NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, March 13, 2010

UTAFITI: ETI WATU AMBAO WANAAMINI KWAMBA HAKUNA MUNGU (ATHEISTS) WANA IQ KUBWA

 • Angalizo: Hii nimeona niisogeze hapa kutokana na mada iliyowekwa kule kwa Kamala.
Picha ipo hapa.
 • Kama anavyopenda kusema Ng'wanambiti, hili nalo neno. Mtafiti wa Saikolojia ya Kimabadiliko aitwaye Satoshi Kanazawa wa Chuo cha Uchumi na Sayansi ya Siasa cha London amefanya utafiti unaoonyesha kwamba, mbali na mambo mengine, watu wasioamini kwamba kuna Mungu (atheists) wana IQ kubwa kuliko wenzao wenye imani hiyo.
 • Kwa kufuata mawazo mapya yanayopingana na matapo makuu ya kiitikadi na kifalsafa yanayotawala katika kipindi wanachoishi, watu hawa wasioamini katika Mungu au wanaopinga itikadi za kihafidhina wanakuwa na nafasi ya kusonga mbele kwa haraka zaidi kimabadiliko kuliko wenzao wasiofanya hivyo. Na watu wenye akili sana ndiyo wana uwezekano mkubwa wa kufuata mawazo na itikadi hizi mpya kinzani.
 • Utafiti huo umeonyesha kwamba vijana ambao walijitambulisha kama wahafidhina halisi (very conservative) walikuwa na IQ ndogo ya 95 wakati wenzao waliojitambulisha kuwa ni waliberali halisi (very liberal) walikuwa na IQ kubwa ya 106.

 • Utafiti huu ulifanyika Marekani ambako kimsingi wahafidhina, mbali na mambo mengine, wanaamini kwamba kuna Mungu, wanapinga utoaji wa aina yo yote wa mimba, ndoa za jinsia moja na huduma za bure za kijamii. Kwa upande mwingine waliberali si lazima waamini katika Mungu, wanaunga mkono utoaji wa mimba na hawahangaishwi sana na ndoa za jinsia moja.
 • Watu wasiokula nyama (vegetarians) wana uwezekano mkubwa wa kuwa waliberali na kwa ujumla wana IQ kubwa kuliko wenzao wanaokula nyama. Kutokula nyama kwenyewe kunaweza kuchukuliwa kuwa kama njia mojawapo ya kujionyesha kuwa una akili au ni bora zaidi. Kamala upo? Ripoti kamili juu ya utafiti huu inapatikana hapa.
 • Eti jamani, mnauonaje utafiti huu?

  Picha iko hapa.

5 comments:

 1. Hapo iko kazi.

  Si yawezekana ni kampeni ya kuwaachisha watu kula nyama?

  Na wafurukutwa wa mazingira nao wakija na utafiti wao kuwa ambao hawali nyama wanachangia saaaaana kwenye suala la climatic change kwa kuwa wanakula nyasi/majani na mimea itakuwaje?

  ReplyDelete
 2. Naweza kukiri wengi ma-atheist niliyo kutana nao NA NIWAJUAO wana akili sana KWA MTAZAMO WANGU na ni watu wanaofikiri sana mambo.

  Lakini siwezi kupitiliza na kudai waamini dini IQ zao ndogo kwa kuwa hata kipimo cha IQ namchezo wakukiona ni dhaifu katika kuhitimisha maswala ya akili za mtu.:-(.

  ReplyDelete
 3. @Chacha kuwa eti wanakukla nyasi na kuleta ishu kwenye climate change?????

  iko hivi, ukitafuta mchicha kula, uuondoi wote, unakata katikati na kuchukua sehemu ya juu, shina lililobakia linachipua vichwa kibao na mchicha unaendelea kuwepo, ila sasa ukila nyama, unamuua, yule mnyama alipaswa kufa na kuoza ili awe mbolea, wewe unamla na kumdumbukiza chooni huku akikuacha namagonjwa kibao, hata akiishi, kinyesi chake hujenga ardhi imara, wewe wala

  @simon, wewe sio atheist kweli???? wewe IQ yako ni ya kuwaida kweli?? si uko juuuu?????

  ReplyDelete
 4. Inaonekana kuwa na mvuto kwa haraka haraka. Na ni wazi kichwa tu cha utafiti wake kina mvuto.

  Hata hivyo, sio kila utafiti ni utafiti kwa maana halisi ya utafiti. Mara nyingine ni rahisi kwa yale yanayoitwa matokeo ya utafiti kuwa ni mtazamo wa mtafiti mwenyewe. Kwamba anachowaza ndicho kinachomwongoza kukusanya data anazozihitaji nk.

  Kwa utafiti huu, labda, ingefaa tukijua mbinu (methodology) alizotumia kufanya utafiti wake. Aliwapataje washiriki wa utafiti, alitumia instrument zipi nk

  Vinginevyo huu waweza kuwa ni utafiti wa mezani kuwasilisha mawazo yake binafsi kwa jina la utafiti.

  ReplyDelete
 5. Hata mimi nina "wasiwasi" na Mtakatifu kwani ile blogu yake ya kifalsafa inaonyesha wazi IQ yake si ya kawaida.

  Bwaya - afadhali umerudi kwani ulikuwa umepotea sana. Ukisoma vizuri utafiti huu, huyu mtafiti mkuu ni Evolutionary psychologist na kidogo inaleta mantiki kufikiri kwamba watu wasiokubali mambo waliyoyakuta wanaweza kuwa na faida kwani inabidi watafute nadharia mbadala. Ndiyo maana baada ya kukataa ile dhana kwamba dunia iliumbwa na Mungu ilibidi waje na nadharia ya Big Bang (ingawa hawasemi vitu vilivyoripuka wakati wa Big Bang na kuunda kila kitu kakiwemo kadunia ketu haka vilitoka wapi.) Na ili kuielezea hii Big Bang hasa ni nini na matokeo yake, wanasayansi hawa wameweza kugundua vitu (vizuri na vibaya) ambavyo vimebadili maisha yetu hapa duniani. Albert Einstein ni shabiki mkubwa wa nadharia ya Big Bang na nadharia zake nyingi muhimu kama Relativity na zinginezo zilitokana na juhudi zake za kuelezea matukio ambayo kiujumla yanayohusiana na Big Bang.

  Ila naungana nawe - tafiti zingine mtu unasoma na kubaki unatikisa kichwa. Kwa mfano tafiti nyingi zilizofanywa na wakoloni enzi zile hazistahili hata kuitwa tafiti. Tafiti nyingi za leo pia zinaathiriwa na watu wanaozifadhili. Ni tatizo kubwa hapa Marekani ambapo unakuta kampuni kubwa la kutengeneza madawa linawaomba madaktari wafanyie majaribio dawa yake na kuwalipa mamilioni ya dola. Mara nyingi madaktari wanaishia kuifagilia dawa husika (hata kama ina madhara) na baada ya miaka michache unasikia kwamba dawa hiyo hiyo ambayo ilisifiwa kwa kufanya miujiza wakati wa utafiti wa kimatibabu miaka michache tu iliyopita sasa ni hatari na inaua watu. Hapo tena wahusika inabidi wakurupuke na kuipiga marufuku...

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU