NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, July 12, 2010

NIMERUDI: SAFARI YANGU YA NYUMBANI, HARAKATI ZA UCHAGUZI, MSIBA, NG’WANAMBITI NA MENGINEYO

 • Kwa muda wa karibu mwezi mzima sasa blogu hii imekuwa katika mwendo wa kusuasua. Sababu kubwa ni kwamba kuanzia tarehe 25/5/2010 – 27/6/2010 nilikuwa nyumbani Tanzania kwa likizo (ya kikazi).
 • Nilikwenda kijijini ili kumwona mama. Kama ambavyo nimeshawahi kusema hapa, mwanamke huyu shujaa ndiye alinilea na kunisomesha tena kwa jembe la mkono na nikiwa kama mtoto wa mwisho, uhusiano wangu naye ni wa kipekee sana.
 • Nilikuwa na miaka zaidi ya mitatu hivi bila kuonana naye na nilikuwa na wasiwasi kwamba pengine nitamkuta akiwa amezeeka sana. Nilishangaa kumkuta akiwa bado ngangari na akiendelea kuchapa kazi zake za kawaida bila wasiwasi. Kizazi hiki tangulizi kwa hakika kilikuwa na nguvu na afya ya ajabu na sina uhakika kama sisi (na hiki kizazi cha dot.com) kama tutaweza kufikisha miaka zaidi ya 80 huku bado tukiwa na nguvu za kutafuta kuni, kuchota maji na kuvuna mpunga!
 • Nilifika nyumbani salama na kazi ya kula kuku (na mbuzi) wa kienyeji ikaanza. Niliweza pia kuchunga ng’ombe na kuchimbua karanga. Familia nzima ilikuwa na furaha sana na nilikuwa na wakati mzuri wa kukaa faragha na mama na kuongea naye vizuri.
 • Bariadi huwa inachanganya sana wakati wa uchaguzi na tayari harakati za uchaguzi zilikuwa zimeshaanza. Niliweza kuongea na wazee kijijini juu ya maoni yao kuhusu uchaguzi huo na hasa tathmini yao juu ya utendakazi na uchapakazi wa wabunge wao wawili – Waheshimiwa John Momose Cheyo wa chama cha UDP na John Andrew Chenge wa CCM. Kuna makala mbili ambazo nimeziandika juu ya suala hili na nitazibandika hapa (na kuzichapisha magazetini) katika kipindi cha wiki mbili hivi zijazo. Watanzania inabidi tuuendeleze na kujivunia utamaduni huu mzuri wa kuchagua viongozi kwa amani kila baada ya miaka mitano.
 • Nilikwenda Dar es salaam ambako nilikaa kwa siku tatu hivi na halafu nikaelekea Arusha mjini ambako nilifanya kazi (na kupumzika) katika kahoteli haka kapya kabisa. Baadaye nilihamia Usa River kwenye chuo cha MS-TCDC ili kuangalia jinsi wanafunzi wa Kimarekani wanavyojifunza Kiswahili wakiwa katika mazingira na utamaduni wa Waswahili wenyewe.
MSIBA
 • Mpwa wangu ambaye alikuwa ndiye mkuu na mwangalizi wa masuala yote pale nyumbani aliugua ghafla wakati nikiwa Usa River. Alipelekwa hospitalini ambako madaktari walijaribu sana kujua kilichokuwa kinamsumbua bila mafanikio. Vipimo vyote – kuanzia Malaria mpaka kichaa cha mbwa – vilirudi vikiwa hasi. Mambo yalipowazidia, na kutokana na uzoefu wao, madaktari walishauri mgonjwa apelekwe kwa madaktari wa kienyeji kwani walikuwa wanaamini kwamba ugonjwa wake haukuwa wa kawaida.
 • Kijana alirudishwa nyumbani siku iliyofuata na alipata nafuu ya ghafla, akala chakula vizuri na kuongea mpaka tukapata matumaini kwamba atapona. Usiku huo hata hivyo alizidiwa sana na kesho yake asubuhi roho yake ikauacha mwili.
 • Kifo hiki kilinishtua na kunisikitisha sana kwani kijana huyu, mbali na kuwa binamu yangu, pia alikuwa rafiki yangu sana! Kuanzia hapo ratiba yangu ilivurugika kabisa. Hata juhudi nilizokuwa nazifanya ili kukutana na binti wa Mkundi (a.k.a Mchungaji) zilikwama. Sijaguswa wala kuhuzunishwa na kifo kama nilivyoguswa na kuhuzunishwa na kifo tatanishi na cha ghafla cha huyu mpwa wangu mpendwa!
Picha hizi nilizipiga mwenyewe. Hapa Marehemu akiwa na mabinti 
zake. Sikujua kama picha hizi ndizo zingekuwa za mwisho!
 
NG’WANAMBITI
 • Jioni ya siku hiyo hiyo ya msiba, wakati nikipanga vitu vyangu tayari kwa safari kesho yake, mlango wa nyumba niliyokuwa nikikaa uligongwa. Nilipouliza mgeni wangu alikuwa nani, nilipigwa na butwaa nilipoisikia sauti kakamavu ya Kikurya ikijibu “Ng’wanambiti”.
 • Mwanaharakati huyu alikuwa amesafiri zaidi ya nusu saa kutoka Arusha mjini tena usiku kuja Usa River kunitafuta baada ya siku nzima mkutanoni. Lilikuwa farijiko la ajabu lililofika kwa wakati hasa uliotakiwa.
 • Tulikwenda mesini tukapata chakula cha jioni na kuongea mambo mengi ya muhimu juu ya mambo mbalimbali yanayoikabili jamii yetu. Nilipata pia bahati ya kuongea na Mama Ng’wanambiti na nilifurahi kugundua kwamba kumbe Ng’wanambiti mwenyewe ni shemeji yangu!
 • Niliongea pia na Mwanautambuzi makini Shabani Kaluse na mbali na kunipa pole ya msiba, tulipanga tukutane Dar es salaam pamoja na Mwanamalenga Fadhy Mtanga ambaye aliniandikia ujumbe mrefu wa kunipa pole. Dada Yasinta naye pia aliniandikia ujumbe mzuri wa kiroho ili kunipoza na kifo hicho. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuruni nyote – Ng’wanambiti, Kaluse, Yasinta na Fadhy.  Ninyi ni ndugu na wema wenu katika kipindi kile kigumu sitausahau. Asanteni sana!
 • Nilipofika Dar es salaam ilinilazimu nipande ndege kukimbia Mwanza kwani mambo yalikuwa hayajatulia na nilikuwa na wasiwasi sana na hali ya mama kwani sikujua jinsi ambavyo angeweza kuukabili msiba wa kuondokewa na mjukuu wake aliyempenda sana! Kutokana na misukosuko hii, nilipoteza ile nafasi ya kuweza kuonana na Kaluse na Mtanga. 
 • Pamoja na misukosuko hii, maisha ni lazima yaendelee na kuanzia sasa blogu hii itarudi katika hali yake ya kawaida. Pia nitaanza rasmi sasa kutembelea vijiwe mbalimbali na kushiriki katika mijadala mbalimbali.
Asanteni sana na Mungu Aendelee kutubariki !!!

********************* 
 • Nilifurahi sana niliporudi na kuvikuta vibinti vyangu virembo vyema vikinisubiri kwa hamu. Furaha iliyoje!!!
12 comments:

 1. Nashukuru sana kwa kuwa 'experience' ya maisha kwa kipindi kifupi namna hiyo. Kwa mpwa wetu twamuombea maisha ya kheri ya mbinguni kwani sote tu njia moja.


  Nanukuu: "Nilifurahi sana niliporudi na kuvikuta vibinti vyangu virembo vyema vikinisubiri kwa hamu. Furaha iliyoje!!!"

  Hiyo ni tungo tata ama kwa kisukuma fallacious statement!!..lol! Siku moja utatueleza ulitumia muda kiasi gani kuwa nao....lol!

  ReplyDelete
 2. Awali ya yote niseme pole sana kwa kuondokewa na mpwa wako. Tunazidi kumwomba Mungu akupeni faraja na kumjalia pumziko la amani la milele. Amina.

  Pia nikupe pole kwa mikiki mikiki ulipokuwa nyumbani hapa maana mambo yakakuzidia tofauti na matarajio yako.

  Na pole ya mwisho, ni ya safari ndefu kwenda Amerika. Tuna imani Mungu atatujalia kukutana.

  Zaidi napenda kutumia jukwaa lako kumshukuru sana na kumpongeza Kadinali Ng'wanambiti kwa jitihada zake hata kuweza kukutana nawe. Kadinali ni mtu wa kipekee sana. Kusema kweli anajitahidi sana hata awapo Dar kukutana nasi.

  Tunajivunia kuwa ndugu tunaojaliana.

  Uwe na wakati mzuri. Salamu kwa familia.

  ReplyDelete
 3. Pole sana mkuu kwa msiba na hata hizo pilika pilika zote ulizokuwa nazo huko nyumbani. Tunamuomba Mungu akupe nguvu wewe na mama na familia nzima huko nyumbani muweze kupita katika kipindi hiki kigumu. Mungu na awawezeshe..- Amen

  ReplyDelete
 4. Pole sana Matondo na karibu tena uwanjani Mungu na azidi kukupa nguvu.

  Kuhusu hutu tubinti twako mbona tunanichanganya sasa kwani unato tungapi? Samahani kwa kiswahili cha kisukuma.

  ReplyDelete
 5. Pole sana ndugu Matondo kwa msiba
  uliokupata,bila shaka sasa utaendelea
  kutupa habari motomoto.Sisi tunaendelea na pilikapilika za kuiendeleza jamii yetu hii ya Tanzania

  ReplyDelete
 6. Pole sana, na karibu tena ukumbini.

  ReplyDelete
 7. Nami napenda kukupa pole kwa mara ya pili na nimefurahi kuona upo nasi tena. Karibu sana kuwa nasi.

  ReplyDelete
 8. Pole sana kwa msiba, na hongera kwa kuweza kuonana na Mama na ndugu wengine.Karibu tena kibarazani maana tulikumiss ile mbaya.

  ReplyDelete
 9. Hongera kwa UHAI na pole kwa pilika zake. Hongera kwa kuyakabili yaliyokukuta na pole kwa kukutwa nayo.
  Hongera kwa kurejea salama na pole kwa mrejeo woote huo.
  Hongera kwa kutujuvya meengi yaliyotokea na yanayotokea na POLE-IN-ADVANCE kwa kuwa tunategemea meengi mengine kutoka hapa. Na twajua si rahisi kuyapata na kuyaweka.
  BARAKA KWAKO NA KWA FAMILIA NZIMA

  ReplyDelete
 10. Pole sana kaka,sote ndio njia yetu.Nimefurahi sana kusikia umerudi salama.

  ReplyDelete
 11. Ndugu Matondo,pole sana kwa msimba. Ndiyo kwanza nasoma hii posti yako, unajua tena summer ndiyo imechanganya na watu tunashinda nje kuota jua kama vile mijusi.

  ReplyDelete
 12. Wapendwa - Asanteni sana kwa maneno yenu ya huruma na kutia moyo. Ni mapitio ya maisha na siye kama binadamu kifo kipo ili kutukumbusha kwamba uwezo, nguvu na maarifa yetu - kama vile wanyama wengine katika msimbo wa maumbile yana kikomo. Na hili linaweza kuwa ni jambo jema!

  Da Mija - kwani kwenye picha hii unatuona tungapi? Sita, vitatu au kamoja? Kuna Kija, Minza na Sumayi. Ningekuwa Usukumani ng'ombe wangeniua!!!

  Dada Schola - nilipita Dutwa siku ya gulio na kulikuwa na watu wengi sana. Nyumbani!

  Tusongeni mbele!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU