NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, March 8, 2010

NAKUMBUKA SIKU NILIYOGEUZWA "DARASA" KABLA YA OPERESHENI KUBWA PALE MUHIMBILI

 • Mwaka 1993 nilifanyiwa upasuaji mkubwa wa sikio langu la kulia pale Muhimbili. Nakumbuka ilikuwa ni asubuhi majira ya saa mbili nilipopelekwa katika chumba cha upasuaji. Taa zinazong'ara sana zilikuwa zikiwaka na manesi walikuwa wanamaliziamalizia kuandaa vifaa.
 • Mara waliingia madaktari wawili wakanisalimia na kuniulizia kama nilikuwa tayari kwa operesheni ile. Niliwajibu kwamba nilikuwa najisikia vizuri sana na kwamba sikuwa na woga. Niliwaambia kwamba sikio hilo lilikuwa limenisumbua mno kuanzia utoto na nilikuwa tayari kuhakikisha kwamba tatizo hilo linatatuliwa.
 • Nilipimwa joto, shinikizo la damu na vipimo vingine. Daktari anayeshughulika na ganzi pia aliingia. Timu nzima ilikuwa imekamilika - madaktari wawili bingwa, mmoja wa ganzi na wasaidizi watatu - wote katika mavazi meupe yaliyong'ara na kuwafanya waonekane kama malaika. Muda si mrefu ujao, maisha yangu yangekuwa mikononi mwao.
 • Wakati nikisubiri operesheni hiyo kuanza waliingia watu wengine kama wanane hivi - wote wakiwa wamevaa majoho yale yale meupe. Mara moja nilitambua kwamba hawa walikuwa ni wanafunzi wa udaktari. Nilikuwa sahihi kwani mara moja darasa lilianza.
 • Daktari kiongozi alianza kuwaambia tatizo langu lilikuwa ni nini na visababishi vyake. Baada ya hapo aliendelea kuwaelekeza hatua za kufuata katika operesheni ile. Aliwaambia kwamba operesheni inachukua kati ya masaa mawili na nusu hadi matano. Kwamba ilikuwa ni operesheni ya hatari na uwezekano wa mgonjwa kufa, kupofuka au kuwa kiziwi wa kudumu ulikuweko. Aliendelea kuwaambia kwamba tatizo lilikuwa ni "gland" moja iliyokuwa ndani kabisa karibu na sikio la ndani na kazi yao ilikuwa ni kutafuta mzizi wa gland hiyo na kuung'oa kabisa. Gland hiyo korofi ilikuwa inatoa kemikali ambazo mwili ulikuwa hauzitambui na hivyo kusababisha sikio na kichwa kizima kuvimba kila mwaka. Aliendelea kuwaambia wanafunzi wake kwamba sehemu iliyopo gland hiyo ilikuwa imezungukwa na mifumo tata ya neva mbalimbali (zikiwemo za macho, sikio la ndani na za mfumo wa fahamu) pamoja na mirija mingi sana ya damu. Kwa hali hiyo kosa lolote dogo, lingeweza kuleta matatizo makubwa.
 • Baada ya darasa lile, yule daktari wa ganzi aliniuliza kwa mara ya mwisho kama nilikuwa tayari. Nilipotikisa kichwa kuashiria ndiyo, basi aliniwekea kifaa cha kupumulia mdomoni na kuniomba nihesabu mpaka 10. Nadhani hata tano sikufikisha. Nilikuja kupata fahamu majira ya saa saba mchana nikiwa kwenye eleveta nikirudishwa wodini. Operesheni ilikuwa imefanikiwa!
 • Inabidi niseme hapa kwamba maelezo ya darasa lile yalinitisha sana; na kidogo nilijisaili kama ilikuwa sawa kisaikolojia kwa daktari yule kutoa darasa la aina ile mbele ya mgonjwa tena anayekaribia kufanyiwa upasuaji hatari kama ule. Isitoshe, habari karibu zote zilikuwa ngeni kwangu. Nilibaki nikijiuliza, mbona sikuambiwa mambo haya mapema?
 • Nilipofika hapa Marekani na kuwaambia watu mkasa huu hawakuamini na waliniambia kwamba nilikuwa natania. Eti jambo kama hilo haliwezi kutokea. Niliambiwa kwamba hapa mahospitali hununua maiti kwa masomo yo yote yanayohusu mazoezi ya ana kwa ana/vitendo.
 • Baadaye nilikuja kugundua kwamba daktari bingwa profesa aliyenifanyia upasuaji ule na aliyefundisha darasa lile asubuhi ile njema ni mmojawapo wa madaktari bora kabisa kwa matatizo ya masikio na pua nchini Tanzania. Nilipokwenda kufanyiwa uchunguzi baada ya kufika hapa Marekani, madaktari waliniambia kwamba operesheni niliyofanyiwa kule Muhimbili ilikuwa imefanyika vizuri mno na hakukuwa na uwezekano wo wote wa tatizo lililokuwa likinisumbua kujirudia tena.
 • Japo sikulipenda darasa lake, daima huwa namshukuru na kumwombea daktari profesa bingwa aliyenifanyia upasuaji ule uliofanikiwa. Isitoshe, nikiwa kama mwanafunzi wa chuo kikuu, operesheni ile nilifanyiwa bure. Nimeambiwa kwamba hapa Marekani operesheni kama hiyo inaweza kugharimu zaidi ya dola 20,000!
 • Isitoshe, ni kutokana na operesheni hii hatimaye niliweza kukutana na ubinadamu wa kweli pale Muhimbili, tukio ambalo liliniathiri sana na kubadili mtazamo wangu kuhusu maisha na nafasi yetu hapa duniani kama binadamu!

18 comments:

 1. Prof Matondo,
  You just made my day.
  Nitaipelekea hii kwenyewe jikoni.
  Umeleta heshima ingawaje kuna kukwazika kidogo ulikokupata, bado hiyo haikuzuia kutoa heshima katika taaluma ya afya. Naam, nimejifunza jambo hapa. Thanks for sharing!
  Sasa wacha nikopi na kushea na wenyewe - MUCHS alumni.

  ReplyDelete
 2. kisa hiki kina sura tatu: kutisha, kuchekesha na kupata tiba sahihi na la muhimu kushukuru na kumuombea daktari bingwa huyu.

  lakini mbali na kununua maiti kwa ajili ya shughuli kama hii huko marekani, hivi isingewezekana profesa kuendelea na somo lake ukiwa nusu kaputi? ya ngoswe muachie ngoswe. labda somo linaingia kielelezo (yaani wewe) kikiwa na fahamu zote.

  ReplyDelete
 3. Mtu mwingine angesikia hayo lazima angeogopa sana, labda na shinikizo la dam likapanda na operesheni yenyewe isifanyike, pole sana na tumshukuru MUNGU ulipona salama

  ReplyDelete
 4. Asante kwa kunitembelea mkuu. Tuko pamoja kuijenga nchi!

  ReplyDelete
 5. duh, safi sana, ila somo kubwa ni KUKUTANA NA UBINADAMU WA KWELI ambao kwa kuuweka bloguni pia umenibadilisha na mimi pia

  ReplyDelete
 6. duh!!! funny and unbelieveable at the same time, kwanini asingefundisha darasa lake baada ya kukulaza? (anaesthetic) maana ingekuwa mimi hapo baada ya maelezo yake ningekimbia! Hehe. Good thing your are fine kaka

  ReplyDelete
 7. MMh vinyweleo vyangu mwili vimisisimka inatisha kidogo,sijui taratibu zinakuwaje huku Uk huwezi kuletewa wanafunzi bila ruhusa yako mgonjwa kama uko ok,kwa wanafunzi kuwepo wakati wa matibabu yako au wakati wa kufanyiwa vipimo.

  Pili naona Madaktari wa huku wako wazi sana kwa wagonjwa tofauti kidogo na nyumbani,mgonjwa unaweza usiambiwe akaambiwa ndugu yako wakaribu matatizo yako kiundani kuliko wewe mwenyewe,sasa sielewi labda ni mimi tu nimeelewa hivyo kutokana na kushuhudia hilo au niko sahihi sina hakika.

  Pole sana kaka ila hakika huyo Daktari bingwa anastahili pongezi kwa kazi yake nzuri aliyoifanya na anaendelea kufanya, mungu ampe maisha marefu ili azidi kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.

  ReplyDelete
 8. Mimi nadhani pengine mtafaruku huu ulitokana na mkanganyiko wa lugha. Kwa vile darasa lilikuwa linafanyika katika Kiingereza (tena kilichochangayika na ile misamiati kamambe ya kitiba), inawezekana Profesa Daktari Bingwa yule alidhani kwamba nilikuwa sifahamu Kiingereza (sawasawa) kama ilivyo kwa Watanzania wengi. Na kama nisingeweza kuielewa mada, basi kusingekuwa na tatizo lolote.

  Japo kweli darasa lile lilikuwa na misamiati migumu ya kitiba ambayo sikuielewa, lakini niliweza kuifuatilia mada vizuri sana. Na huo ndio ulikuwa mwanzo wa tatizo. Sidhani kama darasa lile lingeweza kufanyika kama Profesa angejua kwamba nami mgonjwa wake nilikuwa nanyaka kile alichokuwa akikifundisha! Sijui kama hili ni jambo la kawaida katika utamaduni wetu.

  Nitarudi baadaye kubwagiza maoni yenu. Asanteni!

  ReplyDelete
 9. Ndugu yangu Matondo, mimi nasema pole. Nasema kama mtaalamu wa tiba aliyebobea, kwani kwa sasa mimi ni consultant katika kitengo cha macho upande wa retina. Mwaka 1993 nilikuwa hapo hapo Muhimbili nikichukua shahada yangu ya kwanza ya tiba, sijui ni wakati gani lakini nilikuwa kati ya mwaka wa 3 au 4 wa masomo. Naweza kukuambia haikuwa sawa hata kidogo kutoa darasa la namna hiyo mbele yako wakati wewe ukiwa hujui kwa undani umuhimu wa upasuaji huo na madhara yanayoweza kutokea iwapo kutatokea tatizo.
  Wakati huo maprofesa wetu walikuwa wanawachukulia watu kuwa hawana sababu ya kujua nini kinawasumbua, pia kuna baadhi walikuwa wanataka kuonekana ni wao tu ndio wanajua, baada ya kumaliza shahada yangu ya kwanza 1995, utamaduni huo niliuondolea mbali, na nilikuwa nazungumza na wagonjwa wangu kila kinachotakiwa kuelezwa kwa wote, pamoja na hayo changamoto niliyokuwa nakutana nayo ni wagonjwa wenyewe kutokuwa tayari kuelezwa kinaga ubaga na kunilazimu kueleza angalau ndugu mmoja tu, maana ethics nilikuwa nazijua. Hata wakati nimeenda kuchukua shahada ya uzamili, nilikuta hali bado ni ileile kwa wananchi kutokuwa na mwamko wa kujua masuala mazima ya afya zao, na pia wataalamu walikuwa hawafafanui nini wanachofanya. Pamoja na kwamba nilipunguza uwigo wa magonjwa kwa kuwa specialist, bado nilikuwa najitahidi kutoa elimu. Labda ni Bahati mbaya baada ya kupata shahada nyingine tena baada ya uzamili (masters)ambayo imenipunguzia sana uwezekano wa kukutana na watu tofauti, nimeishia kujikita kwenye sehemu inayonihusu zaidi, kwa wale wanaojua basi nipo kwenye vitreo-retinal field. It is a complex field, kama ukiona hauielewi, basi usidhani wewe ni kilaza.
  Lakini nahitimisha, ya kuwa bado hatuwatendei haki wagonjwa, na wagonjwa bado hawaijui haki yao ya msingi, wengi ukiwapa facts, wanahama na kwenda kwa yule anayewapa fix kujua ya kuwa wapo fit wakati ..... Ndio mwendo mdundo huo.

  ReplyDelete
 10. Hatuwezi kujua labda kuna kitu Mungu alitaka ujifunze kama si sasa labda hapo baadaye.

  @Chib samahani kwa kuwa kilaza, Siku moja nikitoka kumchukua mwanangu shule tulipigwa na baridi ile mbaya, sasa mwanangu akanitupia swali kwamba kwa nini macho hayasikii baridi? na wakati nikiwa natafuta jibu akaniongezea swali, Je macho yamo ndani au nje ya mwili? Nikamuuliza kwa nini unauliza hivyo akasema kwasababu kama yamo ndani ya mwili labda ndiyo sababu hayasikii baridi.

  Haya naomba darasa hapo maana hadi leo bado sijampa jibu kamili.

  ReplyDelete
 11. @damija a.k.a Kilaza, usipokuwa makini katoto kako katakuuliza maswali ya aibu mbele ya wakwe!! Natania Tu japo inawezekana

  ReplyDelete
 12. Da Mija.. DUH! Natumaini Kaka yangu Matondo ataruhusu nichemke ndani ya blogu yake, Mara chache nimeweza kukutana na maswali kutoka kwa watoto ambayo hubaki naduwaa tu, mwaka 2003 nilipoenda nyumbani Mwanza nilibanwa na swali la mtoto ikabidi nimnunulie makamilwa na sungwi kumpongeza.
  Kwa ufupi jicho limejaliwa kuwa na neva chache zinazotambulisha hali ya ubaridi, na pia limejaliwa kuwa na kifuniko kilichojaa mishipa ya damu (eyelid), na wajua joto husafirishwa na damu. Baridi ikizidi watu hupunguza sehemu ya jicho kwa kulifinya kidogo, na hivyo kupunguza uwazi na wakati huohuo eyelid huleta joto kiasi.
  Pia aliyeumba miili ni mwerevu sana, viungo vingi alivyoviweka nje mara zote uhitaji joto kidogo au hali ya ubaridi wa wastani ili ziweze kuwa na kazi itakiwayo. Jicho ni mojawapo, na ndio maana lina mfumo tofauti wa damu na mwili wote, na cha kufurahisha, ni kuwa jicho ni dirisha la karibu kila mfumo uliopo ndani ya mwili. Matatizo mengi ya mwili unaweza kupima ndani ya jicho ukatambua kuwa mtu huyu ana shida kwenye ubongo, mfumo wa damu nk. Naomba niishie hapa

  ReplyDelete
 13. Hapo nimepigwa na mabomu. Mimi ni mmoja wa watu wavivu sana kuuliza ninachoumwa, in fact naogopa kuambiwa unaumwa hivi, sijui utakufa au.... Yahitaji moyo ndugu

  ReplyDelete
 14. Yawezekana ukafa kwa kihoro tu kwa maneno ya daktari.

  Lakini pia waweza kufa kwa kihoro baada ya kuwaona wagonjwa wenzako wenye tatizo lako ambao wamefanyiwa upasuaji na kuona hawarejei wodini kukupa UZOEFU wa kaputi bali wasikia WAMITANGULIA :-(

  ReplyDelete
 15. Na Matondo: si yawezekana ushageuzwa 'darasa' hata na wanao achilia mbali wanafunzi wako mwenyewe? ..lol

  ReplyDelete
 16. Asante MKubwa kwa kunitembelea mzee wa cape town hapa nakutakia siku njema

  ReplyDelete
 17. @Kamala inawezekana kabisa.

  @Chib asante kwa jibu nimeshamwelewesha na muuliza swali. Ila umenikumbusha mbali juu ya Sungwi na Makamilwa, hivi matunda haya yanapatikana Mwanza tu au? Maana sijayaona sehemu nyingine.

  ReplyDelete
 18. pole profesa habari inatisha tisha hivi MUNGU ashukuriwe kwamba ulitoka salama

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU