NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, April 26, 2010

WATU WANAPOPANGA FOLENI USIKU KUCHA WAKISUBIRI KUNUNUA VITABU

 • Profesa Mbele amekuwa akiandika mara nyingi kuhusu tatizo tulilonalo Watanzania la kutopenda kusoma vitabu (tazama hapa na hapa). Markus Mpangala (aka Mzee wa Lundu) naye ameshawahi kuandika makala kadhaa zamifu kuhusu suala hili (tazama hapa na hapa). Baadhi ya sababu zilizotajwa kuchangia tatizo hili ni pamoja na umasikini wa Watanzania, ughali wa vitabu vyenyewe, mfumo mbaya wa elimu (vitabu mashuleni hakuna na tunasoma kwa kutegemea madesa); na kutokuwa na utamaduni wa kujisomea. Pamoja na sababu hizi, swali bado linaweza kuulizwa, kama tuna pesa ya kunywea bia na kitimoto kila siku, mbona tusiwe na pesa ya kujinunulia vitabu?
 • Kila mwaka hapa “kijijini ” Gainesville huwa kunafanyika mauzo ya vitabu vingi vya kila aina kwa muda wa siku tano mfululizo. Mauzo haya yanayojulikana kama Friends of the Library ni makubwa na huwa yanavutia watu kutoka jimbo zima la Florida na majimbo mengine ya jirani.
 • Mwaka huu mauzo haya ya vitabu yalianza juzi Jumamosi (24/4/2010). Watu waliotoka sehemu za mbali ili kuwahi mauzo ya mwanzo mwanzo ambapo vitabu huuzwa kwa bei ya chini sana, walianza kupanga foleni siku ya Ijumaa na walikesha na kulala katika foleni hiyo wakisubiri kesho yake milango ifunguliwe ili waweze kujinunulia vitabu kwa bei nafuu sana.
 • Katika miaka ya nyuma, wapenda vitabu hawa waliruhusiwa kuweka kiti, jiwe au boksi katika foleni kama kishika nafasi. Mwaka huu hata hivyo masharti yamebadilishwa na mtu inabidi uweko mwenyewe katika foleni ili kulinda nafasi yako. Ukiondoka na lako halipo!
 • Katika foleni ile ya Ijumaa jioni kulikuwa na watu wa kila aina - wazee kabisa wenye umri zaidi ya miaka 70, watu wa makamo, vijana, wanawake wakiwa na watoto wao, wazungu, weusi…
 • Kwa Mtanzania, tukiwemo sisi tunaojidai kuwa eti tumesoma, kukesha usiku kwenye foleni ya kununua vitabu pengine haiingii akilini kabisa. Lakini huu ndio utamaduni wa hawa wenzetu, na kwa hili kusema kweli wametuzidi. 
 • Kama nilivyowahi kusema hapa "Taifa lisilojisomea ni taifa la wanakondoo wanaoweza kupelekwa ndiko-siko kwa urahisi sana. Ni taifa lisilojua wala kuhoji matumizi ya raslimali zake. Ni taifa la watu walio tayari kuuza kura zao kwa kuwa tu eti wamepewa jozi ya kanga! Ni taifa lisilo na mwelekeo. Ati, ingekuwaje kama Waafrika (angalau kwa wale tunaokaa mijini na wenye uwezo wa kujinunulia vitabu)  tungekuwa na mwamko wa kujisomea vitabu na kufuatilia mambo kwa kina?" Tutafakari!!!
 • Unaweza kusoma zaidi kuhusu mauzo haya ya Friends of the Library hapa na hapa.

6 comments:

 1. Ahsante sana kaka Matondo kwa mada hii. Sasa hivi nimetoka kwa kaka Mbele kujadili jambo hili. Nami nakusanya nguvu, ndani ya wiki hii hii nitaandika kuhusiana na jambo hilo. Tena ntaandika kutokana na uzoefu binafsi juu ya usomaji wa vitabu.

  Naomba kabla sijatoka hapa barazani kwako niseme, Watanzania tunapenda sana kutafuta visingizio vingi vya kwa nini jambo fulani hatulifanyi, wakati tungehitaji sababu moja tu ya kwa nini tunaweza kufanya.

  Tunatumia mapesa mengi kwenye anasa lakini kutoa pesa kununua kitabu ni jambo la ajabu.

  Karibu kibarazani kwangu, si punde nami nitalisemea hili.

  ReplyDelete
 2. Mwalimu Matondo, haya mapambano dhidi ya adui ujinga ni muhimu, na umetoa mchango mzuri. Ndugu Mtanga ni mpambanaji hodari, nami nimevutiwa na michango yako. Nangojea kwa hamu michango yako ya siku zijazo. Kaza buti.

  ReplyDelete
 3. kizuizi kingine ni upatikanaji wa vitabu wenyewe, angalia wauzao vitabu hapa nchini ni mashirika ya kidini zaidi na hivyo hakuna uhuru wa kupata kitabu ukipendacho lazima udondokee kwenye dogma na hivyo jamii kulazimika kuachia baadhi ya viongozi wa dogma kuwaambia lipi jema na lipi zuri

  inakera ukiingia kwenye maduka ya vitabu, ni vile vinavyokupangia namna ya kufikiri, kwa mfano, ni vigumu kupata vitabu vya utambuzi nchini tanzania na ndo maana ukija pale kwenye kituo chetu unakuta tunatoa 4tokopi ila tushukuru ujio wa mtandao japo lugha bado ni changamoto

  ReplyDelete
 4. Sina uhakika kama hatufanyi kosa ku "Generalize" WATANZANIA WANAPENDA SANA ANASA KULIKO KUNUNUA VITABU . Mnaweza kuniambia ni asilimia ngapi ya hao watanzania wanaoshinda kwenye baa ila wanashindwa kununua vitabu?. KI UKWELI KABISA SINA UHAKIKA KAMA WANAFIKA HATA ASILIMIA TANO YA WATANZANIA WOTE.

  Kwa takwimu za sasa wastani wa pato la mtanzania kwa siku ni chini ya dola moja. Kwa hesabu za haraka kwa mwaka ni chini ya dola 365.
  MNAOISHI UGHAIBUNI MNAJUA GHARAMA ZA VITABU...(kama una utamaduni wa kusoma). sasa niambie huyu Mtanzania atafikiria kununua kitabu au chakula
  Tutakuwa hatujatenda haki kwa kulinganisha Mtanzania na Mmarekani au Mu-Ulaya wa magharibi.

  Kwa "MASLOW'S HIERARCHY OF NEEDS" Watanzania wengi bado tupo chini kabisa kwenye hii "pyramid". Lazima kwanza tuwe na uhakika wa kula, kulala na afya zetu. Kabla hatujafikiria kusoma vitabu na mambo mengine.
  NASEMA HIVI KWA SABABU SI WAMAREKANI WOTE WENYE HUO UTAMADUNI WA KUSOMA VITABU, ila ninakiri wengi wana utamaduni huo, Labda kwa sababu wao wengi wameshavuka "Physiological Needs" katika ile piramidi ya Maslow's.

  ReplyDelete
 5. Ndugu Godwin, nimesikia masikitiko yako kuhusu wastani wa pato la m-Tanzania kwa siku kuwa dogo kiasi hicho. Lakini nina suali.

  Wakati wa michango ya sherehe, mbona sijawahi kusikia watu wakiongelea hiki kipato duni cha m-Tanzania?

  Kreti ngapi za bia zinauzwa Tanzania kwa siku, na kunywewa, kuanzia Dar es Salaam hadi kijijini? Nasema hivi kwa sababu kuna baa hadi kwenye vijiji vingi, achilia mbali vilabu vya komoni, rubisi, mbege, kangara, mnazi, wanzuki, kayoga, nipa, na kimpumu. Pamoja na hicho kipato duni unchosemea, watu wanajichana na hivyo vilaji nchi nzima.

  Wakati wa mashindano ya urembo, ambayo sasa yanaingia hadi kwenye wilaya na vijiji, mbona hiki kipato cha m-Tanzania kwa siku hakitajwi, bali kumbi zinajaa hadi kufurika.

  Kwa nini hiki kipato duni cha m-Tanzania kinaelekea kukumbukwa na kutajwa tu wakati tunapoongelea vitabu?

  Binafsi, nikiwa ni mwalimu ambaye nazunguka sana duniani, nimewalalamikia wa-Tanzania kwa miaka mingi kwa uzembe wao na tabia ya kutoa visingizio kwenye suala la vitabu na elimu kwa ujumla. Hatimaye nimebadili lugha; nawatobolea ukweli kuwa asiyefunzwa na mama yake hufunzwa na ulimwengu. Bofya hapa.

  Kwa kumalizia, napenda kusema kuwa nangojea kwa hamu makala ya Ndugu Mtanga, kwani ameshathibitisha kuwa ana mengi ya kusema.

  ReplyDelete
 6. Ninashukuru mwalimu Mbele kama umefanya utafiti huo. NINAAMINI UMEFANYA.
  Ni rahisi sana kutatua tatizo kwa kujua CHANZO CHA TATIZO, kuliko kuangalia "MATOKEO NA DALILI" zinazotokana na hilo tatizo. Mimi mwenyewe ni mmoja wa Wa-Tanzania ambao hatuna utamaduni wa kusoma vitabu. INGAWAJE NIKIWA SHULE YA MSINGI NILIKUWA HODARI SANA WA KUSOMA VITABU. Na ukweli Maktaba yangu nikiwa shule ya msingi ilikuwa na vitabu vingi vya "ZIADA" kuliko "KIADA".

  Walimu wangu wengi wa shule ya msingi walikuwa "WAWAZI SANA". Kwenye mitihani au darasani kama utaibua kitu kipya asichokijua, atadadisi umekitoa wapi na atasoma kukielewa kama ni sawa, na atakupa vema akijiridhisha. Hii liliniongezea sana amasa ya kutafuta vitu vipya ili nimpatie mwalimu changamoto. NA ILINIJENGEA KATABIA KAKUSOMA VITABU MBALI MBALI KUJUA DUNIA INAKWENDAJE.

  Hali ilibadilika kila nilipokuwa naendelea na elimu ya juu. Walimu walisisitiza kujibu kutokana na "NOTISI ZAO". Walitunga mitihani inayosukuma zaidi KUKARIRI na KUTEMA, kuliko KUELEWA, na kama umeelewa ukajibu sahihi lakini si sawa kabisa na alichoweka kwenye "NOTISI" zake ujue imekula kwako

  Hali ilikuwa mbaya zaidi nilipofika CHUO. Nilikuta nafundishwa na vitabu profesa alivyotumia yeye mwaka 67 kufundishiwa. Na anataka ujibu mtihani wake kutokana na alivyokufundisha. Tofauti na hapo kwa kujifanya umesoma vitabu vingi kupata "ideas" jua wewe lazima urudi SEPTEMBER kwenye conference kama si " Ku-DISKO."

  Kama walimu wenyewe wanaofundisha hawapendi kusoma, unategemea mwanafunzi atajenga tabia hiyo

  Mfumo na mitaala ya Elimu ya TZ pia inachangia. FANYA TAFITI KIDOGO. Utaona wanafunzi wanaosoma shule za KIMATAIFA kidogo wanatabia ya kujisomea vitabu kuliko shule zetu za serikali. Umeshawahi kujiuliza kwanini?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU