NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, January 11, 2010

BINADAMU NA TAMAA YAKE YA KUJIFURAHISHA - ATI, KWA NINI UNAPENDA MCHEZO UUPENDAO?


  • Katika ung'amu fiche (subconscious) wake, nadhani binadamu anafahamu kwamba ana muda mfupi sana hapa duniani. Kutokana pia na ukweli kwamba anakoenda baada ya kukamilisha safari yake hapa duniani hakueleweki, inamlazimu ajifurahishe kwa kadri inavyowezekana wakati akiwa hai hapa duniani.
  • Pengine hii ndiyo sababu mojawapo iliyomfanya agundue michezo mbalimbali. Michezo mingi ya binadamu ukiichunguza vizuri hata unashindwa kupata maana yake hasa ni nini. Chukulia kwa mfano soka - mchezo nambari wani duniani. Watu ishirini na wawili wanashindania kitu cha mviringo na yule anayefanikiwa kumzidi mwenzake na kukiingiza kitu hicho cha mviringo kwenye nguzo mbili zilizosimikwa ardhini, basi anakuwa amefunga goli. Hapo tena binadamu hushangilia na kurukaruka kwa furaha isiyopimika na wengine huwa hawali wala kulala, na wale sugu wapo tayari hata kupoteza maisha yao ili kutetea timu zao wazipendazo.
  • Hebu ichunguze vizuri michezo mingine mfano "golf", mpira wa kikapu, mpira wa magongo, 'baseball', rugby na mingineyo. Kwenye ''golf", mtu anagonga kampira kadogo keupe kwa kutumia gongo maalum na kukaingiza kwenye kashimo kadogo. Wallah! Makofi na vigelegele...Binadamu anatumia mamilioni ya dola katika kujifurahisha na wachezaji ndiyo watu wanaoongoza kwa kulipwa vizuri!
  • Michezo niipendayo mimi ni ile ambayo kwa kiasi fulani inamwonyesha binadamu kama mnyama. Hii kidogo inamwondolea binadamu lile kunguku lake la U-homo Sapiens na "utakatifu" wake; na kuuanika unyama wake hadharani. Nadhani ndondi/masumbwi unaangukia katika kundi hili. Hali kadhalika "Bull Riding". Waweza kunishangaa lakini ukweli ni kwamba binadamu bado ni mnyama na matendo yake mengi yanathibitisha dai hili. Niambie - kwa mfano - inawezekanaje "binadamu" fisadi aibe "vijisenti" vyote vya umma, yeye na familia yake wawe matajiri wa kutupwa na kuwaacha binadamu wenzake waliompa madaraka wakiwa masikini hohehahe kabisa wasiojua hata watakula nini? Unataka kuniambia kwamba mtu huyu kweli ni "Homo Sapiens?". Huwa anahisi na kufikiri nini anapowaona watu aliowaibia wakihangaika katika umasikini na ukosefu wa huduma za msingi? Tazama vizuri halafu uniambie - ubinadamu na U-homo Sapiens wa binadamu uko wapi?
  • Waroma wa kale wao walijenga Colosseum - mtangulizi wa viwanja vya kisasa vya michezo - ambamo inasadikiwa kwamba wapiganaji mashujaa (gladiators) na binadamu wengine wapatao laki tano (500,000) pamoja na wanyama zaidi ya milioni moja walipoteza maisha yao katika michezo ya kutisha iliyokuwa inachezwa humo.
  • Hivi karibuni kumezuka mchezo mpya ambao unaupiku ule wa masumbwi kwa ukatili na unyama wake (tazama video ya kwanza hapa chini). Katika mchezo huu, hata ukimwangusha mpinzani wako, unaruhusiwa kuendelea kumporomoshea mangumi na mateke haidhuru hata kama ameshafleti!
  • Kutokana na ukweli kwamba mchezo huu umeinukia kuwa maarufu sana kwa muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake, ni wazi kwamba binadamu wenye shauku ya kuona unyama wa binadamu ukianikwa kama mimi ni wengi. Ati, wewe unapenda mchezo gani? Unajua ni kwa nini unaupenda mchezo huo?
***************************************

Rampage Jackson - Yeye huwabeba wapinzani wake na kuwabamiza chini!Hapa "Homo Sapiens" anahangaika na madume ya ng'ombe

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU