NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, June 21, 2010

BINADAMU NA UBINADAMU WETU: SHILINGI 5,000 ZINAPOMLIZA MTU MZIMA

 • Nianze na angalizo: Lengo langu hapa siyo kujigamba wala kujionyesha bali ni kuonyesha  (kama vile ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara) jinsi matendo madogo madogo ya kibinadamu yanavyoweza kuwa na athari katika maisha ya binadamu wenzetu hususan wale wenye shida. 
*********************************
 • Tarehe 9/6/2010 nilipanda daladala kutoka Masaki Mwisho kwenda Posta Mpya. Tulipofika mwisho wa safari nilishuka na kuanza kuelekea jingo la Posta Mpya. Kwa mbele yangu alikuweko mzee mmoja ambaye tulikuwa wote kwenye daladala. Mzee huyu alikuwa amevaa kandambili na nguo zilizozeeka.
 • Kwa vile kulikuwa na tope kidogo, mzee yule aliteleza kidogo na kandambili yake ya mguu wa kulia ikakatika. Nilimwangalia akiwa ameghafilika huku akiwa hajui la kufanya na wakati huo huo watu wakianza kumrushia maneno ya kuacha kuzubaazubaa na “kulivaa” tope.
 • Kwa bahati nzuri kando ya barabara kulikuwa na vijana waliokuwa wanauza fulana, magazeti, viatu (vya bei mbaya), mikanda pamoja na kandambili.
 • Nilitoa noti ya shilingi 5,000 na kumpa yule mzee na kumwambia anunue kandambili mpya. Kwa mikono miwili aliipokea ile noti na kunishukuru tena mno “Mungu Akubariki na kukuzidishia mwanangu”. Alisema huku machozi yakimlengalenga. Na kweli alikwenda na kujinunulia kandambili nyekundu mpya. Nilimtakia siku njema na  nikaendelea na mishughuliko yangu.


 • Kwangu mimi ni matendo madogo madogo kama haya ndiyo hasa yanasaidia kuupambanua ubinadamu wetu. Si ajabu mzee huyu asikisahau kitendo hiki kidogo maishani mwake kama mimi nilivyoshindwa kukisahau kitendo nilichofanyiwa na mzee mwenye kibaraghashia cheupe, kanzu nyeupe na kandambili za bluu zaidi ya miaka 17 iliyopita pale Muhimbili.
 • Hebu na tukawasaidie na kuwatendea wema binadamu wenzetu. Hakuna tendo lenye kuliwaza na kuleta furaha na ridhiko la kweli hapa duniani kama kumsaidia binadamu mwenzako hasa mwenye shida!

6 comments:

 1. Naam, kutoa ni moyo, usambe utajiri.
  Ni kweli kuwa kila binadamu atakiwa kufanya kazi na ale kwa jasho lake ili kuondoa utegemezi na uvivu, lakini nyakati nyingine mtu huwa mhitaji bila kutarajia. Ulichokifanya nimeona kimetokana na kuona adhiriko la mtu huyo na ukajiweka katika nafasi yake na ukajiona kuwa ingelikuwa ni wewe imekutokea, ungetamani ashuke Malaika au Msamaria kukusitiri, ndicho ulichofanya.

  Tupambane na ombaomba, wavitu nategemezi, lakini tusikose hekima ya kupambanua na kusaidia walio katika hali ya uhitaji.

  Nakupongeza Prof. Matondo, naongeza kukuombea neema na baraka, uwe kama bomba lenye maji!

  ReplyDelete
 2. Laiti watu wote tungekuwa na moyo wa huruma kama wako hakika tungefika mbali sana.Mungu na akubariki Prof.. kwa kuonyesha upendo kwa wale wenye kuhitaji msaada.

  ReplyDelete
 3. Wapendwa Subi na Edna;
  Asanteni sana kwa maneno yenu ya busara na kupoza moyo. Ukijifanya kiherehere wa kutoa misaada huku nyumbani basi kuna uwezekano wa hao unaowasaidia kuishi maisha ya starehe zaidi kuliko wewe unayehenya na kubeba maboksi huku ughaibuni. Utakuta jamaa hata kazi hawafanyi na kazi yao ni kutandika bia tu wakati wewe unatuma pesa kila mwezi ukidhani kwamba unawasaidia nduguzo kutatua matatizo yao. Hilo nimeshajifunza muda mrefu sana!

  Lakini, kama alivyosema Dada Subi, kuna watu wenye shida za kweli kabisa na ambao wako makini na msaada uutoao. Tangu nizukiwe na Mzee yule pale Muhimbili, pendeleo langu ni kutoa msaada kwa watu ambao siwafahamu na ambao pengine hatutaonana tena! Hii ndiyo mimi hunipa ridhiko la kweli. Ndugu na jamaa hao tunasaidiana katika ulimwengu wetu wa kindugu. Misaada ya kindugu hiyo huwa siizungumzii hapa kwani kwa sisi Waafrika tunaamini kwamba kwa ndugu kusaidiana ni wajibu. Ndiyo maana mjomba usipompa pesa au kumnunulia suti basi atakushangaa sana. Ila sasa naona mambo yameanza pia kubadilika kwani watu wameanza kuwa wachungu kweli kweli.

  ReplyDelete
 4. Ndugu yangu "Matondo",

  Ulichokifanya ni kitu kikubwa sana. Sio tu kwa huyo Mzee, bali na mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukusubiri muda wa kufikiri kwa kuhesabu fedha yako mfukoni wala kujiuliza faida utakayoipata baada ya kumsaidia na wala hukujua ni kiasi gani angekushukuru Mzee huyo kwa msaada wako huo.

  Endelea kuwa na moyo wako huo, wenye upendo mkubwa kwa binadamu wenzako. Wapo wachache sana Watanzania wenye mioyo ya aina ya kwako. Mtanzania mwingine anayenishangaza kwa roho nzuri na mapenzi makubwa kwa nchi yake ya Tanzania ni "Dada Subi".

  Sote tunaona misaada anayoitoa kwa kuwaelimisha watu namna ya kutumia Programu mbali mbali za computer. Na anatoa Elimu hiyo bure na kwa kila mtu. Subi anajitahidi kutuchimbia habari mbali mbali ili nasi tuzipate.

  Mtu mwingine niliyefurahishwa naye kwa kuwa na moyo wa kupenda watu ni "Vicky Ntetema" wa BBC. Tumesoma habari zake kuhusu kujitolea kwake kuwasaidia "Wagonjwa wa Ngozi" - Albino. Sisi wengine wenye mioyo migumu, mnatufanya tujifunze na tubadilike ili tufanane na mioyo ya aina yenu. Mwenyezi Mungu atatusaidia!

  It's Great To Be Black=Blackmannen

  ReplyDelete
 5. Aksante kaka.

  Kadiri unavomfanyia 'mdogo' kati ya walio wake ndivo anavoendelea kukujaalia hata kama hujui ama huoni.

  ReplyDelete
 6. kutoa ni moyo, Tenda wema usingoje shukurani hapa duniani. Ahsante sana kwa moyo wako na uendelee nao na tena uzidishe.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU