NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, May 6, 2010

NIKO TORONTO KANADA TANGU JANA JIONI KUHUDHURIA MKUTANO WA ISIMU YA KIAFRIKA

 
 • Mwaka huu wanaisimu na wakereketwa wote wa lugha za Kiafrika tumekutana katika chuo kikuu cha Toronto ili kuhudhuria mkutano wa 41 wa Isimu ya Lugha za Kiafrika. Ni safari ya masaa kama manne hivi kwa ndege kutoka Florida (kupitia Chicago).
 • Nitatoa mada yangu leo saa tano asubuhi. Mada itakuwa juu ya Ruwaza za Toni (au mkazo-sauti) katika Maneno ya Mkopo katika Kisukuma (Tonal Patterns in Kisukuma Loanwords) na kufanya uchambuzi kwa kutumia nadharia ya Fonolojia inayotamba kwa sasa ya Optimality.
  • Ninakerwa sana na ukweli kwamba Kisukuma - pengine lugha nzuri kuliko zote duniani, na tata sana kiisimu bado haina kitabu cha sarufi hata kimoja pamoja na kwamba ndiyo lugha kubwa kuliko zote Tanzania ukiachilia mbali Kiswahili. Yaani kuna vitabu vingi juu ya Kimasai kuliko Kisukuma. Hii haikubaliki!
   • Ni kwa sababu hii ndiyo maana nimeamua kujifunga kibwebwe na kuandika sarufi makini inayojitosheleza ya Kisukuma kwa ajili ya matumizi ya wanaisimu na wapenda lugha za Kiafrika popote duniani. Natumaini kwamba kazi hii itanichukua miaka miwili (najua Mungu Ataniweka hai tu).
    • Ukitaka kuona kama lugha yako itachambuliwa katika mkutano huu basi tazama muhtasari wa mkutano mzima kwa kubofya hapa na halafu bofya kwenye ACAL 41 PROGRAM.
     • Libeneke litaendelea kwa kadri muda unavyopatikana. 

      7 comments:

      1. Pamoja mwalimu!

       nasubiri kukisoma kitabu hicho :-)

       ReplyDelete
      2. kila la kheri. Tunasubiri kwa hamu hicho kitabu.Upendo Daima!!

       ReplyDelete
      3. Mwalimu, nimevutiwa na mada ya trh 7/5 isemayo "When “safe” isn’t safe: a sociolinguistic assessment of the Bena language in Tanzania" itakayotolewa na Michelle Morrison-Rice University


       Ukierejea utujuze pamoja na mambo mengine...inakuwaje hapo?

       ReplyDelete
      4. Mungu akulinde na kukurudisha nyumbani kwako salama.

       Rariki.

       ReplyDelete
      5. Safe trip mwamlimu.

       ReplyDelete
      6. Ng'wanambiti alisema "...nimevutiwa na mada ya trh 7/5 isemayo "When “safe” isn’t safe: a sociolinguistic assessment of the Bena language in Tanzania" itakayotolewa na Michelle Morrison-Rice University"

       Nilihudhuria mada hiyo. Dai kuu la mtafiti huyu ni kwamba inabidi tubadili vigezo tunavyotumia kupimia lugha zilizo kwenye hatihati ya kutoweka. Vigezo kama vile vilivyowekwa na UNESCO havitupi mawanda mapana zaidi ya kuweza kuelewa sababu na mahusiano ya kijamii yanayoweza kuhatarisha lugha.

       Kwa kutumia vigezo vipya alivyovipendekeza, hata lugha kubwa kama Kibena (wazungumzaji zaidi ya laki tano) inaweza kuwa tayari inateketea kwa ndani japo kwa nje tukiangalia idadi ya wazungumzaji tunaweza kujidanganya kuwa kila kitu kiko salama.

       Ilikuwa mada nzuri na yenye kufikirsha. Ubaya tu ni kwamba katika mikutano mingi mtu unapewa eti dakika 20 tu za kuwasilisha mada yako na dakika 10 za kupigwa maswali. Baadaye nilimtafuta pembeni na tukaongea kwa kina kuhusu utafiti wake.

       ReplyDelete
      7. Nimeyaangalia hayo ya "nadharia ya Fonolojia inayotamba kwa sasa ya Optimality." Ni mengi sana na yako ki-hesabu hesabu (ki-takwimu hivi)!

       Je, kama mimi ninataka kujua isimu (najua fonolojia ni sehemu mojawapo ya isimu) ni lazima niwe mtaalamu wa hiyo "Optimality" au niijue kwa undani?

       Esteemed Reader

       ReplyDelete

      JIANDIKISHE HAPA

      Enter your email address:

      Delivered by FeedBurner

      VITAMBULISHO VYETU