NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, June 17, 2010

PRECISION AIRLINES WANAJITAHIDI

 • Hivi karibuni nilisafiri kutoka Mwanza kuja Dar es salaam na ndege ya Boeing 737 ya shirika la ndege la Precision. Nilifurahishwa na huduma zao nzuri (ukiachilia mbali udogo wa uwanja wa ndege wa Mwanza ambao hauchelewi kusababisha msongamano wa abiria). Ndege ilifika na kuondoka katika muda uliopangwa. Ndege ilikuwa safi na wahudumu walikuwa wachangamfu na wenye bashasha. Chakula  - sandwich moja– pia kilikuwa kizuri.
 • Kule Marekani tumezoea ukipanda ndege katika daraja la kawaida hasa katika safari fupi kama hii basi unapata kimfuko kidogo cha karanga zilizokaangwa na kutiwa chumvi na pengine maji. Ndiyo maana nilipomwona mhudumu akipita na bia za makopo za Kilimanjaro, nilimuuliza kama bia hizo zilikuwa zinauzwa. Binti yule mweusi mrefu mtanashati alicheka sana na kuniambia nimpe pesa zote nilizokuwa nazo ili akaniletee bia. Basi alibakia amesimama pale huku akisubiri nimpe pesa. Nilipomuuliza bei ya bia moja aliniambia tena kwamba nimpe pesa zote nilizokuwa nazo mfukoni mwangu. Ndipo nikajua kwamba alikuwa anatania!
 • Kama vile kunikomoa, aliondoka na kurudi na bia nne. Aliziweka katika kimeza changu, akanikaribisha kwa uchangamfu na kunijulisha kwamba kila kitu katika ndege za Precision kilikuwa bure; na kwamba nikihitaji kitu kingine cho chote basi nisisite kumwambia. Mbele yangu kulikuwa na kundi la vijana kama 6 hivi ambao walikuwa wakisafiri pamoja. Binti yule alionekana akicheka nao kwa uchangamfu mkubwa huku akiwahudumia. Hii ilikuwa mandhari ya kufurahisha kwani tumeshazoea wafanyakazi wachovu ambao muda wote huwa wamenuna. Ilikuwa mandhari nzuri!
 • Nilipendezwa sana na utani na uchangamfu wa mfanyakazi yule mrefu mtanashati. Ndege ilipotua na abiria tukaanza kutoka mfanyakazi yule aliniambia kwamba katika safari zangu zingine ni lazima nihakikishe kwamba nasafiri na Precision Airlines. Nadhani nitafanya hivyo!
Angalizo: Usije ukaniuliza nilifanya nini na zile bia nne za bure nilizoletewa! Tazama hapa kuhusu "kero" za Precision!

3 comments:

 1. hongera kaka! ulikuwa na bahati kumpata huyo. wakati mwingine wanakuwa na kisirani kama vile wamekamuliwa limao kwenye uso....lol!

  ReplyDelete
 2. Mimi napendekeza Precision tuibadili jina na kuiita Air Tanzania.

  Mimi wananiudhi tu jinsi wanavyozungumza Kiingereza chao. Yaani wanabinya pua utadhani wako chooni na kinachotoka hapo Kiingereza si Kiingereza bali mvurugano tu. Mbona wasizungumze Kiingereza bila kubana pua? Au kubana pua ndo kuongeza utaalamu? Malimbukeni tu!!!

  ReplyDelete
 3. Customer Service bado Zero though. Ukienda kununua tiketi wanadengua hao. Hata ukilipa pesa hakuna thanks wala karibu tena. Inaonekana kama vile unawabembeleza. Hata kwenye ndege mambo ni yale yale tu. Naona wewe umebahatisha tu au huyo demu aliyekupa bia zote hizo alikuwa amekuzimia tu. Si ajabu akijulikana atafukuzwa kazi huyu.

  We still have a long way to go hasa kwenye ishu ya customer service. Sijui hawa wasichana wauza tiketi wamewaokota wapi. Utafikiri wapo kwenye mashindano ya urembo kwa jinsi wanavyodengua dammit!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU