NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, July 14, 2010

WANABLOGU MLIOKO TANZANIA - SASA NAWAHESHIMU ZAIDI!!!

Umeme ulipotukatikia ghafla. Ni "Internet Cafe" ya Benki ya Posta Mpya jijini Dar.
 • Nimemuona Dada Koero akilalamika kuhusu mtandao kuwa kimeo. Kwa sisi tunaobeba maboksi kwenye hizi nchi za wenyewe, tumezoea na pengine kuchukulia upatikanaji wa mtandao kasi kama jambo la kawaida tu.
 • Nilipokuwa Mwanza, Arusha na Dar es salaam hivi karibuni ndipo niliiona tofauti na jitihada ambazo inabidi tuzipige ili kuifanya huduma hii muhimu ya mtandao iwe ya kuridhisha. Juhudi zangu za kwenda katika migahawa ya mtandao zilikwama baada ya kugundua kwamba nilikuwa napoteza muda mwingi kusubiri kurasa zihuike badala ya kufanya kile kilichokuwa kimenipeleka huko. Mambo yalikuwa mabaya zaidi jijini Arusha.
 • Baadaye niliamua kununua "modemu" ya Sasatel ambayo watengenezaji wake walidai kwamba ilikuwa na uwezo wa kuniunganisha na mtandao kwa kutumia mikonga ya Voda, Zain, Zantel na Tigo. Kwa bahati mbaya sana laptop yangu iligoma kuipokea na kufanya kazi na modemu hii. Ndiyo maana niliamua tu kukaa kimya na kukiacha chakula kitamu na kichungu kidode!
 • Bado pia kuna tatizo la umeme. Picha hiyo juu ni mgahawa wa intaneti pale Posta Mpya jijini Dar es salaam. Na hapa ndiyo tu nilikuwa nimemaliza kulipia shilingi 2,000 kwa saa moja na ghafla umeme ukakatika. Tulijaribu kusubiri weeee lakini wapi; na ilipofika robo saa mimi nikaamua kuondoka. Dada anayefanya kazi pale ni mchungu na jeuri kweli kweli. Niliondoka pale na kumwacha angali akifoka na kulalama kwamba kukatika kwa umeme halikuwa kosa lake na alikuwa hana mpango wa kurudisha pesa za wateja. Kiendacho kwa mganga hakirudi ati!
   
 • Ni wazi kwamba baadhi ya wanablogu wenzetu walioko nyumbani wanablogu katika mazingira magumu na wanafanya jitihada za ziada kuhakikisha kwamba blogu zao zinasonga mbele. Kama Mwalimu, mimi huwa sipendi kusoma makala au ingizo katika blogu ambalo limeripuliwa tu huku limejaa makosa ya kiuandishi huku likiungwa mkono na mantiki na mtiririko ulioparaganyika. Kuanzia sasa sitakasirika tena kwani ni wazi kwamba inawezekana wanablogu hawa huwa wanaandika makala yao wakiwa katika mazingira haya ya mtandao wa kubahatisha. Baada ya kuona mtandao ule wenye kasi ya kobe kiasi kwamba "kupandisha" picha moja tu ya kawaida kunaweza kuchukua zaidi ya robo saa - wanablogu wenzetu mnastahili pongezi kwa uvumilivu na kujitolea kwenu kublogu.Msikate tamaa na tunatumaini kwamba baada ya huo mkonga wa Taifa kukamilika sawasawa pengine hali ya mtandao nchini itabadilika
  *********************
  Kuhusu Changamoto na Tija za Mikahawa ya Mtandao jijini Dar es salaam, jaribu kusoma hii Tasnifu ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Eindhoven nchini Uholanzi.

8 comments:

 1. Ni kweli inakatisha tamaa nilipokuwa nyumbani mwaka jana hata mie niliacha kublog. Nami nasema Wanablog mlio nyumbani HESHIMA KWENU!!

  ReplyDelete
 2. mmeona kwa nini makala zangu hawa ziko kiuwalu walu kidogo ehe!! maana ukishaandika unakimbia umeme usikatike au mtandao usikatike, achilia suala la u-slow nk

  tumezowea maisha ni mazuri huku

  ReplyDelete
 3. Ni kweli hali ni mbaya kulinganisha na nchi za wenzetu. Lakini, hata hivyo ni hatua ya kujivunia. Na ni lazima tujivunie ukobe kobe huu ambao unatuwezesha hata kujua dunia inaendeleaje.

  Kublogu ukiwa Bongo, inahitaji moyo wa kufa kufa hiviii!

  ReplyDelete
 4. Ahsante Mwalimu Matondo kwa kuleta hoja hii. Ni kweli wenzetu walioko nyumbani wanastahili pongezi kwa kuwa na moyo na hii kazi. Ukweli ni kwamba hakuna cha kujivunia kuhusu huyo kobe. Ni utendaji na uongozi mbaya wa wale tuliowapa kula. Iweje umeme ukatike kila mara? Suala la mtandao wa kasi liko poa karibu katika kila nchi tena bila kimeo chochote. Vipi taifa letu liwe na kobe mtandao badala ya sungura mjanja? Ni uchemkaji wa hao tuliowapa kula kwani kungekuwa na madhara ya kutowajibika basi mambo yangekuwa murua tu.. Hongera wablogishaji wa bongo.

  ReplyDelete
 5. Kama kuna tatizo sugu na lenye manyanyaso ni swala la umeme. Kwanza kuupata kwenyewe kama una kibanda chako ni suluba, kila aliyeupata ana hadithi ndefu ya kuelezea.
  Sasa umefika ndani, umelipia LUKU, bado haupatikani, ukija kwa mgawo, kuna migawo ya aina m bili.
  Mgawo wa kwanza ni ule mgawo rasmi, unatangazwa na watu wanajua, lakini kuna mgowo usio rasmi, katika baadhi ya maeneo, ukiulizwa unaambiwa transfoma ni ndogo, kwahiyo inabidi mpate kwa mgawo, huo hautangazwi na mnakatiwa bila maelezo, sasa achilia mbali hiyo migawo miwili. Kuna huko kukatikatika kwa umeme ambako hatuwezi kusema ni mgawo labda tuupe ina la hitlafu, au sijui tuuite jina gani...sijui, hii ndio Bongo, mkirudi mlioko majuu mje na majenerator!

  ReplyDelete
 6. ticha au mwalim nilirudi nyumbani kwa matatizo mwishowe nimeshindwa kurudi huko hapa nilipo nalaani kwa nini nilirudu kumbe huku nikwetu ila inafika mahali unajilaum kurudi kwenu kuna balaa huku we acha jana wame mpiga risasi prof.hatasijui kwanini wanua wasomi tich namie natafutie japo kazi ya kubeba boksi nije nianze upya ten maana sinamwerkeo tena najuta kurudu nyumbani kwetu nilikozalia hatari jamani naipenda inyo inyo hii nchi yangu

  ReplyDelete
 7. inatosha nicheke tu tehe! tehe! tehe! tehe!. bora mmeliona hilo na kuliweka wazi. umeme, u-slow, au u-hamna mtandao huwa vinatusimamisha ama kutochelewesha kwenda hewani.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU