NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, January 15, 2010

EUPHRASE KEZILAHABI, KAPTULA LA MARX NA SAFARI YETU YA KUELEKEA NCHI YA USAWA

 • Kaptula la Marx ni tamthiliya makini dhati iliyoandikwa na Euphrase Kezilahabi (aka Shaaban Robert wa pili) zamani. Inasemekana kwamba tamthiliya hii ilimletea matatizo na ilipigwa marufuku kuchapishwa nchini Tanzania.
 • Baada ya miaka mingi ya ukiritimba wa chama kimoja na udumishaji wa fikra “sahihi” za mwenyekiti wa chama hatimaye tamthiliya hii ilichapishwa mwaka 1999 na Dar es salaam University Press (DUP). Nilifurahi nilipoiona katika maktaba hapa chuoni, nikaiazima na ndiyo tu nimemaliza kuisoma. Sasa najua ni kwa nini tamthiliya hii ilikaa katika makabrasha ya wachapishaji kwa muda mrefu.
 • Katika Kaptula la Marx kuna safari ndefu ya kwenda katika nchi ya ahadi – nchi ya usawa. Safari hii inaongozwa na Rais Kapera akiungwa mkono na mawaziri wake wote. Njia ya kwenda katika nchi ya usawa, hata hivyo, ni nyembamba sana na mawaziri wake ni wanene futufutu kiasi kwamba wanapata shida kutembea katika njia hiyo.
 • Raisi Kapera ameamua kuvaa kaptula kubwa la Marx ambalo kusema kweli halimwenei sawasawa na anaonekana kama kichekesho. Isitoshe, rais huyu pamoja na mawaziri wake hawajui kabisa njia ya kuelekea katika nchi hii ya usawa na hawana ramani. Kwa hivyo wamepotea.
 • Hatimaye linatokea jitu refu pandikizi linalojiita mtu jitu au beberu. Jina kamili la jitu hili ni KORCHNOI BROWN. Rais na mawaziri wake wanaliuliza kama linafahamu njia itakayowafikisha katika nchi ya ahadi – nchi ya usawa. Jitu hili linamhakikishia rais na mawaziri wake kwamba linaifahamu njia hiyo na linawapa maelekezo yafuatayo:
“Mtakwenda! Halafu mtapinda, mtapinda tena, halafu tena mtapinda, mwishowe mtapindapinda hadi mtakapofika mabonde yenye matope. Mtapita katikati ya matope. Halafu milima, halafu misitu yenye miiba hadi mtakapofika jangwani. Kutoka jangwani mtaingia tena bondeni chini kwa chini hadi baharini. Hakuna mitumbwi wala ngalawa. Mtaogelea, ingawa kuna papa wengi. Mkishavuka mtafika nchi iitwayo Svoboda. Kabla ya kuondoka katika nchi hii itawabidi kupambana na majitu yanayofanana na mimi. Mkitoka hapo mtafika kwenye njia nyembamba. (Akiwaonyesha mawaziri) Hawa hawatapita hawa! Njia hiyo itawafikisha katika nchi iitwayo Fraternite. Kutoka Fraternite mtafika Usawa. Ulizeni tu watu watawaonyesha! Mkifika Usawa mtawakuta Waswahili wenzenu wameketi nje ya ikulu ndogo ya Ravensto” Kaptula la Marx (uk). 20)
 • Kwa hivyo usishangae ni kwa nini baada ya miongo mitano ya uhuru bado hatujaifikia nchi ya ahadi. Inavyoonekana safari yetu ya kuelekea katika nchi hii ilikuwa ndiyo-siyo hata kabla haijaanza. Usishangae kama Ujamaa na Kujitegemea bado ndiyo falsafa na dira yetu elekezi ya kutufikisha katika nchi ya ahadi. Usishangae kama ahadi za wanachama wa chama cha Rais Kapera bado ni zile zile. Usishangae kama kinachoropokwa na wenye mikrofoni leo hakifanani na matendo yao. Usishangae kama "fraternite” ya watu wachache wanaofaidi maziwa na asali ya nchi ya usawa “kwa niaba” ya walio wengi inazidi kuimarika na kujitandaza. Usishangae kama (kama anavyosema George Orwell katika riwaya yake ya Shamba la Wanyama), wanyama wote ni sawa lakini wanyama wengine ni sawa kuliko wanyama wengine. Usishangae………..!
*******************************
 • Msikilize Euphrase Kezilahabi hapa chini akisoma mojawapo ya shairi lake; na huyu mwanafunzi akisoma shairi la Chai ya Jioni ambalo limo katika diwani ya Kezilahabi ya Karibu Ndani.
14 comments:

 1. Mwalimu; vitabu vizuri kama hivi na sisi tunaweza kuvipata wapi? hasa kopi ambazo tunaweza kuzisoma kwenye kompyuta yaani "soft copy" hasa tulio mbali na nchi yetu ya Tanzania ambako kuna uwezekano kwamba vinauzwa mitaani.

  Ahsante na nakutakia siku njema.

  ReplyDelete
 2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 15, 2010 at 4:45 PM

  Matondo: Ujamaa na kujitegemea ni dhana tu. Unadhani hizo imani na ahadi zinatekelezeka?

  Kuna waziri mkuu mmoja baada ya kutoka Havard akasema kuwa SASA ANAJUA KWA NINI TUKO MASKINI. Mkubwa wa pale IKILU ya Magogoni naye akihojiwa na waandishi wa habari wa nje (ambao wanawathamini kuliko wa ndani) akadai kuwa hajui ni kwa nini Tz ni masikini.

  MANAKE NI KUWA: Tunaongozwa na watu wasiojua tunaelekea wapi achilia mbali kwa nini tuko maskini. matokeo yake utasikia mkubwa fulani anajenga/jengewa hotel ya kitalii serengeti, ngorongoro nk

  kwa ajili ya nani wakati muda wake wa kuishi ni mdogo na wanawe karibu asilimia 98 ni wabwia unga? :-(

  INAUMA SANA. Japo sijakisoma ulichituonjesha kinatosha tusije wengine kujinyonga kwani tuna hasira kama shemeji zangu Iringa :-(

  ReplyDelete
 3. Wacha mzee hapa ni barafu ya kufa...

  NY, NY!!!
  Baridi Kichizi!!

  ReplyDelete
 4. SHAIRI HILI LACHAI YA JIONI SIJALIELEWA LIKO KIFALSAFA SANA. ULIKUWA UNAMAANISHA NINI?
  LIZ CHALY

  ReplyDelete
 5. Prof Matondo, ninalitafuta sana hilo Kaptula La Marx. Kesho ninatarajia kwenda duka la vitabu pale Chuo Kikuu Mlimani kulisakanya nami nilisome maana ni shabiki mkubwa wa Kezilahabi.

  ReplyDelete
 6. Fadhy - hapo Mlimani utakipata bila shaka.

  Ndiyo Kezilahabi ni mwandisho bora. Ndiyo maana Profesa Senkoro akambatiza jina la "Shaaban Robert wa Pili"

  Kwa bahati mbaya tumemwachia amekwenda Botswana. Nadhani ametoa kitabu kingine cha mashairi (ana Kichomi na Karibu Ndani). Hebu ulizia hapo Mlimani halafu unitonye kama ametoa vitabu vipya.

  ReplyDelete
 7. hakuna shaka. Kezilahabi nilianza kumsoma kwenye Mzingile na Nagona nikiwa kidato cha kwanza. Miaka sita ilopita nilipata Kichwa Maji. hadi leo hurudia kuisoma kichwa maji kwa kuwa inazidi kunivutia utadhani imeandikwa hivi karibuni.
  leo ndo nimegundua kupitia Wikipedia kuwa sasa anafanya kazi Botswana.
  sijui kwa nini bidhaa adimu kama zile tunaziacha zikawanufaishe wengine.
  hakika naungana na Senkoro kumwita Kezilahabi Shaaban Robert II.
  nitakufahamisha juu ya vitabu hivyo.

  ReplyDelete
 8. Fadhy - Nagona na Mzingile ulimwelewa Kezilahabi alikuwa anasema nini? Japo ni vi-novela vinavyoonekana kutokuwa na mbele wala nyuma, vimeleta changamoto kubwa sana na vimebadili kabisa taaluma nzima ya uhakiki ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa imedumaa.

  Ukitaka kuvihakiki vi-novela hivi pengine itakubidi kwanza usome mikondo mikuu ya Falsafa na hasa tapo la Existensialism na Elimu Nafsiya ya Sigmund Freud. Ndipo tu utakapoweza kufuatilia mazungumzo kati ya Ego, Super ego na wahusika wengineo.

  Kama ana kitabu kipya ambacho ameshachapisha basi nijulishe.

  ReplyDelete
 9. Ndugu yangu, professa nimeyasoma maelezo yake mafupi kuhusu kitabu cha Kezilahabi; kaptula la marx. Natamani sana kukipata lakini mazingira niliyopo si rahisi kukipata. Tabaka tawala haipendi vitabu vyenye mawazo ya kimapinduzi kama hivi vya akina kezilahabi visomwe na watoto wa wasakatonge kwani vitawatia hamasa ya kufanya mapinduzi. Na kweli ni ngumu kwa watoto wa wasakatonge wanaosoma katika shule za kata ambazo ama hazina vitabu kabisa au ina vichache. Tabaka tawala linapenda watoto wa maskina wajengewe ukuta unaowatenganisha na watoto wa wakubwa. Hata katika taasisi za elimu wanafunzi wanafundishwa unyenyekevu kwa watawala na kwa hiyo wanaandaliwa kuwa wasomi waoga ambao hawataweza kuthubutu kukosoa mfumo wa utawala usio wajali wanyonge.Kwa hiyo sishangai ninapoona watu kama akina kezilahabi wenye vipaji muhimu wanapoenda ng'ambo kwani serikali haiwataki watu kama hao wenye mawazo ya kimapinduzi yanayohatarisha maslahi yake. Kwa hali hiyo ni vigumu sana kupata maendeleo katika nchi kama hiyo ambayo inazika fikra za kimapinduzi za wasomi ambao ndio tegemeo la wanyonge. Lakini hata hivyo serikali lazima itambue kuwa kwa kufanya hivyo ndiyo inajihatarishia usalama wake kwani wanyonge hawatavumilia kunyonywa na kunyanyaswa kwa muda wote. Hakuna mtanzani maskini atakayevulia tatizo la mgawanyo usio sawa wa rasilimali ya nchi. Haiwezekani mbunge moja alipwe mil. 12 kwa mwezi na dereva wake alipwe laki nne kwa mwezi kiasi ambacho ni mara mbili ya mshahara wa mwalimu wa diploma. Wakati huo wasakatonge wa tanzania wanalipa kodi lakini hawapati huduma bora za afya na elimu. Kodi zao zinawafaidi watawala. Kama tulivyosikia siku za hivi karibuni eti kila mbunge anapewa sh.mil.90 kwa ajili kununulia magari. je, pesa hizo zingetumika kuboresha huduma za afya na elimu si ingekuwa bora?

  ReplyDelete
 10. naitwa barnaba bukhu khaday, mwanafunzi wa stashahada ya ualimu wa mwaka wa pili marangu ttc

  ReplyDelete
 11. MIMI NAOMBA KWA KUWASAIDIA WATANZANIA TUNGEPATA SOFT COPY KWENYE MTANDAO

  ReplyDelete
 12. KITU KINGINE MH. PROFESA KEZILAHABI UJUNZI NA ELIMU YAKO NI MUHIMU SANA KWETU.MIMI NAONA BORA URUDI UFUNDISHE NYUMBANI ILI KUJENGA MISINGI YAKO KWANI TUNAKOSA MAARIFA YAKO.TUNAHITAJI WATU KAMA NINYI ILI KUBORESHA ELIMU KATIKA VYUO VYETU.

  ReplyDelete
 13. Wadau karibuni kusoma http://sw.wikipedia.org/wiki/Kaptula_la_Marx !

  ReplyDelete
 14. Prof. Euphrase Kezilahabi ni moja ya waandashi wa kiswahili oendwa kabisa kwa uande wangu, nimeweza kusoma vitabu vyake kama KICHWA MAJI, DUNIA UWANJA WA FUJO, ROSA MISTIKA, KAPTULA LA MARX PAMOJA NA diwan yake ya KARIBU NDANI ... MWAKA huu nimeweza kufika mpaka kwao kijiji cha Namagondo kijiji ambacho amekitumia katika kazi yake ya ROSA MISTIKA nilipokirudia kukisoma nilifurahi sana maana nilijikuta narudi ukerewe kifkra

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU