NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, March 7, 2010

UTAFITI: CCM KINARA WA RUSHWA WAKATI WA UCHAGUZI. HEBU TUTAFAKARI!!!

 • Mbali na mambo mengine utafiti uliotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam pamoja na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURURU) unaonyesha kwamba CCM ndiyo chama kinachoongoza kwa rushwa wakati wa uchaguzi (49.5%) kikifuatiwa na CHADEMA (7.0%) , CUF (2.7%), NCCR Mageuzi (0.5%) na TLP (0.5%).
 • Nijuavyo mimi ni kwamba tumefikia mahali sasa ambapo hata wapiga kura wetu wanategemea baisikeli za bure, kanga, vitenge, chumvi, vyerehani, mabati, saruji, pikipiki, sukari na ahadi tamu zisizotekelezeka. Ni wazi kwamba bila kutoa rushwa ya vitu hivi, kamwe hutapata kura hata kama uwe na sera nzuri na uadilifu wa kupigiwa mfano.
 • Kama hali ndiyo hii, ni nani wa kulaumiwa kwa kosa hili? Ni mgombea ubunge/uraisi anayetoa rushwa na ahadi za uongo huku akijua kuwa bila kufanya hivyo hatapata kura au ni mpiga kura ambaye hatoi haki yake ya kikatiba bila kupewa kitu kidogo?
 • Mimi nadhani siyo sawa kuvibebesha lawama vyama vya siasa au wagombea pekee wakati hili ni tatizo la jamii nzima, tatizo ambalo mimi naamini kiini chake ni umasikini na ukosefu wa elimu makini na itikadi kombozi kwa wanajamii. Wanajamii wakifahamu kwamba hizi pea za kanga wanazopewa si za bure na ndizo zinachochea moto wa ufisadi unaoendeleza kudumaza maendeleo yao, mambo yatabadilika. Bado safari ni ndefu!
 • Taarifa kamili ya UDSM na TAKURURU niliyoirejelea hapo juu inapatikana hapa. Niliwahi pia kuligusia suala hili hapa.

2 comments:

 1. Profesa,naafikiana nawe kwa asilimia 100 kuwa wapiga kura hawawezi kukwepa lawama katika suala hili la rushwa.Hata hivyo,binafsi nimekuwa muumini wa theory ambayo sina uhakika wa jina lake.Naomba niielezee kidogo.Binafsi naamini kuwa umasikini wa Watanzania walio wengi unawanufaisha wanasiasa wetu kwa namna flani.Ni mithili ya symbiotic relationship between crime and law enforcement.Kwamba uhalifu ukifuika kabisa,vyombo kama polis na mahakama vitakosa kazi (arguably).

  Ni dhahiri watawala wetu wanafahamu kuwa pindi walalahoi wakijitanzua kutoka katika minyororo ya umasikini unaopelekea wengi wao kuwa na imani potofu kwamba "mkono kwenda kinywani ni muhimu zaidi ya ubovu wa mgombea" basi hizo pishi za mchele,doti za kanga na "takrima" kama hizo hazitaweza kuwa mbadala wa sifa sahihi za anayepaswa kuwa kiongozi.

  Hapa Uingereza kuna hekaheka za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika miezi michache ijayo.Na nikiangalia namna vyama vya siasa vinavyohangaika kuuza sera zao,kisha nikalinganisha na hali ya huko nyumbani,nazidi kushawishika kwamba jeuri ya watawala wetu inaimarishwa zaidi na ufahamu wao kuwa wengi wa wapiga kura wanaweza kughilibiwa kirahisi kuwapigia kura "wagombea wa ahadi" (yaani wanaoahidi kufanya hili na wasifanye wakishachaguliwa lakini wakaja na ahadi hizohizo kwenye uchaguzi mwingine huku wakiziboresha na hiki na kile).

  Ni kweli wapiga kura hawawezi kukwepa lawama kwa uamuzi wao wa "kuuza haki zao" wanapopokea vijizawadi kutoka kwa wagombea dhaifu.Lakini kama alivyosema Karl Marx,mlalahoi hana cha kupoteza zaidi ya nira iliyo shingoni mwake.Wakati Waingereza muda huu wanawapima wagombea kwa uwezo wao wa kuongoza,yayumkinika kusema kuwa kwa huko nyumbani wapiga kura wanaangalia mgombea atatoa nini kuwashawishi wampigie kura.Kwa mlalahoi,leo ni sawa na uhai wake wote,lakini kwa mwenye kujimudu,leo ni siku moja inayofuatiwa na kesho,keshokutwa na kuendelea.Yaani kwa masikini,ufumbuzi wa muda mrefu ndio prority yake kubwa (hata kama sio sahihi kufanya hivyo) na ndio maana doti ya khanga inayotolewa na mgombea wakati wa kampeni inaonekana kuwa muhimu zaidi kuliko madhara atakayosababisha katika kipindi cha uongozi wake.

  Nadhani walalahoi wanapaswa kuelewa kuwa utatuzi wa matatizo ya muda mfupi haupaswi kuwa muhimu zaidi ya utatuzi wa matatizo ya muda mrefu.Kwahiyo takrima zinazoweza kuwafanya wajiskie "vigogo kwa masaa/siku kadhaa" hazipaswi kuwatia "upofu wa muda" katika kutathmini ufanisi wa mgombea.

  Samahani kwa maoni marefu,Prof.

  ReplyDelete
 2. Bwana Evarist;

  Philip Mangula, katibu Mkuu wa CCM wa zamani aliwahi kuonya: “Itafika mahali kura zitakuwa kama mnada, mwenye pesa nyingi ndio mshindi” Nadhani tumeshafikia hatua hii.

  Wakati wa uchaguzi uliopita nilikuwa nyumbani Bariadi kwa siku chache na niliyoyaona huko ndiyo yalinifanya nibadili msimamo kuhusu nani anayepaswa kulaumiwa kuhusu rushwa wakati wa uchaguzi. Kampeni za uchaguzi zilikuwa zimegeuka ndiyo shughuli ya kiuchumi na watu walikuwa hawaendi tena katika shughuli zao za kawaida. Wanakijiji walikuwa wamemakinikia kufuatilia kampeni za wagombea kutoka kijiji kimoja hadi kingine ili tu waweze kuambulia vipande vya kanga na zawadi zinginezo zilizokuwa zikigawiwa. Baadhi ya vijana wajanja waliweza kuambulia pikipiki na hata mitaji kabisa ya kuanzishia miradi mbalimbali ya kijasiriamali. Wapiga kura sasa wamefikia hatua ya kuamini kwamba rushwa ni haki yao; na hili halipaswi kuwa jambo la kushangaza kwa jamii iliyotawaliwa na rushwa kubwa na ndogo kila mahali.

  Kama ulivyogusia hapo juu, tatizo kubwa ni umasikini, “elimu ndogo” na ukosefu wa mwamko wa kiitikadi. Kama wenyewe wasemavyo “There is no free lunch,” wapiga kura hawa inabidi watambue kwamba zawadi hizi wanazopewa wakati wa uchaguzi ni deni ambalo ni lazima watalilipa hapo baadaye. Ni lazima watambue kwamba kuna mtu aliyetoa hizi pesa na wagombea hawa ni lazima wayarudishe mamilioni ya watu baada ya uchaguzi kupita. Na kwa mtindo huu ni ndoto kuutokomeza ufisadi.

  Pengine ndiyo maana bado wanalichukulia suala la ufisadi kwa wabunge wao kuwa alama ya “ushujaa”. Baada ya kujiuzulu kwa kuhusishwa na kashfa ya ufisadi wa rada, Mzee wa Vijisenti alipokelewa kama shujaa kule nyumbani Bariadi. Watu walijipanga barabarani kuanzia Mwanza mpaka Bariadi - mwendo wa safari ya zaidi ya masaa matano. Inasemekana kwamba hakujawahi kuwa na umati mkubwa kama uliokuwa umekusanyika siku ile kumkaribisha mwana wao “shujaa” aliyekuwa amerejea nyumbani akiwa amejeruhiwa. Na sitashangaa kama Mzee wa Vijisenti akaukwaa tena ubunge katika uchaguzi huu.

  Kutokana na ugumu wa kushinda uchaguzi bila kutoa rushwa, haishangazi kuona kwamba vyama vya upinzani navyo vimeingia katika mchezo huu na ukiangalia vizuri, kiwango cha kutoa rushwa kama kilivyoainishwa katika utafiti huu kwa kiasi fulani kinashabihiana na wingi wa wabunge ambao chama husika kiliweza kupeleka bungeni. Ni bahati mbaya kwamba vyama vya upinzani navyo inabidi vicheze mchezo huu wa lazima ama vinginevyo havitaambulia kitu. Na “vicious cyle” hii ya kutisha inaendelea.

  Na hii hunifanya mimi nijiulize: Demokrasia hasa ni nini? Ni kuwa na mfumo wa vyama vingi kama tulio nao Tanzania? Ni ule uwezo wa wananchi kupiga kura kila baada ya miaka mitano? Ati, tuliyonayo Tanzania ni demokrasia?

  Napenda nimalizie kwa kusema kwamba CCM haiwezi kukwepa lawama katika jambo hili. Umasikini uliotamalaki miongoni mwa wanajamii na mifumo duni ya elimu ni matokeo ya sera zake mbovu tangu enzi za uhuru. Na mfumo huu wa demokrasia hii ya “kimazingaombwe” umeasisiwa na kuimarishwa na CCM. Inashangaza kidogo kuona kwamba jamii ingali inafikiri kwamba CCM itajisafisha yenyewe. Tangu lini aliyezoea vya kunyonga akaviweza vya kuchinja?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU