NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, March 25, 2010

"BLOGGING FOR DUMMIES" NA ELIMU YETU YA JADI

 • Leo katika pitapita yangu katika duka moja la vitabu nilikutana na kitabu hicho juu. Niliamua kukisoma na nilishangaa kugundua kwamba mambo mengi ya msingi yanayozungumziwa humo tayari ninayafahamu. Na kama ilivyo kwa wanablogu wenzangu wengi, hakuna aliyetufundisha kublogu na wala hatukuhitaji kusoma vitabu. Tulianza tu, tukajifunza kwa vitendo na sasa tunaweza - kwa kiwango chetu. Tunapokwama tunakimbilia kwa "mkombozi" wetu Dada Subi. Hivi pia ndivyo wengi wetu tulivyojifunza kutumia kompyuta. Hatukuhitaji kusoma vitabu. 
 •  Kimsingi hii ndiyo ilikuwa elimu yetu ya Kiafrika ambayo ilikuja kuvurugwa na wakoloni. Sisi hatukuhitaji kusoma vitabu bali elimu yetu ilikuwa ni ya vitendo na iliyoendana vyema na mazingira yetu. 
 • Japo bara letu liliitwa kuwa la giza na lenye watu wasio na historia wala ustaarabu (kwa vile historia yetu ilikuwa haikuandikwa), leo hii watu wengi wanasaili uamilifu wa elimu tuliyoletewa, elimu ambayo, pamoja na faida zake nyingi, mara nyingi imeonekana kuwa ni dhahnia sana na  isiyo na uhusiano wa moja kwa moja na mazingira yetu.  Mara nyingi elimu hii haimwandai aipataye kwenda kupambana na mazingira na ulimwengu halisi.
 • Elimu ya kweli ni lazima izingatie misingi hii ya elimu yetu ya kiasili na naamini kwamba lilikuwa ni kosa kutupilia  mbali kila kitu tulichokuwa nacho katika elimu yetu ya jadi. Kusoma vitabu tu darasani bila kuelewa maarifa hayo ya vitabuni yana faida gani katika ulimwengu halisi na mazingira yetu ni kuelimika nusunusu tu.
 • Watunga sera za elimu inabidi wazingatie ukweli huu kama kweli wanataka kuwa na taifa la wananchi WALIOELIMIKA! 

2 comments:

 1. Kitendo cha kuvidharau vitabu vyetu wenyewe vilivyoandikwa na watu wetu kwa lugha yetu si cha kiungwana hata kidogo. Vitabu vile ambavyo vilikuwa vya manufaa sana na baadaye 'wenye akilli na waliosoma' wakaona havifai ni hazina ya pekee na utambulisho nambari wani wa kujivunia na kupinga dhana ya kuwa sisi hatukuwahi kuchapisha vitabu vyetu tangu karne zilizopita. Hivyo ni vitabu ambayo vingeongeza tofali katika ujenzi wa historia thabiti. Niliudhika na kukasirika sana Waalimu walipopewa amri ya kuondosha vitabu walivyoviita wao, 'vya zamani' toka stoo na maktaba na kuvipeleka majalalani au kuvichoma moto ili kupisha nafasi ya kuweka vitabu ''vipya, vya kisasa toka ng'ambo vinavyoendana na wakati', nadhani kujuta kwangu sasa kutakuwa maradufu kadiri siku zinavyopita.

  Chako ni chako na ndicho cha kujivunia, huwezi kujivunia cha mwingine. Chako kipende, kitunze ili kikutunze.

  Mi nachukia(ga)!

  ReplyDelete
 2. Hivi unajua kuwa watu hawanunui vitu vya asili na hata "MADE IN TANZANIA" wakitaka mayai ya kizungu na Made in naniliiii???
  Tunakimbia vivuli vyetu

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU