NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, March 24, 2010

LUGHA TUNAYOTUMIA INAONYESHA UNDANI WETU: TUWE WAANGALIFU

 • Misahafu mbalimbali inaonya kuhusu hatari za ulimi; kwamba ni kiungo kidogo lakini madhara yake ni makubwa. Wanasaikolojia wengi na "watenda miujiza" wanaamini kwamba maneno yana nguvu (unakumbuka mambo ya laana?). Inasemekana kwamba hata dunia iliumbwa kwa maneno tu!
 • Wanaisimu jamii pia hudai kwamba lugha anayotumia mtu inaweza kumwonyesha yeye ni mtu wa tabaka gani katika jamii hiyo. Kwa hivyo, kama wewe ni mtu wa tabaka la juu, jamii inakutegemea uongee kwa mtindo fulani unaolitambulisha tabaka lako. Kama wewe ni kiongozi, jamii pia inakutegemea kutumia lugha fulani inayoakisi wadhifa wako katika jamii. Na kama wewe ni mwanamuziki wa kizazi kipya/Bongo fleva/kufokafoka kuna mitindo fulani ya lugha inayokutambulisha ambayo pengine kiongozi au mtu wa tabaka la juu hategemewi kuizungumza.
 • Suala hili limeibuka hapa Marekani baada ya makamu wa Rais Joe Biden kutumia neno "fuck" wakati akimpongeza bosi wake (Obama) kwa kufanikiwa kupitisha sera mpya tata ya mfumo wa matibabu. Kama Snoop Dogg au 50 Cent angelitumia neno hili, nadhani pengine hakuna ambaye angejali sana lakini halitegemewi kutamkwa na makamu wa rais.
 • Tuwe waangalifu na lugha tunayotumia. Maneno yanaweza kuumiza na kuleta makovu ya kisaikolojia yasiyotibika. Msikilize Joe Biden hapa na watu wengine waliowahi kutumia lugha isiyo mwafaka kulingana na matabaka yao hapa na kuibua mijadala mikali. 

  5 comments:

  1. Hili suala lina utata sana, ila daima limenivutia. Nimesikiliza hiyo taarifa juu ya Mheshimiwa Joe Biden.

   Mazingira yaliyomfanya akasema hilo alilosema naona yanaufanya usemi wake univutie. Usumbufu walioupata hadi kufikia hatua hii ya kusaini hii sheria yalikuwa magumu sana. Mtu unapokamilisha kazi ngumu na tata namna hii unaweza kusisimka hadi kutamka jambo ambalo hukupangia.

   Kwa mfano, wakati wa mechi kali ya mpira, ambapo roho za mashabiki zinakuwa juu, na wasi wasi mwingi na mihemko, ikitokea ghafla mchezaji aliyekuwa na nafasi ya kufunga goli akapiga mpira lakini ukakosa kuingia wavuni, mashabiki wanapayuka maneno mengi ya ajabu bila kupangia. Au goli likifungwa, mashabiki wa pande zote wanapayuka maneno ya ajabu. Na mchezaji anayekosa kufunga naye anaweza akatoa "matusi" ya ajabu dhidi ya kitendo chake.

   Hayo ni vigumu kukwepeka. Lakini inavyosemekana ni kuwa Mzee Biden kazoea, na ndio maana watu wanamwandama namna hiyo.

   Neno ambalo ni baya linaweza kuwa na maana nzuri katika muktadha mwingine. Kwa mfano, tunapomwona mwanamuziki akipiga gitaa kwa ufundi wa ajabu, tunasema anapiga gitaa "kama hana akili nzuri."
   Tulipokuwa vijana, tulikuwa tunasema "yule jamaa kwa somo hili ni mshenzi kweli." Au "yule jamaa kwa somo hili ni mwanaharamu kweli."

   Kwa kawaida, hilo neno alilotumia Mheshimiwa Joe Biden linatumiwa na watu wa vijiweni. Kwake yeye kulitumia nimeona ni kichekesho kwa kiasi kikubwa. Nadhani watu watakachofanya ni kuendelea kumsanifu tu, lakini bado wanamwona ni mtu wa heshima, pamoja na haka katatizo kake ka kuropoka.

   ReplyDelete
  2. Profesa Mbele. Asante kwa maoni yako ambayo yamegusia mambo mengi ya msingi. Nimeipenda mifano yako.

   CNN wamekusanya sehemu mbalimbali ambazo Biden aliwahi "kuropoka". Hata Dick Cheney naye enzi zile aliwahi kumtukana jamaa mmoja Democrat bila kuelewa kwamba vinasa sauti vilikuwa laivu. Tazama hapa: http://www.cnn.com/video/?/video/offbeat/2010/03/23/moos.biden.f.bomb.cnn.

   Ulichokigusia hapa ni ule ukweli kwamba kujifunza lugha ni pamoja na kujua muktadha wake wa kimatumizi na kuuzingatia. Lugha ya sokoni, michezoni, darasani, kwenye baa, mazishini na ofisini kwa daktari zinatofautiana. Mzungumzaji asiyelielewa hili ni lazima ataingia katika matatizo. Wanaisimu jamii wanasema kwamba matumizi sahihi ya lugha yanaathiriwa na sababu mbalimbali zikiwemo hizi wanazoziita "6 Whs": Who speaks what to whom, when, where and how.

   Tatizo ni kwamba watu wengine wanaweza wasielewe muktadha na hisia na mihemko ambamo lugha fulani imetumiwa. Ni wazi kwamba Bwana Biden alikuwa na nia njema alipotumia hili neno na ni wazi kwamba alikuwa anampongeza bosi wake. Wasikilizaji na watazamaji wengi hata hivyo wanaweza kabisa wasilione hili na wao wakaishia tu kugubikwa na ukweli kwamba lugha kama hii ni ya watu wa tabaka fulani na kamwe haipaswi kuzungumzwa na mtu wenye wadhifa mkubwa kama yeye katika mazingira na muktadha wo wote ule. Na hapo ndipo kasheshe inapoanzia.

   ReplyDelete
  3. Huyu mheshimiwa kila asimamapo mbele ya mic huwa nakuwa makini. Huwa "anapitiliza" saana na si katika matusi, bali kuongea kisha akafikiria.
   Na ukifuatilia kwa makini, utagundua kuwa Ikulu ya Marekani imemdhibiti saana katika mahojiano na hiyo ni kutokana na "kusema hisia zake" bila kujali athari zinazoweza kutokea baada ya hapo.
   Asanteni saana waalimu kwa mada na maoni yenu.
   YANAELIMISHA

   ReplyDelete
  4. Luugha!
   Hiki kitu kimesababisha mpaka kuna ndugu zangu hawasomi blogu yangu.:-(

   MArekani huwa inanishangaza kwa maana aongeavyo Obama kuna wadaio ni elitist na kumchukia na kuna wadaio anaongea proper kama Mzungu na kumzimia.

   Hapo hapo inasemekana hata kuna waliompenda George Bush kwa kuwa walidai huongea kama mwenzangu na mimi ambaye unaweza kujisikia kunywa naye bia na kumpenda na kudai Al Gore anaongea kama mtu wa tabaka la juu na kumchukia.

   Sasa hapo ndipo moja ya sababu kwangu LUGHA + tabaka + USA =Kunichanganya.:-(

   ReplyDelete
  5. heri kujikwaa kidole kuliko kujikwaa ulimi, wahrnga walisema

   ReplyDelete

  JIANDIKISHE HAPA

  Enter your email address:

  Delivered by FeedBurner

  VITAMBULISHO VYETU