NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, March 12, 2010

KITABU CHA UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA CHA MWL. NYERERE SASA KINAPATIKANA MTANDAONI!


 • Leo katika pitapita yangu mtandaoni nilikutana na habari nzuri zinazohusu kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere na kuchapishwa na Zimbabwe Publishing House mwaka 1994. Kitabu hicho sasa kinapatikana mtandaoni na unaweza kujipatia nakala yako hapa.
 • Inasemekana kwamba Mwalimu Nyerere mwenyewe alishindwa kukichapishia nchini Tanzania kwani hakuna mchapishaji aliyetaka kukigusa ndiyo maana ikambidi akimbilie Zimbabwe kwa rafiki yake Mugabe.
 • Kitabu hiki pia hakipatikani kwa urahisi nchini Tanzania na kuna tetesi zisizothibitishwa kwamba eti kimepigwa marufuku. Kama tetesi hizi zina ukweli wo wote, basi nitashangaa kwani hakuna neno baya la kushangaza ambalo Mwalimu Nyerere analizungumza katika kitabu hiki. Mimi nilikinunua kwa bahati jijini Dar es salaam mwaka 1994 na nakumbuka muuza duka la vitabu aliyeniuzia aliniuzia kwa siri sana.
 • Ni kitabu ambacho kinafaa kusomwa na kila Mtanzania bila kujali itikadi yake ya kisiasa. Na kama nilivyowahi kugusia hapa, video, kaseti na vitabu vyote vya Mwalimu Nyerere vinapaswa kutazamwa kama hifadhi ya historia ya taifa letu na ni vyema vikakusanywa na kuwekwa mahali pamoja ambapo kila Mtanzania (au mtu yeyote duniani) ataweza kuvisoma. Kidogo inashangaza kusikia eti vitabu vya Mwalimu na hotuba zake hazipatikani; au zimefichwa katika makabrasha ya Redio Tanzania na kwingineko. Jamani, Mwalimu Nyerere ni hifadhi na hazina ya Watanzania wote na msijimilikishe kazi zake na kuzificha kwa manufaa yenu binafsi.
 • Baadhi ya nukuu muhimu kutoka katika kitabu hiki zinapatikana hapa na hapa. Unaweza pia kusikiliza hotuba mbalimbali za Mwalimu hapa. Na sasa unaweza kupata nakala yako ya kitabu kizima cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania hapa. Asanteni "wanaume" wa Jamii Forums kwa kuweka nakala ya kitabu hiki katika mtandao. Mungu Ibariki Tanzania!

3 comments:

 1. Kaka Matondo, nilipoisoma tu post yako, nikai-minimize. Kisha fastafasta nika-log in Jamii Forums. Sikupoteza muda, nika-download kwanza file lenye kitabu.
  Sasa nime-maximize post yako kwa lengo moja tu muhimu.
  Kusema ahsante sana kwa taarifa hii muhimu sana.
  Umenisaidia kwa kiasi kikubwa. Ntakesha nakisoma kitabu hiki.
  Ahsante sana!

  ReplyDelete
 2. Bwana Fadhy - ni kitabu kizuri na ndiyo maana mimi nashangaa kwa nini hakipatikani kirahisi huko nyumbani. Kinaonyesha jinsi mwalimu alivyokuwa hapendi mchezo na hakuogopa kukemea maovu hata kama yalikuwa ndani ya nyumba aliyoijenga yeye mwenyewe.

  Naamini kwamba baada ya kumaliza kukisoma, utakereketwa kusema kitu katika kijiwe chako.

  Asante kwa shukrani zako. Lakini pengine shukrani hizo zinastahili ziwaendee jamaa wa Jamii Forums kwa kuiweka hii nakala mtandaoni. Naona hakina hata hati miliki na nadhani Mwalimu mwenyewe alifanya hivyo makusudi. Kwa hivyo hakuna kukoromeana bila sababu!

  ReplyDelete
 3. Mrisho Mpoto ana sema 'ya hadharani tunaficha, ya sirini twaweka wazi'. Sina hakika na kama ni hulka ya serikali ama walio katika serikali.

  Kwa keli kazi tunayo!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU