liwe”. Na hili likitokea hakuna jeshi litakaloweza kurekebisha mambo. Watu wakiamua wameamua na Historia imejaa mifano tele inayoonyesha kwamba nguvu za umma ni kama sunami. Badala ya kujaribu kurekebisha mambo na kuchukua ushauri wa Mwalimu kama vile mbuni asiye na upeo, kundi hili la “wanajangwa” inaonekana limeamua kuficha kichwa mchangani likiamini kwamba kutokomeza mawazo ya Mwalimu pengine ndiyo njia ya mkato ya kuendeleza “jangwa” lao wanalojaribu sana kuhakikisha kwamba linabakia kuwa jangwa. Kundi hili kwa hakika linajidanganya!


Hali hii inaibua hoja nyingine. Kutokana na “ujangwa” huu ambao sasa unaonekana waziwazi, haishangazi kuona kwamba sera nyingi za Mwalimu zilishindwa na kusema kweli inashangaza kidogo kuona kwamba baadhi ya sera zake zilifanikiwa mf. Elimu.


Historia inatuambia kwamba viongozi wengi waliofanikiwa ni wale ambao walikuwa na wafuasi wa kweli, wafuasi ambao walikuwa tayari hata kupoteza maisha yao ili kulinda na kutetea itikadi na harakati zilizoanzishwa na viongozi wao. Na hapa sizungumzii madikteta waliolazimisha itikadi zao kwa wafuasi wao kwa mkono wa chuma na kumwaga damu. Mara nyingi Historia huwa haina huruma na watu wa aina hii bali kuwatupa katika shimo lake la takataka. Huko ndiko waliko akina Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga, Jenerali Bokasa, Jenerali Field Marshal Idd Amin Dada na wengineo wa aina hiyo.


Viongozi ambao hawakupanda mbegu zao katika “jangwa” mara nyingi hawakuwa hata na haja ya kuandika mawazo yao. Wafuasi wao wa kweli walifanya hivyo. Yesu Kristo hakuandika kitabu cho chote lakini wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Buddha pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Lao-Tzu (mwanzilishi wa Taoism) pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Ferdinand de Saussure – mwanaisimu wa Uswisi ambaye anatambuliwa kama baba wa Isimu ya kisasa hakuandika kitabu cho chote pia wakati wa uhai wake. Wanafunzi wake walikusanya “notisi” na mihadhara yake aliyokuwa akiitoa wakati wa uhai wake na kuandika kitabu ambacho kilibadilisha kabisa mkondo mzima wa taaluma ya Isimu. Historia ina mifano mingi ya watu wa aina hii. Ni vigumu mno kwa kiongozi kufanikiwa kama amezungukwa na “jangwa” kama inavyobainika sasa kwa Mwalimu Nyerere.


Mwalimu Nyerere ataendelea kuenziwa na Watanzania, Waafrika na wapenda amani kokote duniani na juhudi za kundi hili linalojaribu kuzima mawazo yake linapoteza muda wake bure. Pamoja na makosa yake yote na kushindwa kwa sera yake ya msingi ya Ujamaa na Kujitegemea Watanzania wanaendelea kumuenzi na kumheshimu kiongozi huyu kwa msimamo wake na kutotetereka katika kutekeleza kile alichokiamini kwamba kilikuwa na maslahi kwa watu wake. Mwalimu Nyerere alihubiri na kutenda alichokihubiri na karibu kila kitu alichokitenda kilikuwa ni kitu ambacho aliamini kabisa kwamba kilikuwa ni kwa maslahi ya taifa lake changa. Jambo hili linawavutia sana Watanzania hasa wakiangalia maisha yake ya uadilifu aliyoishi – yeye pamoja na familia yake. Ni kwa sababu hii mimi naamini kwamba Nyerere na itikadi yake vitadumu!


Pamoja na “ujangwa” uliopo, wakati sasa umefika wa kumaliza ukiritimba katika hotuba (na vitu vingine ambavyo ni hadhina ya taifa letu). Hotuba za Mwalimu Nyerere siyo mali ya Redio Tanzania, mtu wala shirika au kikundi cha watu bali ni mali yetu sote. Ni wakati sasa wa kuziweka hotuba hizi katika mtandao. Hebu tuwe na tovuti maalumu yenye hotuba zote za viongozi wetu wote kuanzia Mwalimu Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa na rais wetu wa sasa Rais Kikwete. Tovuti hiyo itangazwe na itunzwe vizuri kwani itakuwa mojawapo ya hazina muhimu sana kwetu kama Taifa kwa wakati huu na vizazi vijavyo. Wiki ijayo nitazungumzia kosa kubwa kuliko yote la Mwalimu Nyerere!


Niandikie: profesamatondo@gmail.com

Nisome: matondo.blogspot.com

Monday, October 19, 2009

TOTALLY USELESS FACTS.....

....You spend seven years of your life in the bathroom...

MAWAZIRI NA WABUNGE WENYE VYETI VYA KUGHUSHI

Wakati wengine wanasota miaka 6-10 (kwa hapa Marekani) kupata shahada za uzamivu (PhDs) inasemekana waheshimiwa hawa wao waliamua kupita njia za mkato, wakaudanganya umma na kujipatia madaraka tena makubwa sana (na nyeti). Watachukuliwa hatua yo yote au ni "siasa" tu mtindo mmoja?

MAWAZIRI

(1) Dk. Mary Nagu (Viwanda, Biashara na Masoko)

(2) Dk. Diodurus Kamala (Ushirikiano wa Afrika Mashariki)

(3) Dk. Makongoro Mahanga (Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana)

(4) Dk. David Mathayo David (Kilimo, Chakula na Ushirika)

(5) Dk. Emmanuel Nchimbi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT)


WABUNGE

(1) William Lukuvi (Ismani-CCM)

(2) Victor Mwambalaswa (Lupa-CCM)


(3) Dk. Raphael Chegeni (Busega-CCM)

Kwa habari kamili soma hapa

Halafu mwangalie huyu mwenzao hapa uone tofauti!

Sunday, October 18, 2009

UKAHABA AFRIKA KUSINI NA KOMBE LA DUNIA MWAKA KESHO (VIDEO)

Nimeiona hii video katika CNN. Eti kuna wasiwasi kwamba kombe la dunia mwaka kesho litaifanya biashara ya ukahaba kushamiri zaidi Afrika Kusini. Hii ni haki kweli au ni kwa sababu kombe hili linafanyika barani Afrika kwa hivyo ni lazima hawa jamaa wachonge? Kwa kuwa ukahaba ni tatizo la dunia nzima, je, ulikuwa tatizo pia hata katika nchi zingine ambako kombe hili limeshawahi kushindaniwa? Au pengine hali ya ukahaba Afrika Kusini ni mbaya zaidi kuliko sehemu zingine duniani? Nimetatanishwa!

Friday, October 16, 2009

KAMWE USINYWE POMBE NA KWENDA KUIBA

Mtu na babake wametoa kali ya mwaka kule Alabama. Baba ana miaka 37, mtoto wake wa kiume ana miaka 19. Kwanza walianza wakazitwika bia mpaka wakawa njwii halafu wakaamua kwenda kuvunja nyumba ili kuiba usiku wa manane. Kweli wakafanikiwa na wakaiba funguo za gari, dola karibia 200 na vito vyenye thamani inayokaribia dola 100 wakati wenye nyumba wakiwa wamelala.

Wakati wanajaribu kuondoka soo likabumburuka. Wenye nyumba wakaamka. Kwa akili za haraka haraka jamaa wakajibanza sehemu na hatimaye wakajificha chini ya kitanda katika chumba cha kulala. Soo likapoa. Baadaye baba akafanikiwa kuchepuka na kumuacha mtoto mvunguni mwa kitanda. Kumbe mtoto akawa amezimika mle mvunguni kutokana na kilevi.

Basi wenyeji wakalala kama kawaida mpaka asubuhi. Ndipo mama mwenye nyumba akashtukia ishu. Kuchungulia mvunguni mwa kitanda akamkuta mtoto mwizi akiwa ameutandika usingizi bila wasiwasi. Akakimbia kwenda kumwita jirani. Jirani alipokuwa basi mambo yakachangamka zaidi kwani yule kijana mwizi aliyekuwa amezimika mvunguni ni mjukuu wake. Polisi wakaitwa. Mwizi kuamshwa akawa anamuulizia baba yake. Polisi wakaondoka naye kwenda kumchukua baba yake na wote haooo korokoroni. Tangu hapo pombe siyo supu ati!

Itazame hii ishu hapa.

KWA MLIOKUWEKO: MNAZIKUMBUKA IMANI NA AHADI ZA MWANATANU?


Kumbe bado hazijabadilika na bado nazikumbuka karibu zote kwa kichwa. Duh!


IMANI YA CCM


  • Binadamu wote ni Sawa
  • Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake
  • Ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru


AHADI ZA WANACHAMA WA CHAMA CHA MAPINDUZI


(1) Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja

(2) Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote

(3) Nitajitolera nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.

(4) Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.

(5) Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

(6) Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.

(7) Nitashjirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.

(8) Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

(9) Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.

Thursday, October 15, 2009

HUYU RUBANI VIPI?

Mimi huwa sipendi kusafiri wa ndege na huwa napanda ndege tu kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kusafiri kwa haraka zaidi. Mwaka 2006 kindege cha Precision Air kilihangaika kweli kutua pale Ibadakuli Shinyanga na ingawa nilikuwa naendelea mpaka Mwanza niliomba nishukie hapo hapo kwani sikutaka tena kwenda kupata mateso katika kutua kule Mwanza. Jamaa walinikubalia kushuka kwa shingo upande. Ningekuwa kwenye ndege kama hii sijui ingekuwaje. Kuna mwingine anayeogopa kusafiri kwa ndege au niko peke yangu? Watu wa utambuzi mna suluhisho kuhusu tatizo hili?Tuesday, October 13, 2009

VIDEO MBALIMBALI ZA MWALIMU NYERERE HIZI HAPA

Katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 tangu Muasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atutoke, hizi hapa video zake mbalimbali. Japo zina urefu tofauti tofauti na zingine hazizidi hata dakika moja, kwa pamoja zinaonyesha falsafa yake tetezi na misimamo isiyolegalega ya Mwalimu. Natoa shukrani kwa wadau mliojitolea kuzitundika video hizi katika Youtube na Google Video. Kwa hotuba zaidi za Mwalimu Nyerere tembelea http://nukta77.blogspot.com. Mungu ibariki TANZANIA!

ANAKIRI SERIKALI YAKE ILIFANYA MAKOSA


CHIMWAGA 1995 (Nukta 77)


MUUNGANO
RUSHWA


UBAGUZI WA RANGI


MAZINGIRA


WALIMU
KODI


LINALOWEZEKANA LEO LISINGOJE KESHO


MIKOPO NA MADENI


NCHI YETU HAINA DINI (UNAWEZA KUISHIA 1:25)


HOTUBA KATIKA KIINGEREZA


KAMA SIKU ZAKO HAZIJAFIKA .....

Tarehe 15 Septemba, 2009 wanyongaji katika jimbo la Ohio kule Marekani walihangaika kwa zaidi ya masaa mawili wakijaribu kumnyonga muuaji, mbakaji na mteka nyara aitwaye Romell Broom (pichani) aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa mpaka kufa kwa njia ya sindano ya sumu. Kutokana na matumizi yake ya madawa ya kulevya kwa muda mrefu, wanyongaji walishindwa kupata mshipa wa damu katika mikono yake ili kupitisha sumu ambayo hudhoofisha kwanza mwili na baadaye mapafu na moyo na hatimaye kusababisha kifo. Pamoja na mnyongwaji kujaribu kuwasaidia wanyongaji wake kwa kulala ubavu ubavu katika meza ya kunyongea na kujaribu kukunja ngumi ili kutunisha mishipa ya damu, wanyongaji hao hawakufanikiwa na baada ya masaa mawili Gavana wa jimbo la Ohio Ted Strickland aliamru unyongaji huo usimamishwe.

Walitaka kumnyonga tena baada ya wiki moja lakini wanasheria wake wakawa tayari wameshakata rufaa na kesi hiyo bado inaunguruma mahakamani. Na Romell Broom bado yupo tu anadunda. Kweli kama siku zako hazijafika hapa duniani binadamu hata wafanyeje ni bure! Kwa habari zaidi soma hapa. Mwenyewe anaeleza hapa yaliyomsibu siku ya Septemba 15, 2009 alipokutana na kifo uso kwa uso.

Monday, October 12, 2009

OBAMA KAZI ANAYO - JAMAA WANAFURAHIA ANAPOSHINDWA NA KUKASIRIKA ANAPOSHINDA

KWA NINI WAAFRIKA "TUNAKATAZWA" KUABUDU MABABU ZETU WALIOTUTANGULIA?

Jana asubuhi katika viwanja vya St. Peter Square kule Vatican Papa Benedict XVI alimtangaza "Baba" Damien De Veuster (January 3, 1840–April 15, 1889) kuwa Mtakatifu. "Baba" Damien De Veuster anakuwa Mtakatifu wa kwanza kutoka jimbo la Hawaii. Nilitembelea Hawaii mwaka wa 2005 kwa wiki mbili na Molokai -mahali alipoishi kwa miaka mingi akiwahudumia wagonjwa wa ukoma mpaka alipofariki (kwa ukoma pia) - ni mojawapo ya vivutio vya utalii.

Kama tunavyojua, "watakatifu" hawa (ambao ni lazima wawe wameshakufa) katika kanisa la kikatoliki huombwa na kuabudiwa; na inasemekana wana uwezo wa kutenda miujiza. Ili kutangazwa mtakatifu inabidi angalau miujiza miwili ya kiuponyaji itokee na iambatishwe moja kwa moja na anayetaka kutakatifishwa. Huu ndiyo utaratibu ambao Mwalimu Nyerere itabidi afuate kama kweli kanisa la kikatoliki linataka kumfanya kuwa Mtakatifu.

Swali langu ni hili: Mbona Waafrika wakisali na kuomba kwa mababu zao waliowatangulia wanaambiwa kwamba wanaabudu mizimu na wakiwaabudu hawa watu "waliotakatifishwa" na kanisa ni sawa?

NAKUMBUKA SIKU NILIYOTUNUKIWA ZAWADI KWA KUWA MWALIMU BORA WA MWAKA!

Katika vyuo vikuu vingi (na hata shule za msingi, sekondari na vyuo vinginevyo) hapa Marekani kuna tuzo linaloitwa "Teacher of the Year Award" Tuzo hili nadra hutolewa kwa mwalimu ambaye ameonyesha uwezo, ubunifu, mafanikio na njia za kipekee katika kufundisha. Mimi nami nililipata tuzo hili hapa Chuo Kikuu cha Florida mwaka wa masomo wa 2004-2005.

Ili kulipata tuzo hili ni utaratibu mrefu na uchaguzi wake hufanywa kwa uangalifu sana. Mbali na kupendekezwa, inabidi wanafunzi wako waandike barua wakieleza kwa kina jinsi ufundishaji wako ulivyowabadilisha na ni kwa nini wanafikiri kwamba unastahili kupata zawadi. Inabidi waseme ni kwa jinsi gani ufundishaji wako uko tofauti (na bora zaidi) na wa walimu wengine ambao wameshawahi kuwafundisha. Pia msimamizi wako (mkuu wa idara/kitengo) pamoja na walimu wenzako ni lazima waandike barua kukuunga mkono (watatembelea madarasa yako ili kujionea wenyewe jinsi unavyofundisha kabla hawajaandika barua zao). Halafu mwenyewe inakulazimu uandike insha ndefu kujieleza jinsi ufundishaji wako ulivyo tofauti na walimu wengine, falsafa inayokuongoza darasani na mtazamo wako mzima kuhusu nafasi ya mwalimu darasani na katika jamii kwa ujumla. Ni lazima pia uambatishe silabasi zote za masomo uliyowahi kufundisha, mifano ya mazoezi na mitihani ya mihula, "handouts" na vikorokocho vingine vingi. Halafu kamati maalumu iliyo chini ya "Dean" inakaa kupitia walimu wote waliopendekezwa na kufanya uteuzi wa mwisho.

Kwa upande wangu wanafunzi wenyewe walijikusanya wakashauriana wakaandika barua, wakawatafuta na wanafunzi wangu wa zamani nao wakaleta barua zao na kisha wakapeleka pendekezo lao katika kamati teuzi. Nilipata bahati ya kusoma baadhi ya barua zao na nilishangazwa na mambo ambayo waliyaeleza. Nilivutiwa na kuguswa mno!

Mbali na kupata bango la kumbukumbu (plaque), mshindi pia unapata cheki ya dola 5,000, unahongereshwa rasmi siku ya mahafali ya wanafunzi (na ukitaka unaweza kutoa hotuba) na unakaribishwa katika dhifa maalumu pamoja na rais wa chuo pamoja na viongozi wengine. Kwa ujumla hii ni siku nzuri ambayo mwalimu unaona kwamba juhudi zako pamoja na kipaji chako cha uelimishaji kweli kinaheshimiwa na kuthaminiwa. Inafurahisha na kutia moyo sana!

Mimi naamini kwamba huu ni utaratibu mzuri sana katika kuwaonyesha walimu wetu kwamba tunawajali na kuuthamini mchango wao na sioni ubaya wo wote kama nasi tukianzisha utaratibu kama huu (tena bila upendeleo wo wote) kwa walimu wetu katika ngazi mbalimbali.

Mwalimu wa binti yangu aliyeko darasa la pili alituambia hivi wazazi tuliokuwa tumekusanyika kumhongeresha (pamoja na kumpelekea zawadi) baada ya kushinda tuzo hili mwaka jana katika shule yake ".....Nitajibidisha zaidi mwaka ujao na wanafunzi wangu wataona mambo mapya na kujifunza kwa urahisi zaidi" Hili ndilo lengo hasa la tuzo hili - kuwapa motisha walimu kwa kuwaonyesha kwamba tunathamini na kuheshimu mchango wao - hasa wale wenye vipaji vya pekee na wanaojitolea sana katika kuelimisha watoto wetu!

Na siku moja natamani kurudi nyumbani na kutumia kipaji changu na mambo ambayo nimejifunza huku katika kuelimisha taifa langu!

ATI, MAFISADI NAO NI BINADAMU?

Niliulizwa swali hili na mwanafunzi anayesomea shahada ya uzamifu (Ph.D) katika Anthropolojia. Mwanafunzi huyu anafanya utafiti wake katika Jamhuru ya Kidemokrasia ya Kongo na alipokuwa huko wakati wa kiangazi mwaka jana alipata bahati ya kutembelea Gbadolite Рyaliyokuwa makao makuu na makazi ya aliyekuwa raisi wa Zaire marehemu Mobutu S̩s̩ Seko Nkuku Ngbendu wa Za Banga (Tafsiri - The all-powerful warrior who, because of his endurance and inflexible will to win, will go from conquest to conquest, leaving fire in his wake).

Mwanafunzi huyu hakuelewa inawezekanaje mtu anatumia mamilioni ya dola za umma kujijengea makao makuu ya kifahari kama yale wakati watu wengi katika nchi yake hawana huduma za msingi kabisa kama chakula, maji, matibabu, elimu na usafiri? Aliendelea kudai kwamba watu kama Mobutu kimsingi siyo binadamu kwani, kwa maoni yake, hakuna binadamu ambaye anaweza kufanya yale aliyoyaona kule Kongo na akabakia kuitwa binadamu.

Alipoondoka nilibaki nikifiriki hasa sisi binadamu ni nani na nini hasa kinachotufanya tuitwe binadamu. Ati, wana hisia na utu gani akina “Mobutu” wetu (ambao ni wengi sana barani Afrika) ambao hawana ubinadamu na wanachojali ni kunenepesha matumbo yao – wakiwaibia watu masikini na kuwasikinisha kabisa bila kujali cho chote? Ni kweli watu hawa wana furaha, hisia za ridhiko, mafanikio na utu? Huwa wanafikiri nini wakiona watoto wanasomea chini tena katika majengo mabovu wakati pesa za kununulia madawati na kujengea majengo ya shule wamezificha katika akaunti zao za siri? Huwa wanajisikiaje watoto mamilioni wanapokufa na malaria wakati pesa za kununulia vyandarua na dawa za malaria wamezitumia kujengea majumba ya kifahari? Huwa wanajisikiaje wakiwaona akina mama wakitembea maili sita kwenda kutafuta maji wakati pesa zilizotengwa kwa shughuli hiyo wamezitumia kujinunulia maghari ya gharama kubwa na kupeleka watoto wao nje kusoma? Wanajisikiaje? Mafisadi wana ubinadamu wowote? Ati, mafisadi ni binadamu?

Kwa habari kuhusu Gbadolite soma hapa. Hata Mtume Onesmo N. Ndegi wa Living Water Center Makuti Kawe Dar es salaam haelewi kabisa!

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU