NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, May 31, 2010

TANZANIA TANZANIA, NINAKUPENDA KWA MOYO WOTE: UZALENDO, USASA NA UTANDAWAZI

 • Mwalimu Nyerere alikuwa "jiniazi". Mbali na kufanikiwa kuutokomeza ukabila, propaganda zake za "zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM" na porojo zingine zilizokuwa zimefumwa mumo kwa mumo katika masomo ya siasa mashuleni, elimu ya watu wazima, nyimbo za mchakamchaka na hata JKT, zilifanikiwa kutufanya vijana (wa enzi zileeeee) tuipende sana Tanzania. 
 • Ni kwa sababu hii kamwe huwa sioni aibu "kujimwambafai" kwamba mimi ni Mtanzania  halisi ninayetoka kwenye nchi yenye amani, upendo (sijui kama bado upo), isiyo na ukabila (ingawa hii inaua lugha zetu za kiasili), Tanzania yenye Mlima Kilimanjaro (ingawa inasemekana na kuaminika kwamba uko Kenya), Tanzania iliyo mzalishaji pekee wa Tanzanite (ingawa pengine Kenya ndiye muuzaji mkuu), Tanzania yenye Serengeti, Zanzibar na kila aina ya utajiri (ambao sijui kama Mtanzania wa kawaida anaufaidi). Ndiyo maana  sijawahi kufikiria hata siku moja kwamba nitaweza kuukana uraia wa nchi hii na kuchukua uraia wa nchi nyingine. 
 • Kuna kitu fulani cha thamani na cha fahari sana kuwa Mtanzania, na kwa hili Mwalimu Nyerere anastahili pongezi.  
Ndiyo maana ukiingia katika ofisi hii...


Utakutana na Tanzania na Utanzania papo kwa papo

(1) Utakaribishwa Tanzania...

(2) Na si ajabu ukaondoka na kofia ya Tanzania

(3) Au kunywea chai kwenye kikombe cha "I Love Tanzania"
 
 • Japo ni hivi, bado huwa nasikitika na kupatwa na kigugumizi ninapoulizwa kama kweli niyasemayo ni ya kweli. Kama ni kweli kwamba nchi hii niipendayo sana ina amani, maliasili za kutosha na ilibahatika kuwa na mmojawapo wa viongozi bora kabisa barani Afrika (Mwalimu), mbona bado ingali masikini hivi? Hali huwa mbaya zaidi ninapobanwa kuhusu suala la ufisadi - ile tabia kengeufu tena angamizi ambapo "mashing'weng'we" wachache tu waliofanikiwa kuipakata keki ya taifa wanaiguguna wao kwa wao bila kujali wenzao wanaokufa na njaa. Kwa hili huwa sipendi kuitetea Tanzania na huwa naiacha iparurwe.
 • Kizazi cha dot.com - hiki kinachokulia katika utandawazi na usasa kinajivunia Utanzania? Kina sababu ya kufanya hivyo? Inabidi tuwe na wasiwasi?
Angalizo: Nimeandika kwa "kuparaza" tu kwani mtandao ninaotumia una vituko kwelikweli. Kama kuna makosa ya hapa na pale katika mantiki au vinginevyo, natangulia kuomba msamaha!

2 comments:

 1. Kaka Matondo hongera sana kwa kuipenda vilivyo Tanzania yetu ambayo siku hizi imekuwa maarufu sana kwa kaulimbiu za kupendeza masikioni. Subiri kidogo tu, utaisikia mpya nyingine

  ReplyDelete
 2. Hodi wana blog jamani nifungulieni mlango
  Mkibunga najumuika nanyi wanaharakati katika kujadiliana mambo mbali mbali ya siasa,michezo,elimu na mengine mengi ya kijamii mie mgeni katika uwanja huu hata sijui la kufanya kuiboresha blog yangu nimekuwa nikiisoma sana blog ya matondo prof.Mimi naitwa leo alphaxard jasson ni mwalimu mwanaharakati ninaye tamani siku moja nchi yetu iongozwe na kiongozi mwenye utashi na dhamira safi.prof.matondo ni mwanasengerema najongea kwenye ulimwengu huu.niandikieni jamani. mkibunga activist.blogspot.com

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU