NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, January 29, 2010

FIKRA YA IJUMAA - MFULULIZO MPYA (KWA WAPENDAO KUFIKIRI)

 • Kuanzia sasa kila Ijumaa nitakuwa nabandika hapa "fikra" au wazo la kufikirisha. Safu hii mpya itakuwa inaitwa "Fikra ya Ijumaa". Fikra hii inaweza kuwa katika umbo la swali au nathari na inaweza kuhusu falsafa, dini au maisha tu kwa ujumla. Karibuni tunoe ubongo!

 • Leo napenda tuanze na Epicurus na maoni yake kuhusu kifo. Yeye alikuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi kati ya mwaka 341 na 270 K.K. na ambaye alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sayansi kutokana na mafundisho yake ya kutoamini vitu hovyo hovyo hata kabla ya kuvipima na kuvichunguza sawasawa.
 • Kulingana na Epicurus, lengo kuu la falsafa lilikuwa kuleta furaha na maisha ya utangamano – maisha yasiyo na maumivu wala hofu ambayo aliyaita maisha yenye aponia.
 • Kuhusu kifo alifundisha kwamba kifo kilikuwa ndiyo mwisho wa mwili na roho na kwa hivyo hakipaswi kuogopwa. Hebu fuatilia hoja kuu za Epicurus kuhusu kutoogopa kifo hapa chini.
 1. Unapokuwapo kifo chako hakipo; na kisichokuwepo hakiwezi kukudhuru
 2. Kifo chako kinapokuwepo wewe haupo; na kisichokuwepo hakiwezi kudhuriwa
 3. Ni upumbavu kuogopa ambacho hakiwezi kukudhuru
 4. Ni upumbavu pia kuogopa ambacho hakiwezi kudhuriwa
 5. Katika wakati wo wote ule ama wewe unakuwepo au kifo chako kinakuwepo
 6. Kwa hivyo katika wakati wo wote ama kifo hakiwezi kukudhuru, au huwezi kudhuriwa na kifo.
 • KWA HIVYO (anahitimisha Epicurus): Ni upumbavu katika wakati wo wote ule kuogopa kifo!
 • Baada ya kufuatilia kwa makini hoja hizi za Epicurus, unakubaliana naye? Unakiogopa kifo? Hii ndiyo fikra ya kwanza ya Ijumaa hii!!! Muwe na wikiendi njema!

8 comments:

 1. naweza kukubaliana naye kwa masharti fulani fulani au maelezo fulani juu ya kifo. ila nakubaliana na ufundi wa hoja alioutumia juu ya kilichopo na kisichokuwepo.

  iogopi kifo kwa sababi ni haki yangu ya msingi sana, lakini kifo changu kimeshapangwa!!! najiaminisha (ndivyo ilivyo) kuwa maisha nje ya mwili ni mazuri saaana kwa hiyo kufa nifuraha. siwezi kujiua kwani sio jukumu langu kufa ila niko tayari kufa

  ReplyDelete
 2. Nafikiri wengi hawaogopi kifo , ila waogopacho ni kile wakioanishacho na kifo, ikiwa ni mpaka Jehanamu kwa baadhi ya wafuatao dini zenye Mbinguni na Motoni.

  Na wale waaminio ukifa unazaliwa kama kiumbe kingine (Reincarnation) wanaogopa kufa kwa kutokuwa na uhakika watazaliwa tena kama Panya au Paka au tu kitu kingine ambacho chaweza kuwa kwa fikira zao za kibinadamu wanahisi ni kibaya zaidi ya walivyokuwa Binadamu.

  Nafikiri ni hofu tu ya yahusianayo na kufa na sio kifo chenyewe kitishacho watu.

  Kwa mfano tukichukulia Kifo cha KUJINYONGA:

  Naamini kufa hakuchukui hata sekunde na HAKINA MAUMIVU ingawa shughuli yenyewe ya kujinyonga yaweza kuchukuwa muda katika kifo cha kujinyonga na maumivu ya kifo cha kujinyonga yako katika KUJINYONGA na sio katika KIFO!

  Sijui kama naeleweka lakini!:-(

  ReplyDelete
 3. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 30, 2010 at 7:52 PM

  Mimi siogopi kufa ila naogopa kutangulia :-(

  ReplyDelete
 4. Dr. Motondo,
  sikubaliani baadhi ya maandishi ya Philosopher Epicurus, haswa kwenye suala la kifo, na pale anaposema kwamba "death should not be a cause of worry as when it would come we would not feel it." Bila shaka yeye alikuwa anaongelea natural death, kifo ambacho hufika kwa wakati wake, bila hata kutegemea. Hapa nadhani hakuna atakaye bishana na hilo. Lakini kama alivyosema Mr. Kituru, kuna baadhi ya vifo ambavyo, kwa mfano kifo cha kujinyonga/kunyongwa, vifo ambavyo vunatokana na maradhi ya muda mrefu na maumivu makali, ex. Ukimwi, au saratani na kifo cha kunywa sumu,hapa nadhani hata yeye mwenyewe angekuwa na mawazo tofauti.
  Kwa mfano, tukichukulia kifo cha Socrates, philosopher mwingine, labda maarufu zaidi kutoka Greece (Athenia) ambaye alilazimishwa kunywa sumu (Hemlock) baada ya kudaiwa kuwasaliti watu wake, kifo kama hicho, sidhani kama kuna mtu ambaye anaweza kukitayarishia shingo.
  Sababu nyingine, kwa mtazamo wangu, ni life expectancy ya wakati huo kule Ughiriki, ambako inaesemekana watu walikuwa hawazidi miaka 40 au 50, hii inamaanisha kwamba watu wengi walikuwa wanakufa wakiwa bado vijana. Kwa maisha ya sasa hivi, huo ni umri mdogo sana, ambao waathirika wengi wanatoka katika nchi maskini. Lakini nchi nyingi zilizoendeela, haswa kwenye group la OECD zikiongozwa na Japan, watu wanaishi mpaka miaka 100. Sababu zote hizi, nionavyo mimi, zimebadilisha maana, na umuhimu wa kifo kuliko ilivyokuwa zamani.

  ReplyDelete
 5. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 31, 2010 at 9:34 AM

  Anony, ukiwa na miaka 40 bado we kijana ama KIJEBA? :-(

  Unadhani kuishi miaka 100 kuna tija yoyote? :-(

  ReplyDelete
 6. Mr. Wambura sielewi wewe unaishi wapi, lakini katika nchi zilizoendelea, miaka 40 bado ni kijana sana, kwa sabau, kwa mfano nchi kama Canada, ambapo ndipo ninapoishi, life expectancy ni miaka 80.4. Mtu anaruhusiwa-kuretire akifikisha miaka 65, au early retirement at 62. Hivyo basi, kama una miaka 40, unatakiwa uendelee kufanya kazi kwa miaka 22 kabla hauchukua hiyo early retirement. Hii ndio sababu katika nchi nyingi zilizoendelea, umri wa miaka 40 ndio kwanza unaanza kutroti katika kusukuma gurudumu la maendelo. Hivyo katika kukomenti nilikuwa nazingatia kipengele hicho.
  Naweza kuelewa mantiki ya swali lako kulinganisha na hali halisi ya Tanzania, ambapo watu wanaretire officially wakifikisha miaka 55, yaani miaka 12 pungufu ya Canada, na ambayo ni karibia sawasawa na life expectanty ya Marekani miaka ya 1930s. Vinginevyo nakubaiana na wewe kwamba binadamu akifiksha miaka 40 au 50, anakuwa ameisha kula chumvi ya kutosha tu, ingawa hataweza kuwa sawa na mjapani ambae anguarantee ya kufikisha miaka 100.
  Ama kama kuishi miaka 100 ni tija, kwa upande wangu kama nilivyochangia kwenye swali la Dr. Matondo, nadhani ni tija, kwa sababu endapo 40 yrs ndio ulikuwa umri mrefu kabisa kwa wanachi wa Athenia, kwa hiyo, suala la kifo lilikuwa machoni mwao kila siku. Unakuwa ki-umri huku ukifahamu kabisa kwamba, pindi utakapoanza kuingia maturity age, ndio mwisho wa maisha yako. Hii inakupa mtazamo tofauti kuhusu maisha ya kawaida na kifo chenyewe. Lakini leo hii, japo tunafahamu kwamba kifo ni AULA, lakini wengi hatutegemei kufa kutokana na maradhi madogomadogo kama vile flu, au infection diseases ambayo ndiyo yalikuwa chanzo cha vifo vya watu wengi hapo zamani za kale. Hata wasomi wa sasa hivi katika nchi nyingi zilizoendelea, badala ya kuandika jinsi ya kupokea kifo kwa urahisi, suala ambalo pengine wataliachie viongozi wa kidini, wanaandika kuhusu jinsi ya kuwaangalia na kuwatunza watu wenye umri mkubwa, na ambao inaelekea itakuwa tatizo kubwa katika hizi jamii kutokana na mapinduzi ya KISAYANSI.


  KARUMANZIRA.

  ReplyDelete
 7. Dhana kubwa ya filosofa huyu nionavyo mimi ni kuwa "kifo na uhai haviwezi kuwa experienced kwa wakati mmoja" ukiwa unaishi, kifo hakipo,ukifa, huna uhai.Ila hofu ya kifo ipo palepale kwa kuwa kila mtu anajua ipo siku kifo kitamkuta na ataachana na dunia kabisa. Kama alivyosema Mtakatifu Kitururu,tafsiri ya baada ya uhai kutoka(mtu akisha kufa) inachangia sana kuleta hofu.

  Binafsi ninaona tamaa ya maisha ya duniani hapa huchangia sana ktk huleta hofu ya kifo. Wanaojinyonga binafsi naona hawaogopi kufa.

  ReplyDelete
 8. Anony hapo juu. Hoja nzuri. Nakubalia nawe kwamba kuna vifo vya kutisha na vya maumivu makali sana kama hivyo ulivyovitaja. Pia kutokana tu na hali inayomkuta mtu uhai unapomtoka - kuoza, kuliwa na mafunza na hatimaye kuwa mifupa ni mambo ya kuogofya.

  Unaonaje mantiki ya mwanafalsafa huyu na suluhisho lake. Pia, kama alivyosema Ng'wanambiti, sina uhakika kama kuna tija au tofauti yo yote kwa mtu anayeishi miaka 50 na yule anayeishi miaka 100. Kuna faida yo yote? Ipi?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU