NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, February 3, 2010

BADO NAKUMBUKA SIKU NILIYOKUTANA NA UBINADAMU WA KWELI PALE MUHIMBILI


 • Mwaka 1993 nililazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa operesheni kubwa ya sikio ambalo lilikuwa likinisumbua tangu utotoni. Kwa bahati nzuri operesheni hiyo ya masaa zaidi ya manne ilifanikiwa vizuri na baada ya siku chache tu nilikaribia kuruhusiwa kurudi nyumbani.
 • Nakumbuka Ijumaa moja mchana wakati nikiwa nimelala, niliamshwa kwa upole na mzee mmoja aliyekuwa ameambatana na kijana wa makamo. Kwa kuangalia tu mavazi yake nilitambua mara moja kwamba alikuwa ni Mwislamu. Mzee huyo aliniuliza jina langu na tatizo lililokuwa likinisumbua. Aliniuliza nilikokuwa nimetokea. Nilipomwambia kwamba nilikuwa natoka mkoa wa Shinyanga aliniuliza kama nilikuwa na ndugu pale Dar es salaam. Aliendelea kuniuliza kama nilikuwa nahitaji chakula spesheli kutokana na operesheni yangu. Aliniuliza kama nilihitaji pesa kidogo kwa ajili ya kununulia matunda na maji ya matunda hapo nje. Aliniuliza kama kulikuwa na baridi wakati wa usiku na kama nilikuwa nahitaji shuka la ziada au blanketi. Nilipomwambia kwamba nilikuwa na kaka pale Dar es salaam ambaye alikuwa ananiangalia, alinitakia uponaji wa haraka, akaniaga na kwenda kuongea na wagonjwa wengine.

  • Nilishangazwa sana na upendo ulioonyeshwa na Mzee huyu nisiyemfahamu. Baadaye nilimwona akiwapa pesa wagonjwa wengine katika wodi lile. Baadaye wagonjwa wa muda mrefu na hasa kutoka mikoani waliniambia kwamba walikuwa wanamtegemea mzee yule (na waislamu wengine ambao walikuwa wakifika hapo kwa wingi kila Ijumaa) kwa pesa za matumizi madogo madogo na kwamba alikuwa anafika kila Ijumaa kuwaangalia.
  • Jambo hili na wema niliouona siku ile pale Muhimbili ulinigusa sana. Hebu fikiria kama binadamu tungechukua angalau saa moja tu katika shughuli zetu za kila wiki /mwezi na kusaidia angalau mtu mmoja aliye katika shida. Hebu fikiria kama watu wote tunaojidai kuwa washika dini tungefanya hivi angalau mara moja kwa wiki. Hebu fikiria…. Matendo madogo kama haya yanatosha kubadili maisha ya mtu hata yule aliyekaribia kukata tamaa akidhani kwamba dunia hii ilikuwa imemsahau na kumtupa.

  • Tena matendo madogo kama haya huwa hayafutiki kirahisi katika mioyo ya wale tunaokutana nao. Ndiyo maana bado namkumbuka yule mzee mwenye kanzu nyeupe, kibaragashia cheupe na kandambili za rangi ya bluu, mzee aliyeninyoshea mkono wake wa upendo na ubinadamu pale Muhimbili miaka 17 iliyopita!

  6 comments:

  1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!February 3, 2010 at 10:20 AM

   Dkt, hongera kwa kupata kuuona wema hapo zamani :-)

   hata hivo nakushangaa saana kwa kutamani jambo hilo wakati watu wetu muda wao umechukuliwa na mambo mengine. Na kwa kiasi kikubwa nafasi na wakati wetu imechukuliwa na IGIDAJI wa maji toka ILALA na Bwiru (RUARAKA kwa kenya!). Mkubwa Chalzi Hilary aliwahi kushangaa kuwa kila baada ya mita 100 kuna BAR hapo Dar na zote zinajaa pomoni :-(

   Nakumbuka mwaka 2000 nilipoamua kwa hiyari yangu kuacha KUGIDA na kula NYAMACHOMA nilipoteza 98% ya rafiki zangu kwa kuwa waliniona miye msaliti na hatuwezi kupanga dili kwa maji. Walinifukuza kila nilipowakuta hapo kijiweni!

   Hivo swala la kupanga muda wetu kwa ajili ya kuwapatia afueni wagonjwa na wenye uhitaji halipo kwa kuwa tukimaliza kazi hukimbilia kunako VITI virefu na kuanza kugida! :-(

   na hili haliko kwa wagidaji tu hata wale tujiitao WENYE UPAKO toka kwa LOHO MTAKAVITU sorry mtaka-tifuuu kama Mt Simon kitururu hilo si kipaumbele chetu :-(

   lakini ukweli unabaki palepale kuwa uwe na hela ama kapuku kutembelea wagonjwa na wenye uhitaji huleta faida zaidi ya hasara :-)

   ReplyDelete
  2. hii inatukumbusha mengi, yatukumbusha juu ya kazi yetu iliyotuleta duniani ambayo ni kutoa upendo kwa wengine.

   imenikumbusha na kunikuna sana hii.

   kuna shule za kata zisizo na walimu, napanga kuanza kujitolea mara moja kwa juma kufundisha shule hizi
   pia ntapanga na wife juu ya wagonjwa

   ReplyDelete
  3. TOUCHY!!!!
   Tofauti ninayoiona ni kuwa HAKUJITAMBULISHA, HAKUSEMA ANATOKA WAPI, ANAFANYA HIVYO ILI IWE NINI WALA KUJIWEKEA KUMBUKUMBU.
   Ni ilee ya TENDA WEMA UENDE ZAKO
   Miaka 17 baadae, bado anaombewa na Kaka Matondo.
   Swali ni kuwa alianza lini kabla hajakutana nawe?
   Anaombewa na ameombewa na wangapi kabla yako?
   Je baada yako?
   Unadhani baraka hizi zinaweza kulinganishwa na nini?
   UBARIKIWE KWA FUNZO HILI
   NIMEJIFUNZA KITU KIKUUUBWA SANA.

   ReplyDelete
  4. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!February 4, 2010 at 10:37 AM

   @Msee ya Changa-Moto: Mie ninatofautiana nawe kiduuuuchu :-(

   nadhani mjamaa huyo kutojitambulisha ni jambo jingine jema wakati mwingine. kufanya jema si lazima ufahamike sana ni sawa na kufunga ama kusali kama bwana mkubwa anavosema 'usalipo usiwe kama wanafiki....ingia chumbani na bwana aonaye toka sirini atakujazi....ufungapo usiwe kama wanafiki....midomo mikavuuuu....ufungapo piga pamba za nguvu na tia mafuta midomoni ili usionekane kuwa unashinda njaa kwa kuwa mkulu huko juu anakuona' (nimechanganya na tafsiri yangu, hivo usilie sana mkubwa).

   imajini kama angejitambulisha ingekuwaje? Dkt si angeshawishika kumtafuta amkumbushe ilhali yawezekana jamaa ashasahau kwa kuwa yeye anachojua ni kutenda tu? na angeshawishika kumtafuta (pengine kujua kama yuko hai ama la) angejitambulishaje?

   ONA HII: mzee, mimi naitwa Masangu, ni mzaliwa wa Unyantuzu....er..unakumbuka mwaka 1993 ulikuja wakati nimelazwa ...blah blah....Na mzee akikuuliza ...eh nakumbuka...una shida gani tena nikusaidie...si itakuwa embarrassment kwa Masangu?

   kwa hiyo la msingi ni ule wema ulotendwa na si kujulikana. Kwa kuwa Dkt anakumbuka na alichotendewa (hata kama halikutimia lakini ule utu ulooneshwa) na kama anadhani ana deni ama lilikuwa jambo jema sana na anataka kulipa fadhila kama hiyo itabidi atende kama hivo ama karibu na hivo.

   wabheja sana ng'wanawane :-)

   ReplyDelete
  5. Ng'wanambiti - nakubaliana nawe. Lengo la wema ulioonyeshwa na mzee yule si kujulikana.

   Na njia nzuri ya kuuendeleza ni kwenda kuwatendea wengine vivyo hivyo - bila kutaka kujulikana wala kutegemea shukrani. Nadhani upendo wa aina hii ni nguzo mojawapo katika dini nyingi duniani ingawa mara nyingi ubinadamu hutuzingira na kutufanya tutake kushukuriwa na kusifiwa tunapotenda wema! Na tunapofanya hivi basi tunaharibu kila kitu.

   ReplyDelete
  6. Kaka Chacha, nilichokuwa namaanisha ni kuwa "kilichonigusa" ni kutojitambulisha kwake.
   Ina maana alilotaka ni kutenda wema na kwenda zake asingoje shukrani.
   Ninalomaanisha ni kuwa NDIVYO INAVYOTAKIWA KUWA.
   Samahani kwa kuandika kama anayeongea (tena kiHaya haya hiviiii)
   Ila nami nilimaanisha umaanishavyo kuwa "la msingi ni ule wema ulotendwa na si kujulikana"

   ReplyDelete

  JIANDIKISHE HAPA

  Enter your email address:

  Delivered by FeedBurner

  VITAMBULISHO VYETU