NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, May 11, 2010

UNAOGOPA KUSAFIRI KWA NDEGE? SOMA HAPA UONE KAMA UNAWEZA KUISHINDA AEROPHOBIA!!!

Jana wakati natoka Toronto Canada jambo la ajabu lilitokea. Japo kulikuwa na misukosuko na ndege ilikuwa inatikisika sana, sikuwa na hofu wala mshtuko. Mwenyewe nilijishangaa kwani kwa kawaida katika hali kama hii ningekuwa ninatoka jasho na nimeshikilia kiti kwa nguvu zangu zote. Inawezekana nimeishinda  Aerophobia - hofu ya kusafiri kwa ndege!

Sina uhakika lakini pengine inawezekana. Mbali na mambo mengine, nimesoma na kujielimisha sana juu ya ajali za ndege.  Baadhi ya mambo niliyojifunza ni haya:
 1. Usafiri wa ndege ndiyo salama zaidi kuliko usafiri mwingine wo wote.
 2. Uwiano wa uwezekano wa kufa kwenye ajali ya ndege kwa mashirika ya ndege yenye ndege mbovu ni mara moja tu kwa safari 724,000. Kwa mashirika ya ndege yenye kuzingatia usalama, uwiano ni chini ya mara 1 kwa 10,000,000. Na kama unasafiri kila siku kwenye ndege kwa miaka 30 mfululizo, uwiano wa uwezekano wa kufa kwenye ajali ni mara moja kwa 787.
 3. Uwezekano wa kupigwa na radi ni mara moja kwa 750,000 na kama utaishi mpaka kufikisha miaka 80 basi uwezekano wako wa kupigwa na radi ni mara 1 kwa 6250.
 4. Uwiano wa uwezekano wa kufa katika ajali ya gari ni 1 kwa 67. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kufa katika ajali ya gari kuliko kufa katika ajali ya ndege.
 5. Isitoshe, kuna vitu vingi vinavyoweza kuhitimisha maisha ya binadamu ikiwemo kurogwa (washirikina mpo?). Hapo ulipo kuna mifumo tata lukuki katika mwili wa binadamu ambayo kila mmoja ni lazima ufanye kazi barabara vinginevyo binadamu aweza kuanguka na kukata roho na kuwaacha watu wakisema eti ametupiwa jini kumbe ni kiharusi, kisukari, mshtuko wa moyo na mengineyo.
 6. Isitoshe, kama alivyosema Marcus Aurelius (a.k.a Mwenye hekima) - mtawala wa himaya ya Roma ya kale kutoka mwaka 161 mpaka kifo chake mwaka 180 B.K, kuna tofauti gani kati ya yule anayeishi siku tatu na yule anayeishi vizazi vitatu? Ati, kuna tofauti yo yote ukifa leo na ukifa baada ya miaka 50 kuanzia sasa? Kama ipo ni ipi?
 • Baada ya kusomasoma huku na huko na kutafakari sana, nimefikia hitimisho kwamba pengine ni upuuzi tu kuogopa kusafiri kwa ndege kwani uwezekano wa kufa humo ni mdogo mno.Inabidi tuogope zaidi kufa katika ajali za barabarani kuliko kufa katika ajali za ndege.........Lakini siku moja wakigundua ndege ambayo haitikisiki sitalalamika! Kwa maoni zaidi kuhusu kifo gonga hapa na halafu usikose kumtazama huyu rubani mbabaishaji hapa chini.6 comments:

 1. safi saana. wamekubrain wash ehe!

  ila swwali la vizazi vitatu na siku tatu liko sawa

  ReplyDelete
 2. Kamala nawe bwana - wakati mwingine ku-brain wash-iwa ni vizuri hasa katika mambo yasiyo na faida kama hili. Kwani kuogopa na kutetemeka kwangu kwenye ndege kulikuwa kunasaidia nini? Kuna mambo mengi sana ambayo tunayaogopa lakini ukichunguza vizuri hofu zetu hazina msingi, na mengi kati ya hayo wala hatuwezi kuyazuia wala kuyapinga.

  Usipokufa kwenye ajali ya ndege (ambayo ni nadra sana) basi utakufa kwenye ajali ya gari, UKIMWI, kujikwaa na kuanguka wakati ukitembea na au kulala tu halafu ukashindwa kuamka. Kama alivyosema Epicurus - tufurahie maisha na kuacha kutishwa na mambo ambayo wala hatuna uwezo nayo kama hili la kujiharishia ndege ikianza kutikisika!!!

  ReplyDelete
 3. Fani zote zinahitaji umakini. Lakini hizi za kushikilia roho za watu (udereva, udaktari, urubani na nyinginezo kama hizo) zinahitaji watu waliotulia zaidi. Ubabaishaji wa rubani hauwezi kulinganishwa na miyeyusho ya mwalimu kama mimi kwa wanafunzi.

  Kuhusu hofu, nakubaliana na Kamala. mengi tunayoyaogopa hayanaga maana kabisa. Ni sawa na kuogopa kitu hewa. Lakini bahati mbaya ni kwamba huwa hatuchagui kuogopa!

  ReplyDelete
 4. Nipo nanyi nyooote.
  Nikiwa form 2, nilikuwa nashinda "custom" kwa rafiki yangu Nahodha wa Mv Bukoba ambaye alikuwa akinieleza namna ambavyo Meli ndicho chombo salama zaidi duniani na kuwa ajali zake huchukua masaa kabla hazijapoteza kila kitu (tofauti na ndege).
  Nikaja kuingia kimuhemuhe na kumhoji rubani. Tobaaaa. Anakwambia ndege ndio kitu salama zaidi kuliko aina yoyote ya usafiri na ma-data makubwa makubwa kama hayo uliyotoa.
  Nilichoamini na ninaendelea kuamini ni kuwa hata kama chance ya kufa ni 1 kati ya watu wooote uimwenguni, kinachotakiwa ni MOJA HIYO USIWE WEWE. That's all matter. Hizo namba wanazoweka huwa zinasaidia kama uko kwenye ground. Ukiwa angani unawaza "kwani nani anajua kuwa katika hizo safari 1 kwa 10,000,000, yangu haipo?
  Kwa hiyo suala sio ni idadi gani iliyopo. Suala ni kuwa HUTAKI KUWA IDADI HIYO,hata kama ni nusu ajali kwa kila mwaka.
  Nawaza kwa akili na naamini kwa maoni haya mshajua kuwa nami SI mpenzi wa ku-fly

  ReplyDelete
 5. Sasa Mzee wa Changamoto vipi tena? Mimi najaribu kupona aerophobia nawe unanirudisha kule kule.

  Unajua binadamu sie ni viumbe wa ajabu sana. Tunapocheza bahati nasibu (Lotto) tunategemea kushinda hata kama uwezekano wa kufanya hivyo ni 1 katika watu 100,000,000. Hii ni bahati ya mtende!

  Tunaposafiri kwa ndege pia tunadhani kwamba sisi tutakuwa ndiyo 1 kati ya hao 10,000,000 watakaokumbwa na ajali. Kama vile kushinda lotto hapo juu, basi kufa katika ajali ya ndege napo tukuchukulie kama bahati ya mtende ati! Na "bahati" hiyo ikikuangukia wewe hapo ndipo kazi sasa.

  Kwingineko: Mbona hatufikiri namna hiyo kila siku tunapoingia kwenye gari ambapo uwezekano wa kufa katika ajali ni mkubwa zaidi?

  Kuanzia mwaka kesho pengine nitakuwa nakwenda Tanzania kila mwaka mara moja au mara mbili na bila kupambana sawasawa na hii aerophobia mbona kitakuwa kizungumkuti.

  Kwa hivyo Mzee wa Changamoto, nimedhamiria kweli mwenzio kupambana na japo ni kweli kwamba "suala sio ni idadi gani iliyopo. Suala ni kuwa HUTAKI KUWA IDADI HIYO" naamini kwamba mimi sina bahati ya mtende ya ama kushinda lotto (nimeshaacha kucheza siku nyingi tu) au kufa katika ajali ya ndege (nitaendelea kupanda bila woga)

  ReplyDelete
 6. Huyo aliyejenga karibu na uwanja wa ndege namna hiyo hatari tupu. Usiku sijui wanalalaje. Duh!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU