Mbona Waafrika/Watanzania tunawapapatikia sana wazungu kiasi cha kufikia kubaguana sisi kwa sisi? Ni kwa sababu ya makovu ya utwana wa kisaikolojia ambayo tuliachiwa na wazungu wakati wa biashara ya utumwa, ukoloni, ukoloni mamboleo na sasa utandawazi?
Ukienda katika mahoteli makubwa yanayoitwa ya "kitalii" huduma utakazopata utajua tu kwamba mtu mweusi hutakiwi kuwa pale. Watumishi wote watakuwa wanakimbilia wazungu. Na wakati mwingine mtu mweusi - hata kama nawe una dola zako kama hao wazungu - utanyimwa huduma kabisa, na au kubezwa. Tazama hapa.
Sasa hata kwenye ndege ni mzungu kwanza! Isome habari hii kutoka gazeti la Tanzania Daima hapa ambapo Watanzania walishushwa katika ndege ya Precision Air iliyokuwa inatoka Arusha kwenda Dar es salaam na kupakia wazungu badala yake - pamoja na kwamba Watanzania hao walikuwa na "booking" ya muda mrefu! Inafurahisha kusikia kwamba abiria hawa Watanzania waligoma kushuka katika ndege hiyo. Inabidi tusimame kidete matukio kama haya ya kubaguliwa yanapotokea ingawa kusema kweli unahitajiwa mkakati wa kijamii kuweza kurekebisha hali hii - kama inarekebishika kwani utandawazi unazidi kuchochea moto huu wa Mwafrika kujidogosha yeye pamoja na utamaduni wake.
Huku katika nchi za wazungu watu weusi tunabaguliwa, na nyumbani nako tunabaguliwa? Tukimbilie wapi?
Mh. John Pombe Magufuli akitunukiwa shahada ya uzamifu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Balozi Fulgence M. Kazaura.
Mama yake alikuweko kumshangilia mwana aliyefanikiwa kukifikia kilele.
John Pombe Magufuli (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), ni mmojawapo kati ya mawaziri vijana, makini na wachapakazi sana katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Jana alitunukiwa shahada ya uzamifu (PhD) ya Kemia katika mahafali ya 39 ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Mh. Magufuli alitunukiwa shahada hiyo baada ya kufanya utafiti, kuandika na kuitetea tasnifu yake juu ya matumizi ya maganda ya korosho katika kuzuia kutu.
Sote tunajua jinsi shahada za uzamifu zilivyo ngumu na zinavyochukua muda mrefu. Pamoja na majukumu yake mengi ya kuongoza wizara muhimu ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, bado alipata muda wa kufanya utafiti, kuandika tasnifu yake na hatimaye kuitetea kwa mafanikio.
Kwa kutambua umuhimu wa elimu ya juu, na bila kuamua kupita njia za mkato kama wenzake hawa, tunapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Tunategemea kwamba Ph.D hii imemwongezea maarifa mapya na kwamba ataendelea kufanya kazi yake kwa ufanisi na umakinifu zaidi. Hongera Mh. Dkt. John Pombe Magufuli!
Picha hii kutoka kwa Mjengwa imenikumbusha sato wa Mwanza. Hapo unanunua wawili, kitunguu kimoja na nyanya nne tano hivi, unakipanda kilima cha Bugando kupitia pale shule ya Sekondari ya Mwanza halafu unajitengenezea kachumbari yako safi. Ukiongezea chumvi na pilipili kidogo pembeni basi mlima wa ugali unateketea bila wasiwasi. Safi sana!
Kilichonivutia katika tangazo hili, ambalo sikumbuki nililiona kwenye blogu ya nani (pengine Othman Michuzi), ni lugha iliyotumiwa. Vipi kama mjasiriamali huyu angeandika tangazo hili kwa Kiswahili. Kulikuwa kweli na ulazima wa kutumia Kiingereza? Au pengine tangazo limelengwa kwa wateja wanaojua Kiingereza mf. watalii. Hongera mjasiriamali Hassan lakini "please don't kill me with food!"
Hii ndiyo ilikuwa timu ya kwanza ya gazeti ya Kwanza Jamii - Muuguzi na Mchambuzi wa masuala ya kiafya dada Subi Sabato, Profesa Joseph Mbele, Profesa Charles Bwenge, Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima, Mchambuzi wa masuala ya kisheria Eliamini Laltaika, Padri Privatus Karugendo, Mwanamuziki, Mtunzi na Mchambuzi Freddy Macha na Mhakiki na Mchambuzi Born Again Pagan.
Makala hizi hata hivyo zimesomwa na watu wachache sana na hakuna aliyejaribu kutoa maoni. Katikati ya hizo kulikuwa na moja yenye kichwa cha habari kisemacho "Ulimwengu Wa Mahaba (Mada endelevu): Hiki Ndicho Kinachomsisimua Mwanamke". Makala hii ilikuwa imesomwa mara 352 ukilinganisha na mara 40 kwa makala ya Profesa Mbele, mara 23 kwa makala ya Profesa Bwenge na mara 29 kwa makala ya Joseph Mihangwa.
Nilipoangalia upande wa maoni mapya, maoni yote yalikuwa ni juu ya makala yenye kichwa kisemacho "Wanaume wana haraka ya kufanya sex". Hivi ni kwa nini hasa watu hawapendi kusoma makala muhimu zinazochambua na kuhoji mambo ya msingi katika jamii?
Gazeti la Kwanza Jamii limejibidisha sana kuandika makala za wachambuzi makini mbalimbali (akiwemo Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa) lakini taarifa nilizokuwa nazo miezi michache tu iliyopita ni kwamba gazeti hilo lilikuwa halifanyi vizuri sana kutokana na ukweli kwamba watu hawapendi kusoma makala ndefu za kichambuzi. Watu wanapenda kusoma makala fupi fupi zenye vichwa na mada za kusisimua kama vile yanavyofanya magazeti ya udaku ambayo ndiyo yanatamba sana. Pengine ni kwa sababu hii ndiyo maana nimeona gazeti hili limeanza pia kupenyezapenyeza makala za kimahaba ili kuvutia wasomaji.
Japo jambo hili linakatisha tamaa, kama isemavyo kauli mbiu ya Mzee wa Changamoto "Better to write for yourself and have no public, than to write for the public and have no self." inabidi tuendelee kujibidisha kuelimisha umma japo ni kwa mwendo wa kobe. Wanablogu wenye blogu za kiuchambuzi inabidi tusikate tamaa kwa blogu zetu kutosomwa na watu wengi kama blogu zinazoandika mambo ya "macelebrity, umodo, udaku na mavazi". Mimi naamini kwamba kazi yetu si bure ati!
Hawa jamaa kweli wako siriazi na mambo ya rushwa na upendeleo. Polisi mmoja hapa Florida amefukuzwa kazi kwa kupewa vijiko viwili vya "Ice Cream" na kundoka bila kuvilipia, jambo ambalo liliashiria utumiaji vibaya wa madaraka yake.
Polisi huyo alikuta duka linalouza ice cream limefungwa lakini alimshawishi muuzaji aliyekuwemo ampatie vijiko viwili. Baada ya kupata ice cream yake polisi huyo alitoka nje na kwenda kufaidi ice cream hiyo ya bure na mpenzi wake aliyekuweko nje ya duka.
Iligundulika baadaye kwamba polisi huyu huyu pia aliwahi kula na kuondoka bila kulipa katika hoteli moja. Katika mkasa huu, polisi mwenzake ilibidi amlipie. Mkasa huu unapatikana hapa.
Vipi tungekuwa na sheria na kanuni kali kama hizi dhidi ya rushwa, upendeleo, na matumizi mabaya ya madaraka; na tukazitekeleza?
Ukiniuliza swali ni uvumbuzi gani wa mwanadamu unaonivutia sana jibu langu la moja kwa moja litakuwa ni “jetliners”. Kila mara ninapoingia katika dege na halafu linaruka bila matatizo na kubakia angani kwa masaa zaidi ya 10 likiwa limejaza watu na mizigo huwa namvulia kofia binadamu kwa ugunduzi wake huu maridadi ajabu!Na mara yangu ya kwanza kusafiri na Boeing 747 nilishangaa mno (pengine kutokana na ushamba wa Kisukuma!)
Nilipoingia katika dege la Boeing 747 lililokuwa linamilikiwa na shirika la Alliance Airlines (Afrika Kusini) nilishangaa sana kwani dege lilikuwa limejaza wasafiri na mizigo tele mpaka nikakosa mahali pa kuweka begi langu nililokuwa nimeingia nalo.
Baada ya kuangalia umati ule wa watu nilikuwa na wasiwasi sana kama dege lile kweli lingeweza kuruka na kukaa angani masaa manane hadi tisa mpaka tufike London. Lakini kweli tena bila matatizo dege hilo lilijikongoja na muda si muda likawa limeruka na kweli baada ya masaa tisa angani tulifika London.
Kuanzia siku ile ndege imegeuka kuwa jambo linivutialo sana na nimeshasoma vitabu vingi na magazeti juu ya Historia ya juhudi za binadamu kujaribu kuruka, aina mbalimbali za ndege za kiraia, ajali kubwa za ndege, wagunduzi mashuhuri n.k. Wewe ni ugunduzi gani wa binadamu unaokuvutia zaidi?
Na mpaka leo kila mara ninapoingia katika dege daima huwa sikomi kushangazwa na teknolojia hii. Natumaini kwamba siku moja itawezekana kutengeneza madege ambayo hayatingishiki wala kusukwasukwa huku na huko hali ya hewa inapochafuka huko mawinguni. Huwa sipendi dege likianza kufanya hivi.
Niliwahi kuligusia jambo hili kwa kifupi hapa. Jana kulikuwa na kipindi katika History Channel ambacho kiliongelea suala hili kwa kina kwa mtazamo wa kisayansi. Ni wazi kwamba wanasayansi mbalimbali wakiwemo wanaastronomia wana wasiwasi pia na jambo hili.
Sikiliza sehemu ya mwanzo ya maelezo hayo ya kisayansi hapa chini. Hapa Marekani tayari kuna watu ambao wameanza kujiandaa kwa kujikusanyia chakula, silaha na kujenga ngome za chini ya ardhi.
Kutokana na wasiwasi wa jambo hili, sinema ya 2012 imekuwa mojawapo ya sinema zilizofanya vizuri sana hapa Marekani. Tazama utangulizi wake hapa. Nimeshaitazama na ni muvi nzuri - na niliwaona watazamaji wengine wakiwa na nyuso za huzuni na hata kudondokwa na machozi.
Sisi nyumbani Afrika, tunapaswa kuwa na wasiwasi na jambo hili na hata kuanza kujiandaa?
Wanawake na wanaume ambao wako "single" na ambao ndio mara yao ya kwanza kuonana wanakusanyika katika chumba halafu taa zinazimwa. Mtindo huu umeanzia kule Atlanta na sasa unaenea sehemu zingine.
Maongezi yote yanafanyika gizani. Baadaye taa zinawashwa na kwa mara ya kwanza watongozanaji hawa wanaonana kwa mara ya kwanza.
Lojiki ni kwamba ukivutiwa na mtu gizani bila shaka utavutiwa naye zaidi katika mwanga.
Wengine wanasema mbinu hii ni nzuri na wengine wanapinga.
Tazama video hapa. Mimi nadhani huyo jamaa kwenye picha hapo juu ana uhuru zaidi wa kumwaga beti zake kuliko haya mambo ya gizani.
Nakumbuka mwaka 2001 mama alipokuja kunitembelea wakati ule nikiwa bado mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA). Alishangaa sana alipoona utitiri wa wazungu (chokoraa) wasio na makazi wakiomba pesa mabarabarani. Alisema kwa mshangao "kumbe kuna wazungu masikini!"
Watu wengi pia wakisikia njaa moja kwa moja wanafikiri kwamba nchi inayozungumziwa ni lazima iwe ya "ulimwengu wa tatu". Kinachowajia akilini ni picha za vile vitoto vya Kiethiopia vilivyokondeana huku viking'ong'wa na mainzi vikiwa tayari kukata roho kwa ajili ya njaa. Kumbe hata hapa Marekani njaa ipo!
Ripoti ya Wizara ya Kilimo ya Marekani iliyotolewa juzi imeshawangaza watu wengi. Ripoti hiyo inasema kwamba kuna njaa hapa Marekani na mwaka jana Wamarekani wapatao 49,000,000 waliathirika na njaa au hawakuwa na chakula cha kutosha. Hii ni sawa na kusema kwamba kwa kila Wamarekani sita, kulikuwa na Mmarekani mmoja ambaye hakuwa na chakula (cha kutosha)
Kama inavyotegemewa watu wengi wanaoathirika na njaa ni masikini (ambao kutokana na siasa za kitabaka, kibaguzi na kinyonyaji za muda mrefu mimi nadhani wengi wao watakuwa ni Wamarekani Weusi na wahamiaji kutoka Amerika ya Kusini). Inashangaza kidogo kuona kuwa nchi tajiri kuliko nchi nyingine yo yote hapa duniani nayo inakumbwa na tatizo la njaa. Pengine picha hiyo juu itabidi tuifanyie mabadiliko ili kuakisi uhalisia huu mpya: njaa si tatizo la Afrika peke yake!
Rais Obama ameahidi kwamba serikali itaongeza misaada zaidi kwa watu masikini. Isome taarifa hiyo fupi hapa.
Mechi hii ilichezwa tarehe 5/11/2009. Wenye jezi nyekundu ni New Mexico University (NMU) na wenye jezi nyeupe ni Bringham Young University (BYU)
Huyu mchezaji korofi jina lake ni Elizabeth Lambert wa NMU. Cha ajabu ni kwamba pamoja na "vituko" vyote hivi hakupewa kadi nyekundu. Hata hivyo ameshafukuzwa katika timu hiyo.
New Mexico, pamoja na Elizabeth Lambert wao, walilazwa 1-0 na hivyo kutolewa katika mashindano hayo.
Jana (Novemba 17, 2009) kulikuwa na makala nzuri katika gazeti la New York Timesjuu ya ufisadi wa Teodoro Nguema Obiang ambaye ni mtoto wa raisi wa miaka mingi wa Equatorial Guinea - Teodoro Obiang Nguema Mbasogo. Inaaminika kwamba Teodoro Nguema Obiang ambaye pia ni waziri wa misitu na kilimo wa Equatoria Guinea ndiye anaandaliwa kuchukua madaraka ya uraisi baada ya baba yake kuachia madaraka. Mambo chomozi katika makala hiyo ni haya:
Equatorial Guinea inashika nafasi ya tatu katika utoaji wa mafuta barani Afrika ikitanguliwa na Naijeria na Angola. Mwaka 2007 pekee, Equatorial Guinea ilijipatia dola bilioni 4.8 kutokana na mauzo yake ya mafuta.
Paradoksi ni kwamba zaidi ya robo tatu ya wananchi wa Equatoria Guinea ni masikini hohehahe kabisa wanaoishi kwa pato la chini ya dola 1 kwa siku!
Wakati huo huo, mtoto huyu wa rais ambaye bado ana miaka 38 tu ni tajiri wa kutupwa na ni wazi kwamba utajiri huo ameupata kwa kupitia rushwa na ufisadi. Mfano mali zake za kifahari hapa Marekani – bila kutaja akaunti zake za Uswisi na utajiri wake mwingine ni kama ifuatavyo:
(7) Huja kupumzika Marekani zaidi ya mara tatu kila mwaka na kila anapokuja huja na pesa taslimu zaidi ya dola 1,000,000 tena bila kuwajulisha watu wa uhamiaji. Hili ni kosa la jinai kwa sheria za Marekani lakni kwa vile Marekani ndiye mnunuzi mkuu wa mafuta ya Equatorial Guinea, maofisa wa uhamiaji humfumbia macho.
Kwa hivyo:
(8) Ukiwa na mafuta, Marekani itakuruhusu ufanye cho chote unachotaka – hata kama ni kuvunja sheria zake! Ukijifanya jeuri wanakuja kuchukua mafuta yako kwa nguvu (muulize Saddam Hussein atakwambia)
Kwa ufisadi huu kweli, Afrika tutaweza kuendelea? Kinachoumiza moyo ni kuona kwamba umma wa Afrika, pengine kutokana na ukosefu wa elimu ya kweli pamoja na umasikini bado umelala na unaruhusu raslimali na utajiri wake uliopindukia kimo kufaidiwa na akina Teodoro Nguema Obiang wachache. Inasikitisha sana! Tazama hii clip hapa chini juu ya “vichaa wa Afrika"
Inaonekana madawa ya kuongeza nguvu kwa wenye VVU yana athari nyingi, zikiwemo usahaulifu, maumivu ya neva na kuzeeka mapema. Isikilize ripoti hii hapa chini. Tangu hapo kinga ni bora kuliko kuponya ati!
Mimi sivuti na lengo langu hapa siyo kuwatetea wavuta sigara. Wanasayansi wameshathibitisha kwamba uvutaji wa sigara ni tabia ya hatari inayoua mamilioni ya watu kila mwaka kutokana na saratani ya mapafu na magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa upumuaji. Kutokana na sababu hii uvutaji wa sigara umepigwa marufuku karibu katika kila kona ya dunia. Sehemu zingine zimefikia hatua ya kutunga sheria zinazowabana wavuta sigara kutovuta hata wakiwa majumbani mwao. Mwezi uliopita chuo kikuu cha Florida kilipitisha sheria ambayo inapiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo yote ya chuo – ndani na nje. Sijui wavuta sigara watafanyeje!
Swali langu ni hili: mbona tumekomalia sana sigara utafikiri kwamba uvutaji ndiyo tabia pekee-angamizi? Mbona tabia zingine za hatari kama unywaji wa bia (ambao pia, mbali na matatizo mengine, umeshathibitishwa kuwa kisababishi kimojawapo kikuu cha aina mbalimbali za saratani na hasa zile za matumbo) hatuzikomalii kama uvutaji sigara? Vipi kuhusu ulaji wa nyama hasa zile “nyekundu” ambao nao pia umeshathibitishwa kwamba ni hatari kwa afya? Wavuta sigara wanaonewa?
Mimi ni mmoja kati ya watu wasiopenda tabia za kinafiki za kujifanya kuchukia tabia moja angamizi na kukumbatia zingine za aina hiyo hiyo. Ndiyo maana huwa sielewi mtu anaponiambia eti ameamua kuacha kula nyama ili kulinda afya yake na wakati huo huo anazitandika bia sawasawa, kuvuta sigara na hata kuwa “kiwembe”.
Ni mawazo yangu tu. Pengine mwanafalsafa Kitururu angeweza kusema ninachojaribu kukisema hapa kwa ufasaha zaidi!
Wasikilize watafiti hapa wakijadili athari za ulaji wa nyama, uvutaji wa sigara na unene wa futufutu (obesity) kwa afya.
Ni wazi kwamba hivi sasa mashindano ya urembo ni biashara kubwa sana ndiyo maana yametanda kila kona kuanzia taifa, mikoa, wilaya, tarafa, kata na pengine muda si mrefu yatafika ngazi ya vijiji na hata familia!. Japo mashindano haya yanajumuisha watu wa kila aina wakiwemo watoto wadogo (bofya hapa), kwa kiasi kikubwa vigezo vinavyotumika ni vile vya Kimagharibi ambako ili mwanamke awe "mrembo" ni lazima awe mwembamba hasa hata kama ni ule wembamba wa kiutapiamlo!
Kimsingi hii ni kinyume na dhana ya jumla ya uzuri tuliyokuwa nayo sisi Waafrika ambapo mwanamke wa kwelikweli aliyekuwa akisifika alikuwa ni yule tipwatipwa, mwenye umbo mkatiko (vijana wanaita umbo namba 8), matako makubwa na miguu minene iliyosanifiwa (wenyewe wakiita miguu ya bia a.k.a usafiri wa uhakika!).
Wembamba kwetu sisi ulikuwa ni dalili ya maradhi na ukosefu wa lishe bora (unamkumbuka Clementine katika diwani ya Wimbo wa Lawino?). Wakati huu tulikuwa bado hatujajiingiza sana katika maisha ya deko na kula vyakula vya "kisasa" vilivyokuzwa kisayansi na kushindiliwa makemikali na sumu za kila aina. Kwa hivyo kansa na magonjwa mengine tunayoambiwa sasa kwamba yanasababishwa na unene hayakuwa tatizo sana kwetu. Sasa mambo yamebadilika! Soma makala ya Profesa Mbele kuhusu suala hili hapa.
Inavyoonekana wanawake tipwatipwa, baada ya kuona kuwa wanapigwa dafrau, nao wameamka na kuanza kufanya mashindano yao ya "urembo" pamoja na kufungua vilabu vyao wenyewe (gonga hapa na hapa). Hapa chini ni picha chache za mashindano ya aina hii ambayo nimeambiwa kwamba yalifanyika kule California na kwamba baadhi ya washiriki walikuwa ni Watanzania! (Mdau aitwaye Kessy anayeishi Las Vegas alihudhuria onyesho hili na ndiye ameniletea picha hizi - Asante Bwana Kessy)
Tanzania mashindano kama haya yapo? Kama yapo yanatazamwaje na wanajamii? Kweli Vodacom watakubali kumwaga mamilioni yao kwa mashindano kama haya?
Mshereheshaji Baadhi ya Washiriki
Mchuano wenyewe
Bwana Kessy ameleta link ya video hii ya youtube na kusema kwamba (nanukuu) "mwanamke true wa Kiafrika anapaswa kuwa hivi na siyo skiny kama hawa mamiss Tanzania" Kazi kwenu wadau. Mimi ni mjumbe tu na mjumbe daima huwa hauwawigwi ati!
Katuni hii imenikumbusha mambo mawili: Kwanza suala la unene. Kitamaduni unene ulikuwa ni jambo la kujivunia na sidhani kama ulikuwa na madhara makubwa kama tunavyoambiwa sasa. Kila mtu alikuwa na ndoto ya kunenepa na vitambi vilionekana kama ishara ya kufanikiwa kimaisha. Watu walikuwa wanafanya kazi sana na tulikuwa tunakula vyakula vya kiasili - siyo kama sasa ambapo utandawazi umetuvuruga kabisa. Soma hapa,hapa na hapa kuhusu hili suala.
Pili: tabia yetu ya kutukuza wazungu, uzungu na vitu vyao vyote. Japo utawala wao uliisha, kisaikolojia jamaa bado wametuminya kweli kweli! Niliwahi kulalamika kuhusu suala hili hapa. Natumaini hatutafikia hii hatua aliyofikia huyu "Mswahili" mwenzetu kwenye katuni.
Igeni mfano wa Mtoto wa Dandu, Saida Karoli na Mr Ebbo!
Niliwahi kuandika kwa kifupi juu ya matumizi ya Kisukuma katika nyimbo za Mtoto wa Dandu. Katika maakala hii fupi (ambayo imetoka katika gazeti la Kwanza Jamii la leo 10/11/2009), ninatoa wito kwa wasanii wa kizazi kipya kuiga mfano wa Mtoto wa Dandu, Saida Karoli na Mr Ebbo na kuimba katika lugha zao za mama au hata kutia vionjo vya "kikabila" katika nyimbo zao. Kwa kufanya hivi watakuwa wanatoa mchango wao chanya katika vita vinavyoendelea duniani kote kujaribu kuzitetea lugha za kienyeji ambazo ziko katika hatihati ya kuangamizwa na utandawazi. *****************************************************************************
Wanamuziki wa Kizazi Kipya – Tumieni Lugha Zenu za MamakamaAlivyofanya Mtoto wa
Dandu (Cool James)
Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima
James Maligisa Dandu a.k.a Mtoto wa Dandu a.k.a Cool James a.k.a Ng'wanamalia a.k.a CJ Massive a.k.a Ng'wanawapelana a.k.a Nzokaihenge alikuwa na kipaji cha hali ya juu katika muziki. Ndiyo maana muziki wake ungali unapendwa sana miaka saba sasa tangu aage dunia kwa ajali ya gari tarehe 27/8/2002. Sikupata bahati ya kumwona lakini yeye pamoja na Saida Kalori na Mr Ebbo pengine ndiyo waimbaji wa kizazi kipya ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kuzitukuza lugha zao za mama katika nyimbo zao - na hivyo kutupilia mbali ile dhana kwamba kizazi kipya hakiwezi kuguswa na nyimbo zenye ladha ya kikabila. Mtoto wa Dandu japo hakuimba katika Kisukuma moja kwa moja kama afanyavyo Saida Karoli, hapa na pale hakuisahau lugha yake ya mama iliyomkuza na kumlea kule Mwanza (Kisukuma). Hapa ni baadhi ya mifano tu ya matumizi ya Kisukuma katika nyimbo za mwanamuziki huyu mashuhuri aliyeondoka akiwa bado mchanga.
Jina lake mara nyingi alipenda kujiita Nzokaihenge yaani nyoka mwenye makengeza (nyoka makengeza). Alikuwa akijiita pia Ng'wanawapelana yaani mtoto mwenye hasira. Ni kawaida ya Wasukuma kujisifu na hapa ndicho alichokuwa akikifanya Mtoto wa Dandu. Ati, umeshawahi kuona nyoka mwenye makengeza maishani mwako? Unadra wa nyoka wa aina hii ndiyo ujumbe aliokuwa akitaka kuuwasilisha. Kipaji chake cha kipekee katika muziki kilikuwa nadra na muziki wake unaonyesha hivyo mpaka leo. Alipenda pia kujiita Ng'wanamalia - mtoto wa Maria. Hii inaonyesha kwamba pengine jina la mama yake ni Maria (Wasukuma hawana sauti " r" na hivyo mara nyingi huitamka kama "l" - kinyume na Wakurya)
Korasi mashuhuri inayosikika katika nyimbo zake nyingi inasema hivi:
Nimeshakuwa mtu wa thamani (heshima) Hata nikienda ugenini siwezi kukalia gogo Inabidi nipewe kiti kizuri cha kukalia
Inavyoonekana pia alikuwa ni mtu wa kutoa shukrani. Katika baadhi ya nyimbo zake anaonekana akimsifia na kumshukuru Jumanne Kishimba - tajiri mkubwa kule Mwanza na mmiliki wa duka kubwa la Imalaseko Supamaketi jijini Dar es salaam. Anasema hivi:
Jumanne Kishimba Ulinamoyo gwape giti buluba Hangi okumuka mpaga Bulaya
Tafsiri
Jumanne Kishimba Una roho nyeupe mithili ya pamba Tena umeshajulikana mpaka Ulaya
Akijisifu kidogo kama ilivyo kawaida ya Wasukuma anasema hivi:
Mtu mwenye akili haelemewi na mzigo (msemo wa Kisukuma) Nimezindikwa na (madawa ya) nyoka mwenye makengeza
Huyu ndiye Mtoto wa Dandu ambaye hakuusahau utamaduni wake. Huyu ndiye Nyokamakengeza ambaye hakuionea aibu lugha yake ya mama. Huyu ndiye Mtoto wa Maria ambaye hakuuonea aibu Usukuma wake. Huyu ndiye Cool James ambaye alikuwa anatambua kwamba asingeweza kuwa “cool” bila kuwa na utamaduni wake mwenyewe.
Hebu fikiria kama wanamuziki wengi wa kizazi kipya wangeiga mfano wa Saida Karoli, Mr Ebbo na Mtoto wa Dandu, wakaimba nyimbo katika lugha zao za mama (Saida Karoli - Kihaya) au kuingiza vipengele vya lugha zao za mama katika nyimbo zao kama Mtoto wa Dandu (Kisukuma) na Mr Ebbo (Kimasai). Hatua hii ingesaidia sana kukikumbusha kizazi hiki kilichopumbazwa na “usasa” kwamba lugha zao za mama zipo, zina hadhi kama lugha nyingine yo yote na zina manufaa ya kimatumizi hata katika ulimwengu huu wa kisasa. Kwa hivyo dhana ya kwamba lugha hizi ni za kizamani, zimeshapitwa na wakati na hakuna sababu ya kujifunza au kuzizungumza tena haina ukweli wo wote. Ingefurahisha kama nini kama wanamuziki hawa wangetimiza wajibu huu wa kitamaduni na kuziunga mkono lugha zetu za asili katika wakati huu zinapopita katika mikikimikiki ya kudharauliwa na kuonwa kwamba hazifai tena.
Kimsingi huu ni wito wangu kwa waimbaji wa kizazi kipya - tumieni lugha zenu za mama katika nyimbo zenu. Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatoa mchango wenu wa thamani sana katika kuzipa uhai lugha zenu zilizowakuza na kuwalea, lugha ambazo zimo hatarini kufa baada ya vizazi vichache vijavyo kama mtaendelea kuzidharau, kuzionea aibu na kuziona kuwa hazina faida wala nafasi katika ulimwengu wa kisasa.
Mungu aendelee kumpumzisha salama Mtoto wa Dandu a.k.a Cool James a.k.a Ng'wanamalia a.k.a Ng'wanawapelana a.k.a Nzokaihenge a.k.a CJ Massive. Muziki wake kwa hakika utadumu!
Kwa watu wengi wa nchi za Magharibi mbwa ni sehemu ya familia na ana haki sawa na memba mwingine ye yote katika familia. Mbwa anaweza kuwa na bima ya afya na hata kuachiwa urithi; na anapofariki basi familia nzima huomboleza na kumzika kwa gharama kubwa.
Ili kuvutia waumini wapya, hivi karibuni makanisa kadhaa hapa Marekani yameanzisha misa maalum kwa ajili ya mbwa. Misa hizi zinadumu kwa nusu saa ambapo mbwa huombewa wakiwa wamejilaza vitandani huku wakifaidi vitafunwa mbalimbali. Kwa habari zaidi kuhusu habari hii gonga hapa.
Kwetu sisi Waafrika jambo hili linaonekana kama vile utani na sijui Wakristo wana maoni gani kuhusu misa za aina hii. Kazi kweli kweli!
(2) Kama ni lazima upigane, zingatia siri hii. Ukiona unazidiwa - mtegee mpinzani wako anaporusha ngumi na wewe rusha hapo hapo tena kwa haraka ya kufumba na kufumbua. Hii ina matokeo matatu: Kwanza ngumi yake inaweza kukupata kwanza na kukufletisha kabla ya kwako haijatua usoni mwake (epuka hili lisitokee). Pili - ngumi yako inaweza kumpata kwanza na kumfletisha kabla ya kwake haijatua kidevuni mwako (hakikisha hili linatokea). Tatu - ngumi yake na yako zinaweka kutua kwa wakati mmoja na wote mkafletishana (na hii siyo mbaya sana). Nilifundishwa siri hii zamani sana. Tazama video hapa chini (dakika 1:18).
Mbali na kuwa chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo, watafiti sasa wanasema kwamba unene ukiwemo ule wa futufutu (obesity) ni kisababishi kikubwa cha aina mbalimbali za kansa. Kwa mfano, watafiti sasa wanasema kwamba:
Unene unasababisha asilimia 49 ya kansa za mfuko wa uzazi, ikifuatiwa na asilimia 35 ya kansa za matumbo. Unene pia unasababisha asilimia 28 ya kansa za kongosho (pancreatic cancer), asilimia 24 ya kansa za figo, asilimia 21 ya kansa za kibofu cha mkojo, asilimia 17 ya kansa za matiti na asilimia 9 ya kansa za utumbo mkubwa (colorectal cancer)
Mbaya zaidi - watu wanene wanaongoza kwa kufa na kansa kwa sababu mara nyingi wanapopata kansa, kansa zao huwa hazitibiki kwa urahisi kama za wenzao wembamba
Mimi nadhani kwamba utafiti huu haukuzingatia sababu zingine zinazosababisha kansa yakiwemo mazingira na mfumo wa maisha ya watu. Nyumbani tuna/tulikuwa na watu wanene lakini kutokana na tabia ya watu kufanya kazi sana pamoja na kula vyakula vya kiasili (ambavyo havijabadilishwa kisayansi ikiwemo kutiwa mahomoni ya bandia, mbolea kali na madawa mengine) hata Shirika la Afya Duniani linakiri kwamba Afrika lilikuwa ni bara lenye wagonjwa wachache kabisa wa kansa. Na halafu utandawazi mpya ukaja.
Leo hii tumebadilisha maisha yetu, tunakula vyakula vile vile tunavyoletewa kutoka nchi za Magharibi na mfumo wetu wa maisha umebadilika. Matokeo yake sasa kuna mripuko wa kansa za kila aina na unene - jambo ambalo miaka michache tu liliyopita ilikuwa jambo la kujivunia - sasa linaonekana kuwa ni jambo la hatari! (Tazama pia hapa na hapa)
Isome ripoti kamili hapa na tazama video fupi ya CNN kuhusu jambo hili muhimu hapa.
Pengine hili ni swali la kipuuzi lakini imebidi niliulize kutokana na kisa kilichonipata jana.
Baada ya kutoka kazini nilipita dukani kununua mboga na nikaona maua waridi (roses) mazuri sana. Dazeni moja ilikuwa inauzwa dola 6.99 tena bado freshi kabisa na yamefungwa na kurembwa vizuri. Bei ya kawaida kwa maua kama haya ni dola 13.99 - 29.99.
Basi nikanunua dazeni moja ili kumpelekea mama watoto wangu.
Nilipotoka nje nikakutana na mwanaume Mmarekani mweusi ambaye alikuwa ameambatana na wanawake wawili.
Wale wanawake wakanisifia kwa kusema "Nice roses. She is going to be very happy today"
Yule mwanaume yeye akanitupia swali "Bro, what did you do?" Wale wanawake wawili wakaanza kucheka.
Ilinichukua muda kidogo kumwelewa lakini nilipopambazukiwa nilielewa alikuwa anamaanisha nini: mtu unamnunulia maua umpendaye wakati umemkosea na unataka kuomba msamaha. Wakati huo nilikuwa karibu na gari langu na sikupata muda wa kumjibu muuliza swali ambaye tayari alikuwa ameshaingia dukani.
Katika kipindi kimoja cha televisheni niliwahi kusikia wanasaikolojia wakisema kwamba mwanaume anayetembea nje ya ndoa/penzi ana uwezekano mkubwa zaidi wa kumnunulia mke/mpenzi wake "orijino" maua kutokana na kusutwa na dhamiri "sense of guilty". Wanasaikolojia hawa walitoa ushauri kwa wake/wasichana kufanya uchunguzi mara moja kama waume/wapenzi wao wataanza kuwapa zawadi na hata kuwanunulia maua wakati si kawaida yao. Hii inaweza kuwa ni matokeo ya ule msuto wa dhamiri.
Kule usukumani, ilikuwa lazima kumnunulia umpendaye zawadi - ndogo au kubwa - kulingana na uwezo wako. Kanga, hereni, viatu, "chachandu"- kitu cho chote ambacho kingemfanya ajisikie kwamba unampenda na kumjali. Nadhani, mbali na kuhongeresha, maua (waridi) pia yanatimiza lengo lilelile kama hizi zawadi za Kisukuma.
Kwa wanaume: Kwa nini mnanunua maua?
Kwa wanawake: Kama mpenzi/mume hana kawaida ya kukuletea zawadi/maua na mara moja anaanza kufanya hivyo, utajisikiaje?Ni kweli utaingiwa na wasiwasi?
Wakati mwingine sisi tulioko ughaibuni Kiswahili kipya kinatupiga chenga. Mnamaanisha nini siku hizi mnaposema eti Kanumba amefulia? Natumaini si tusi (la nguoni) au neno baya!
Profesa mmoja mwanaume ambaye pia alikuwa mkuu wa idara mojawapo hapa chuoni ameachia ngazi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi wake.
Inasemekana kwamba alikuwa nao wengi kwa mpigo na mpaka sasa wasichana watatu wameandika barua kuelezea jinsi walivyolaghaiwa naye.
Alikuwa akiwatumia wanafunzi wake picha zake za uchi kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Alikuwa akilipwa dola 106,000 kwa mwaka.
Wanafunzi wake wa zamani wamtetea na kusema kwamba ni mmojawapo wa maprofesa wazuri sana - ingawa alipenda mno kuongelea mambo yake binafsi pamoja na familia yake.
Swali: Vipi tungekuwa na kasheria kama haka kule nyumbani? Mnakumbuka yale mambo ya mabinti "kushikwa" na hata "kudisco" wakimzembea Profesa? (sijui sasa kama mambo haya bado yapo yanatendeka au pengine utandawazi umeyamaliza!)
Kwa habari zaidi kuhusu hii ishu soma hapa na hapa
Imegundulika hivi karibuni kwamba kati ya dola bilioni 6.6 ambazo Marekani iliipatia Pakistan ili kuisaidia kupambana na magaidi wa Kitaliban na al-Qaida, ni dola 500 tu zilizotumika kwa lengo hilo.
Badala yake, rais aliyepita wa nchi hiyo, Jenerali Pervez Musharraf, alitumia kiasi kikubwa cha pesa hizo kujaribu kuinua uchumi wa nchi yake uliokuwa ukididimia. Pesa zingine zilitumika kuimarisha majeshi ya Pakistan (ambayo daima ipo katika hatihati ya vita dhidi ya jirani yake India).
Kilichonivutia katika ripoti hii ni kwamba hakuna panapotajwa kwamba Musharraf aliiba pesa hizi na kuzificha kwa manufaa yake binafsi - jambo ambalo pengine tungelitegemea kwa viongozi wengi wa Waafrika.
Badala yake, kiongozi huyu wa kijeshi, aliweka maslahi ya nchi yake mbele na kuamua kuzitumia pesa hizo kuinua uchumi wa nchi yake pamoja na kuimarisha majeshi yake ukiwemo ule mradi tata wa mabomu ya Nyuklia.
Ati, Afrika leo tungekuwa wapi kama viongozi wetu wangetumia pesa za misaada na mikopo (ambazo tumekuwa tukipewa/tukikopa tangu uhuru) kwa kuendeleza nchi zao badala ya kukimbilia kuzificha katika mabenki ya Uswizi?
Pamoja na matatizo yake yote, pamoja na udikteta wake wote - kwa hili namuunga mkono Jenerali Pervez Musharraf na huu ni mfano wa kuigwa na viongozi wa Afrika!
Jana hapa Marekani ilikuwa ni sikukuu ya Halloween- sikukuu ya kipagani iambatanayo na mambo ya kishetani shetani japo inasherehekewa pia na "Wakristo".
Basi jana katika mchezo wa mpira wa kikapu wa NBA kati ya San Antonio Spurs na Sacramento Kings kilitokea kisa cha kushangaza.
Mchezo ulipoanza, na bila kutegemea, alitokea popo ambaye alianza kukatiza uwanja kutokea goli hadi goli. Kidogo kulitokea mtafaruku huku wachezaji wakijaribu kumkwepa popo huyo. Mchezo ulisimamishwa kwa muda.
Popo huyo alipokuwa akijaribu kukatiza tena uwanjani, Manu Ginobili, mchezaji wa San Antonio Spurs kwa kasi ya kutisha alimtandika kwa kutumia mkono wake wa kushoto.
Popo alidondoka chini, Manu Ginobili akamwokota na kumpatia mfanyakazi aliyekuweko, akatia "sanitizer" mikononi na gemu likaendelea.
Matokeo: San Antonio Spurs 113, Sacramento Kings 94.
Ingekuwa nyumbani si ajabu hii ingesemwa kuwa ni kazi ya "kamati ya wazee" kumbe...
Tazama video hapa chini kumwona Ginobili akimfanyizia popo huyu mwenye bahati mbaya.
Baadaye alipata chanjo ya kuzuia vijidudu na aliwaonya watoto wasijaribu kuwaua popo kama alivyofanya kwani inaweza kuwa ni hatari.