NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 25, 2010

KUANZIA MWAKA HUU WA MASOMO NGUO ZA SHULE NI LAZIMA HAPA NINAPOISHI

 Mabinti: Kija, Minza na Sumayi
 • Baada ya kuchoshwa na mitepesho, wanafunzi kujitoboa masikio, pua, midomo, ndimi na sehemu nyinginezo; na mashindano ya fasheni mpya za nguo mashuleni, hatimaye Wilaya ya Alachua (hapa ninapoishi) imeamua kwamba kuanzia mwaka huu wa masomo ulioanza juzi, wanafunzi wote wa shule za umma ni lazima wavae sare za shule. 
 • Hapo juu mabinti ndiyo mara yao ya kwanza kuvaa nguo za shule na walikuwa wanashangaa kweli. Wao wanataka wavae nguo za akina Hanna Montana, iCarly na wenzi-rika wao wengine wanaowaona kwenye runinga. Wao wanataka nguo na viatu fasheni mpya mpya ili "wapendeze". Ilibidi kuwakalisha chini na kuwaelimisha umuhimu na faida za kuvaa nguo za shule. 
Sumayi: shule ya vidudu
 • Niliwaambia kwamba, nguo za shule kwanza zinapendeza - hoja ambayo waliikataa katakata. Pili, zinatupunguzia mzigo sisi wazazi wa kununua nguo za shule mara kwa mara kulingana na fasheni mpya zinazovaliwa na marafiki zao shuleni. Niliwaambia kwamba tulikuwa tunapoteza pesa nyingi sana (hoja hii waliikubali) Tatu, nguo za shule zinasaidia kuondoa tofauti ya matabaka kwani kwa sasa watoto wa masikini wasio na uwezo wa kununua nguo za akina Hanna Montana na watoto wa matajiri watakuwa wanavaa nguo za aina moja. Kwa hivyo hakuna kuchekana (hoja ilikubaliwa). Nne, nguo za shule pia zinawatambulisha kuwa wao ni wanafunzi na kuwa mwanafunzi ni jambo la kujivunia (hoja ilikubaliwa nusunusu).
Minza - darasa la kwanza
 • Tano niliwaomba wanipe maoni yao kuhusu suala la wanafunzi wenzao wanaotoboa pua na midomo. Walisema kwamba hawapendi na walikuwa wanashangaa sana wanapoona mwanafunzi amejitoboa. Niliwaambia kwamba sasa kujitoboa kumepigwa mafuruku na kuvaa mikufu na mazagazaga mengine kumepigwa marufuku. Kuvaa nguzo zinazolegea (mitepesho) pia kumepigwa marufuku. Hata viatu vyenye magurudumu na mapambo nje navyo haviruhusiwi. Walipenda na kufurahishwa sana na mabadiliko haya mapya na maoni yao mwishowe yalikuwa ni ya kuunga mkono.
 Minza na Sumayi
 • Mpaka mwisho wa mkutano wetu naona nilikuwa nimeshinda na kila mtu alikuwa na furaha. Nyumbani mimi hata sikuwahi kujiuliza ni kwa nini tulikuwa tunavaa nguo za shule. Pamoja na kwamba kulikuwa na upinzani mkali kuhusu sera hii mpya (wazazi wakereketwa walikuwa wanadai kwamba uhuru wao unaminywa), nimefurahi kwamba hatimaye imepitishwa kwani ina faida nyingi kama ambavyo nimegusia hapo juu.

7 comments:

 1. Yaani nimefurahi kweli na natamani kama ningeishi huko na wanangu wangeenda shule huyo maana duh" kaazi kwelikweli. Kwani sasa inakuwa kama mashindano maana kila mtoto anavaa anavtotaka, anafanya mitindo ya nywele, kujipamba ndo usisema kwa upande wangu nawaza nikasema sioni kama ni nidhamu lakini wanasema ukienda sehemu ukikuta watu wanatembea uchi nawe tembe.

  Shangazi zangu wamependeza kwelikweli na nawatakia masoma mema na pia kuwa wasikivu kwa wazazi/walezi pia walimu. Mbarikiwe sana.

  ReplyDelete
 2. Matondo, binti zetu wanapendeza kweli, sijui nijilaumu ni kwanini nilichelewa kuoa, hahaahaa. Maana pale kwangu ipo timu ya midume mitatu ambapo kwa mtizamo wangu wanaweza kuwa wamefeli huu mtihani kwa kigezo cha umri mdogo. Vingine tungeanza kujadili biashara ya mahari kuanzia sasa.

  Ama kweli wewe mwalimu wa kweli, mpaka umeweza kuwashawishi wazungu kukubali matumizi ya unifomu! hapa kwetu hilo hilitakubalika kamwe.

  Hata hivyo siwezi kuwalaumu pia kwa sababu hii ni jamii ya watu ambayo kila kitu kipo kwenye hali ya usawa. Ukiangalia kwa jirani nyumba ndiyo hizo hizo, gari ndiyo hizo hizo yaani hakuna hata jambo ambalo mtu anaweza kujionea yeye ni kidume kiuwezo. Binafsi ninaufurahia mfumo wa maisha ya Wafini.

  Dhana halisi ya wanafunzi kuvaa unifomu zaidi ya kupendeza ni kuondoa matabaka kati ya wanafunzi waliotoka kwenye famila tajiri na wale waliotoka katika familia masikini.

  Katika nchi masikini endapo sheria zitaruhusu uvaaji holela kwa wanafunzi, nadhani wanafunzi watokao kwenye familia duni watavunjika moyo kwa kiasi kikubwa kwa wao kutoweza kushindana kimavazi na wenzao waliotoka kwenye familia tajiri.

  Jambo ambalo linaweza kuleta madhara makubwa ya kisaikolojia kwa wanafunzi waliotoka kwenye tabaka la familia masikini, hili kwa uhakika laweza kuathiri uwezo wao wa kujifunza.

  ReplyDelete
 3. naaam wakati wote hizi ndizo sababu za kuvaa uniform shuleni hasa hii: "nguo za shule zinasaidia kuondoa tofauti ya matabaka"

  ReplyDelete
 4. Mmmmh! kazi ipo,huku kwetu ni tofauti kabisa wanafunzi nilazima kuvaa sare za shule,ila hutokea mara moja kwa term ndio huwa wanasiku maalum ya kuvaa nguo wanazotaka.

  Kaka hongera maana kinashangazi umefafa nao sana wote! maskini wifi yangu hakuambulia hata mmoja labda kidogo rangi,lakini kwa sura huulizi,wasalimie sana sana kina shangazi.

  ReplyDelete
 5. Tunaomba basi umuweke na wifi japo tumpongeze kwa kuwa na mabinti wazuri hivi.

  ReplyDelete
 6. Nilitaka kusema wifi hakuna??? Kama hakuna sema tuje tukusaidie kulea hapo mabinti...Inaonekana wamelelewa vyema and they are very happy.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU