NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, January 5, 2010

NIMEGUSWA SANA NA PICHA HIZI ZA MAREHEMU SIMBA WA VITA

 • Hapa ni wakati akiwa amelazwa Muhimbili. Hii ni nadra kwani tumezoea kuona wakubwa hawa wakikimbizwa "bondeni" au kwa malkia wanapougua utafikiri kwamba kwa kufanya hivyo kifo hakitawabamba. Nimeiangalia picha hii mara nyingi sana!

 • Hata jeneza na kaburi lake Mtanzania huyu halisi ni la Kitanzania - si yale majeneza yaliyoagizwa kutoka nchi za nje, majeneza ghali yaliyonakshiwa na kupambwa kistadi kwa vito na manemane.
 • Hii ndiyo nyumba ya kudumu ya Komredi Simba wa Vita. Hebu Mola na ampe pumziko jema mwana huyu halisi wa Tanzania aliyeipenda nchi yake na kuitumikia kwa moyo wake wote!
Hapa chini ni sehemu ya makala nzuri ya mhariri wa gazeti la Kulikoni yaliyochapishwa jana katika ukurasa wa saba wa gazeti hilo.

********************************************************************************

Yeye na Mwalimu Julius Nyerere mbali na kutotaka masihara kazini walionyesha maisha ya kutojilimbikizia mali. Mzee Kawawa alipotoka madarakani wanaomfahamu wanasema hakuwa na kitu na kama si sheria za pensheni kwa wastaafu, angeweza kuwa mmoja wa watanzania wa kusaidiwa kwa michango ya ndugu ili apate kutibu afya yake iliyokuwa ikidorora licha ya kupata kuwa kiongozi mkuu kitaifa.


Ndio maana aliweza kwenda kuishi eneo kama Madale, nje ya Dar es Salaam na si Oysterbay au Masaki - Kawawa hakuwa na uwezo wa kujenga sehemu hizo ambako mawaziri wakuu wa miongo hii wamejenga, tena kabla hawajafika alipofika, walishakuwa wamejenga mahekalu.

Ndio maana kwa kutambua mchango wake kwa Taifa ama kwa kupigania utawala bora na haki za watu moja kwa moja au kwa yeye kujinyima na kuwa mfano bora, Januari mwaka 2007, Kawawa alitunukiwa tuzo ya Dk. Martin Luther King.

Moja ya maneno yanayoweza kubaki kuwa wosia kwetu ni yale aliyoyasema wakati wa kukabidhiwa tuzo hiyo ambapo kwa kuwa nilikuwepo wakati akikabidhiwa pale kwenye ubalozi wa Marekani niliiona ari aliyokuwa nayo kutamani kuendelea kutoa mchango wake kwa Taifa ingawa nguvu hakuwa nazo tena kutokana na umri.

“Heshima iliyotukuka mliyonipa si tu imeniletea faraja, bali pia ni kichocheo cha kuendelea kuwatumikia Watanzania pale ambapo nitaweza kuwatumikia bila kujali itikadi zao za kidini au za kisiasa, kwa manufaa ya taifa kwa ujumla,” alisema Kawawa na kuongeza: “Sasa nafuga nyuki na nipo tayari kumfundisha mwenzangu yeyote ufugaji wa nyuki wa kisasa,” alisema akieleza maisha yake baada ya siasa kuwa ni ya ukulima.

Pia katika hotuba yake hiyo aliasa viongozi na wanasiasa akisema: “Naomba mtupie macho makundi madogo madogo ambayo sauti zake hazijasikika, yapatiwe misaada ili yapate uwezo wa kujikwamua kiuchumi, yapate fursa sawa katika jamii ili uwezo walionao utumike kuleta maendeleo.”

Mimi sikuwa na mabilioni ya fedha, hivi ningeyapata wapi? Mwalimu Nyerere hakuwa mtu mwenye tamaa, hata hakujilimbikizia mali, hii iwe ni changamoto kwa wana CCM.

2 comments:

 1. hivi kwa nini aliitwa simba wa vita? harafu siasa za huyu bwana na nyerere duh!
  hakupelekwa nje kwa sababu walijua ya kwamba atakufa tu si aliishazeeka? bila shaka huko nyuma aliishapelekwa nje kutibiwa. hivi kikongwe cha mika 80 waweza hangaikia afya yake kwa gharama kibao? ki kifo ni halali kwake?

  ReplyDelete
 2. Kamala!!!

  Picha hizo zimenigusa pia.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU