NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, February 4, 2010

WHAT IS IN A NAME? MTOTO WA KITANZANIA ANAPOITWA ANGELINA PITT PROMISE!!!

 • Wanaisimu tunaamini kwamba lugha ni sauti za nasibu. Tukisema hivi tunamaanisha kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kitaja (mf. neno meza) na kitajwa (mf. kitu chenyewe meza). Tukiamua leo kubadilisha kitaja na kuiita meza kwa kutumia neno la kubuni gambasingu, kitajwa kitabakia kuwa kile kile. Ndiyo maana kitajwa kile kile kimoja (meza) kina majina tofauti katika lugha mbalimbali duniani.
 • Mantiki hii hii pengine inaweza pia kutumika katika majina ya binadamu. Hakuna sababu yo yote ya msingi ambayo inamfanya Ng'wanambiti ajiite Ng'wanambiti. Leo hii akiamua kubadilisha jina na kujiita Mpendamatobolwa haitabadilisha cho chote. Atabakia kuwa Ng'wanambiti yule yule.
 • Majina hata hivyo yana uamilifu na uangavu wa kijamii, kimazingira na kitamaduni. Katika jamii nyingi za Kiafrika, kwa mfano, majina yalikuwa hayatolewi hovyo hovyo. Siku, wakati na majira ya kuzaliwa wakati mwingine yalizingatiwa. Matukio muhimu wakati wa kuzaliwa kwa mtoto pia yalizingatiwa. Kama mlikuwa mapacha pia mlipewa majina yaliyoutambulisha upacha wenu. Majina pia, mbali na kuashiria kabila la mtoto (ambalo hasa falsafa, imani, desturi na tamaduni zake ndizo ziliongoza mtazamo na falsafa ya mwanajamii juu ya maisha na mahusiano yake na binadamu wengine hapa duniani), majina mengi yalionyesha pia ukoo wa mtoto huyu.
 • Ndiyo maana leo nikisikia mtu anaitwa Mubelwa mara moja najua anakotoka na pengine naweza hata kuuliza maana yake nini. Nikisikia Lutabasibwa au Kaijage mara moja pia nafahamu. Nikisikia Chacha Wambura najua mara moja kwamba inabidi niwe mwangalifu kwani kuna "kutemwa". Nikisikia Ngonyani pia naelewa. Hali kadhalika Mpangala, Koero, Matiya, Mbele, Chahali, Mija, Masue n.k.

 • Dini kutoka nje zilipokuja, ziliingilia utaratibu huu na kuuvuruga lakini hata hivyo hazikufanikiwa sana kwani Waafrika wengi tuliendelea kuzingatia majina yetu ya ukoo. Na Wakristo wengine "watukutu" kama mimi tuligoma kuitwa Mtume Petro, tukabakia na majina yetu ya Kiafrika - Masangu Matondo Nzuzullima!
 • Sasa hivi kuna mtindo mpya ambapo hata majina ya ukoo tumeanza kuyatupilia mbali. Pengine katika wakati tulionao, utambulisho wa kikabila na ukoo si jambo la muhimu tena. Ati, kuna umuhimu gani wa mtu katika wakati huu wa utandawazi kujitambulisha kwamba yeye ni memba wa ukoo wa akina Kitururu?
 • Nilishangazwa kidogo hivi karibuni rafiki yangu mmoja alipopata mtoto na kumpa jina la Angelina Pitt Promise (nimelibadilisha kidogo ili nisigombeshwe). Nilipouliza mbona mtoto hana jina la (ukoo wa) baba ambaye ni Mchaga, nilijibiwa (tena kwa Kiingereza) "we don't do inheritance". Eti kwa jinsi mtoto alivyo mzuri (inasemekana anafanana fanana na Angelina Jolie mke wa Brad Pitt ingawa wazazi wake wote ni Watanzania weusi) anategemewa kuwa modo wa kimataifa siku za usoni. Niliuliza, kuwa modo wa kimataifa ni lazima kuwa na jina la Kimagharibi? Mbona Flavian Matata anatamba kimataifa na u-Matata wake?
 • Ati, lipi ni jina bora hapa: Angelina Pitt Massawe au Angelina Pitt Promise?

9 comments:

 1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!February 4, 2010 at 6:07 PM

  Dkt: mojawapo ya changamoto tulizonazo kwetu siye wa kizazi cha dotcom ni kudhani majina ya wenzetu ni bomba sana kuliko ya kule 'bush'

  lakini hii inatokana na kutokujielewa kwakuwa mimi ningependelea jina kama Manka ama Aika Massawe kuliko kuweka hayo mawili ya mwanzo.

  ama kwa hakika mimi ni mmoja wa wapenzi wa majina ya asili na ndo sababu natumia hata jina nililopewa wakati nahudhuria ngoma za 'manyalali' huko usukumani :-)

  ReplyDelete
 2. Kwanza nikushukuru saaana Kaka Matondo kwa kuliandika hili kwa umakini na ufanisi zaidi.
  Labda hapa ntapata jibu la swali langu nililouliza hapa (http://changamotoyetu.blogspot.com/2008/11/ni-kweli-majina-yetu-huathiri.html)

  ReplyDelete
 3. Asante matondo kwa mada naomba kuuliza swali la kiisimu, hivi leo nikizaa mtoto wa kiume nikamwita Farida au Margareth au Joyce kuna tatizo? Huwa najiuliza sana hilo swali. Haya Mwl unasemaje hapo?

  ReplyDelete
 4. Ng'wanambiti - Ngugi wa Thiong'o ameliongelea kwa kirefu suala hili katika kitabu chake cha Decolonizing the Mind. Kidogo inashangaza kuona kwamba tumeanza kugeuza hata majina ya ukoo. Sina tatizo na mtoto kuitwa Angelina Pitt Massawe. Nina shida na mtoto kuitwa Angelina Pitt Promise!

  Mzee wa Changamoto - nilikuwa sijaisoma makala uliyoirejelea. Ni kweli. Ndiyo maana huwa nashangaa mtoto anapoitwa Sipendeki au Shida. Nitaisoma vizuri makala hiyo na nitarudi tena kuongezea kama nitakuwa na cho chote cha kuongezea.

  Mwanamke wa Shoka - ingawa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kitaja na kitajwa, lugha hupata uamilifu kutokana na watumiaji wake. Na kwa vile wanajamii wameamua kwamba majina kama Farida, Margareth na Joyce ni ya jinsia ya kike, pengine watakushangaa ukiyatumia kwa mtoto wa jinsia ya kiume. Tegemeo la wanajamii-lugha wakisikia mtoto anaitwa Farida ni kuona kuwa ana sifa ya [+ a kike].

  Kwa vile tamaduni za jamii zinatofautiana, ndiyo maana tunaamini kwamba kujifunza lugha ngeni darasani hakutoshi. Inabidi kwenda kuishi na wasemaji wa lugha hiyo. Pengine utashangaa kukuta katika jamii fulani sifa za kisemantikia zimebadilika na mtoto wa kiume akaitwa Farida. Hii hata hivyo ni nadra kutonana na ukweli kwamba majina mengi yanahusiana. Mf. hatutegemei kukuta mwanamke akiitwa Peter kwa sababu jina hili lilikotoka lina sifa ya [+a kiume] na sisi tumezirithi sifa hizi kama zilivyo. Tukitaka kubadilisha sifa hizi ni lazima tubadilishe kidogo na kulivisha umbo la "kike" - Petra. Hali kadhalika Farid [+a kiume] kutokana na Farida [+ kike].

  Hitimisho: Kwa kuzingatia lugha kama lugha, hakuna sababu za msingi zinazokufanya usimwite mtoto wako wa kiume Farida. Ni sababu za kijamii na kitamaduni zinazokufanya usifanye hivyo! Kama unataka ufafanuzi zaidi sema.

  ReplyDelete
 5. Kwanza Mwl nikushukuru kwa kunipa jibu makini nimeanza kuelewa sasa, ila naomba niendelee kuuliza..

  Nanukuu katika aya ya tatu ya jibu ulilonipa,.."Na kwa vile wanajamii wameamua kwamba majina kama Farida...."

  Swali langu ni kwamba je majina ya vitu hupatikanaje? mfano neno shamba au barabara au kiazi, Je jamii ilikaa ikaamua kwamba kipande hiki cha ardhi kiitwe shamba na si barabara? au majina hutokea tu kwa bahati nasibu? maana nakumbuka kuna wakati wanablogu tulikaa tukaamua kutunga jina la blog kwa kiswahili mjadala ulikuwa mkali na tukaishia njiani, nitautafuta ule mjadala niutundike pale kibarazani kwangu uone, Na kwa vile wewe ni mtaalamu katika hili nadhani utasaidia.

  Ni hilo tu Mwl.

  ReplyDelete
 6. Da Mija - kama tafsiri ya lugha hapo juu inavyosema, lugha ni sauti za nasibu na hakuna vikao vinavyofanyika ili kuamua. Zipo jitihada nyingi zilizofanyika kuweza kukaa chini na kuunda lugha lakini bila mafanikio. Kule Nigeria, kwa mfano, wanaisimu fulani wamekuwa wakijaribu kuunda lugha ya taifa inayojumuisha lugha kuu za nchi hiyo - Kiyoruba, Kiibo na Kihausa lakini bila mafanikio. Tanzania tuna BAKITA lakini nayo mara nyingi inachelewa kuunda misamiati. Wataalamu wake wanapoteza muda mwingi kufanya vikao na wanapoelewana na kuchapisha msamiati wao unakuta kuna maneno ya kinasibu tayari yanatumika mitaani. Kwa hivyo maneno na Kiswahili chao wanachokipendekeza kinabakia kuwa katika vitabu tu.

  Wanaleksikografia (watunga kamusi) wa Kiswahili wameshajiwekea misingi ya kufuata wanapojaribu kutohoa maneno kutoka lugha ngeni. Neno kama kompyuta linapokuja katika Kiswahili, ni lazima kwanza litafutiwe maana katika lahaja za Kiswahili zilizozagaa katika pwani ya Afrika Mashariki (na kwingineko). Wakikosa neno katika lahaja hizi, wanatafuta katika lugha nyingine za Kibantu. Wakikosa huko wanaendelea kutafuta katika lugha zingine za Kiafrika. Wakikosa huko basi wanalikopa kama lilivyo na kulivisha umbo la Kiswahili. Kama nilivyogusia hapo juu, utaratibu huu unachukua muda na wanapokuja kupendekeza maneno yao, unakuta maneno mengine tayari yameshakubaliwa na watumiaji mitaani na mara nyingi maneno yao wanayopendekeza yanabakia kuwa vitabuni tu. Wakati mwingine pia wanafanikiwa (mf. ikulu, kaya, mashiganga...)

  Tatizo kubwa ni kwamba Wanaleksikografia hawa hawafanyi kazi kwa ushirikiano. Ndiyo maana utakuwa Wakenya wana maneno yao (-tarakilishi), Tanzania tuna ya kwetu (kompyuta, ngamizi?) na kule Kongo wana ya kwao. Sijui Watanzania tutaendelea kuwalazimisha hawa wengine kuzungumza Kiswahili chetu mpaka lini.

  Kuhusu blogu - tayari jamii inatumia neno blogu na sijui kwa nini mnataka kutafuta neno jipya. Kama ni hivyo, basi hatua za kufuata - kama mnapenda ni hizo hapo juu. Pengine kuna neno katika lahaja za kiswahili, lugha za Kibantu, lugha za Kiafrika lenye kubeba dhana halisi ya blogu...Soma makala hii: http://www.ifeas.uni-mainz.de/SwaFo/swafo6/6_12_kingei.pdf na hii:http://www.lingref.com/cpp/acal/36/paper1422.pdf kuhusu mchakato mzima wa ukopaji wa maneno katika Kiswahili

  ReplyDelete
 7. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!February 10, 2010 at 9:18 AM

  Matondo: Nanukuu-'Pengine utashangaa kukuta katika jamii fulani sifa za kisemantikia zimebadilika na mtoto wa kiume akaitwa Farida'. MWISHO WA KUNUKUU

  Sina hakika kama najua hilo NENO-kisemantikia...lol

  Lakini naomba niwape taarifa kuwa makabila jamii ya kikurya unaweza kukuta mwanaume ameitwa majina ya kike kama Robi, Bhoke, gati, nyambura na kadhalika. Mf. yule mzee alohudumu katika serikali ya mwalimu aliitwa BHOKE Munanka. Bhoke ni jina la kike.

  Mojawapo ya sababu za kuitwa hivo ni kama vile mwanamke ambaye ameolewa na akapata mateso sana toka kwa mumewe na hivo kabla hajauacha mwili huwa anatoa wosia kuwa atakapokufa YEYOTE KATIKA FAMILIA NA UKOO WAKE ATAKAYETAKA KUMUITA (mtoto atakayezaliwa) BASI AMUITE MWANAUME. KWA MAANA YA KUWA akizaliwa mtoto wa kiume aitwe jina lake kama Bhoke n.k. kwa kuwa hataki kuteseka tena katika maisha yajayo. Atakayemuita mwanamke mtoto huyo hataishi.

  Uzoefu unaonesha kweli kuwa watoto wote wa KIKE waloitwa majina ya bibi zao (ilihali walitaka waitwe majina yao kwa watoto wa kiume) watoto hao huwa hawaishi kwa kuwa huwa wanakufa vifo vya ajabuajabu hata kabla ya miaka miwili.

  Kama wazazi wakiona hitlafu na wakakumbuka mapema na kuwabadilishia majina hupona :-(

  Mpaka sasa sina hakika kama naweza kujua nguvu ya jina katika kuhuisha na kutoa uhai wa mtoto.

  Kwa hiyo, Da Mija anayo ruksa ya kumuita mtoto wake wa kiume jina la kike KAMA TU BABA WA MTOTO NI MKURYA....lol

  ReplyDelete
 8. Ng'wanambiti - mfano na ufafanuzi mzuri. Lugha inaamuliwa na jamii na huu mfano wenu Wakurya ni mfano mzuri sana. Da Mija - fanya utafiti wa kina uone kama binti anaweza kuitwa Sayi Usukumani, Farida kwa Waswahili au Margareth kwa Wazungu. Naamini kuna makabila mengine yenye vighairi (exceptions) katika majina ya kike na kiume na siyo Wakurya peke yao....

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU