NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, January 19, 2010

KUNA WAKATI KUTONGOZA ILIKUWA NI FANI.

 • Vijana wa siku hizi huita kushusha mistari. Wengine husema ni kuwa kwenye fani, kusomesha au kumwaga sera. Kwa Kiswahili sanifu ni kutongoza. Mpaka hivi karibuni, kwa kawaida, mvulana ndiye alikuwa anatongoza na msichana alikuwa akitongozwa.
 • Enzi zetu kule Usukumani ulihitajika utaalamu wa hali ya juu sana wa kushusha mistari kama kweli mtu ulitaka kuwa mkali kwenye “gemu” (msishangae, leo natumia lugha ya vijana tu!). Kwa upande wao, mabinti wa Kisukuma enzi zile nao hawakuwa “goigoi”; na kutongoza ilikuwa ni shughuli iliyohitaji ustadi na umakinifu wa hali ya juu. Mtu ilikuwa lazima ujiandae kabla hujamparamia binti na kuanza kumwaga sera zako. Na ilihitajika lugha maalum kwa lengo hili.
 • Lugha hii ilikuwa tamu na iliyojaa taswira, tashbiha, tashtiti na mbinu zingine zikiwemo misemo, methali, nahau na tamathali zinginezo. Ilikuwa ni lugha tajiri sana iliyoweza kuchora mawanda na mandhari ya kuliwaza; na kuweza kumhakikishia binti kwamba wewe ulikuwa ndiye! Ilikuwa ni lugha iliyoweza kumwingiza binti katika ulimwengu wa jazanda mpaka akalainika….
 • Kwa vile mimi nilichepuka mapema na kwenda shule ya sekondari mbali na nyumbani, sikupata bahati ya kuifahamu lugha hii sawasawa. Nakumbuka kila niliporudi kijijini wakati wa likizo rafiki yangu mmoja aitwaye Nkuba Guyambila Milyango alikuwa akijitolea kunifundisha lugha hii. Kwa upande wa barua, pale kijijini kulikuwa na bingwa mmoja wa erotographomania (uraibu wa kuandika barua za mapenzi) aitwaye Yohana Masingija Nkilonhiga Balila (R.I.P). Huyu alikuwa mtaalamu sana wa kutumia lugha hii maalum katika maandishi na vijana walikuwa wakimmiminikia ili awashushie mistari katika karatasi. Gazeti la SANI pia lilikuwa maarufu sana na vijana tulikuwa tunakariri karibu kila kitu kilichokuwa kinatokea katika Harakati za Pimbi.
 • Kwa sasa nadhani lugha hii imeshakufa au inakufa. Sasa uchumi umetawala na mtu haijalishi tena kama unajua kupanga mistari ama la. Kama una pesa, gari na unapiga pamba sawasawa basi hakuna neno. Mambo yamebadilika sana.
 • Kama mkereketwa wa masuala ya lugha na utamaduni, nimekuwa nikiwaza uwezekano wa kuihifadhi lugha hii katika maandishi kabla haijapotea kabisa. Ni lugha iliyobeba utamaduni mwingi na naamini kwamba litakuwa ni jambo jema kama itahifadhiwa. Naangalia uwezekano wa kufanya hivyo.
 • Nimeikumbuka lugha hii baada ya kuona “vibwagizo” kadhaa katika gazeti la wanafunzi. Baadhi yake vinasema hivi:
************************
 1. You should come with road signs. All those curves. And me with no brakes!

 2. You are really hot. You must be the reasons for global warming.

 3. If I had a rose for every time I thought about you, I would be walking through a garden for ever.

 4. You are so hot. You’d make the devil sweat!

 5. If being sexy was a crime, you would be sentenced to life in prison

8 comments:

 1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 19, 2010 at 10:51 AM

  Duh! Dkt. ni kweli hiyo mistari ya kilugha ishakwenda na utandawazi-wizi :-(

  huko usukumani sasa tunajifunza kiswahili ili kumridhisha binti; utamsikia njemba anajinadi 'pendo limekudondokea!' na ukiunganisha maneno hayo na lafudhi ya kisukuma ni burudani tosha :-)

  na hata wanapokubaliana ile lugha ya kisukuma sidhani inatumika kwani niliwahi kusoma pahala kwamba njemba ya kisukuma akitaka vituz anamwambia mwenziwe kuwa 'nataka kifua chako na changu kipambane' :-( Hiyo inamaanisha kuwa maneno yale uloyazungumzia hapo juu hayapo tena bali wanakopa kwenye kiswahili ambacho hata hivo hakina mashiko.

  ukija kwa wakurya ndo vurugu tupu :-(
  Naona aibu kuendelea :-)

  ReplyDelete
 2. Ng'wanambiti - unazungumzia Chagulaga nini? Hiyo ya vifua kupambana imenichekesha.

  Ninayoikumbuka mimi ilikuwa lugha nzuri sana...ngoja nitaandika kimakala kifupi nikaweke hapa uone....

  Wakurya mnajulikana kwa ukali na hata Wasukuma nadhani tunawaogopa...Mkishasema nje kuteme mura basi hapo mtu kama una uwezo wa kukimbia kimbia.

  Halafu eti ugali mnaita BUKIMA!

  ReplyDelete
 3. Kaka kuna mpaka "agents" unawalipa nasikia wapo huko Marekani, people pay up to $3000 just to get "tips" on how to get the ladies, niliona on Tyra Banks Show. Personally naona hakuna haja ya kufanya vitu vyote hivyo but at the end of the day mimi ni "msichana" so lol...hivi females hawaruhusiwi kutongoza ama vipi?

  Ila hiyo mistari mwisho nimekufa kabisa! Hahahahahahahahahaha

  ReplyDelete
 4. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 20, 2010 at 9:15 AM

  @Candy: females wanaruhusiwa kutongoza lakini uzunguni :-(

  kwetu huku binti akitongoza kijana inakuwa ni simulizi mtaani na anaonekana ni changudoa :-(

  NDIYO-kama mabinti mnazo hisia za kuwatokea wanaume lakini ndo hivo tena mila, desturi na mazingira hayaoneshi kumfanya binti kutongoza.

  NIULIZE: hivi binti wa KIZUNGU akitongozwa naye huuma kucha, kuweka vidole vyake mdomoni, kuvunjavunja vijiti/nyasi na kuchimbuachimbua udongo? :-)

  @Matondo: lugha zetu haziko sawa kabisa. Utakuta ukiongea jambo kwa lugha fulani inaweza kuwa tusi kwa kabila jingine. Jamii moja ya kikurya ikisema 'kinyero' wakimaanisha 'mboga/kitoweo' kwa wajita na jamii yake ni tusi kubwa ikimaanisha sehemu ya kutolea haja kubwa!

  Hivyo usikonde sana UGALI kuwa BUKIMA :-(

  Nadhani kuna haja ya ku-document maneno kama haya ili kuepusha embarrasmment, au vipi? :-)

  ReplyDelete
 5. @candy, wewe ukilizimikia lijamaa kama LiKitururu au Li-Nngw'nambiti lielezee tu usione soo.

  @matondo ule mstari namba mbili umenitoa meno mpaka hap internet cafee wakanishangaa!!!!!

  ReplyDelete
 6. hii ni sanaa kama sanaa zingine. sio wotee wanaimudu vema. wengine sie hutokwa na jasho na kigugumizi huja pia. yataka moyo ati, au?

  dkt nzuzulima ni vema umekumbuka mapema kuchapisha mambo ya kale katika uwanda wako. historia zetu watanzania zimetokomea kwa kukosa umakini na kukumbuka kuziweka katika maandishi. baadhi ya zilizopo zimekuja kuandikwa na wazungu (mfano mtembelee prof mbele na kitabu kuhusu mlima kilimanjaro). hivi niko mbioni kuandika kamusi ya kinyakyusa. iliyopo imeandikwa eti na msweden. kaikosea kwa kiasi fulani, ingawaje juhudi zake ni za kuzipigia upatu.

  ReplyDelete
 7. Haya makubwa jamani!!!!

  ReplyDelete
 8. jamani mimi kuna demu kashanihangaisha sana sasa nifanye nini ili nimpate nimuazie vipi kutokana ananihangaisha sana

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU