NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 18, 2010

NILICHOJIFUNZA BAADA YA KUFUNDISHA HESABU WATOTO WA DARASA LA TATU HAPA MAREKANI

Picha hii inapatikana hapa.
 • Kama ambavyo niliwahi kudokeza katika maoni hapa, mwaka uliopita wa masomo (Agosti 2009 – Juni 2010) nilikuwa ninajitolea kufundisha hesabu wanafunzi 19 wa darasa la tatu hapa Marekani kwa masaa mawili kila wiki. Shule niliyokuwa nafundisha ni shule nzuri yenye wastani wa daraja la A (hapa shule hupewa alama A-F kulingana na mafanikio ya wanafunzi katika mitihani mbalimbali ya kijimbo, na vigezo vingine).
 • Lengo langu hasa la kujitolea kwangu, mbali na mwenyewe kujifunza na kujipatia ridhiko la kisaikolojia, lilikuwa hasa ni kujua mbinu zinazotumiwa na wenzetu katika kufundisha watoto wao hesabu na masomo mengine ya sayansi, masomo ambayo kule nyumbani yanaogopwa sana na wanafunzi na yamekuwa yakididimia mwaka hadi mwaka. Nilichagua hesabu kwa sababu ndiyo somo mama na lisiloepukika karibu katika kila nyanja hapa duniani (bofya hapa).
Kwa kifupi, mambo makuu niliyojifunza ni haya:
 • Hesabu hazifundishwi kavu kavu kama hesabu bali zimeingizwa na kuoanishwa na michezo ya namba katika kompyuta, vitabu mbalimbali, michezo ya watoto na hata nyimbo wanazoimba, ikiwemo kutunza na kuhesabu akiba zao za pesa (kila mtoto hutakiwa kujiwekea akiba katika kikopo na kuweka rekodi daftarini). Kwa hivyo watoto wanajifunza dhana za msingi kama kujumlisha, kutoa, kuzidisha na hata kugawanya kwa urahisi zaidi. Kati ya wanafunzi 19, ni wanafunzi wawili tu ambao walikuwa wakilalamika kwamba walikuwa hawapendi hesabu.
 • Badala ya kuzifanya hesabu kuwa somo kavu na lenye kuogopwa sana, kumbe inawezekana kulifanya liwe la kuvutia na hata kusisimua. Tofauti ni kwamba walimu hawa wana karibu kila kitu wanachohitaji na huwezi kuwalinganisha na walimu wetu ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu sana.
 • Kuna utaratibu mzuri sana wa tuzo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri karibu katika kila kitu darasani – kuanzia yule anayefanya mazoezi yake yote kwa wakati unaopangwa, kusaidia wenzake darasani, kujibu maswali kwa usahihi (na kwa haraka), kufanya miradi mizuri na mambo mengineyo. Tuzo hizi huwasisimua sana wanafunzi kwani wazazi pia hushirikishwa.
 • Wazazi ni sehemu muhimu ya elimu ya watoto wao. Wazazi hupewa barua na kuombwa kuwasaidia watoto wao katika kufanya kazi za nyumbani kwa kuhakikisha kwamba wanafahamu dhana inayolengwa katika kila zoezi la nyumbani. Hapa mtoto hawezi kufanya vizuri shuleni bila msaada wa wazazi. Kwa hakika kuna jambo la kujifunza hapa hasa kwa wazazi wetu ambao wamewahi kulalamikiwa kwa kutojihusisha kwao sana na elimu za watoto wao.
 • Wazazi pia huchochewa kuhudhuria baadhi ya shughuli za watoto wao shuleni kama michezo ya kuigiza na wakati wa uwasilishaji wa miradi yao ya sayansi na hesabu. Wazazi huja na maua na zawadi mbalimbali kwa watoto wao, picha hupigwa, video huchukuliwa kwa ajili ya kumbukumbu na wanafunzi hupongezwa na kuhongereshwa.  
 • Kuhusu sayansi, watoto huanza kufanya majaribio ya msingi tangu wakiwa bado watoto. Isitoshe sayansi, kama vile hesabu, haifundishwi kavu kavu kama tulivyofundishwa sisi. Wanafunzi wa darasa la tatu kwa mfano huanza kusoma vitabu vifupi juu ya historia fupi juu ya wanasayansi mbalimbali  - walizaliwa wapi na lini, utoto wao ulikuwaje, waligundua nini na kwa nini ugunduzi wao ni muhimu leo. Vitabu hivi huwasisimua sana wanafunzi na si ajabu kukuta wengine wakisema kwamba wanataka kuwa kama Isack Newton watakapokua, wapo wanaoapa kwamba ni lazima watagundua dawa ya kansa n.k. Sayansi, kama vile hesabu, inaweza kuwa somo la kusisimua sana kama ikifundishwa vizuri. Siyo ule mtindo wetu kule nyumbani ambapo tunakariri tu hata bila kuelewa tunakariri nini.
  • Wanafunzi hawa pia, hawana vipingamizi vya lugha kama ilivyo kwetu ambapo kusema kweli tunafundishwa katika lugha ambayo hatuielewi na dhana dhahnia kama vile gravity, atomic weight n.k. inakuwa vigumu sana kuzielewa. Walimu wetu pia nao, pengine kulingana na mazingira duni wanamofanyia kazi pamoja na maslahi yasiyoridhisha kusema kweli hawana muda wa kujaribu vitu vipya darasani mbali na mwongozo wa wizara husika unavyosema. Nilishangaa sana, kwa mfano, binti yangu wa miaka tisa, aliponieleza kwa usahihi kabisa jinsi mzunguko wa maji (water cycle) unavyofanya kazi na kwa nini sayari kama Mars hazina mvua! 
  • Ngoja leo niishie hapa. Mwaka huu nimejitolea kufundisha sayansi darasa la nne (masaa mawili kwa wiki) na lengo langu ni lile lile – kusaidia na hasa kujifunza zaidi mbinu wanazozitumia katika ufundishaji wao. Lengo langu ni kuandika kitabu chenye kutoa maoni na mwongozo binafsi wa ufundishaji wa hesabu na sayansi katika madarasa ya mwanzo katika shule zetu za msingi kule nyumbani!
  Hapa chini ni baadhi ya maswali ya mtihani na mazoezi ya nyumbani kwa wanafunzi wa darasa la tatu. Kwa mtu wa isimu (ngwini) kama mimi, baadhi yake yalikuwa “vigongo”  na ilinibidi nigangamare kweli ili kuyakokotoa!

  ********************** 
   (1) Pam gave her friend Tammy the numbe riddle below. Solve it.

   I am a 2-digit number less than 84. The sum of my digits is 9. The ones digit is twice the tens digit. What number am I?

   (2) Bill was staring across the street where bicycles and tricycles were stored. He counted a total of 13 wheels. How many bicycles and tricycles were in the lot?

   (3) The library at Miller Elementary School has an odd number of tables. Some tables will seat 4 students and some tables that will seat 6 students. A total of 32 students can sit at the tables with no empty seats. What is the number of tables of each type?

   (4) Amanda eats supper from 6:30 to 7:00. Then she watches a half-hour television program. She takes 5 minutes to brush her teeth, 15 minutes to take a bath, and 5 minutes to dress for bed. How much time is left for Amanda to read if she goes to sleep at 8:30?

   (5) A magician weighed his twin rabbits and identical hats together and got 18 pounds. He then weighed one hat and got 3 pounds. What was the weight of one rabbit?

   (6) A turtle crawls up a 12 foot hill after a heavy rainstorm. The turtle crawls 4 feet, but when it stops to rest, it slides back 1.5 feet. How many tries does the turtle make before it makes it up the hill?

   Tuendelee kujifunza na kwa anayetaka maswali zaidi ya hawa watoto wa darasa la tatu aseme….

   1 comment:

   1. Sijui kama watu wa Ikulu wanasoma hizi blogs. Lakini ningekuwa na madaraka yo yote makubwa serikalini ningekuita na kukupa kazi pale wizara ya elimu kitengo cha mitaala na utamaduni ili mawazo yako haya yaweze kufanyiwa kazi mara moja.

    Tanzania tunao watu wazuri sana nje na hatufanyi juhudi yo yote kuwarudisha nyumbani. Sekta ya elimu ndiyo primary na mawazo kama haya mnayojifunza huko nje yangetusaidia sana. Please honorable Kikwete, bring this guy home....

    ReplyDelete

   JIANDIKISHE HAPA

   Enter your email address:

   Delivered by FeedBurner

   VITAMBULISHO VYETU