NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, January 6, 2010

MAKAMPUNI YETU NA "JINAMIZI" LA MASHINDANO YA UREMBO


Profesa Mbele amekuwa akisema mara kwa mara kwamba Watanzania tunapenda sana kuponda raha. Tunachangishana mamilioni ya shilingi ili kufanya harusi za kifahari lakini hatuwezi kuchangishana ili kujenga shule au kununua madawati kwa ajili ya watoto wetu wanaosomea chini; au kuchimba visima vya maji vijijini tulikotoka. Tunasema hii ni kazi ya serikali.

Kwangu mimi swali ambalo nimekuwa nikijiuliza ni hili: ni kwa nini makampuni mengi yanamwaga mamilioni ya shilingi kila kukicha ili kufadhili mashindano ya urembo ambayo yametanda kila kona (Miss Tanzania, Miss mkoa, Miss Wilaya, Miss Tarafa, Miss Kata, Miss Kitongoji, Miss Kijiji, Miss familia?, Miss Totoz, Miss chuo kikuu, Miss vyuo vya Ualimu, Miss Shule za Msingi, Miss Chekechea, Miss Serengeti Breweries, Miss Vodacom, Miss Tigo, Miss…)?

Inavyoonekana hakuna kabisa shida ya ufadhili katika mashindano kama haya na starehe nyinginezo. Vipi kama tungeelekeza nguvu hizi katika uimarishaji wa sekta zinazotoa huduma za kijamii hasa kule vijijini? Tungeweza kuchimba visima vya maji vingapi? Tungeweza kununua madawati mangapi? Tungeweza kujenga mashule mangapi?

Mwanzoni niliyalaumu makampuni haya kwa hoja kwamba mengi ni ya kigeni na kwa hivyo hayana moyo wa kizalendo wa kujihusisha na miradi ambayo kweli inaweza kuleta mabadiliko ya kudumu katika jamii. Baada ya kufikiri sana, nimegundua kwamba sina haki ya kuyalaumu makampuni haya. Yenyewe yapo kwa ajili ya lengo moja tu – kufanya biashara na kujipatia faida - tena kubwa kwa kadri inavyowezekana! Ili kufikia lengo hili, inabidi yatangaze bidhaa na huduma zake kwa umma. Mashindano ya urembo ni njia mojawapo nzuri sana ya kufikia wateja wengi kwa kadri inavyowezekana tena kwa wakati mmoja.

Mashindano haya ya urembo yanatangazwa sana na vyombo vya habari (televisheni, redio na magazeti) tangu washindani wakiwa katika maandalizi, wanapoingia kambini kujifua na mpaka siku yenyewe ya mchuano. Na mara nyingi wageni waalikwa katika mashindano haya ni viongozi wakubwa wakubwa wa serikali (aka vigogo). Wakati mwingine washiriki wake (eti “warembo!”) wanafikia hadi kualikwa ikulu ambako wanaandaliwa mlo maalum (dinner) na kupata nafasi ya kuzungumza na wakuu wa nchi. Wanafanyiwa yote haya kwa sababu tu ya kuwa washiriki wa mashindano ya urembo!. Mambo yote haya yanatangazwa na vituo mbalimbali vya televisheni na ni wazi kwamba hii ni nafasi nzuri sana kwa makampuni haya kutoa milioni chache na kupata muda mzuri mrefu wa kujitangaza. Hivi karibuni, kwa mfano, Miss Vodacom Tanzania wa (2009) alipokelewa jijini Mwanza kama “ngole” (malkia) na jiji zima lilizizima.. Kampuni la Vodacom lililokuwa limedhamini mashindano hayo lilikuwepo pale ili kutunisha misuli yake ya kibiashara.

Washiriki wa Miss East Africa (2009) katika "dinner" Ikulu

Ukijitolea kujenga shule, kuchimba visima vya maji au kununua madawati kule kijijini, ni chombo gani cha habari kitakachotangaza habari hizi hasa ukizingatia kwamba vyombo vyote vya habari vimejikita mijini na kamwe haviripoti habari za vijijini (isipokuwa matukio ya kutisha kama mauaji ya vikongwe na albino). Ni waziri gani atakayeacha raha zake za mjini aje kuhudhuria ufunguzi wa visima vya maji au shule kule kijijini? Unafikiri utaalikwa kwenda kula “dinner” Ikulu eti kwa kuwa umenunua madawati kusaidia wanafunzi waliokuwa wanasomea chini?

Kwa hivyo, hili si tatizo la makampuni haya kukosa uzalendo. Ni tatizo letu sisi kama jamii. Mwamko na mkazo wetu haupo katika mambo ya msingi na hasa yale yanayowakera na kuwatesa Watanzania wenzetu wanaokaa vijijini (ambao ndio wengi). Huduma zote muhimu zimerundikana mijini (ingawa nako si wote wanaozipata) na hata vyombo vya habari ambavyo vina jukumu kubwa katika kuelimisha na kuiamsha jamii navyo pia vimebakia kuwa mijini. Hata vyama vya siasa vya upinzani vimeingia katika mkumbo huu (halafu eti vinategemea kuishinda CCM yenye mabalozi wa nyumba kumi kumi katika kila kijiji!). Tunahitaji mabadiliko ya kifikra kama kweli tunataka kuleta mabadiliko ya msingi na ya kudumu katika jamii yetu. Na vijijini ndipo mahali hasa pa kuanzia!

10 comments:

 1. Asante kaka Matondo kwa kuliona hili kweli umetumia jicho lako la ndani. Hakuna kitu kinanisumbua kama MAENDELEO VIJIJINI sielewi kabisa ni kwa nini vijiji vimesahaulika namna hii, nimekaa nikatizama pia kwa jicho langu la ndani nikaona kwamba hapa bila kusimama na kuanzisha kitu tutaishia kulalama tu, sisi tunaoona hili tatizo tupangeni mkakati utakaoweza kusaidia watu kugeuzia akili zao vijijini pia. Nafikiri tukipanga vizuri na kuomba msaada wa serikali tutafanikiwa, huwa nafikiria sana kuanzisha kitu GENIUS SEARCH vijijini, unatafuta watoto wa shule unawaweka kambini na kutafuta kiboko yao. Hii kwa mtazamo wangu inaweza kuanza kusaidia watu kuangalia na vijijini pia, ni mfano tu ambao najaribu kuufikiria..., naamini tutafika tu.

  ReplyDelete
 2. umenena vyema, mimi sikuzote sikuwahi kuona kama hili ni tatizo, yaani unaona mamiss haooo ikulu kumpa hi mkuu wa nchi, mamiss???

  hii inaonyesha akili zetu na mawazo yetu na ndio maana mpaka kufa nitamshukulu mwalimu wangu wa maarifa ya utambuzi.

  tutoe msaada tu vijijini bila kujali isfa wala vyombo vya habari. sisi tuwe mfano na tuanze sasa kutumikia vijiji vyetu. utashangaa, kama viongozi tena wakuu wana nafasi ya kushiriki mambo kama haya, kwanini makampuni nayo yasitumie muda huo kujitangaza?

  vyombo vyetu vya habari navyo vimejaa habari hizo hizo tu za kipuuzi puuzi

  kwamfano sassa hivi ninachangamoto ya kumsomesha kijana mmoja wa kijijini kwetu mwenye akili na anasomea katika mazingira ya shida sana na mwaka huu anaingia kidato cha nne.

  ukitaka kuijuia jamii yetu waangalie viongozi walioko madarakanina wajao, kama sisi mitaani tunachangishana kwenda harusini nk, iweje tukiwa madarakani tusihudhulie mashindano ya ulimbwende na ujinga mwingine wakati watu wetu wanamatatizo tuliyozidi kujigamba kuwa tunataka kuwasaidia kuyamalilza?

  labda niishie hapa lakini hii si habari ndogo.

  ReplyDelete
 3. Machizo yanitoka ndugu yangu. Umenena!

  ReplyDelete
 4. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 7, 2010 at 11:15 AM

  hili nalo neno Prof!

  ReplyDelete
 5. Da Mija - wazo zuri hilo. Pengine hiyo itasaidia watu wa kijijini nao kutupiwa jicho na siyo mpaka kusubiri kikongwe au albino auawe ndipo wasikike. Hili ni suala la kimtazamo. Mwalimu Nyerere alihangaika sana kuhakikisha kwamba mabwanashamba wanakaa vijinini ambako hasa ndiko shughuli zao ziliko. Hili lilishindikana. Bwana shamba anakaa mjini na anakuja mara moja moja kutoa maelekezo ya jinsi ya kupanda mihogo halafu anatokomea zake mjini. Vyombo vya habari ambavyo vimefumuka kila kona vinaweza kuibadilisha hali hii vikitaka.

  Kamala unasikika vyema. Mkazo wetu uko katika mambo mengine ambayo pengine wala hayasaidii sana.

  Ng'wanambiti - ni kweli. Hili nalo ni neno!

  ReplyDelete
 6. Kamala naandika nikikupigia makofi. Umenena! Nyongeza si vibaya nikibaki nazo mwenyewe.

  ReplyDelete
 7. Woooote !!! mmesema mnalalamikia viongozi lakini mimi naona kuna mabadiliko si kama zamani kwa kweli kuna huduma zinakwenda vijijini na wananchi pia wameelimika huduma chini ya kiwango wanaikataa hamjayaona hayo ? mi nafikiri yaongezeke zaidi na vichocheo ni sisi wananchi tusisubiri serikali.

  ReplyDelete
 8. Shukrani Profesa Matondo kwa kuliweka suala hili wazi namna hii.

  Mambo ya Tanzania yanasikitisha hadi mwisho mtu unatamani kucheka. Nami najihisi kucheka, kwa kuwazia kuwa hatimaye jamii itatuweka kitimoto wanablogu kwamba tunaliaibisha Taifa kwa vile hatuna mashindano ya Miss Blogu :-)

  ReplyDelete
 9. Profesa Mbele;

  Siku hizi hata hivyo nimeanza kuona mabadiliko kidogo kuhusu haya makampuni, na hasa Vodacom. Wamekuwa wakinunua madawati, kujenga nyumba za walimu, zahanati, kuchimba visima vya maji n.k. Na kwa vile viongozi wake wa shughuli hizi ni maarufu sana katika jamii (mf. Mwamvita Makamba) basi hata shughuli hizi zisizo za kiustareheshaji zimekuwa zikiripotiwa sana katika vyombo vya habari. Mkazo hata hivyo bado upo katika michezo na starehe zinginezo.

  Mashindano ya Miss Blogu aah umenichekesha sana. Lakini inawezekana. Si tunao akina Yasinta, Da Mija, Koero, Rachel Siwa na wengineo?

  Naona pia kuna "Blog Awards" Zinaandaliwa. Sijui kama waandaaji ni Global Publishers au pengine ni Vodacom sijui. Habari zake ziko hapa:

  http://abdallahmrisho.blogspot.com/2011/04/tanzania-blog-awards.html

  ReplyDelete
 10. Nkoyi, nimeupenda sana wimbo wa Ng'wanakanundo.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU