NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, January 21, 2010

"HAKUKUWA NA UZAZI WA MPANGO BARANI AFRIKA KABLA YA KUJA KWA WAKOLONI" NI KWELI?

 • Jamani, naomba mnisaidie. Jana nilihudhuria semina ya mwanafunzi mmoja wa "Medical Anthropology" anayefanya utafiti wake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mojawapo ya dai kuu katika mhadhara wake ni kwamba eti hakukuwa na uzazi wa mpango barani Afrika kabla ya kuja kwa watawala kutoka Ulaya.
 • Kwa vile sifahamu cho chote kuhusu mambo haya, sikuweza kuuliza swali mbele ya halaiki lakini baadaye wakati wa mapumziko na vinywaji nilikwenda kuongea naye. Nilimuuliza kama hitimisho lake lilikuwa la ukweli. Nilimwambia kuhusu familia kule kijijini ambako watoto katika familia nyingi wamepishana miaka mitatu mitatu. Hiyo inawezekanaje kama akina mama wa kijijini hawajui cho chote kuhusu uzazi wa mpango? Nilimwambia pia kuhusu elimu ya jadi katika makabila mengi ambako mabinti waliwekwa ndani na kufundwa kuhusu mambo mbalimbali likiwemo hili la mimba na uzazi.
 • Aliniambia kwamba kitu pekee kilichokuwa kinawasaidia (na kinaendelea kuwasaidia) akina mama wa Kiafrika wasipate mimba za dabo dabo ni kunyonyesha. Aliniambia kwamba kunyonyesha kunapunguza uwezekano wa kupata mimba kwa asilimia 80 hasa katika miaka miwili ya mwanzo. Ndiyo maana katika familia nyingi alizozichunguza kule Kongo watoto wengi wamepishana miaka miwili miwili ambacho ndicho kipindi cha wastani cha akina mama kunyonyesha.

 • Aliendelea kuniambia kwamba uzazi wa mpango ni tata mno kiasi kwamba hata yeye (msomi) wakati mwingine huwa hana uhakika na "vipindi vyake vya hatari" - sembuse akina mama wa Kiafrika vijijini tena wasio na "elimu"? Sikupenda kumbishia bila hoja nzito na nilimwacha japo kwa shingo upande huku nikijiahidi kwenda kujisomea kuhusu suala hili na kisha nije nimtafute tena “tubishane”. Lakini pia nikafikiria kwamba pengine vitabu nitakavyovisoma vitakuwa vimeandikwa na watafiti kutoka nje ambao mtazamo wao ni tofauti na ule wa Kiafrika.
 • Ni kweli hakukuwa na uzazi wa mpango wa aina yo yote barani Afrika kabla ya kuja kwa wakoloni?

5 comments:

 1. Ni mjadala mzuri sana, nimesoma hapa huku nikiwa natabasamu. Sio kwamba nafurahia kwa vile hakukuwa na uzazi wa mpango hapana. Kuna program inaendeshwa hapa ni familia tatu ambao kila familia ina atoto kumi. Kwa mimi naona kama wana aina fulani ya homa kwa sababu ukiangalia na kuona jinsi wanavyoishi ni fujo tu. Sidhani kama wapo salama kwa maisha ya hapa. Nasema hivi kwani kwetu Afrika huwa tunasaidiana lakini hapa hawa kumi ni kazi yako mama/baba peke yako.

  ReplyDelete
 2. Profesa,nafikiriunajua kuwa watu hao hawana utafiti wa kina. Watu walikuwa na nia asili, na kalenda za asili. Kusema ni sababu ya kunyonyesha pekee ni uongo.
  Kwa ujumla njia za uzazi wa mpango sio maarufu sana Afrika kama watu wanavyozania.

  ReplyDelete
 3. Profesa, Matondo. Huyu mwanafunzi hakuwa mtafiti wa kweli, nadhani ameegemea zaidi kwenye proganda kuliko ukweli kuhusu suala zima la uzazi wa mpango katika jamii za kiafrika. Zamani katika jamii nyingi za kiafrika, mwanaume alikuwa haruhusiwi kufanya tendo la ndoa na mkewe hadi mtoto amefikisha miaka miwili,sasa huyu mtafiti anamaanisha nini kuhusu uzazi wa mpango? labda kwake uzazi wa mpango ni kutumia contraceptive pills pekee!!!!!!!!!!!!

  Hapo awali kwenye jamii nyingi za Kiafrika msichana akipata mimba kabla ya ndoa huwa anatenganishwa na jamii. Kuzingatia adhabu kama hii mimba za ovyo zilikuwa zikiepukika pamoja na kuwa wasichana na wavula waliruhusiwa kutembeleana kwa uwazi. Hapa namaanisha kuwa ilikuwa jambo la kawaida kwa nyumba yenye wasichana wengi, wavula huwa hutembelea nyumba hiyo kwa uhuru mkubwa, wazazi walikuwa na heshima, mara nyingine waliwapisha vijana kukutana na hata kulala pamoja na haikuwa rahisi kukutana kimwili. Cha kushangaza kasi ya mimba haikuwa kama ya sasa ambapo utamaduni wa mwafrika umevamiwa na ule magharibi.

  ReplyDelete
 4. Kwa kweli sina hoja ya msingi ila naona kuwa mafunzo mengi ya unyago na jando katika familia nyingi yalilenga kwenye afya ya mama ndo maana wengi waliweza kuishi miaka 90 na kuendelea!
  Je weliwezaje kuishi bila kubemendwa? utapia mlo? waliwezaje kuwa kati ya miaka 2 hadi mitatu kwa familia nyingi? Kondom zilikuwa hamna!!J P Ntisi

  ReplyDelete
 5. Edward Alex MkweleleJanuary 21, 2010 at 10:45 PM

  PROFESSOR, UZAZI WA MPANGO ULIKUWEPO KABLA YA KUJA KWA WAKOLONI KULIKUWEPO NA UZAZI WA MPANGO ULIARIBIWA NA HAO WAZUNGU WALIPOKUJA AFRIKA, KWANZA ZAMANI HATA KUOLEWA ILIKUWA WATU HAWAOANI/KUFUNGA NDOA/ARUSI WAKIWA WATOTO WADOGO KAMA ILIVYO SASA BAADA YA KUJA WAZUNGU, HATA NGONO ZILIKUWA HAZIFANYWI HADI SIKU YA KUOANA, ULIPOKUJA USASA ULIOLETWA NA HAWA WAZUNGU WATU WALIANZA NGONO HATA KABLA YA NDOA, PIA KULIKUWA NA MADAWA YA KIENYEJI YA KUZUWIA MIMBA, KWA MFANO BAADHI YA MAKABILA MWANAMKE AKIJIFUNGUWA HUWA ANAFUNGWA KWA DAWA ILI ASIPATE MIMBA HADI MTOTO AKUWE, KULIKUWA NA DAWA ZA KUCHANJA , ZA KAMBA KUFUNGA MKONONI, NA PIA HIYO YA KUNYONYESHA KWA MUDA MREFU, HATA HIVYO NI NINI DEFINATION YA UZAZI WA MPANGO, NI MUDA GANI MWANAMKE AKAE BAADA YA KUJIFUNGUA ILI APATE MTOTO MWINGINE, ASIJE AKACHANGANYA KATI YA KUZAA WATOTO WENGI NA UZAZI WA MPANGO KUZAA WATOTO WENGI HAINA MAANA SI UZAZI WA MPANGO, UZAZI WA MPANGO KWA KIDUCHU TU NI GAPS BETWEEN CHILDREN, FANYA UTAFITI TANZANIA KUTOKA KWA WAZEE WA ZAMANI WATAKUAMBIA UZAZI WA MPANGO ULIKUWEPO, KUNA SISTER MMOJA WA KIZUNGU YUKO NDANDA MISSION/HOSPITAL ANAITWA SISTER BRIGITA YUKO TANZANIA TOKA ENZI USICHANA WAKE ANAJIHUSISHA SANA NA MASWALA YA UZAZI NA UZAZI WA MPANGO WA JADI AMEENDIKA VITABU VINGI SANA TU NA HUWA ANAFANYA KONGAMANO YA MASWALA HAYO JARIBU KUFUATILIA HUKO NDANDA UNAWEZA KUMPATA. HATA HIVYO KWA SASA UKILINGAISHA AFRICA NA ULAYA UTAONA WAO NDO HAWAFUATI UZAZI WA MPANGO KWA SASA UKITEMBEA HAPA LONDON MITAANI UTAWAONA WATOTO WADOGO WA MIAKA KUMI NA MBILI WAMEBEBA WATOTO WAO NA AKIFIKA KUMI NA SITA TAYARI ANAWEZA KUWA NA WATOTO WATATU, NI TATIZO KUBWA KATIKA NCHI ZA MAGHARIBI WATOTO KUZAA WATOTO WENZAO, UK NA USA ZINAONGOZA.

  NI MIMI EDWARD ALEX MKWELELE edwardmkwelele@yahoo.co.uk

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU