NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, August 12, 2010

HATUA ZA KUOMBA NAFASI ZA MASOMO UGHAIBUNI - NA ERNEST MAKULILO

 • Nimegombana na kukosana na watu wengi kutokana na hili suala la nafasi za masomo. Watu wengi wanafikiri kwamba kwa kuwa mtu uko huku Marekani au Ulaya basi ni rahisi kuwatafutia nafasi za udhamini, kazi na masomo. 
 • Ukiwaambia kwamba hii ni jamii ya uwazi na kila kitu kinafanyika kwa kufuata taratibu zilizopangwa hawaelewi na wanakuona kwamba una roho mbaya na hutaki kuwasaidia. 
 •  Ambacho hawakielewi ni kwamba hata kama ungekuwa mkuu wa chuo, usingeweza kumsaidia nduguyo ambaye hajatimiza masharti ya uombaji wa nafasi ya masomo. Kwa mfano, mwaka jana katika Chuo Kikuu cha Florida, mkuu wa chuo cha udaktari alifukuzwa kazi baada ya kubainika kwamba alikuwa amemsaidia mwanafunzi mmoja kutoka familia ya kitajiri ambaye hakutimiza masharti sawasawa. Hapa hakuna cha shangazi wala mjomba na nafasi zote za udhamini na masomo zipo wazi mtandaoni. 
 • Hapa chini ni mahojiano ya mdau na mkereketwa wa masuala haya Ernest Makulilo aliyoyafanya na gazeti la Mwananchi la tarehe 10/8/2010. Ndugu Makulilo anagusia mambo ya msingi ambayo vijana wa Kitanzania wanaotafuta nafasi za masomo Ulaya na hasa Marekani inabidi wazingatie. Ukweli ni kwamba kuna nafasi nyingi za udhamini na masomo katika vyuo mbalimbali hapa Marekani. Blogu mbalimbali kama vile Makulilo, Wavuti, Naomba kazi na zinginezo zinajitahidi kuziweka wazi. Vijana wa Kitanzania amkeni kama wenzenu wa Kenya na kujaribu bila kuchoka kuomba nafasi hizi za udhamini. 
***********************
ALIHANGAIKA kutafuta nafasi za masomo ya elimu ya juu, hatimaye akaja kuipata nafasi hiyo nchini Marekani. Baada ya kufanikiwa, Ernest Makulilo, Mtanzania anayeishi na kusoma nchini Marekani ameamua kuwasaidia wengine jinsi ya kuomba nafasi za masomo ya juu katika nchi za Ulaya na Marekani ikiwa ni mchango wake kama anavyoeleza katika mahojiano haya na mwandishi wetu.

Swali: Sababu zipi zilikusukuma kuwasaidia wanaotafuta nafasi za masomo nje ya nchi?

Jibu: Kwanza naomba niseme kuwa  nilianza kuitoa huduma hii rasmi Julai mwaka 2007, na huu ni mwaka wangu wa  tatu. Sababu kubwa ya kuingia katika huduma hii ni kwa kuwa nilihangaika sana kutafuta nafasi za masomo  hadi kufanikiwa kuja hapa Marekani. Hivyo nikawa na taarifa nyingi za mtu unawezaje kupata nafasi hizi kwa  Marekani na Ulaya.

Sikuona kama ni jambo la busara  kwa kuwa mimi nimehangaika basi na wengine nao wahangaike, hivyo niliamua  kurahisisha njia ya watu wanaopenda kutaka kusoma zaidi kwa kupata udhamini ughaibuni.

Kitu kingine kilichonisukuma kujikita katika suala hili ni kuwa na blog (gazeti tando) mahsusi kwa ajili ya kuweka taarifa za misaada ya masomo kwa watu wa nchi maskini.

Niligundua kuwa blog nyingi zilizopo Tanzania zina vitu mchanganyiko, nikaonelea ni vema basi nianzishe kitu ambacho mtu akisema anataka nafasi za masomo basi ajue wapi pa kwenda na kupata msaada.

Swali: Ukoje mwamko  wa Watanzania katika kupata taarifa za vyuo ambazo wewe umekuwa ukizitangaza?

Jibu: Mwamko wa Watanzania ni mdogo sana tofauti na mataifa ya Afrika Magharibi, Amerika ya Kusini na Asia.  Watanzania wengi bado wana ile dhana na kasumba kuwa ili mtu aende Ulaya au Marekani kusoma ni lazima atoke katika familia tajiri au ya kisiasa. Hivyo wengi hukata tamaa mapema. Kitu kingine kinachosababisha mwitikio mdogo kutoka kwa Watanzania ni wengi wao kukosa ari   ya ushindani  kama ilivyo kwa Wakenya na watu wa nchi za Afrika Magharibi.

Ukiachilia hayo, wengi hudhani upatikanaji wa nafasi hizi ni kitu rahisi mno. Ninapompa mtu taratibu za vitu gani ajiandae navyo ili aweze kuwa mshindani mkubwa na kufanikiwa kupata nafasi, wengi hukata tamaa. Baadhi ya Watanzania  tunapenda vitu mteremko sana wakati uhalisia si huo tena. Dunia hii ni ya ushindani, inabidi Watanzania tubadilike, tuendane na ushindani uliopo katika dunia ya  kibepari. Tuachane na fikra za kijamaa)

Swali: Je wewe ni wakala wa vyuo  au unaiendesha vipi huduma hii?

Jibu: Mimi si wakala wa chuo au taasisi yoyote ile. Na hakuna mtu, chuo au taasisi yoyote ile inayonilipa kwa huduma hii. Naiendesha huduma hii kwa imani kwamba kuna watu wana ndoto kubwa za maisha yao, lakini ndoto hizo mara nyingi hufa kutokana na ufinyu au ugumu wa upatikanaji wa elimu ya juu Tanzania na katika nchi nyingi zinazoendelea. Hivyo ninachokifanya ni kuhakikisha watu hawa wanatimiza ndoto zao za kielimu na maisha yao kijumla.

Aidha nimekuwa nikizipitia  tovuti mbalimbali za vyuo na taasisi ambazo zinatoa udhamini wa elimu kwa watu wanaotoka nchi zinazoendelea. Nikishapata taarifa hizi, nazichuja kwa umakini na kuzihakiki kisha nazitangaza kwenye tovuti zangu ambazo ni   www.makulilo.blogspot.com pamoja na  www.scholarshipnetwork.ning.com. Kwa wale wenye maswali zaidi kuhusu taarifa fulani niliyoitangaza huniandikia barua pepe nami huwajibu kwa kutoa ufafanuzi husika.

Swali: Nani hasa walengwa wa huduma zako na kwa nini?

Jibu: Walengwa wakuu ni watu wenye nia na sifa ya kufanya shahada za Uzamili na Uzamivu, kwa Kiingereza Masters Degree na PhD. Kuna nafasi nyingi  za makundi haya mawili kuliko wale wanaotaka  kusoma shahada ya kwanza.

Kwa digrii ya kwanza,  inakuwa ngumu kupata udhamini kwa kuwa sababu nchi  zote ambazo lugha mama si Kiingereza, hutumia lugha zao kama Kijerumani, Kifaransa na nyinginezo kufundishia  katika daraja hili.

Hali hii huwa kikwazo kwa waombaji wengi kwa kuwa wanalazimika kujifunza lugha hizi na baada ya kufaulu mitihani ya lugha ndio upate nafasi. Nchi zinazotumia lugha zao za ndani ni kama Sweden, Denmark na  Ujerumani. Lakini kwa shahada ya pili na tatu, nchi hizi zimekuwa zikitumia pia Kiingereza

Swali: Kwa hiyo unawaeleza nini Watanzania kuhusu hali hii?

Jibu: Ninachowaambia  wasome shahada ya kwanza Tanzaniaa au katika  nchi nyingine za Afrika kisha shahada ya pili na tatu waende Ulaya, Marekani au nchi za mabara mengine.

Swali: Kuna watu wengi wanaotumia njia hii ya mitandao kutafuta na kuomba  nafasi za masomo  bila mafanikio, nini sababu?

Jibu: Kuna sababu nyingi zinazomfanya mtu akiomba asipate. Hili nitalifafanua kwa kirefu.Kwanza watu wafahamu kuwa kupata nafasi za masomo ughaibuni si jambo la bahati bali vigezo na kufuata taratibu husika. Kwa kukosa vigezo au kwa kushindwa kufuata masharti, wengi wamekuwa wakikimbilia kusema kuwa hawana bahati au kuna upendeleo.

Kwa mfano ili mtu aweze kupata udahili na kisha udhamini, vitu vifuatavyo ni muhimu:Mosi, matokeo bora ya vyuo, vyuo vingi vinataka wastani wa daraja la pili la juu yaani Upper Sercond kwa Kiingereza.Pili, mwombaji aandike malengo yake kwa  umakini na ufasaha kupitia kitu kiitwacho Statement of Purpose/Interest. Ukiandika kwa kulipua hata kama una matokeo mazuri, sahau kupata udhamini.

Tatu, kuna kitu kinaitwa  Writing Sample, hii ni kazi ambayo umeshawahi kuandika kama insha au utafiti wowote ule wakati unasoma. Lengo lake wanataka kujua uwezo wako wa kuandika mambo ya msingi. Nne,ni barua ya kukupendekeza kutoka kwa walimu wako au mahala unapofanyia kazi.Hawa nao wanapswa waiandike vizuri, waonyeshe uwezo wako wa taaluma na kazi.

Pia kuna zoezi la kupima uwezo wa lugha kwa muombaji. Uingereza wana mitihani ya TOEFL na IELTS, wakati Marekani wana mitihani kama GRE na GMAT. Waombaji wahakikishe vyeti vyao vimethibitishwa uhalali na wakili au mahakama kama si nakala halisi.

Baada ya hatua hii na ukishakuwa na vigezo, omba vyuo ila kumbuka vyuo unavyoomba viwe  vimeshatangaza udhamini wa masomo kwa wanafunzi  kutoka nje ya nchi husika. Lakini pia mwombaji asitosheke kuomba chuo kimoja. Anatakiwa kuomba vyuo zaidi ya ishirini ili kuwa na uhakika wa kupata udhamini mkubwa na ulio mzuri.

Swali: Unanufaika vipi   kama mtu binafsi kwa kuendesha huduma hii?

Jibu: Mafanikio makubwa ninayopata ni kuwa na furaha ya kweli kutoka moyoni. Ninafurahi sana watu wanapozipitia tovuti zangu,  kuzifanyia kazi na kisha kufanikiwa. Furaha hii ni zaidi ya pesa kwangu, maana mimi kujua mbinu hizi si kwa ujanja au werevu nilionao kwa wengine. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu kanipa maarifa haya, sina budi kuyafikisha kwa wengine wanaotafuta elimu au maisha.Moyo huu ndio ulionisukuma pia  kuanzisha mfuko wa kijamii utakaoitwa  Makulilo Foundation kwa lengo la kuongeza  wigo wa taarifa na mbinu zaidi za upatikanaji wa nafasi za masomo.

13 comments:

 1. Kaka, unaweza kurejea kuandika pointi zako katika 'bullets' mara mia na bado nitaendelea kukuomba uziandike tena na tena. Nasema hivi kwa kuwa nimekuwa nikiimba hadi nimeamua kabisa kuweka-saved draft email kwa ajili ya kuwajibu watu ambao kila kukicha, utapokea swali la kuomba msaada wa 'kutafutiwa' au 'kupatiwa' ufadhili wa masomo (scholarships). Nimeshaandika weee hadi nimejisemea, wacha tu wanichukie ni sawa na dua ya kuku, mwewe haimpati. Watakapokumbana na hali halisi, au wakakutana na watu wakawahadithia yayo hayo, pengine watapaka kufahamu na kuelewa.

  Nimefurahi sana kwa jinsi Makulilo alivyojibu kwa ufasaha habari hii. Amesema kinagaubaga, sifahamu mtu atataka maelezo gani zaidi ya haya aliyoyasema, hasa ukizingatia kuwa yeye ni mdau mkuu aliyevuka mito na mabonde katika kusaka nafasi hizi.

  Hii nimeihifadhi, pengine nitajaibandika tena mwakani kuierejea maana nina uhakika wanaotuma ujumbe hawakomi si leo wala kesho. Alimradi kila leo watu wanazaliwa, basi kila siku watakuwepo wanaohitaji kuelimishwa.

  ReplyDelete
 2. Matondo, heko kwa kulileta hili hadharani. Binafsi napenda kuwapongeza Subi na Makulilo kwa kazi hii nzuri. Mara nyingi sana marafiki za toka nyumbani wamekuwa wakisumbua kuwa niwafanyie mpango kuja kusoma hapa Finland, lakini nimekuwa nikiwapa majibu sawa kabisa na haya ya ndugu Makulilo. Huwa nawaeleza wazi kuwa huku haya masuala ya kubebana hayapo na hata pengine nawaambia kwa system ya hapa Finland unaweza hata ukawa na First class lakini usifanikiwe kupata admission, maana hapa Finland hakuna cha tuition fee, ukishafanikiwa admission basi wewe ni kupambana na living cost. Nimekuwa nikiwaeleza kuwa hawa Wafini wako makini sana na wanahitaji consistency jinsi unavyojieleza na pia wanazingatia sana suala la deadline, siyo hayo tu zaidi nimeweza kuwapa maelekezo ya namna ya kuandika barua za motivation lakini nilichugundua ni kwamba marafiki zangu hawakuwa makini katika haya na pengine wanadhania sikuwa na moyo wakuwasaidia kwa kile wanachoamini sikuweza kuwafanyia mchongo.

  Si jambo zuri kuzamia meli na kuja majuu kama wenzetu wa magharibi ya Afrika wanavyofanya pengine. Lakini niseme watanzania uoga umetuzidi, kulinganisha na wenzetu wa magharibi na hata jirani zetu wakenya. Nimeshakutana na waafrika ambao wanaishi hapa lakini hata sifa tu za kuja kusoma hapa hawana. Mwisho napenda kuwaasa ndugu zangu watanzania ambao wanayo nia ya kutaka kusoma hapa Finland, wawe huru kuwasiliana nami ili mradi tu wawe wamemaliza digrii ya kwanza kwenye vyuo vikuu vya nyumbani.

  ReplyDelete
 3. Duh!!
  Mie hawa si ndio walewale ninaoshindwa(ga) kuwashukuru
  Utasemaje ili juhudi na mambo yake yaonekane kuwa tofauti?
  Kinachonifurahisha (kwa mfumo wa kusikitika) ni kuwa analoweka nafasi hizi mahala kama kwa michuzi, watu wanam-crash
  Sijui tunapenda nini sisi?
  HONGERA KWA WALIOKULEA HIVYO MAKULIKO, Da Subi, Kaka Matondo na wengine wenye mioyo kama yenu

  ReplyDelete
 4. Kwa Michuzi watu hawana dogo na ndiyo utaona roho za Watanzania zilivyo mbaya. Mtu anajitahidi kweli kusaidia watu lakini jambo hili likaachwa na akaanza kushambuliwa yeye pamoja na mkewe. Mara ooh, kao mzungu kwa ajili ya makaratasi. Hii ina uhusiano gani na scholarships. Yaani we acha tu.

  Lakini huyu jamaa anafanya kazi nzuri sana. Angetupa data tuone ni Watanzania wangapi wamefanikiwa kupata scholarship kupitia blogu yake. Tunamwomba sana asikate tamaa...

  ReplyDelete
  Replies
  1. hivi kiwango chachini cha kuapply chuo ni form6 au hata form4 mwenye passmark nzuri?

   Delete
 5. nina certificate in business administration in account waweza kunisaidiaje?
  protazmagesa@gmail.com

  ReplyDelete
  Replies
  1. Soma kwanza digrii ya kwanza ndiyo itakuwa rahisi kidogo. Ni nadra sana kupata udhamini hawa wa nchi za nje kama huna digrii ya kwanza. Kila la heri na USIKATE TAMAA !!!

   Delete
  2. ni kweli lakin wapo wengi wanaosoma their firs degree uko abroad nahisi ni wasiwas wako tu

   Delete
 6. Ok... Shukran sana ndugu...
  Sasa Mimi nahitaj Fanya hvo na nlijaribu kuomba na nilipta majibu hivi karibuni...
  Vigezo nilikua navyo maana nilihitimu shahada ya kwanza ya computer engineering na sasa wamenipangia nikasome vitu vingine... Yaani nikasomee Rangeland Science.. CANADA....... Sasa hii inakuaje

  ReplyDelete
 7. Lakini kuna Scholarship zinatokaga specific for Undergraduate. Sasa mtasemaje ni nadra sana kupata udhamini wa kusoma degree ya kwanza nje ya nchi?

  ReplyDelete
 8. Lakini kuna Scholarship zinatokaga specific for Undergraduate. Sasa mtasemaje ni nadra sana kupata udhamini wa kusoma degree ya kwanza nje ya nchi?

  ReplyDelete
 9. Nimemaliza master of Arts in Tourism, Culture & Society. Ninahitaji sana kupata maelekezo ya kina juu ya upatikanaji wa scholarships za PhD huko nje ya nchi. Naomba msaada wako tafadhali, tuwasiliane kwa email jshenyagwa@fahariyetu.net

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU