NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, April 7, 2010

UTAMADUNI WA KUSOMA VITABU NI MSAMIATI MZITO TANZANIA


Nimekutana na makala haya katika blogu ya Markus Mpangala (aka Mzee wa Lundu) na nikavutiwa nayo. Ni uchambuzi wa kina kuhusu suala gumu juu ya uzembe wa kujisomea tulio nao Watanzania. Makala hii imekuja katika wakati mwafaka sana kwani Jumapili ya wiki hii nilishuhudia kufunguliwa kwa maktaba ya umma iliyokuwa imefungwa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati karibu na hapa ninapoishi. Nilipita pale na nilikuta mstari mrefu sana wa watu wakisubiri kuingia maktabani....

Taifa lisilojisomea ni taifa la wanakondoo wanaoweza kupelekwa ndiko-siko kwa urahisi sana. Ni taifa lisilojua wala kuhoji matumizi ya raslimali zake. Ni taifa la watu walio tayari kuuza kura zao kwa kuwa tu eti wamepewa jozi ya kanga! Ni taifa lisilo na mwelekeo. Ati, ingekuwaje kama Watanzania (angalau kwa wale tunaokaa mijini na wenye uwezo wa kujisomea)  tungekuwa na mwamko wa kujisomea vitabu na kufuatilia mambo kwa kina? Mfuatilie Mzee wa Lundu katika makala hii changamshi hapa chini. 

*****************************


Mara nyingi napendelea kutembelea mgahawa wa vitabu wa Soma(Soma Café) uliopo mtaa wa Regent, Mikocheni. Na kila mwezi nafanya ukaguzi kujua kuna gani vitabu vipya ama vya zamani ambavyo sikuwahi kuvisoma.

Katika kuhudhuria Soma Café iliwahi kujadiliwa ni kwanini Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu au tutajengaje utamaduni wa kusoma vitabu nchini mwetu. Ingawaje hoja zilikuwa zinalenga kuwalaumu Watanzania kwa desturi hiyo, lakini mama Dimere Kitunga alikuwa na hoja tofauti kwayo.

Yeye alidai endapo Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu mbona Biblia au Korani zimefika hadi vijijini na vinasomwa sana? Swali hili lilikuwa changamoto kubwa, na ingawa mjadala huo ulifanyika kitambo lakini siyo vibaya kwa Watanzania kuendelea kujiuliza udhaifu huu.

Pamoja na hoja kadhaa za wachangiaji, lakini inaelekea mama Dimere Kitunga alitushika pabaya siku hiyo. Na kwakuwa kusudio lake lilikuwa kuona tunajibu vipi hoja hii basi ilinipa changamoto na kujiuliza maswali mengi sana kuhusu desturi hii ya kutosoma vitabu.

Ni rahisi sisi Watanzania kwenda kushinda baa na kunywa bia kisha kuota vitambi halafu wengine siku inayofuata wanajigamba kuwa wamechoka kwakuwa walikuwa baa, lakini suala la kutafuta vitabu na kujisomea kama utamaduni halisi imekuwa taabu kwetu. Hali hii imejenga taswira ya watu kupenda habari za udaku kwamba msanii fulani huko Ughaibuni ana mimba au amejianika hadharani hadi nguo za ndani kuonekana.

Ama ni rahisi watu kujisomea habari kwamba kondomu yapasuka mwanamke aangusha kilio, ni rahisi sana kusomwa na kuvutiwa tu na maudhui ya mahusiano ya jambo hilo na mazingira yetu. Si vibaya kusoma habari makini, na siyo vibaya kusoma habari nyepesi endapo tu wepesi wake unaleta matokeo chanya kwa jamii na uelewa.

Hata hivyo asilimia 99 ya habari za udaku ni upuuzi mtupu, na imekuwa rahisi kwa baadhi ya watanzania kuchukua nafasi ya kusoma habari hizo. Utamaduni wa kusoma vitabu umetoweka, na upo kwa wachache sana.

Ni rahisi kwetu kwenda mitaani au kukaa vijiweni huku tukipeana michapo motomoto, lakini asilimia nyingi ya michapo hiyo ni upuuzi. Na tabia ya kuendekeza upuuzi ni kuwa mtumwa kisha kujenga jamii ya kitumwa iliyokosa ufahamu na kuendekeza ujinga na kujenga taifa la watu wasiojua lolote.

Tukumbuke kwamba kiwango cha ujinga kimeongezeka ndani ya taifa letu. Hili lilisemwa wazi katika kikao cha bunge kilichopita na waziri anayehusika na dhamana ya elimu nchini Profesa Jumanne Maghembe kwamba ujinga kwa sasa umeongezeka kwa 30% sasa, tofauti na enzi za Mwalimu Nyerere na sera za ujamaa.

Ni dhahiri kiwango cha ujinga hiki hakiwahusu wasiosoma pekee bali kuanzia kwa wanazuoni yaani wasomi wa ngazi za juu na wasiokuwa wasomi. Jambo hili ni mkusanyiko wa jamii ambayo inapimwa kwa kiwango cha uelewa wa mambo. Sasa kwa asilimia hizi, tutajengaje utamaduni wa kusoma vitabu?

Utamaduni wa kujitafutia vitabu au kujiwekea utaratibu wa kujua ni vitabu gani vimeingia madukani na vinahusu nini haupo miongoni mwetu. Ndiyo maana nasema swali la mama Dimere Kitunga lina changamoto nyingi. Na kama tunaweza kukiri tumekuwa wazembe katika suala zima la usomaji vitabu, basi ni muhimu kujiuliza pia ufahamu wetu wa mambo.

Kama kawaida, ninapoingia katika maduka ya vitabu, jambo la kwanza ni kuangalia aina ya vitabu vilivyopo ambavyo vipya au vile ambavyo sikuwahi kuvisoma huko nyuma. Wakati Fulani niliamua na naendelea kukusanya riwaya zote za Joran Kiango zilizotungwa na hayati Ben Mtobwa.

Dhumuni langu ni kutaka kuhifadhi kazi zote za Ben Mtobwa, na nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini wakati nikifanya hivyo kunajitokeza hali ya mshangao kwa baadhi ya watu kuona suala hilo, lakini wapo tayari kwenda baa na kunywa pombe na kula nyama choma. Na wengine wanaweza kutumia muda mrefu wakitumia huduma za Facebook au Twitter, lakini siyo rahisi kuamua kujisomea vitabu pia.

Na kwa sasa zipo njia nyingi za kujisomea vitabu kwani baadhi ya watunzi wameweka vitabu vyao kwenye mtandao jambo ambalo linarahisisha usomaji pia kupata habari juu ya vitabu vipya. Kwasasa maduka yapo hadi mtandaoni, kwa mfano teknolojia ya uchapaji vitabu ya LULU, ambapo baadhi ya watunzi huchapa hapo vitabu vyao na kuviuza kwa wasomaji.

Huduma hiyo inarahisisha kujua ni vitabu gani na mwandishi gani ametoa kazi mpya. Au huduma za Amazon ambapo utaweza kuona vitabu(endapo unatafuta) ambavyo huuzwa. Haya ni mapinduzi makubwa sana katika masuala ya vitabu.

Lakini suala hili limekuwa likifanywa na wachache kwani wengi wetu tunasingizia vipato vidogo lakini ndani ya vipato hivyo tunaweza kushinda baa na marafiki tukinywa pombe na kula nyama choma kuliko kujua kulikoni katika maduka ya vitabu.

Na kwa wengine hata kujisomea magazeti imekuwa taabu kubwa sana. Katika mgahawa wa Soma Café mijadala ni mingi,michezo ya watoto na vitabu hupatikana hapo vya kila aina, lakini ni wachache wanaotumia muda wao kwenda kujionea kuna nini.

Nakumbuka mwezi mei mwaka 2009 wakati wa ziara ya mtanzania Fred Macha, wapo waliojaribu kuuliza alifanya nini katika warsha zake, lakini kutumia muda kwenda British Council, nyumba ya Sanaa, na Soma Café kumsikiliza anatujuza nini kutokana na kuishi kwake ughaibuni na suala zima la uandishi wa raia au usomaji wa vitabu, hawataki kulitenda.

Kwa hili tunatakiwa kujiuliza ni namna gani tunaweza kujenga dhana ya ‘networking’ au kutumia warsha na makongamano ya vitabu ili kujenga utamaduni wa kuongeza ufahamu. Suala hili limekuwa gumu kueleweka na naona watanzania halichukulia kama ajenda muhimu maishani mwao.

Na wimbi la kutojisomea vitabu limeshamiri katika jamii yetu huku tukitegema matokeo chanya kwa kulea uzembe. Ndiyo maana tunaona kiwango cha ufahamu wa mambo ni duni sana katika jamii yetu, kila mtu anawazia hela ya kula, ,lakini hatutambui hela ya kula ni pamoja na kula vitabu yaani kujisomea.

Wimbi hili la kulea jamii isiyopenda vitabu imetmalaki sana, na hata wanazuoni wetu hawataki kujijuza ziadi ya kile walichonacho katika taaluma zao. Na hili niliwahi kujadili na rafiki yangu Ambroce Nkwera, ambaye anaeleza kwamba hadi vyuo vyetu vikuu vimejaza wazembe wengi ambao hutumia muda kusoma vitabu kwa manufaa ya kushinda mitihani pekee.

Mbali na umri mdogo wa wanavyuo hao ambao huamabatana na ufahamu duni, ni dhahiri suala hili limekuwa likizidi kujenga jamii isiyopenda kusoma vitabu. Siyo siri ukitaka kuboresha lugha,ufahamu wa masuala mbalimbali ni muhimu kujisomea vitabu.

Vitabu vinao utajiri mwingi sana, na nakumbuka katikia moja ya mijadala pale Soma Café, mwandishi mahiri afrika Shafi Adam Shafi alilaumu sana jamii yetu kwa kulea utamduni mbovu wa kutojisomea vitabu. Pamoja na malalamiko ya ukosefu vya vitabu vya Kiswahili, lakini kwa hakika tunavyo vitabu vingi tu lakini watanzania tumelala usingizi mnono wenye madhara kwa taifa letu.

Ukipita kwa wauzaji wa vitabu mitaani utapambana na vijitabu vya kipuuzi ambavyo waandishi wake hujigamba kwa kusimulia mambo ya kipumbavu kabisa. Vipo vijitabu ambavyo nachelea kusema ni ujinga hata kuviingiza sokoni na ujinga kuruhusu kuviingiza sokoni kwababu havina msaada wowote kwa jamii.

Orodha ya vijitabu hivyo kwa namna nilivyochunguza vimejazana kwa majina ya mapenzi yaani jamii yetu imechukulia suala la ngono na mahusiano ya kimapenzi kama ajenda muhimu hivyo kujisomea vijitabu vyenye kila dalili za kutoongeza ufahamu wowote. Nakumbuka Shafi Adam Shafi aliwahi kusema, unaweza kuona vitabu vipya lakini havina lolote la maana.

Anasema vitabu vingine ukivisoma ni kama umesimama katikati ya shimo la takataka kwani havishtui wala havina lolote ambalo jamii inaweza kujivunia kwa maana ya kujielimisha kwalo. Na mbaya zaidi mambo mengi ya kipuuzi yameshika kasi nchini mwetu.

Tunalea watoto wetu kwa misingi ya kuwafanya watumie muda mwingi kutazama runinga, kuwnunulia simu, na kuwshirikisha kwenye mambo ambayo hayana msaada wowote kwao. Na wimbi la kulea watoto kwa misingi ya tamaduni za kigeni yaani zile ambazo tunadhani bora, lakini suala la kuwasomea vitabu,kuwanunulia vitabu ni ajenda ngumu huku tukisingizia umasikini.

Ninajisikia vibaya kukumbuka hali ilivyo nchini mwetu Tanzania huku tukitumia kigezo cha umasikini kuhalalisha ujinga wetu. Je, ni mzazi gani Mtanzania ambaye siku kama ya leo anaenda kwenye duka la vitabu? Ni mzazi gani ambaye anampeleka mtoto wake kwenye duka la vitabu?

Ni mara ngapi mtoto amehimizwa umuhimu wa kujisomea vitabu?Sasa, kama watoto wanalelewa hivyo, je, tunaweza kutegemea kuwa Taifa letu litaweza kushindana na wenzetu wa ughaibuni katika ulimwengu huu wa leo na wa kesho ambao unategemea elimu na maarifa? Ni lini na vipi watanzania tutajenga utamaduni wa kusoma vitabu?

Na la maana zaidi ni kwanini tufikie hatua ya kuona suala la usomaji vitabu linaambatana na utajiri? Je ni kweli kwamba kwa mwaka mzima hatuwezi kujinunulia hata kitabu kimoja? Nini hatima ya nchi yetu katika usomaji vitabu? Na nini hatima ya Taifa letu la Tanzania katika maendeleo?

7 comments:

 1. Mkuu! sina neno jinginge zaidi ya kusema ASNATE ingawaje neno lenyewe ni dogo sana. Pamoja daima.

  ReplyDelete
 2. ASANTE mkuu, nilikuwa kasi hata nakosea kuandika. Pamoja daima

  ReplyDelete
 3. Mimi kuna watu wengi walinishauri nitunge kitabu cha simulizi ZANGU, wakidai eti nina kipaji cha utunzi, na ambao mpaka leo bado wanAnisisitiza nitunge sitasita kuwataja, ni dada Yasinta na dada Mija Sayi, hao wamenishauri sanA nitunmge vitabu.

  Lakini nikiangalia uwepo wa soko nadhani nitakuwA napoteza pesa zangu bure.
  Ikumbukwe kuwa kutunga mpaka kutoa kitabu kunahitaji gharama.

  Iwapo kuna mfadhili atajitolea kudhamini maandishi yangu basi niko tayari kutunga kitabu cha simulizi za kufikirika lakini zenye mafunzo bure bileshi.
  Lakini wako wapi wafadhili jamaniii.....

  Niliwahi kuzungumza na mzee mmoja mwenye ukwasi ambaye ni rafiki wa baba yangu, kuwa anao watoto mayatima wangapi ambao anawafadhili tu kwa kuwalipia ada za shule, akasema hakuna...
  To me it was like he! huyu bwana hata kesho akifa atakumbukwa kwa lipi?

  Kuna watu wanakwasi tena wa kutosha lakini hawatoi misaada mpaka pale ambapo ataoneshwa kwenye TV na kwenye Magazeti, Misaada haitolewi mpaka iwe kuna maslahi fulani kama sio ya kujijenga kisiasa basi itakuwa ni ya kutafuta popularity...hivi ni kwa nini lakini..

  Rafiki yangu Kamala na Chacha pale kwenye vi NGO vyao nao wanatafuta mahali ambapo waki-attach na write up zao wafadhili watapenyeza rupia.....LOL
  dada yangu Yasinta naye ka NGO kake pale Ruhuwiko hawatafaidi mpaka Awakamue wafadhili...LOL
  Ok nilichotaka kusema hapa ni kwamba hata hizi NGo zinaweza kujitolea katika write up zao za kuombea mkwanja wakajumuisha na ufadhili wa vitabu vinavyozungumzia madhila wa wanawake na watoto, pammoja na yale madhila ya baadhi ya wanaume wachache wanaoshikishwa adabu na wake zao...LOL
  Si vizuri maandishi haya yakaishia humu bloguni......

  JAMANI NASEMA VUKAAAANI.......

  ReplyDelete
 4. Koero nawe! duh!

  Kaka Matondo: katika mada ndefu nilowahi kuthoma hapa hii ndefu kuliko...lol

  Nimeipenda though kwani mie nami nina kale kaugonjwa ka-procrastination...lol Naweza nkajiwekea azimio la kusoma vitu fulani fulani lakini dah! ngumu sana....lol

  Nipeni dawa ya kuacha huo uvivu wa kusoma jamani

  ReplyDelete
 5. Kusoma inategemea na malezi kwani ukilelewa katika familia ipendayo kusoma basi nawe utapenda kusoma. Na jingine ni kwamba nyumbani TZ tunachelewa sana kuanza kusoma vitabu. Koero kwani ni uongo wewe huna kipaji cha kuandika?

  ReplyDelete
 6. Sasa utakuta hata baadhi yetu watoa maoni hatuisomi habari yote. Tuna-skim.
  Na tunatoa maoni katika juu ya umuhimu wa kusoma katika toleo ambalo ambalo hatujalisoma lote.
  Mmmmhhh!!!!
  Kaka umempa "mvivu" Koero sababu. Ndio tusahau sasa kuhusu itabu chake maana kishaanza mambo ya "wafadhili"
  Ggggrrrrr!!!!!!!!

  ReplyDelete
 7. Mwanafalsafa wa Lundu - ni kweli, pamoja daima. Napenda sana uchambuzi wako japo kuna mambo machache machache ambayo huwa sikubaliani nawe. Haya tutayazungumza siku nyingine. Nilipenda jinsi ulivyokuwa ukiukoromea ubepari na ubabe wa Wamarekani enzi zile....Endelea kutumulikia njia.

  Koero - Suala la kukosa wasomaji lisikukatishe tamaa hata ushindwe kuandika na kuielimisha jamii. Lichukulie kama ni kujitoa kwako mhanga katika kuipigania jamii potelea mbali hata kama kitabu chako kitasomwa na mtu mmoja.

  Isitoshe kama unayo "mitandao" sahihi utakuja kushangaa kitabu chako kimeshafanywa kuwa cha lazima kwa wanafunzi wote nchini. Andika; na watu wa kukushangilia, kukutia moyo na kukushauri tupo!

  Ng'wanambiti - ku-procrastinate ni tatizo la wengi. Tatizo langu wakati mwingine ni kutomaliza nilichokianza. Yaani naweza kuanza kukisoma kitabu halafu nakaribia mwisho kabisa namaliza stimu na nashindwa kukimalizia. Halafu nachukua njia ya mkato na kumsaidia mwandishi kukimalizia kitabu kichwani mwangu. Uzembe na nidhamu ya kutia aibu kabisa.....

  Yasinta - Ni kweli malezi ya kifamilia yanaathiri maisha ya baadaye ya mtoto. Lakini kama mazingira; na watoto wa rika lake hawapendi kujisomea hata yule aliyelelewa katika familia ya kujisomea atalegalega tu.

  Ni kweli pia kwanza tunaanza kusoma vitabu tukiwa na umri mkubwa kidogo. Binti yangu wa darasa la tatu hapa anasoma vitabu vya Harry Potter na hadithi nyingine ambazo pengine kule nyumbani ningezisoma wakati nikiwa shule ya Sekondari! Kuna tofauti kubwa sana.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU