NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, April 15, 2010

MABINTI: MKILIIGA NA HILI BASI TUMEKWISHA....

 • Mabinti, igeni kujikondesha. Tumieni dawa za Mchina kurekebisha maumbo. Tumieni mkorogo na kuzibabua ngozi zenu nzuri. Igeni kila kitu mnachoweza kutoka nje lakini hili kamwe msiliguse: MSIACHE KUNYONYESHA VICHANGA VYENU!!!
 • Utafiti uliofanywa hivi karibuni na kuchapishwa katika jarida la kitaaluma la afya ya watoto la Pediatrics, unaonyesha madhara makubwa kwa nchi za Kimagharibi na hasa Marekani kutokana na tabia ya kutopenda kunyonyesha watoto wanapozaliwa.
 • Kwa kifupi, utafiti huo unaonyesha kwamba kama akina mama wangezingatia mapendekezo ya serikali yanayowataka kutowapa watoto wachanga chakula kingine zaidi ya maziwa ya mama kwa miezi yote sita ya mwanzo, basi Marekani ingeweza kuokoa DOLA BILLIONI 13 kila mwaka na vifo vya watoto wachanga vinavyokaribia 1,000.
 • Wanasayansi wanakubaliana kwamba mbali na maziwa ya mama kuwa ndicho chakula bora kabisa kwa mtoto, pia ni kinga kwa magonjwa mbalimbali kama vile maambukizi ya masikio na tumbo, kuhara, magonjwa ya kupumua ikiwemo Athma, kisukari cha watoto, leukemia ya watoto na magonjwa mengine mengi. Kunyonyesha pia kunasaidia kupunguza uwezekano wa akina mama kupata kansa ya matiti, kisukari, kansa ya mfuko wa uzazi, msongo wa mawazo baada ya kujifungua na inasemekana pia ndiyo kinga bora ya kuzuia mimba.  
 • Mimi naamini kwamba kunyonya maziwa ya mama ndicho hasa kinachookoa maisha ya watoto wengi wa Kiafrika. Mimi, kwa mfano, kama kitinda mimba nilinyonya kwa miaka zaidi ya mitano na watu wengi walikuwa wakinitania kwamba pengine ndiyo sababu niligeuka kuwa "kipanga" (huu ni utani!). 
 • Kwa wenzetu wazungu, matiti "yanaheshimika" sana na ni nadra mno kumwona mwanamke wa kizungu akinyonyesha mtoto hadharani. Akifanya hivyo basi ni lazima afanye kwa siri. Kwetu ni tofauti na si jambo la ajabu kumwona mtoto akiwa anapata lishe yake mbele ya watu bila wasiwasi.
 • Sasa tunashuhudia mfumuko wa magonjwa mapya kama aina mbalimbali za saratani na kisukari, magonjwa ambayo pengine yameanza kutuandama sana kutokana na  kubadilisha mfumo wetu wa maisha pamoja na kuanza kula vyakula vya Kimagharibi. Sijui itakuwaje tukiiga na hili la kuacha kunyonyesha vichanga vyetu. 
 • Kama kuna jambo ambalo hatupaswi kuliiga basi ni hili la kuacha kunyonyesha vichanga vyetu.  Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa.

3 comments:

 1. Wambie kaka.

  Utakuta wanawanyima watoto lakini wanawaruhusu baba wanyonye...! :-(

  Kaazi kwelikweli

  ReplyDelete
 2. mhhh @chacha...........

  nitamconvice mai waifu katika hili

  ReplyDelete
 3. kweli watoto wanatakiwa wanyonye mpaka aache mwenyewe titi

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU