NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, February 22, 2010

TUWAJENGEE KUMBUKUMBU NZURI WATOTO WETU

 • Haka kamalaika hapo chini kanaitwa Johari Long'hwe Matondo (kamefikisha miaka miwili jana). Wakati wa Krismasi mwaka jana kalitaka sana kupatiwa hizi blanketi zenye mikono ziitwazo "Snuggie". Na kweli kalipopata kalifurahia mno kiasi kwamba hata kulala ilikuwa shida. Natumaini kwamba taswira kama hizi zitakakumbusha baadaye kuhusu Krismasi hii iliyofana sana, pamoja na utoto wa kenyewe uliobarikiwa!
 • Ati, wewe unakumbuka nini hasa kuhusu utoto wako? Mimi nakumbuka mambo mengi yakiwemo vibano nilivyokuwa napata kutoka kwa baba mdogo (Mungu Amlaze mahali pema peponi) aliyekuwa hapendi mchezo na shule. Alikuwa hapendi kuona kosa lolote katika daftari la shule na siku hiyo kama ulikuwa umekosea swali shuleni basi ulijua kwamba kibano kikali kilikuwa kinakusubiri nyumbani.
 • Hata bado nakumbuka siku moja mbaya kabisa nilipokuwa darasa la pili au la tatu. Ilikuwa siku ya mkosi kweli kwani nilipofika shuleni tu asubuhi nikiwa nimechelewa nilikula viboko vinne. Basi kuanzia asubuhi ile viboko viliniandama na mpaka kufikia jioni nilikuwa nimefikisha viboko zaidi ya ishirini na vitano.
 • Inavyoonekana binadamu tunatunza kumbukumbu mbaya kwa umakinifu zaidi kuliko kumbukumbu nzuri. Pengine ni muhimu tujitahidi kuwapa watoto wetu kumbukumbu nzuri na upendo usiolegalega. Kuna faida nyingi za kufanya hivyo!


6 comments:

 1. Nakumbuka nilipokuwa shule ya msingi,nafasi ya kwanza ktk masomo ilikuwa ni kawaida yangu,basi darasa la sita nilishika nafasi ya nane kati ya wanafunzi wote! Nakumbuka nililia saaaaaana kana kwamba nafasi ya kwanza ilikuwa ni haki yangu ya msingi.

  ReplyDelete
 2. sijui nakumbuka nini mimi! ila majina mabovu ya walimu wetu

  ReplyDelete
 3. Matondo, mie nakumbuka simulizi ya jinsi nilivokuwa 'nateswa' wakati wa kilimo. Kwa kuwa mie ni mmojawapo wa watoto wa kwanza na hakukuwa na masuala ya 'house girls' kama siku hizi basi wazee walipkuwa wakienda kulima walichimba shimo la kuweza kunihifadhi usawa wa kifua na kunitumbukiza humo na kisha kunifukia a.k.a kunizika nusu.

  Hapo ningelia weee mpaka basi huku wazee wakichapa kazi :-(

  Ningenyonyeshwa na kisha kurudishwa humo shimoni....

  Kazi kwelikweli...lol

  ReplyDelete
 4. @Chacha, hiyo kali, tuandikiea story nzima na kuitundika kijijini kwenu tuione

  ReplyDelete
 5. Happy Birthday Johari, ukue upesi, uwe na akili shuleni, uje utetee akina mama na watoto

  ReplyDelete
 6. Mie nakumbuka nilikuwa na miaka 6 ilikuwa siku ya mkesha wa xmas,mama yangu alikuwa ni mwl, na fundi wa kushona nguo,ilikuwa ni siku ya zamu yangu na mdogo wangu kushonewa nguo za xmas alianza vizuri lkn kabla hajamaliza Ghafla aliugua akanguka chini hakuweza tena kuongea mpaka baada ya wiki 3,kulikuwa na mdogo wetu mdogo ananyonya wa miezi 9 ilibidi achukuliwe na mke wa mjomba wetu, nakumbuka mimi na mdogo wangu anaenifutia tulikuwa tunapiga magoti na kusali kumuomba mungu amponye mama yetu,hiyo haitonitoka kichwani mungu ni mwema sala zetu zilijibiwa kwa kumponya mama yetu.

  Mwaka huo huo,babu yetu mzaa mama alifariki siku ya mazishi yake ilikuwa jioni jua karibu linazama kulikuwa kama kuna rangi ya orange au kama nyekundu hivi,basi hiyo nayo kwangu ilinikaa kichwani kila inapojitokeza rangi kama hiyo huwa nakumbuka sana mazishi ya babu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU