NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, September 24, 2010

FIKRA YA IJUMAA: NAMFAGILIA MZEE ANTHONY MATONYA !!!

 • Watu wengine hupenda kusifia watu mashuhuri – wanasiasa wenye majina, madikteta wa kutisha, wanafasihi waliobobea, mashujaa wa kupigiwa mfano, wafalme waliotukuka, wanautambuzi makini, vigogo wa ufisadi, wastareheshaji makini, makamanda wa vita wasioshindika, waanzilishi wa fikra mpya, wanaharakati waliokaramka, wanazuoni washika kurunzi, matajiri wa kutupwa, warembo kupindukia na wengineo wa aina hiyo.
 • Mimi leo nataka kumtukuza Mzee Anthony Matonya – ombaomba mashuhuri nchini Tanzania. Mzee huyu kipofu anajulikana kwa staili yake ya kuomba kwa kulala chali kando ya barabara na kuinua kopo lake juu – bila kujali ukali wa jua la Dar es salaam.
 • Serikali imeshajaribu sana kumwondoa mjini pamoja na ombaomba wengine (ikidai kwamba eti wanatia aibu na kuchafua mazingira), lakini baada ya muda mfupi, mzee huyu kipofu huchomoza tena jijini Dar es salaam tena kwa staili yake ile ile.
 • Ati, ni azma gani na kutokata tamaa kupi kunakozidi huku kwa Mzee Matonya? Ni bidii gani ya kazi inayozidi hii ya Mzee Matonya ya kulala chali siku nzima katika jua kali la Dar es salaam huku ukibezwa na kughasiwa? 
 Hapa akiwa Morogoro. Picha ni kutoka Dullonetwork.
 • Kwa hakika tuna mengi ya kujifunza kuhusu uchapakazi, uvumilivu na kutokata tamaa kutoka kwa mzee huyu kipofu ombaomba. Na hii kwa kifupi ndiyo fikra ya Ijumaa ya wiki hii. Wikiendi njema na mbakie salama!

7 comments:

 1. wanautambuzi makini!! nadhani uliyem-link hapa ni mwanafunzi wa utambuzi! ila duhu! si hata rais wetu anaomba kwa ajili ya taifa?? iweje matonya aaibishe??

  ReplyDelete
 2. Kamala umenichekesha!

  Lakini labda ni kweli inabidi Matonya ampe kozi Rais wetu ilikuimpruvu staili ya Rais ya kuomba akiwa katika ziara za kuombaomba Duniani.:-(

  ReplyDelete
 3. Kweli Simon, kama Matonya alifukuzwa kwa kuomba mjini, je sisi Waafrika ambao tuna-omba-omba kwa matajiri tutafukuziwa wapi?
  Au ni style, au ni unadhifu, au ni....

  ReplyDelete
 4. Matonya ametengenezwa na kina Kikwete hata akiomba na kupewa humfikishia mkewe na vitegemezi. Si kama hawa ombaomba wenye suti wanaoficha ulaya kama huyo msukuma mwenzako Chenge. Ni unafiki na ukatili kwa ombaomba kumfukuza ombaomba. Niliwahi kuuliza ni omba omba yupi ana haki ya kumfukuza mwenzake pale Yusuf Makamba wakati ule mkuu wa mkoa wa Dar alipoamuru Matonya mwenyenzi afukuzwe. Makamba aliniita mchochezi. Ila ukweli ni kwamba Matonya ni ombaomba mkweli na mstaarabu kuliko hao wezi wa EPA Kagoda na Richmonduli.

  ReplyDelete
 5. @ Simon Kitururu

  "Lakini labda ni kweli inabidi Matonya ampe kozi Rais wetu ilikuimpruvu staili ya Rais ya kuomba akiwa katika ziara za kuombaomba Duniani.:-("

  Yaani mnataka rais wetu naye awe anakwenda na kopo na kulala chali anapoenda kuombaomba huko nje. Nyie watu mnachekesha kweli. Yaani nimecheka mpaka mbavu zimeniuma. Wanablogu nyie mna mambo si mchezo...

  ReplyDelete
 6. Ukweli ni kwamba hakuna usawa - hata miongoni mwa ombaomba!!!

  ReplyDelete
 7. Msome Mchambuzi Ndimara Tegambwage hapa kuhusu ombaomba wetu nambari wani:

  http://ndimara.blogspot.com/2010/10/ombaomba-ya-kikwete-inanufaisha-nani.html

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU