NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, December 30, 2009

HATA GOOGLE???

UTAFITI: MATUMIZI YA MTANDAO YANAIMARISHA KAZI ZA UBONGO KWA WAZEE

  • Utafiti uliofanywa hivi karibuni nchini Marekani unaonyesha kwamba matumizi ya mtandao (internet) kwa wazee yanaimarisha utambuzi (cognition) na kazi za ubongo wao. Utafiti huu ulihusisha wazee wa jinsia zote wenye umri kati ya miaka 55 na 78. Wazee hawa waligawanywa katika makundi mawili. Moja halikutumia mtandao na kundi jingine lilitumia mtandao mara kwa mara.

  • Matokeo yalionyesha kwamba kazi za ubongo wa wazee katika kundi ambalo lilikuwa linatumia mtandao mara kwa mara ziliimarika zaidi kuliko za wazee katika kundi ambalo halikutumia mtandao. Mabadiliko makubwa yalionekana katika sehemu za ubongo zinazoshughulika na kumbukumbu (memory), lugha, kusoma na upambanuzi.

  • Matokeo haya yamewafurahisha wanasayansi na wanasema kwamba pengine matumizi ya mtandao yanaweza kuwa silaha mojawapo dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na upotevu wa kumbukumbu na utambuzi kama vile Alzheimer.
  • Sina uhakika kama kweli wazee wa Kiafrika wanahitaji mtandao kuimarisha kazi za ubongo wao. Mimi nadhani kwamba michezo kama vile bao, drafti na hata kuhesabu ng’ombe wanaporudi nyumbani kila jioni ni mazoezi tosha yanayoweza kusisimua kazi za ubongo, mazoezi ambayo yamesaidia kuwafanya wazee wengi wa Kiafrika kubakia makini kiutambuzi (cognitively) hata katika umri mkubwa. Sijui kama tulikuwa na wagonjwa wengi wa Alzmeimer barani Afrika kabla ya hili wimbi jipya la utandawazi tunaolishuhudia kwa sasa. Isitoshe, tulikuwa tunakula vyakula vya kiasili na mfumo wetu wa maisha ulituwezesha kufanya kazi sana. Sasa mambo yamebadilika sana na pamoja nayo magonjwa ya moyo, saratani, kiharusi na si ajabu "dementia" na Alzheimer sasa yanatuandama.


  • Kwa habari zaidi juu ya utafiti huu soma hapa. Kwa maelezo ya kitaalamu zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa.

Monday, December 28, 2009

UPUMBAVU WA BINADAMU HUU HAPA (USITAZAME VIDEO HII KAMA UNAKEREKA KIRAHISI - dk 2:22)

  • Akilinganishwa na wanyama wengine binadamu ni kiumbe dhaifu sana. Hana meno wala makucha makali kama ya simba, hana mbio kama za duma (cheetah), ngozi ngumu kama ya tembo, harufu chefuzi kama ya fungo, ujanja wa kujificha peupe ili kuwakwepa maadui kama wa kinyonga wala nguvu za kifaru.
  • Pamoja na udhaifu wake huu, uwezo wake wa kufikiri umemwezesha kuzikwaa ngazi za mfumo tata wa kiikolojia hadi kufikia kileleni kabisa. Leo hii binadamu ndiye anayetawala viumbe wengine – uwezo ambao wengine wanaamini kwamba alipewa na Mungu siku ile Mungu alipokamilisha kazi yake ya kuiumba dunia na vyote vilivyomo.
  • Kinachoshangaza hata hivyo ni ukweli kwamba binadamu anautumia vibaya uwezo wake kama mtawala wa viumbe vyote - bila kujali kama uwezo huu ni zawadi aliyopewa na Mungu au kama ni matokeo ya mamilioni ya miaka ya mapambano yake dhidi ya mazingira yanayomzunguka.
  • Wakati wanyama wengine wanaua wanyama wengine kwa lengo la kujipatia chakula au kujikinga wenyewe wasigeuzwe chakula, inasemekana binadamu ndiye kiumbe pekee anayeua wanyama wengine kwa nia ya kujifurahisha tu. Kwa mfano, binadamu anaua wanyama wengine ili tu ajipatie pembe, kwato, meno au ngozi ili akapambe chumbani kwake au kujiwekea kumbukumbu.

  • Tamaa hii ya kujifurahisha imemfanya binadamu kujaribu kuwafuga au kuwakusanya wanyama mbalimbali katika maeneo maalumu (zoo). Ukitembelea maeneo haya utawakuta simba, twiga, tembo, “tiger” na wanyama wengine wakiwa wamekata tamaa kutokana na maisha ya kitumwa wanayoishi. Hiki ndicho nilichokiona, kwa mfano, kule San Francisco na Honolulu - madume ya simba kutoka Afrika yaliyokata tamaa na ambayo yanashinda siku nzima usiku na mchana yakiwa yamefungiwa katika vibanda au vieneo vidogo vilivyozungushiwa seng’enge, nondo au ukuta mrefu.

  • Katika video hapa chini (tafadhali usiiangalie kama unakerekeka kirahisi), ni “tiger” ambaye alicharuka, akamjeruhi mmoja wa waangalizi wake kwa kuung’oa kabisa mkono wake wa kushoto na hapa anaonekana anajipatia mlo wake bila wasiwasi. Sijui tukio hili lilitokea wapi na lugha inayozungumzwa hapa siifahamu. Kwangu mimi, hata hivyo, hili ni fundisho kwa binadamu ambaye amevuka mipaka na kuutumia vibaya uwezo wake kama mtawala wa viumbe vingine. Kwa nini umfuge mnyama hatari kama “tiger?”
  • Katika kuhitimisha tashtiti na upumbavu huu wa binadamu, naamini kwamba “tiger” huyu aliuawa, pengine kwa kupigwa risasi. Mtu unaweza kujiuliza, aliuawa kwa kufanya kosa gani? Kwa kuwa “tiger”?
  • Tuwe waangalifu na kujua mipaka yetu kama binadamu, walimu, viongozi, wanafunzi, waume, wake, n.k. Vinginevyo itakuwa ni kama walivyosema waswahili “akili nyingi………" Au “majuto ni……”

video

PENGINE SIKU MOJA TUTASAFIRI "UCHI" KWENYE NDEGE

  • Kwa abiria wa ndege mambo yalianza kubadilika baada ya mashambulizi ya kigaidi ya 9/11 nchini Marekani. Sheria kali zaidi ziliwekwa ili kuimarisha usalama na abiria walianza kufanyiwa uchunguzi mkali zaidi kabla ya kupanda ndege ili kuanza safari zao. Kumbe huu ulikuwa ni mwanzo tu.

  • Richard Colvin Reid alipojaribu kuripua ndege kwa kuwasha kifaa kilichokuwa kimefichwa katika viatu vyake baada ya kuchanganya kemikali alizokuwa ameingia nazo kwenye ndege sheria zilibadilika. Abiria wote sasa walitakiwa kuvua viatu vyao ili vichunguzwe vizuri na mitambo ya usalama kabla ya kuruhusiwa kupanda ndege. Vimiminiko vyote pia vilipigwa mafuruku – dawa za mswaki, mafuta ya kujipaka na pafyumu. Vichupa vidogo vidogo pekee ndivyo viliruhusiwa.

  • Baada ya Mnigeria kujaribu kuripua ndege ya shirika la ndege la Northwest juzi, inasemekana baadhi ya mashirika ya ndege yameanza kupiga marufuku abiria kusimama au kuondoka katika viti vyao saa moja kabla ya ndege kutua. Wachambuzi wengi wa masuala ya usalama wa anga wanapendekeza kwamba ili kukata mzizi wa fitina, itakuwa lazima kupiga marufuku abiria kuingia na mzigo wo wote katika ndege. Vitu pekee vitakavyoruhusiwa ni dawa ambazo abiria anazihitaji safarini. Kompyuta za mkononi na vibegi vyote vidogo vidogo itabidi vitiwe katika mabegi yatakayosafirishwa katika sehemu ya mizigo ya ndege – ambako nako mitambo mikali zaidi ya kiusalama itaanza kutumika ili kuchunguza mizigo yote.

  • Isitoshe abiria wote watatakiwa kupita katika mashine mpya ambazo nasikia zinaonyesha sehemu zote za mwili. Mashine hizi zinalalamikiwa sana na watu wa masuala ya haki za binadamu ambao wanadai kwamba kimsingi zinaonyesha kila kitu zikiwemo sehemu za siri na hasa kwa wanaume (tazama video hapa chini).

  • Mtu unaweza kujiuliza, juhudi hizi za kizima moto za Wamarekani zitatufikisha wapi? Inavyoonekana Al Qaida hawalali na kila siku wanakuja na njia mpya za kuweza kutekeleza malengo yao. Baadhi ya watu wanasema kiutani kwamba kama bandika bandua hii itaendelea basi si ajabu siku moja tutatakiwa kusafiri uchi!

  • Kama nilivyogusia hapo juu, juhudi hizi za Wamarekani, japo ni nzuri, ni za kizimamoto tu na hazigusii hasa kiini cha tatizo lenyewe. Wataalamu wengi wanakiri kwamba hakuna silaha ambayo inaweza kumshinda adui ambaye yuko tayari kupoteza maisha yake ili kupigania na kutetea kile anachokiamini. Hivi ni vita vya kifikra/kiitikadi/kimtazamo na suluhisho lake linabidi litafutwe huko. Suluhisho lake kamwe halitapatikana kwa kudondosha mabomu kama Marekani inavyofanya sasa kule Afghanistan na sehemu zingine ambako itikadi kali za kiisilamu zimejitandaza.
  • Kinachotia wasiwasi zaidi ni kuona kwamba itikadi hizi za kihafidhina zinaenea hapa hapa Marekani na kuna visa vingi vinavyotokea ambapo vijana wa Kimarekani wamethibitika kwamba wamekwenda Somalia na Pakistani kujiunga na “kaka” zao wa Kiislamu katika uwanja wa mapambano. Watu wanajiuliza, Marekani itajipiga mabomu yenyewe? Suluhisho la mgogoro huu ni nini?


Saturday, December 26, 2009

MNIGERIA AJARIBU KURIPUA NDEGE KULE DETROIT

  • Wakati ulimwengu ukisherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo, abiria mmoja raia wa Naigeria alifanikiwa kuripua "kifaa" fulani katika ndege iliyokuwa inajaribu kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Detroit.
  • Ndege (Airbus 300) ni ya shirika la ndege la Northwest na ilikuwa inatoka Amsterdam Uholanzi kwenda Detroit, Michigan nchini Marekani. Ilikuwa imebeba watu 278. Ndege hiyo iliweza kutua salama
  • "Kama kawaida" Mnigeria huyo ameelezwa kuwa na uhusiano na makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali.
  • Kwa habari zaidi kuhusu habari hii soma hapa. Kama nilivyotegemea, watoa maoni katika tovuti mbalimbali tayari wanashambulia Unigeria na Uafrika wa mshambuliaji. Tazama video hapa au hapa.

Monday, December 21, 2009

ATI, ULITABASAMU LEO???

UTAFITI: MA"BABY FACE" HUISHI MAISHA MAREFU ZAIDI

Mwanamuziki Kenneth "Babyface" Edmond (miaka 51)
  • Sote tunawafahamu. Wengine ni wanablogu wenzetu. Japo wana umri mkubwa lakini nyuso zao zinaonekana kuwa za kitoto. Hata wanapotuambia umri wao hatuwaamini na tunawabishia kwa sababu wanaonekana wangali vijana na kamwe hawalinganishiki na wenzao wanaodai kuwa nao sawa kiumri. Nyuso zao huwa zimetakata na ngozi zao nyororo zisizo na doa la chunusi wala mwonekano wa kuzongwa na maisha daima huonekana kung’ara. Huwa tunawaita ma“baby face”. Kwa Kisukuma watu hawa huitwa “bagidanamhala” kama ni wanaume au “bagidagiguluha” kama ni wanawake.

  • Katika utafiti uliofanywa nchini Denmark, wanasayansi wamethibitisha kwamba ma“baby face” huishi maisha marefu zaidi kuliko wenzao wenye nyuso zilizokomaa. Utafiti huu ulijumuisha jozi za mapacha wapatao 1,800 wenye umri unaozidi miaka sabini. Baada ya kuwapiga picha nyuso zao, makundi matatu ya watu tofauti tofauti ambao hawakujua umri sahihi wa mapacha hawa waliombwa kukadiria umri wao.

  • Baada ya miaka saba, mapacha walioainishwa kama ma“baby face” ndiyo walikuwa wakiendelea kuishi kwa wingi ikilinganishwa na wenzao wenye nyuso zilizoakisi umri wao kwa usahihi; na matokeo haya hayakuathiriwa na jinsia wala mazingira. Kwa hivyo, wanahitimisha wanasayansi hawa, kuwa na uso wa “kitoto” kunahusiana moja kwa moja na kuishi maisha marefu. Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu tembelea hapa.

Wednesday, December 16, 2009

WATOTO WA KUBAMBIKIWA: NANI WA KULAUMIWA? KUNA UMUHIMU WA KUPIMA DNA?

  • Tatizo la kubambikiana watoto inaonekana ni tatizo la tangu zamani.
  • Kabla ya mapinduzi makubwa katika taaluma ya chembechembe za urithi katika miaka ya hivi karibuni, hakukuwa na njia za kisayansi za kuweza kuwathibitishia akina baba kama kweli watoto “waliowazaa” ni wao. Leo hii inawezekana kuhakikisha kwamba huyo mtoto wako asiyekufanana ni wako kwa asilimia 99.99%
  • Katika gazeti la The Guardian la tarehe 10/4/2009 kulikuwa na habari yenye kichwa kilichosema “DNA proof: 60pc of Male Parents not Biological Fathers”. Habari hii pia iliwekwa katika Blogu ya Jamii. Habari hiyo ilimkariri mkemia mkuu wa serikali Bwana Ernest Mashimba akitoa data kwamba katika vipimo vyote vya DNA ambavyo ofisi yake ilikuwa imevifanya, ilibainika kwamba asilimia 60 ya akina baba hawakuwa wazazi halali wa watoto hao bali walikuwa wamebambikiwa tu. Gazeti la Habari leo katika ukurasa wake wa mbele pia liliandika: Wanaume Wengi Wasingiziwa Watoto: katika kila wawili waliopima, mmoja amebambikiwa
  • Katika maoni mengi yaliyotolewa na wadau katika Blogu ya Jamii (kwa bahati mbaya mengi ni ya kiosha vinywa), akina mama hasa ndiyo walioandamwa na kubebeshwa lawama utafikiri kwamba wanajitundika hizo mimba. Mimi nadhani hili ni tatizo la kijamii ambalo linabidi kutazamwa kwa kina na pande zote zinazohusika. Ni lazima tujue, kwa mfano, sababu hasa zinazowafanya akina mama kutembea nje ya ndoa zao wakati huu ambapo gonjwa la UKIMWI linaangamiza maisha ya watu.
  • Swali jingine la msingi ambalo nilijiuliza baada ya kuisoma habari hii ni hili: kuna ulazima kweli wa kupima DNA ili kuthibitisha kama mtoto ni wako ama la? Sipingi matumizi ya DNA katika kutibu magonjwa au kuamua mizozo ya urithi na mengineyo. Ninachopinga ni matumizi ya “kiushabiki” ya DNA mf. ili kuthibitisha kama mtoto aliyezaliwa ni wako eti kwa sababu tu mtoto huyo anamfanana muuza mkaa wa nyumba ya jirani au Mpemba mwenye meza ya mbogamboga katika genge la pale mtaani kwenu.
  • Katika jamii nyingi za Kiafrika mtoto hakuwa “mali” ya mzazi pekee bali alikuwa mali ya ukoo mzima. Ndiyo maana, baba mzazi alipofariki, wanaukoo wengine walipewa jukumu la kumlea mtoto huyo na kuhakikisha kwamba anakua salama. Kwa hali hiyo, kujua “baba hasa” wa mtoto ni nani halikuwa jambo la muhimu sana. Japo leo hii utandawazi unatusukuma na kututenga na utamaduni wetu, kuna mambo ambayo inabidi tuwe waangalifu nayo, na hili ni mojawapo.

    Je, leo hii ukipima DNA na kugundua kwamba kumbe “babako” aliyekulea, kukusomesha na kukusaidia kwa hali na mali katika maisha yako si “babako mzazi” bali alibambikiwa tu utafanyeje? Utamkana? Utamlaumu nani? Na ukipima DNA na kugundua kwamba hivyo vitoto vyako virembo vimalaika vya Mungu uvipendavyo kikweli umebambikiwa utafanyeje? Utavikana? Utamtaliki mkeo?
  • Hebu tusije tukaiga hii tabia ya kupima DNA bila sababu za msingi kwa vile tu eti tumeona katika Maury Show. Huko watu hufurahi na kurukaruka (kama huyu chini) wanapothibitishwa kwamba si wazazi halali wa watoto waliobambikiwa kwa sababu jamii yao imesimikwa katika ubinafsi; na wanakuwa wameziepuka zile gharama kubwa za “child support” – gharama ambazo wangehangaika nazo mpaka huyo mtoto wa kubambikiwa afikishe miaka 18!

Tuesday, December 15, 2009

GAZETI LA KWANZA JAMII SASA KUCHAPISHWA MARA MOJA TU KWA MWEZI!

MABADILIKO KWANZA JAMII

Wapendwa wasomaji wa gazeti hili la KWANZA JAMII,

Baada ya kutafakari kwa kina, Bodi ya Uhariri na Uongozi wa KWANZA JAMII tumefikia uamuzi wa kulifanyia mabadiliko gazeti lenu hili ili tuweze kukidhi mahitaji yenu. Hadi hapo tutakapopata uwezo wa kuwa na rasilimali watu ya kutosha na uwezo wa kifedha kumudu kuchapa kila wiki aina ya makala za kiutambuzi na kielimu mlizo na kiu nazo zaidi, KWANZA JAMII litakuwa likichapa makala hizo mara moja kwa mwezi, hivyo basi, kuanzia toleo hili, KWANZA JAMII litakuwa likitoka mitaani kila Jumanne ya kwanza ya KILA MWEZI, kwa maana ya mara moja kwa mwezi. Tunaahidi KWANZA JAMII litakuwa likitoka likiwa na ubora zaidi ya wa sasa. Vinginevyo, unaweza kuendelea kusoma KWANZA JAMII mtandaoni kila siku na kwa maana hiyo kufuatilia na kuchangia katika mijadala hai. Kwa taarifa kamili soma hapa.

Inavyoonekana mambo hayaendi vyema katika gazeti hilo ambalo lilikuwa likijibidisha sana kuchapisha makala za uchambuzi. Nimeligusia suala hili katika makala yangu itakayochapwa wiki ijayo ambayo kimsingi ni jibu la makala ya Padri Privatus Karugendo.

ATI: UNAONA "OPTICAL ILLUSION" YO YOTE KATIKA PICHA HII?

  • Jamani. Nimeambiwa eti kuna "optical illusion" kali katika picha hii. Nimeichunguza kwa karibu dakika mbili nzima lakini sijaona kitu kingine kipya mbali na kile nikionacho. Kama kuna anayeona cho chote basi atwambie. Isije ikawa kama kule kwa Kamala ambako tulifumba macho weee bila kuona cho chote.

VIONGOZI WETU WANAPOZABWA VIBAO

  • Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi alipozabwa kibao, Watanzania wengi tulilalamika sana na kusema kwamba kitendo hicho kilikuwa hakiendani na maadili yetu kama jamii iliyosimikwa katika misingi ya upendo, heshima, amani na mshikamano. Ndiyo maana watu hawakuridhika na adhabu aliyopewa mzabaji huyo (mwaka mmoja jela) na wakataka apewe adhabu kali zaidi ili liwe fundisho.
  • Wapo pia ambao walilaumu mfumo mzima wa ulinzi wa viongozi. Walihoji kwamba inakuwaje rais mstaafu mzima azabwe kibao tena mbele ya halaiki? Ingekuwaje kama huyo mzabaji angekuwa na silaha nyingine kali?
  • Nimekikumbuka kisa hiki baada ya waziri mkuu wa Italia, bilionea mtanashati Silvio Berlusconi kutandikwa ngumi jana na kung'olewa meno mawili, kupasuliwa mdomo pamoja na uso wake kutapakaa damu. Picha zilizopatikana zinamwonyesha bilionea huyo mwenye mbwembwe akiweweseka mithili ya bondia aliyeelemewa katika shindano (tazama video ya Youtube hapa chini).
  • Katika kisa cha rais Mwinyi baadhi ya watu (ma-anonymous) katika blogu mbalimbali walionekana kutoshtushwa sana na kitendo hicho na wakakiona kama matokeo ya kukua kwa matabaka katika jamii. Dai kuu kutoka kundi hili la watoa maoni ni kwamba watu wamesikinika mno na wamefikia hatua ya kukata tamaa, na pengine vitendo kama hivi ni dalili tu za volkeno ya kitabaka inayofukuta mumo kwa mumo. Sina uhakika kama dai hili lina mashiko yo yote.
  • Katika blogu mbalimbali, watu wengi pia wamefurahishwa na kitendo cha Berlusconi kung'olewa meno mawili na kupasuliwa mdomo wakidai kwamba bilionea huyo ni mtu asiyejali, ni mzinzi sana na anapendelea operesheni za kujitengeneza sura. Wanadai kwamba kama bilionea, haelewi hali halisi ya maisha ya Mwitalia wa kawaida.
  • Kisa hiki kinaweza pia kutufanya tujiulize swali hili: Je, viongozi wetu (wote) kweli wanajua hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida (masikini anayeishi kule kijijini) au nao wamegeuka kuwa MaBerlusconi?
  • Hebu basi viongozi wetu wasisubiri mpaka kuzabwa vibao ndiyo wakumbuke jukumu lao la msingi - kuboresha maisha ya umma uliowaweka madarakani. Ni maisha bora kwa kila Mtanzania ati!

Monday, December 14, 2009

TOVUTI MPYA YA HABARI, MUZIKI, KAMUSI, MAFUNZO YA KOMPYUTA NA MENGINEYO

Pole na shuguli za kutupasha habari mbali mbali zinazotokea ndani na nje ya Tanzania.

Naomba nafasi katika blog yako ili niwajulishe ndugu zangu watanzania kwamba nimetengeneza website www.rusumo.com ambapo wataweza kusikiliza nyimbo mbali mbali za Tanzania kama vile taarab,segere,dance,bongo flava,gospel na nyimbo za kigeni kama vile raggae,za kihindi,pop na nyengine nyingi tu.

Pia kuna dictionary ya kisasa kabisa ambayo ina lugha zote za Ulaya na baadhi ya lugha za Asia,katika dictionary hii baada ya kupata tafsiri ya neno pia unaweza kuona picha za neno hilo kwa kubofya upande wa pili wa Ukurasa.

Kadhalika wadau wataweza kuona hali ya hewa na wakati wa sehem mbali mbali za dunia.
Karibuni sana wadau, ni mimi

MSAFIRI ISMAIL RUSUMO.
www.rusumo.com

Saturday, December 12, 2009

KABINTI KANGU KA PILI KAMEFIKISHA MIAKA SITA

Ni hako katikati. Kanaitwa Zofa Minza Matondo. Kako shule ya vidudu na mwaka kesho kataanza darasa la kwanza. Ni kamalaika ka Mungu kazuri, kapole, kacheshi, kenye huruma na kanakopenda sana kusoma vitabu!
 
    Keki ilitakiwa iwe na "microphone" ya Hannah Montana. Kazi kweli kweli. 
      Marafiki kadhaa walikuweko kusherehekea na kuimba "Happy Birthday, happy birthday to you Zofa" 

        Best friend naye alikuweko!
            Baada ya maakuli na shamrashamra nyinginezo, ilibidi kuingia katika "Nascar". Hapa dad anahakikisha kuwa hatua zote za kiusalama zimezingatiwa. Happy Birthday Zofa Kija Matondo! (Kosa - jina linapaswa kusomeka Zofa MINZA Matondo)

            Friday, December 11, 2009

            KUNA AULIZAYE; "UKO WAPI PROFESA MATONDO?"

            • Swali hili liliulizwa kwa Mjengwa. Japo nililijibu kwa ufupi (tazama maoni), muuliza swali sikumsikia tena. Naliweka hapa ili tuendelee kulijadili.
            ***************************
              Profesa Matondo, upo wapi?

              nyumba yangu
              nyumba zangu

              ANGALIA HII:

              ng'ombe yangu
              ng'ombe zangu

              AU ni

              ng'ombe wangu
              ng'ombe wangu

              NA HII PIA:

              mama yangu
              mama zangu

              AU ni

              mama wangu
              mama wangu?

            LEO "NIMEADHIRIKA" - HALAFU NIKAKUMBUKA NYUMBANI

            • Tumefunga shule jana kwa wiki tatu hivi. Basi leo, baada ya sherehe ya kumaliza muhula kule idarani, nikapita katika duka moja la kimataifa linalouza sato ambao linadai kwamba wanatoka Ziwa Victoria moja kwa moja (Kamala anasema wana sumu sana siku hizi). Basi hapo nikajipapatua nikanunua wanne. Sato hao wameshasafishwa tayari na nilipofika nyumbani nikawaosha wangu wangu.


            • Sikutaka mapishi yenye "korogesheni" nyingi bali nilitaka kuwapika chukuchuku yaani bila mafuta wala viungo vingi. Ni vitunguu, nyanya, pilipili na mchicha kwa wingi - ni kama supu, ni kama mbogamboga (yaani nusu kwa nusu). Huwa napenda kuwala hawa na kipande cha mkate. Chukuchuku lenyewe ni kama linavyoonekana hapa chini.


            • Ngoma ilikuja nilipotaka kuweka chumvi. Kumbe hakukuwa na chumvi hata kidogo ndani ya nyumba. Nilipiga simu kazini kwa mama kuulizia kama kulikuwa na chumvi sehemu nyingine ambayo siijui (wanawake hupenda kujiwekea akiba ya vitu muhimu). Bahati mbaya naye akawa katika mkutano na hivyo sikumpata. Kutoka hapa nyumbani kwenda madukani kidogo kuna kamwendo - na kusema kweli sikutaka tena kuendesha.
            • Jirani yangu hapa (mzungu tena polisi) alikuwa nje anacheza na watoto wake. Yaani nilitamani kweli nimzukie na kumwomba chumvi lakini nikasita. Japo mahusiano yetu naye si mabaya, kama kawaida maisha ya hapa ni ubinafsi na kila mtu kivyakevyake. Kuna siku ambazo huwa tunasalimiana na hata kuzungumza kidogo, siku zingine tunapungiana mikono tu na siku zingine hatusalimiani kabisa.
            • Basi nilizima jiko, nikamtumia mama ujumbe kumwomba aje na chumvi akirudi kutoka kazini halafu nikajipumzisha huku roho ikiniuma kwa kuchelewa kufaidi chukuchuku langu. Kisa hiki kimenifanya nikumbuke nyumbani Shinyanga ambako kuazimana chumvi (na vitu vingine) bado ni jambo la kawaida sana! Ugenini ni ugenini tu na nyumbani daima kutabakia kuwa nyumbani ati!

            Thursday, December 10, 2009

            WANAFUNZI SIKILIZENI - MSIDHARAU SOMO LA HISABATI - HALIEPUKIKI!!!

            • Hebu tazama jamaa hapa chini alivyokokotoa mahesabu haya. Bila kuambiwa faida hasa ya ukokotoaji huu, wanafunzi wengi huliona somo la hisabati kama lisilo na maana wala faida. Somo hili muhimu pia huwa halifundishwi vizuri na pengine ndiyo somo linaloongoza kwa kuchukiwa na wanafunzi - na lina walimu wakali sana! Unawakumbuka walimu wako wa Hisabati?

            • Albert Einstein - pengine mwanasayansi mashuhuri kuliko wote - aliwahi kusema kwamba hisabati ndiyo lugha pekee inayoweza kueleza kila kitu.
            • Plato - anayetambuliwa na wengi kama baba wa Falsafa na mtu wa kwanza kufungua chuo alichokiita akademi - aliweka tangazo hili katika mlango wa kuingilia akademi yake" Let no one ignorant of geometry enter" Kwa hivyo kama wewe ulikuwa hujui/hupendi hisabati kamwe usingeweza kutia guu katika akademi ya Plato.
            • Pamoja na ukweli kwamba hisabati si somo rahisi (kama kuna somo rahisi!) mimi nadhani pia kwamba wanafunzi hawaambiwi hasa umuhimu wa somo hili katika karibu kila kitu ambacho watafanya baadaye; na mara nyingi ufundishaji wake ni shaghalabaghala tu. Mwalimu anakuja darasani, anatoa mifano miwili mitatu halafu anaanza kuuliza maswali. Ukikosea unaambulia viboko.

            • Mimi pia sikuona sababu ya kukazana kukokotoa mahesabu bila kujua hasa faida yake ni nini. Nilipoanza masomo yangu ya shahada za uzamili na uzamifu pale UCLA ndipo moto uliponiwakia. Pale nilitakiwa kuchukua madarasa ya "Mathematical Linguistics" na "Computational Linguistics". Madarasa haya - ambayo ni ya muhimu sana na wahitimu wake kusakwa na makampuni mbalimbali ya simu, michezo ya video, Google na mengineyo - yanataka ujuzi wa hali ya juu wa misingi ya hisabati na lojiki. Pamoja na ukali wao wote, niliwakumbuka walimu wangu wa Hisabati.

            • Ukweli ni kwamba hesabu haziepukiki na wanafunzi wetu inabidi waambiwe hivyo. Hata kama wakizikimbia leo, kuna uwezekano mkubwa kwamba watakutana nazo huko mbele.

            Wednesday, December 9, 2009

            LEO NI SIKUKUU YA UHURU - TUTAFAKARI SAFARI YETU

            • Mwaka 1954, kiongozi kijana msomi na mwenye bashasha aitwaye Julius Kambarage Nyerere akishirikiana na wazalendo wenzake wachache alianzisha chama cha TANU ili kupigania uhuru wa Mtanganyika.


            • Baada ya kupigania uhuru kwa amani hatimaye usiku wa manane wa kuamkia tarehe 9/12/1961, Union Jack - bendera ya himaya ya Mwingereza - ilishushwa na bendera ya Tanganyika ilipandishwa. Tanganyika ilikuwa nchi huru!

            • Mwalimu Nyerere na viongozi wenzake walikabidhiwa nchi na Gavana wa mwisho wa Kiingereza. Unaweza kuwaona Rashid Mfaume Kawawa (Simba wa Vita) na Oscar Kambona wakiwa tayari kuchapa kazi.

            • Katika kuonyesha matumaini tuliyokuwa nayo, tulimpa Meja Nyirenda mwenge wa uhuru na kumwomba aende kuuwasha na kuusimika katika Mlima Kilimanjaro. Alifanya hivyo!

            • Tulichagua bendera yetu iliyoonyesha historia, utamaduni na utajiri wetu wa kiasili.

            • Ngao yetu ya taifa iliakisi moyo wetu wa umoja, ushirikiano na uchapakazi.

            • Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa kiongozi wa awamu ya kwanza (1961 - 1985). Uongozi wake ulijitahidi kujenga jamii ya watu walio sawa na huru kupitia siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Japo siasa yake ilishindwa; na anakiri kwamba serikali yake ilifanya makosa, kiongozi huyu aliishi maisha ya kiadilifu sana na mpaka leo bado anaonwa kama kiongozi bora ambaye alihubiri na kutenda alichokihubiri. Alijali maisha ya Watanzania wa kawaida. Wengi wanamkumbuka!


            • Mwaka 1964 na chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Tanzania. Muungano huo, japo uko kwenye hatihati, ungalipo mpaka leo hii. Ni moja kati ya vitu ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa anajivunia sana!


            • Baada ya Mwalimu Nyerere, ilikuja awamu ya pili (1985 - 1995) iliyoongozwa na Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi. Hiki kilikuwa ni kipindi cha misukosuko ya kiuchumi duniani na uongozi wake kidogo ulilegalega. Watanzania walimbatiza kiongozi wao Mzee Rukhsa! Sera ya serikali ilibakia kuwa ile ile iliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere - Ujamaa na Kujitegemea.


            • Awamu ya tatu (1995 - 2005) ilikuwa chini ya Mheshimiwa Benjamin William Mkapa - mwanafunzi wa Mwalimu Nyerere ambaye pia alisemekana kuwa na uadilifu na uchapakazi wa hali ya juu. Mwalimu Nyerere mwenyewe ilimbidi aende Chimwaga katika Mkutano Mkuu wa CCM kumpigania. Kiongozi huyu alikabidhiwa nchi ambayo haikuwa na nidhamu na maadili mema katika ukusanyaji wa mapato; na rushwa na ufisadi ulikuwa katika kiwango cha juu sana. Alileta nidhamu serikalini, ukusanyaji wa mapato na hakupenda mchezo. Inasemekana kwamba kwa kufanya hivyo alijijengea maadui hasa wale ambao walikuwa wamezoea ulaji katika awamu iliyopita. Kiongozi huyu anaandamwa na kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka yake. Ngoja tuone Historia itakavyomhukumu.


            • Awamu ya nne (2005 - ) ipo chini ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kiongozi kijana kuliko wote waliotangulia, mchapakazi na mwenye bashasha. Kauli mbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania vilileta msisimko mpya wa maendeleo kwa wananchi. Pamoja na kujitahidi kutekeleza kauli mbiu hii kwa vitendo, serikali yake imeandamwa na kashfa mbalimbali za ufisadi na mawaziri wake kadhaa walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao na wengine bado wana kesi mahakamani. Anategemewa kushinda kipindi cha pili katika uchaguzi mkuu mwaka kesho. Sera rasmi ya serikali bado ni Ujamaa na Kujitegemea na imani na ahadi za MwanaCCM bado ni zile zile.

            LEO TUNAPOSHEREHEKEA SIKU YA UHURU TUTAFAKARI:

            • Ati, kuna nchi ya ahadi ambayo tunajaribu kuifikia? Kama jibu ni ndiyo, nchi hiyo ikoje? Tunayo dira sahihi ya kutufikisha huko? Vipi kuhusu viongozi tuliowakabidhi majukumu teule ya kuandaa dira sahihi na kutuongoza kuelekea katika nchi yetu ya ahadi? Ni viongozi makini? Wanajua nchi yetu ya ahadi iliko? Kama wanajua, ni kweli wana lengo la kutufikisha katika nchi hiyo au wanatuzungusha jangwani tu? Tufanye nini?
            • Nyote nawatakieni sikukuu njema ya uhuru wa Tanzania. Mungu Aibariki nchi yetu nzuri yenye amani, upendo na utajiri wa kila aina.

            Tuesday, December 8, 2009

            JAMANI...NI MWISHO WA MUHULA...

            • Ni mwisho wa muhula (tunafunga shule kesho kwa wiki tatu) na kazi zimepamba moto kwelikweli. Hata wanafunzi wale wazembe na watoro sasa wako kila mahali wakiulizia watakavyoweza kupata kufanya vyema katika mitihani yao ya mwisho na hatimaye kuweza kupata alama nzuri. Kazi kwelikweli!
            • Nitarudi kama kawaida wiki kesho au baadaye wiki hii.

            Friday, December 4, 2009

            PADRI KARUGENDO NA UFUNUO WA MAGAZETI YA UDAKU

            • Padri Privatus Karugendo ni mmoja kati ya waandishi, wahakiki na wachambuzi makini sana wa masuala mbalimbali katika jamii yetu. Katika makala haya, anajaribu kuonyesha mchango chanya wa magazeti (yanayoitwa ya) udaku katika jamii na anatoa wito wa kuyaangalia magazeti haya kwa mtazamo mpya. Unakubaliana naye?
            **********************
            Magazeti ya udaku ama magazeti pendwa kama wenyewe wanavyotaka yaitwe duniani kote, yana sifa mbalimbali, ikiwemo kutangaza uongo na hata umbeya. Pamoja na ukweli kwamba magazeti ya aina hii nchini yanasomwa na wengi, bado tunayadharau na kufikiri kwamba yanasomwa na watu wasiokuwa makini.

            Kamusi ya Kiswahili sanifu inaelezea neno udaku kuwa ni tabia ya kutafuta na kutaka kujua habari za watu; kilimilimi na umbea. Kuyabatiza magazeti haya kuwa ya udaku, ni lengo zima la kutoa ujumbe kwamba haya ni magazeti ya umbea na uzushi.

            Hoja ninayoijenga katika makala hii si kununuliwa kwa magazeti au kutonunuliwa; bali ni kutaka kumshirikisha msomaji ufunuo nilioupata juu ya magazeti ya udaku. Mimi pia nilikuwa kati ya watu waliokuwa wakiyapiga vita magazeti ya udaku. Nimeandika makala nyingi nikipinga utamaduni wa watu kuacha kusoma vitabu na magazeti makini na kukimbilia magazeti ya udaku. Niliamini kabisa kwamba wale wote wanaoyasoma magazeti ya udaku si watu makini.


            Inawezekana kabisa nikawa sijafahamu vizuri sababu inayowasukuma watu kusoma magazeti ya udaku; na inawezekana kwamba pia wale wanaoyaandika magazeti ya udaku wana malengo na nia tofauti na ile niliyofunuliwa. Hata hivyo ukweli unabaki pale pale kwamba magazeti ya udaku yanaandika maswala ya jinsia kuliko magazeti tunayoita ni makini.


            Karibu magazeti yote ya udaku kurasa za mbele zinapambwa na masuala ya jinsi. Mifano ya magazeti haya na habari zinazoandikwa ni mingi. Inahusu wanasiasa kushiriki ngono; mafumanizi, ufuska wa kupindukia na nyingine nyingi. Ingawa hapa ninatoa mfano wa habari katika magazeti machache tu, ukweli ni kwamba karibia magazeti yote ya udaku yanaandika mambo ya jinsia na yaliyo tofauti. Kila gazeti linajitahidi kuibua kitu kipya ukitaka kufahamu hali ya jinsia ilivyo katika taifa letu la Tanzania, soma magazeti ya udaku.


            Wanaharakati wa kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi wanaharakati wa haki za binadamu na wanaharakati wote wanaotetea usawa wa jinsia watakubaliana na mimi kwamba niliyoyataja hapo juu ni masuala ya jinsia. Ni nadra sana kuona magazeti makini yakibeba maswala ya jinsia kwenye kurasa za mbele. Ikitokea wakiwemo ni katikati na yanapewa nafasi ndogo kinyume na yanavyofanya magazeti ya udaku.

            Inawezekana kwamba ni habari hizo zinakuwa zimeandikwa na kuchunjwa na wamiliki au na hata serikali. Habari nyingine zinachujwa na viongozi wa dini na zile ambazo ni nyeti zaidi, zinafunikwa na kufichwa kabisa hadi kristo atakaporudi mara ya pili! Nchi nyingi zilizoendelea zimeheshimu na kukumbatia usawa wa kijinsia.


            Magazeti tunayoita makini yanaandika habari za siasa za wanasiasa na matukio yanayowahusu wanasiasa hasa katika kurasa zile za mbele. Haina maana kwamba haya nayo si muhimu katika jamii. Ila ni kwamba magazeti yale tunayoyaita makini hayazingatii habari za jinsia.


            Pia waandishi wa magazeti haya tofauti na ilivyo kwa magazeti ya udaku, hawajitumi kutafuta habari kwenye vyanzo mbalimbali. Mara nyingi wanajikita kwenye vyanzo vya kiserikali; kusubiri pale maelekezo au kusubiri mikutano ya viongozi wakuu na waandishi wa habari. Pia wamejenga utamaduni wa kutafuta habari za matukio mbalimbali kama vile vifo, kupigwa, kubakwa kutoka kwa makamanda wa polisi wa wilaya na mikoa.

            Matokeo yake ni kwamba haya magazeti yetu makini, ukisoma moja, huna haja ya kusoma jingine. Wakati mwingine unakuta karibia magazeti yote yana habari ile ile kwenye kurasa za mbele.


            Hata ukisoma kurasa za ndani unakuta habari zinafanana. Kwa wale wanaosikiliza mapitio ya magazeti kwenye runinga watakubaliana na hoja yangu maana anayepitia magazeti akishasoma habari za gazeti linalotangulia, anabaki kusema habari hii imejirudia karibia katika magazeti yote” jambo hili linaeleweka vizuri, maana magazeti haya vyanzo vyao vya habari ni vilevile. Hawatafuti habari, wanasubiri kuletewa habari. Wanasubiri kuambiwa ni lipi la kuandika na lipi la kuacha. Kwa njia hii wanajikuta wanayaweka masuala ya jinsia pembeni.


            Magazeti ya udaku hata yote yakitoka siku moja ni vigumu yawe na habari zinazofanana. Waandishi wao wanatafuta habari. Hawategemei kupata habari kutoka maelezo au kusubiria viongozi au watu maarufu katika taifa letu. Wanaingia ndani ya jamii na kutafuta habari zinazogusa maisha ya watu. Wanaibua mambo mengi ya jinsia. Wanaibua ukatili majumbani, wanaibua vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanayofanyiwa wanawake na watoto, wanaibua matendo ya udanganyifu katika ndoa, wanaibua rushwa ya ngono, kwa kifupi wanaibua mambo yote yanayokwenda kinyume na maadili.


            Ni kiasi gani yale yote yanaibuliwa na magazeti ya udaku yanafanyiwa kazi, ni swali la kujiuliza, ni kiasi gani yanayoibuliwa yana ukweli, pia ni swali la kujiuliza. Je, mashirika ya kutetea haki za binadamu, mashirika ya harakati za kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi ni kiasi gani wanatumia habari za udaku kuimarisha mapambano yao na mfumodume? Je, na wanaharakati wanayanyanyapaa magazeti ya udaku? Wanayanyanyapaa magazeti yanayoandika na kuibua masuala ya jinsia?


            Swali jingine, ambalo nimeligusia mwanzo mwa makala hii ni kiasi gani wamiliki na wahariri wa magazeti ya udaku wanafahamu umuhimu wa habari wanazoziandika? Ni kweli kwamba wanaandika habari hizi kuibua masuala ya kijinsia au imetokea tu bahati mbaya wakati wakiwa kwenye harakati za kutafuta fedha? Au walifanya utafiti na kugundua kwamba vijana wengi wanapenda kusoma habari zinazoelezea mahusiano ya mwanamke na mwanaume? Habari za mapenzi,, habari za ngono na mambo yote yanayofanana na hayo? Vijana ni wengi – hivyo biashara ni kubwa?


            Je, wanaandika kuuza magazeti yao? Ili wapate fedha na kuwa matajiri? Kuwa matajiri kuisaidia jamii au kuwa matajiri kwa faida yao na familia zao? Au wanaandika kufundisha jamii? Wanaandika kuibua masuala ya jinsia kwa lengo la kusambaratisha mfumo dume ili kuleta usawa wa kijinsia? Wanaandika kwa vile wao ni wanaharakati au nao pamoja na kuandika kwa vile wao ni wanaharakati? Au nao pamoja na kuandika majumbani kwao wanaendeleza mfumo dume?

            Kuna haja ya kuyaangalia magazeti ya udaku kwa mtazamo mpya! Hata kama wanaoyaandaa wana malengo megine, lakini yale wanayoyaibua kuna haja ya kuyafuatilia; kuna haja ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini ukweli. Kwa njia hii kuna haja ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini ukweli. Kwa njia hii tunaweza mchango mkubwa katika kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu na kuzingatia usawa wa jinsia.


            Wakiandika juu ya fumanizi, tukio hili lifuatiliwe. Wakiandika juu ya ukatili majumbani kwa vile wanatoa majina ya watu na wakati mwingine maeneo ya tukio, ni vyema matukio haya yafuatiliwe kwa karibu. Wakiandika juu ya rushwa ya ngono, jambo hili lifuatiliwe.

            Wakiandika juu ya wabunge wetu kuwa na nyumba ndogo kule Dodoma kuwasafirisha watoto wadogo hadi Dodoma ili kufanya nao vitendo vya ngono, jambo hili lifuatiliwe ili waheshimiwa wetu wawajibishwe na kusaidiwa kuyabadilisha maisha yao.
            Wakiandika juu ya waheshimiwa wabunge kununua dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa wingi wakati wa vikao vya Bunge, jambo hili lifuatiliwe. Kwa nini wabunge wetu wahitaji nguvu za kiume kufanya tendo la ngono wakati wako mbali na familia zao? Bungeni wanahitaji nguvu za kufanya kazi? Lolote litakaloandikwa na udaku lifuatiliwe, hasa kama linaibua habari za jinsia.

            Chanzo: Global Publishers

            Thursday, December 3, 2009

            SHIDA YA MAJI YA KUNYWA VIJIJINI - TATIZO LA KUJITAKIA?

          • Swali hili limezuka baada ya kuyasoma maoni ya Profesa Mbele hapa; na kuziona hizi picha.
          • ARE MEN WIRED TO CHEAT? - SASA NI ZAMU YA TIGER WOODS!!!

            • Tiger Woods - mwanamichezo tajiri kuliko wote duniani na anayeheshimiwa sana kutokana na maisha yake ya faragha, kujali familia, utayarifu wake wa kusaidia masikini, upendo na msimamo wake usiotetereka, moyo wa kishujaa wa kushindana; na kutokubali kushindwa hatimaye naye ameangukia katika mtego ambao umeshawaangusha watu wengi "mashuhuri/macelebrity" hapa Marekani - kutembea nje ya ndoa.

            • Tangu apatwe na ajali ya gari ya kutatanisha nje ya nyumba yake tetesi zilianza kuzagaa kwamba kilichomletea majeraha usoni si ajali ya gari bali ni mkong'oto kutoka kwa mkewe.

            • Muda si muda zikaibuka tetesi kwamba Tiger ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mmoja anayekaa New York. Mwanamke huyo alikana shutuma hizo lakini mwingine akaibuka na kudai kwamba kweli yeye ni nyumba ndogo ya Tiger, na amekusanya barua pepe na "text messages" alizokuwa akitumiwa na Tiger. Ujumbe mmoja kutoka kwa Tiger unasema "I will wear you out...when was the last time you got (***?). Mwingine unasema "Send me something very naughty...Go to the bathroom and take (a picture)." Soma habari zote hapa na hapa.
            • Watu walikuwa wanachukulia habari hizi kuwa ni udaku tu lakini maelezo ya Tiger mwenyewe ambayo ameyaweka katika tovuti yake yamethibitisha kwamba baadhi ya tuhuma hizi ni za kweli na hii imezua sokomoko kweli.
            • Swali ambalo watu wengi wanajiuliza ni hili: Kwa nini mtu mashuhuri na anayeheshimika kama Tiger aamue kutembea nje ya ndoa wakati akijua kabisa kwamba jambo hili litajulikana na kumharibia kila kitu? Ni lazima kutembea nje ya ndoa?
            • Kwangu mimi swali hili ni la kipuuzi kwani "macelebrity" hawa ni watu tu wa kawaida tu, tena wanaowindwa na kila mwanamke kwa sababu wanaonwa kama njia rahisi ya kujipatia utajiri na umaarufu. Kama akina "baba askofu" - watu ambao wameandaliwa na kufundwa kwa miaka mingi kuyashinda majaribu ya aina hii - wanaanguka katika majaribu haya, sembuse hawa "macelebrity?"
            • Zamani kidogo niliweka katika blogu hii utafiti wa kisayansi ulioonyesha kwamba kutembea nje ya ndoa kwa wanaume siyo jambo la kushangaza kwani binadamu ni mnyama na wanyama wote wana hulka hii (SOMA HAPA). Wanasayansi wanasema kwamba kuna mnyama mmoja tu ambaye ndiye amethibitika kwa asilimia 100 kuwa na mwenzi mmoja tu katika maisha yake yote - mnyoo fulani unaoishi katika matamvua (gills) ya samaki. Sijui kama akina Yasinta, Koero na Mwanamke wa Shoka wanakubaliana na matokeo ya utafiti huu. Kazi ipo!

            Tuesday, December 1, 2009

            MAUAJI YA MAALBINO - AIBU KUBWA KWA TANZANIA NA UTANZANIA WETU

            • Baadhi ya mambo yaliyotajwa katika makala hiyo:

            • -Kuna zeruzeru wapatao 7,000 nchini Tanzania.
              -Mauaji ya zeruzeru yalianza miaka miwili iliyopita.
              -Mpaka sasa zeruzeru wapatao 44 wameshauawa nchini Tanzania na 14 nchini Burundi.
              -Mwili mzima wa zeruzeru uliokatwakatwa unaweza kuuzwa kwa dola 75,000 (nauliza: mnunuzi ni nani? Waganga wa kienyeji kweli ni matajiri kiasi hiki au hii ni biashara ya "wenyewe?")
            • Kwa sisi Watanzania ambao tulikuwa tumezoea "kujimwambafai" na kujinadi kwamba nchi yetu ni ya amani na iliyobarikiwa kuwa na kiongozi makini aliyesaidia kulikomboa bara la Afrika na kupandikiza moyo wa upendo, mshikamano, utaifa na umoja miongoni mwetu, jambo hili linatia aibu sana.
            • Kwa vile wanafunzi wangu wanajua kwamba ninatoka Tanzania (nimeshatamba mara nyingi darasani nikijivunia Nyerere, Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Zanzibar, watu wapole, Kiswahili Sanifu, Ziwa Nyanza, amani na mengineyo), leo mwanafunzi mmoja katika darasa langu la Language in African Society aliniuliza swali kuhusu mauaji ya maalbino. Alikuwa ameisoma makala hiyo juu na hakuamini kama ni kweli na sasa alitaka kuhakikisha kutoka kwangu. Alitaka pia kujua kama masuala ya lugha yanachangia.
            • Ilinibidi nitoe maelezo ya kina (kuitetea Tanzania yangu) na kuliweka jambo zima katika muktadha wa kitabaka, umasikini, ukosefu wa elimu, ufisadi na hata utandawazi. Hii ilinichukua dakika 30 nzima na wanafunzi walikuwa na huzuni kweli. Kama Mtanzania, niliona aibu mno!. Hii ni karne ya 21 ambapo binadamu amepiga maendeleo makubwa ya kisayansi na kiteknolojia, na sisi bado tunawawinda Watanzania wenzetu kwa mapanga kama wanyama tena kwa sababu za kishirikina! Mwisho wa darasa baadhi yao walibaki ili kunipa pole.
            • Nilipowauliza kwa nini walikuwa wananipa pole, mwanafunzi mmoja anayependa sana Afrika na ameshatembelea Tanzania, Kenya, Uganda na Swaziland alisema hivi: "tunajua unaipenda sana Tanzania na bila shaka jambo hili linakuumiza" Alikuwa sahihi!
            • Japo mpaka leo sijui sababu hasa (ingawa nafikiri pengine umasikini, ujinga, ufisadi, utandawazi na tamaa ya utajiri wa kufumba na kufumbua ni baadhi ya sababu) zilizotufikisha katika janga hili, inabidi kama jamii tusimame kidete na kupambana kwa nguvu zote. Jambo hili ni AIBU SANA kwa kila Mwafrika, ni AIBU SANA kwa kila Mtanzania, ni AIBU SANA kwa kila "Homo Sapiens (kama kuna Homo Sapiens!)

            ATI, KWA NINI ULIAMUA KUANZISHA BLOGU?

            • Nimeiona hii katuni ikanifikirisha. Kila mmoja wetu ana sababu yake ya kuanzisha blogu: kuelimisha, kuburudisha, kutangaza biashara, kubadilishana mawazo, kutahadharisha, kukosoa, kupongeza, kujipatia umaarufu, kuipigania jamii, kuhakiki, kushambulia, kujiongezea kipato, kukomoa, kueneza mawazo kombozi (hata kama siyo), kutapanya mitazamo na mitindo bora ya maisha (hata kama siyo), ku....Ati, ni kwa nini wewe uliamua kuanzisha blogu? Ungali umemakinikia lengo lako la awali au umeshapogoka, ukalitelekeza lengo lako kuu na kufuata "mkumbo" ili pengine kuweza kuvutia wasomaji katika blogu yako?. Sina nia mbaya na msije mkanielewa vibaya Ni hii katuni tu imenifikirisha! Samahani!

            WATU 25 WENYE "AKILI SANA" KATIKA MWONGO HUU

            (1) Larry Page and Sergey Brin (Waanzilishi wa Google hapo juu)
            (2) Steve Jobs - Mwanzilishi-mwenza wa Apple (Iphone, Ipod...)
            (3) Steven Chu - Waziri wa Nishati wa Marekani, Mshindi wa Tuzo ya Nobel (1997) katika Fizikia.
            (4) Hillary Clinton - Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani
            (5) Muhammad Yunus (Bangladeshi) - Mkurugenzi wa Grameen Bank na mshindi wa Tuzo ya Nobel (2006)
            • Mwafrika pekee katika orodha hii ni Kwame Anthony Appiah - mzaliwa wa Ghana ambaye ameshika nafasi ya 13. Kwa sasa ni Profesa wa Falsafa katika Chuo Kikuu cha Princeton.
            • Manmohan Singh - Waziri Mkuu wa India ameshika nafasi ya 11. Tazama orodha kamili hapa. Bofya kwenye kisanduku cha "View all" chini kushoto.

            Orodha hii imeandaliwa na Wamarekani na hatuambiwi ni vigezo gani vilivyotumika. Kama tungeandaa orodha ya watu 10 wenye "akili sana" nchini Tanzania kwa miongo sita iliyopita (yaani tangu tupate uhuru), orodha hiyo ingekuwaje? Vigezo?

            JIANDIKISHE HAPA

            Enter your email address:

            Delivered by FeedBurner

            BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO