NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 30, 2010

FIKRA YA IJUMAA: MDAHALO WA KUKATA NA SHOKA KATI YA “BABA MTAKATIFU” NA MZEE WA KIYAHUDI. TUTAFAKARI !!!

 • Hiki ni kisaasili cha Papa (AKA “Baba Mtakatifu”) na mzee mmoja wa Kiyahudi asiyejua kusoma wala kuandika aitwaye Moishe. Tafadhali kisome kwani kuna jambo kubwa la kujifunza kuhusu maisha na maarifa yetu; na jinsi tunavyoyatazama mambo. Nimekifupisha!
*****************

 
 • Karne moja hivi iliyopita, Papa aliamua kwamba Wayahudi wote ilikuwa lazima wauhame mji wa Roma. Baada ya uamuzi huo kupingwa na Wayahudi wengi, na kutaka aonekane kwamba ni mtu anayependa maelewano, Papa alikuja na pendekezo moja zuri ambalo alidhani kwamba lingewafurahisha Wayahudi na wakati huo huo kuweza kuwaondoa kutoka mji wa Roma bila mtafaruku mkubwa. Aliamua kwamba angefanya mdahalo na mtu ye yote atakayeteuliwa na Wayahudi kuwawakilisha. Kama mwakilishi yule angeshinda mdahalo ule basi Wayahudi wangebakia katika mji wa Roma. Lakini kama Papa angeshinda mdahalo basi Wayahudi wangelazimika kuuhama mji wa Roma mara moja!
 • Wayahudi walianza kutafuta wasomi, wanaakademia, wanafalsafa na watu wengine wenye maarifa ili kuchagua mmoja aliyebobea ambaye angeweza kupambana na Papa katika mdahalo ule. Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, hakuna msomi hata mmoja wa Kiyahudi ambaye alikubali kukabiliana na Papa. Wakiwa katika hatua ya kukata tamaa hatimaye mzee mmoja mfanya usafi (janitor) aitwaye Moishe alijitokeza. Mfanya usafi huyu asiyejua kusoma wala kuandika alikubali kukabiliana na Papa katika mdahalo ule wa kukata na shoka.
 
 • Kwa vile hakuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza na kupangilia hoja kwa mantiki na mpangilio, Moishe alipendekeza kwamba mdahalo ule ufanyike katika ukimya kabisa, yaani bila kuzungumza. Papa alikubali.
 • Siku ya mdahalo ule wa kukata na shoka ilipofika, Moishe na Papa walikaa katika viti vilivyotazamana. Kwa dakika nzima ya kwanza, walikaa wakitazamana tu huku wakiwa kimya kabisa. Hakuna aliyesema neno lolote kwa mwenzake.
 • Dakika ya pili ilipoanza, Papa alinyosha mkono wake wa kulia na kunyosha vidole vitatu. Moishe alimwangalia naye bila kusita alinyosha mkono wake wa kulia na kunyosha kidole kimoja. Papa alipoona hivyo alinyosha kidole kimoja na kukizungusha juu ya kichwa chake. Moishe alijibu kwa kunyosha kidole chake kuelekea chini kwa msisitizo.
 • Kuona hivyo Papa alitoa ule mkate unaoliwa kanisani na waumini kila Jumapili na glasi moja ya mvinyo na kuviweka katika meza iliyokuwa mbele yake. Moishe alijibu kwa kutoa tofaa (apple) kutoka katika mfuko wake na kuliweka katika meza mbele yake. Kuona hivyo Papa alinyanyuka na kusema kwa sauti kubwa, “Nimeshindwa! Myahudi huyu ni mweledi mno. Ameshinda na Wayahudi wanaweza kubakia Roma!.”
 • Baada ya mdahalo huu mkali makadinali wote walikaa wakimzunguka Papa na kumuuliza kilichotokea katika mdahalo ule. Papa aliwajibu, “Kwanza niliinua vidole vyangu vitatu kuonyesha utatu wa Mungu. Myahudi yule aliinua kidole kimoja kunikumbusha kwamba bado kuna Mungu mmoja tu – kitu ambacho ni kweli katika dini zetu mbili. Baada ya hapo nilizungusha kidole changu juu ya kichwa changu kuonyesha kwamba Mungu Alikuwa Ametuzunguka. Myahudi alijibu kwa kunyosha kidole chake chini kuashiria kwamba Mungu Alikuwepo pale pale tulipokuwa tumekaa. Nilitoa mkate na mvinyo ili kuonyesha kwamba Mungu alitufia na kutufutia dhambi zetu, Myahudi alitoa tofaa kunikumbusha juu ya dhambi zetu wanadamu. Alikuwa na jibu kwa kila swali nililouliza. Sikuwa na kingine cha kufanya
 • Wayahudi nao kwa upande wao walikuwa wamekusanyika kushangilia ushindi wa Moishe. Walitaka sana kufahamu jinsi mfanya usafi yule mzee asiyejua kusoma na kuandika alivyoweza kumshinda Papa katika mdahalo ule. “Sawa nitawaambia” Alianza Moishe huku wasomi na wanafalsafa wa Kiyahudi wakisikiliza kwa makini.
 • Kwanza alinyosha vidole vyake vitatu kunionyesha kwamba Wayahudi walikuwa na siku tatu tu kuuhama mji wa Roma. Mimi nilinyosha kidole kimoja kumwambia kwamba hakuna hata Myahudi mmoja ambaye alikuwa tayari kuondoka. Alinyosha kidole chake na kukizungusha juu ya kichwa chake ili kuniambia kwamba hakuna hata Myahudi mmoja ambaye angebakia katika mji huu. Mimi nilinyosha kidole changu chini ili kumwonyesha kwamba Wayahudi wote tulikuwa tunabakia hapa hapa.”
 “Halafu kukatokea nini?” Aliuliza mwanamke mmoja kwa shauku kubwa
“Sijui” Moishe alisema. “Alitoa mlo wake wa mchana nami nikatoa wa kwangu.”
 • Na kisaasili chetu kinaishia hapa…Umejifunza nini?
******************

3 comments:

 1. Nilipomaliza kusoma kisa hiki nilijikuta nacheka, nacheka huo mtizamo wa mawazo.
  Tafsiri ya kitu inaweza ikatofautiana kati ya mtu na mtu, hasa kati ya msomi na mtu wa kawaida. Hekima ni ikitu cha ajabu sana, hekima haihitaji kwenda shule, unaweza ukaenda shule na bado ukashindwa hekima na ambaye hajawahi hata kukanyaga darasa.
  Nakumbuka kijiini, kulikuwa na mgonjwa aliyeshikwa na tumbo la kuhara. Bahati nzuri siku hiyo alikuwepo dakitari aliyekuja likizo, yeye akasema kabla mgonjwa hajapata tiba inabidi choo kichukuliwe, ila apewe maji yaliyochanganywa na chumvi.
  Mgonjwa hali ikawa mbaya, kila muda uliokwenda, kwani vipimo vilichukua muda. Babu yetu akainuka akazunguka nyuma ya nyumba akachuma majani ya ndulele, akamwambia ayatafune na kumeza maji yake, hutaamini baada ya dakika chache tumbo likatulia.
  Nilijiuliza ina maana ugonjwa mwingine hauhitaji `udakitari'?
  Sio lazima kila jambo lipelekewe msomi, mambo mengine yanahitaji hekima, na hekima haihitaji shule saana.
  Ngoja nimalizie hapa kwani nami nina kisa nataka kuwapa karibuni blogini msome.

  ReplyDelete
 2. Ni fkira pevu, ni falsafa ambayo Moishe nampongeza kuwa nayo. Na vilevile ulikuwa mjadala mkali ambao kwa hakika unaweza kudhani ni waigizaji.

  Tukirudi katika mani zetu hizi kwa hoja ya papa kuhusu utatu, turudi katika Itolia ya utatu, naamini mzee Moishe alikuwa akisimamia kitu cha msingi na kinachoakanganya hasa tukija katika utatu na mungu mmoja. Itolia ya utatu ndiyo maana mzee wa kiyahudi alitumia kidole kimoja. labda amwgiji wa teolojia watavuka waseme basi na kukiri mzee Moise alisimamia kitu ambacho wayahudi wa kweli wanaamini-kidole kimoja(mungu mmoja)

  Lakini katika hekima ni jambo ambalo halipo darasani, katika kuamini na kama kinachoaminiwa kinathibitishwa ni sahihi na muumini wake, mfano mzee Moishe, naamini anastahili kuwa na falsafa yake bora inayoapaswa kufunzwa kwetu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU