NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, January 12, 2010

NAHITAJI MSAADA - NATAFUTA PICHA ZA MAREHEMU DR. RUGATIRI MEKACHA


NATAFUTA PICHA ZA MAREHEMU DR. RUGATIRI MEKACHA

Wadau, nahitaji msaada. Natafuta picha za aina yo yote za Marehemu Dr. Rugatiri Mekacha ambaye alifariki tarehe 29/9/2001 nchini Japan ambako alikuwa amekwenda kikazi katika Chuo Kikuu cha Masomo ya Kigeni cha Osaka. Dr. Mekacha ndiye alinipa misingi ya isimu wakati ule nikiwa bado mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Nilipopata nafasi ya kwenda kusomea shahada za uzamili (Masters) na Uzamifu (Ph.D) katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA), Dr. Mekacha alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili na alihakikisha kwamba ninapata kila kitu nilichohitaji kwa ajili ya safari hiyo. Hata baada ya kufika UCLA, aliendelea kunishauri katika masomo yangu na mambo mengine ya kimaisha. Kwangu Dr. Mekacha hakuwa mwalimu tu bali rafiki na mshauri.

Ni kwa sababu hizi ndiyo maana nimeamua kuhariri kitabu ili kumkumbuka na kumuenzi. Kitabu hiki (ambacho maelezo yake mafupi yapo hapa chini) kiko tayari kwenda kwa mchapishaji. Kitu pekee kinachonikwamisha ni picha. Mchapishaji amesisitiza sana kwamba itapendeza kama kutakuwa na picha ya Dr. Mekacha ambayo itawekwa mwanzoni mwa kitabu hicho. Juhudi zangu za kupata picha zake hata hivyo zimekwama kabisa. Kama ningeweza kwenda Tanzania ningeenda nyumbani kwao Nata Serengeti kuzitafuta.


Kutokana na tabia yake ya ucheshi na uanaharakati pamoja na kutambulika kwake, nashawishika kuamini kwamba lazima kuna wadau ambao wana picha zake. Kama mpo basi naomba sana mnitumie picha zake zo zote zile kupitia barua pepe ifuatayo: profesamatondo@gmail.com. Pia kama kuna mdau ambaye yuko Musoma/Serengeti na angependa kunisaidia kwenda kijijini Nata Serengeti kufuatilia picha basi naomba tuwasiliane. (Ng'wanambiti upo?). Nitalipia kila kitu.
Natanguliza shukrani zangu za dhati.

Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima

Chuo Kikuu cha Florida

*********************************************************
KUHUSU KITABU CHA KUMBUKUMBU YA DR. MEKACHA

Kitabu kinaitwa: “Bantu Languages and Linguistics: Papers in Memory of Dr. Rugatiri Mekacha”. Ni mkusanyiko wa makala (16) nzuri za masuala ya lugha na isimu katika lugha za Kibantu. Makala hizi zimeandikwa na wanaisimu wenye umashuhuri duniani kote na tunatumaini kwamba kitabu hiki kitatoa mchango mkubwa katika kuzieleza na kuzifafanua lugha za Kibantu ambazo kusema kweli bado zinahitaji kufanyiwa uchambuzi wa kina wa kiisimu kulingana na nadharia za kisasa. Lugha zilizochambuliwa katika kitabu hiki ni Kiswahili (makala mbili - moja imeandikwa kwa Kiswahili), Kisukuma (makala mbili), Kisetswana (makala mbili - Botswana na Afrika Kusini), Kikurya, Kichewa (Msumbiji na Malawi), Kilungu (Zambia), Kikhayo (Kenya), Kibemba (Zambia) na Kihaya. Pia kuna karatasi nne zinazojadili masuala mbalimbali ya lugha nchini Tanzania; ikiwemo sera mpya ya lugha ambayo inapendekeza kukifanya Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia kuanzia shule za msingi.

2 comments:

  1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 13, 2010 at 8:59 AM

    Masangu, hongera kwa kitabu hicho...tutapenda kupata nakala kwani naona kuna makala za kisukuma na kukuria ambazo kwangu 'pendo limezidondokea' :-)

    tuko pamoja

    ReplyDelete
  2. picha... labda kwa watu waliopo UDSM

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU