NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, May 19, 2010

MGEMA AKISIFIWA...TUJIFUNZE KUTOKANA NA MISUKOSUKO YA KAMPUNI LA TOYOTA

 • Kampuni la Toyota lilikuwa limejijengea heshima kubwa duniani kote kwa kutengeneza magari yanayoaminika na yenye kudumu kwa muda mrefu. Ndiyo maana utayaona mashangingi (Toyota Land Cruisers) yakikata mbuga kwenye matope na kwenye barabara za kila aina miaka na miaka. Hali kadhalika Toyota Corolla, Camry, RAV4 na aina nyinginezo. Ndiyo maana watu wengi walishangaa waliposikia kwamba Toyota ilikuwa imeanza kutengeneza magari yenye matatizo ya kiusalama.  
  • Mimi pia nimeathiriwa na tatizo la Toyota kupuuzia sifa zake za msingi zilizoifanya Toyota iwe Toyota. Mwaka 2008 nami nilijitutumua nikanunua Toyota FJ Cruiser mpya tena yenye kila kitu ndani. Hili ni gari la ukubwa wa kati ambalo lilielezwa kuwa ni kama Land Cruiser ndogo na muundo wake ukawa unafananafanana na Hummer ndogo. 
   • Kwa nje ni gari zuri linalovutia sana
   • Milango yake inafunguka kwa pamoja, na kiu yake ya petroli ni ya kawaida tu.
    • Tatizo hata hivyo ni kwamba ukiliendesha kwa muda mfupi tu utagundua kwamba karibu kila kitu kilichomo ndani ni plastiki na unaweza kuona kabisa kwamba limetengenezwa kwa kufinyangwafinyangwa tu bila umakinifu wa kutosha. Baadhi ya vitu vya ndani vinadondoka au kuchanika vyenyewe hata miaka mitatu halijamaliza. Kwa hakika hii si tabia ya magari ya Toyota tuliyokuwa tumezoea. Ndiyo maana imebidi nilitelekeze na kurudia mkweche wangu wa zamani.
    • Wachambuzi wengi wanaamini kwamba katika juhudi zake za haraka haraka kulipiku kampuni kinzani la General Motors, Toyota ilijikuta inakata njia za mkato na kusahau sifa zake za msingi zilizoifanya ijizolee sifa duniani kote kwa kutengeneza magari ya kuaminika na yanayodumu sana. Pengine ni yale yale ya mgema akisifiwa......
    • Hata sisi, ni mara ngapi tumeipuuzia misingi na kanuni zetu ongozi tulizojiwekea maishani, kanuni pweke anuai zinazoupambanua usisi wetu kwa lengo tu la kuwafurahisha, kuwaridhisha au kushindana na binadamu wengine au kujinufaisha? 
    •  Tunayo mengi ya kujifunza kutokana na misukosuko inayolikumba kampuni la Toyota.

      5 comments:

      1. Pole sana kwa kadhia ya mgema Toyota.

       Kuna wakati Michael Jackson alipata kusema, "when you are on the top of the world, there is no where to go, than going down."

       ReplyDelete
      2. Tatizo watu huchoshwa na sifa zile zile kila siku kitu ambacho kinaweza kumsababishia asifiwaye kwa upole akanua asifiwe pia kuwa ``Jamaa ni mpole lakini kwa kula hawezekani´´ kitu ambacho kinaweza kikaharibu kumeremeta kwa sifa ya kwanza.

       SIfa kitu cha ajabu sana kwa kuwa ukichunguza utastukia hakuna asiyependa sifa.

       ReplyDelete
      3. Nilikuwa nataka kubwatuka kwa kuwa sina hamu ya kununua gari labda wewe Kaka Matondo UDONETI kwangu :-)

       Lakini paragrafu ya pili toka mwisho imenibinya na kunifikirisha saidi....meseji senti :-(

       ReplyDelete
      4. ulilinunu shilingi ngapi ili nikusaidie kusikitika??

       mimi natembelea baiskeli ya kichina, ni noma pia

       ReplyDelete
      5. Fadhy - angalizo zuri kutoka kwa Michael. Ni kweli kwani kilicho juu ni lazima kishuke. Ndiyo maana leo madola yote yaliyowahi kuwika (Babiloni, Roma, Misri, Maya na mengineyo) yalishaanguka baada ya kukifikia kilele. Ni kwa mantiki hii hii leo watu wengi wanaipa Marekani pengine miaka 50 - 100 hivi kabla nayo haijafuata mkumbo huu.

       Mtakatifu - Pengine hii inaakisi lile jumuisho kwamba hakuna aliye mkamilifu na sifa ni dhana nasibu tu. Si ajabu ukakuta kwamba hata upole katika tamaduni zingine ni sifa hasi (mf. siamini kijana wa Kikurya kama Ng'wanambiti au morani wa Kimasai anapaswa kuwa mpole).

       Na pengine kujirundikia sifa kwa kadri inavyowezekana ndiyo njia mojawapo sahihi ya kuukaribia ukamilifu tunaoutamani sana kuufikia!

       Sifa za Mtakatifu Kitururu - mtakatifu, mcheshi, mwanamuziki, mwanafalsafa, mpole?, mtanashati, rasta?...unaweza kuendelea...Na ujumla wa sifa hizi (nzuri na mbaya) ndio unatupa japo fununu tu undani hasa wa huyu Mtakatifu. Kwa hivyo sifa nyingi ni bora zaidi - haijalishi kama ni nzuri au ni mbaya - hasa ukizingatia kwamba uzuri au ubaya wa sifa ni dhana tu!

       Ng'wanambiti - Hata nikikudonetia gari lililofinyangwafinyangwa tu kutengenezwa itakusaidia nini? Na kwa nini hutaki kununua gari? Hupendi kuingia Mataranyirato na shangingi jipya V8 "full loaded" lenye vioo "tinted" na bonge la runinga ndani wanakijiji wakakusanyika kukusifia kwamba wewe ndiye umefanikiwa kuliko wote pale kijijini? Mtanzania gani wewe usiyependa misifa na mashindano?

       Mwanatahajudi - Dola kibao baba.

       Baisikeli ni usafiri mzuri kwani mtu unapata mazoezi, unaepuka foleni za magari na pesa za petroli. Tatizo ni usalama kama uko mjini kwani jamaa wenye magari hawajali kama nawe ni kiumbe mwenye haki sawa na wao wa kutumia hata hicho kipembe cha barabara unakoendeshea kibaisikeli chako. Huku kwa wenzetu mambo kidogo ni afadhali kwani barabara nyingi zina sehemu maalumu ya wapanda baisikeli. Hata huku hata hivyo ni lazima kuwa mwangalifu! ASANTENI!!!

       ReplyDelete

      JIANDIKISHE HAPA

      Enter your email address:

      Delivered by FeedBurner

      VITAMBULISHO VYETU