NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, February 5, 2010

FIKRA YA IJUMAA: WIMBO WA MTOTO WA KIPOFU OMBAOMBA MPIGA MARIMBA (NA E. KEZILAHABI)


Ijumaa hii, hebu tufikirie vizuri maneno ya huu wimbo ambao unaimbwa na mtoto wa kipofu ombaomba mpiga marimba. Wimbo huu unapatikana katika riwaya ya Euphrase Kezilahabi ya Mzingile.


Tumetembea katika msitu wa kurasa potovu

Na kutafuna kila neno na kila aina ya wino

Tumemeza yapashwayo kunywewa

Na kucheua yatakiwayo kumezwa.

Vipofu na vichaa wataurudisha ulimwengu

Katika nyayo zilizofichama gizani

Ondoeni mwanga katika bonde la taaluma

Kupunguza ajali na maluweluwe.

Muhimu ni kuona gizani

Bila kupapasa kuta hafifu za karatasi.

Wanaojidai kuona wametufikisha

Ukingoni mwa bahari yenye papa na nyangumi,

Na wanatushauri tuogelee katika mihadhara

Ambayo vichukua sauti vyake ni mitutu ya bunduki

Na viti vyake ni vichwa vya nyuklia.

Kesho hapatakuwa na msemaji

Msikilizaji wala mshangiliaji

Bali mcheko wa utupu katika jangwa

Ukishindana na mlio wa vizazi

Ambavyo havikupata kuzaliwa"


Euphrase Kezilahabi. 1991. Mzingile. Dar es salaam University Press (uk. 28)

2 comments:

  1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!February 5, 2010 at 3:38 PM

    mh! ama kweli hakuna jipya duniani. ni ama lipo ama lilitabiriwa na kwa kutabiriwa kwake hata kama ni leo tayari lipo :-(

    unaozungumziwa hapa si ufisadi huu jamani :-(

    ReplyDelete
  2. Ng'wanambiti - kama unataka kuchemsha ubongo, tafuta tuvitabu hutu tuwili twa Kezilahabi utusome. Nagona na Mzingile. Ni tuvitabu tufupi sana lakini ni kazi kweli kweli.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU