NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, July 29, 2010

HIZI NDIZO FAIDA ZA KUPANDA DALADALA (SEHEMU YA KWANZA)

 • Ninapokuwa Tanzania na hasa Dar mimi hupenda kusafiri kwa daladala (na mara chache sana kwa teksi). Pamoja na ukweli kwamba sina gari, kuendesha Dar ni changamoto kwelikweli. Kuna wakati mmoja niliendesha kutoka Masaki kwenda Posta Mpya na mambo niliyopambana nayo siku ile niliona kwamba pengine ni bora tu kupanda daladala. Mbali na kutukanwa na madereva wengine (hasa wa daladala) na kupigiwa honi mfululizo, shida kubwa ilikuwa ni maegesho mwisho wa safari yangu. Nilizunguka mjini kwa muda mrefu bila kupata sehemu ya kuegesha mpaka jamaa mmoja akajitolea kuniegeshea gari langu (na kulilinda) kwa malipo. Mjini shule ati!
 • Tabia yangu hii ya kupanda daladala hata hivyo kumbe ni kero kwa baadhi ya watu ambao hawaelewi ni kwa nini mtu anayebeba maboksi Marekani kama mimi ashindwe kununua hata ka-Corolla na aishie kupanda daladala. Nimewahi kuambiwa eti nina roho ya kimasikini, mshamba, nimezubaa na majina mengine ya kushangaza. Ambacho hawaelewi waita majina hawa ni kwamba si kila mbeba maboksi wa Marekani anaweza kumudu kununua gari. Marekani dola hazimwagwi barabarani ati! Basi mimi huishia kucheka tu na kujikalia kimya. Maisha!
 • Mbali na kwamba ni usafiri rahisi na unaopunguza msongamano wa magari barabarani (ukiachilia mbali kubanana, mwendo wa kasi na kunukishiana vikwapa) kuna faida nyingi zinazonifanya nipande daladala.
 • Kwanza: Kama mwanaisimu, lugha inayozungumzwa kwenye daladala pengine ndiyo inaakisi kwa ufasaha zaidi mabadiliko yanayotokea katika jamii. Baada ya kukaa nje kwa muda, daladala kwangu ni maabara ya kujifunzia misemo, nahau, misamiati, vijembe na mitindo mipya ya lugha. Kiswahili kinachozungumzwa na makondakta, wapiga debe na abiria kina utajiri wa tamathali za semi na vikolombwezo vingine vinavyoakisi kwa uangavu wa kutosha mabadiliko yanayotokea katika lugha. Na kwa vile lugha haikakawani katika ombwe, mara nyingi mabadiliko katika lugha huakisi pia mabadiliko katika jamii husika kwa usahihi wa kutosha.
 • Pili: Daladala ndiyo sehemu bora kabisa ya kusikilizia hali halisi na matatizo ya wananchi wa kawaida. Ukitaka kujua dukuduku la watu wa tabala la chini (ambao ndiyo wengi), matatizo na hata matumaini yao, basi panda daladala. Katika daladala utavisikia visa vya akina mama wajawazito waliopoteza maisha yao kwa vile tu hawakuwa na pesa za kulipia operesheni za uzazi ambazo pengine zingeokoa maisha yao. Katika daladala utawasikia wananchi wakilalamikia uzembe wa viongozi, rushwa na upendeleo katika ugawaji wa vyandarua vya kuzuia mbu na huduma zingine za jamii. Katika daladala utasikia uchungu, kilio na matumaini ya jamii. Katika daladala utasikia kuzaliwa na kufa kwa penzi changa. Katika daladala……. Badala ya kuitisha mikutano pengine ingekuwa bora kama viongozi wangepanda daladala japo mara mbili kwa mwezi, wakakaa kimya humo na kuwasikiliza waongozwaji wao. Naamini kwamba wangejifunza mengi zaidi kuliko yale wanayojifunza katika mikutano yao ya hadhara iliyojaa wapambe na shamrashamra za kila aina!
 • Tatu:   Katika daladala ndimo pia unaweza kuvipata visa vya kweli vya kusisimua kama hiki nilichokishuhudia laivu katika daladala ya kutoka “uzunguni” Mbagala kwenda Posta Mpya. Tulipofika pale Mtoni Mtongani jamaa mmoja ambaye alikuwa ametinga pamba za kwelikweli alikuwa anashuka. Aliposhuka, konda aliamru mchuma uondoke. Yule jamaa mtanashati aliruka juu na kumwamru konda atulize ngoma. Jamaa alirudi ndani ya daladala na kutangaza kwa sauti kubwa kwamba alikuwa amedondosha HIRIZI yake ya hatari sana na kwamba kama hirizi hiyo isingepatikana basi safari ya daladala ile ingekuwa na mikosi. Basi wasafiri wote kwa juhudi walianza kuhangaika kuangalia huku na huko. Na baada ya muda, mama mmoja aliokota kidude cheusi na kukinyosha juu.

“Ni hii?”
“Ndiyo yenyewe”
 • Alijibu yule jamaa mtanashati kisha akachukua hirizi yake na kwenda zake. Tukio lile lilitawala mazungumzo katika daladala ile mpaka tulipofika mwisho wa safari yetu. Mazungumzo yale, mbali na mambo mengine, yalionyesha jamii ambayo bado imejikita sana katika imani za kishirikina, jamii yenye hofu ya “nguvu za giza" katika karne hii ya sayansi na teke linalokujia!
 • Nitaendelea kuelezea faida zingine katika toleo lijalo. Nawatakia safari njema wapanda daladala wenzangu! 

4 comments:

 1. kali, na sasa kuna kipindi kwenye tv kinaitwa dala dala

  ReplyDelete
 2. Nakubaliana nawe mwalimu Matondo. Mbali na urahisi wa kwenda hapa na pale, ni usafiri ambao wananchi wengi wa kawaida tunaweza kuumudu. Tunasubiri hizo porojo zaidi na tafadhali usisahau masuala kama vile vibaka na kadhalika.

  ReplyDelete
 3. Ndio mkuu, kwenye daladala kuna kila kitu, hujasikia jamaa walisafiri toka Msasani hadi Gongolamboto, wakaoana na mwisho wa sfari wakawa wameshatalikiana.
  Jamaa mmoja ndani ya daladala alimkuta binti mrembo wakapendana baada ya mazungumzo marefu, wakaamua kufunga uchumba. safari inaendelea.
  Baadaye yule binti akapata kiti, kwani wakati wanaongea na huyu jamaa walikuwa wamesimama. Yule binti akawa amekaa na mshefa mmoja ana laptop yake, akavutiwa naye, manake licha ya laptop, alikuwa na blacberry, enzi hizo zinatamba sana.
  Wakaanza mazungumzo, na baadaye binti akaona huyu ndiye anayemfaa siyo yule anayepaka rangi, wakaahidiana uchumba. Huyu mpaka rangi baadaye akapata kiti nyuma ya hawa jamaa, akawa sio mpaka rangi tena ni bosi.
  Akajaribu kumshika yule binti bega ili ageuke waendelee kuongea, lakini binti akajifanya hamsikii na kuendelea kuongea na mpenzi mpya.
  Baadaye huyu mpenzi mpya akagundua jamaa nyuma anampa kero mpenzi wake, ikabidi ageuke na kuanza kuzozana na jamaa.
  'Wewe vipi mbona unaingilia wake za watu'
  'Mke wako huyu, unaumwa nini, mimi nilishaoana naye mapema wakati tupo foleni ya Magomeni..'
  'Acha mzaha wako, yeye alishakupa talaka wakati tupo kwenye foleni ya Karume acha kunitania, wewe wakati unapaka rangi alisha kupiga kibuti..'
  Mzozo huo ulikwenda hadi tunafika Banana, na hapo binti akashuka na kuwapa talaka wote wawili.
  Ina maana kuwa kwenye daladala kuna mazuri na mabaya,
  Na ndani ya daladala unatakiwa uwe na subira, kwani unaweza ukasimama na mguu mmoja kwa masafa marefu, ukiushusha unasikia umenikanyaga, huna adabu wewe, mjinga wewe nk na humo usiwe na `alergy' ya harufu, kwani kila harufu ipo. Humo kuna kuoa , na kuachana, humo kuna ...
  Hebu soma hii kwanza :

  http://miram3.blogspot.com/2009/08/mfadhaiko.html

  Inaatosha kwa leo

  ReplyDelete
 4. hata kama umejaaliwa kumiliki gari binafsi ni vema siku moja moja ukapanda hizi matatu za dar es salaa. ukipanda dala dala badala ya gari lako huna presha ya parking, kuishiwa mafuta na kusimamishwa na trafiki. pia kunako foleni wewe unauchapa usingizi mtamu sana. kama haitoshi unafanikiwa kuwaona wapitao nje na maeneo kuyajua(kama umekaa dirishani)

  kamala lakini kipindi cha tv cha daladala bado hakijaakisi sawasawa dala dala zetu, yaani matusi, kubanana, kuibiana simu, akina kaka kujisogeza kando ya makalio ya kina dada kwa kisingizio cha gari kujaa na kadhalika. hakika daladala ni maabara.

  prof nadhani mtu anaweza kuandika tasnifu ya uzamili ama uzamivu kabisa hapa, au?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU