NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, September 3, 2010

FIKRA YA IJUMAA: KIZUNGUMKUTI CHA "WASOMI" NA Ph.D ZAO!!!

UCLA - 2004 (Baada ya kuhenya kwa miaka 6)
 • Kwa walio wengi Shahada ya Uzamivu (Ph.D) huashiria kilele cha mafanikio na ukomo wa safari yao ya kusaka elimu na maarifa darasani. Ni shahada inayoheshimika sana duniani kote kiasi kwamba watu wengi hufikia hatua ya kukata njia za mkato ili kuipata. Watu hawa huona fahari kubwa kuitwa madaktari wa falsafa hata kama udaktari huu ni wa bure na hawakuusomea wala kuufanyia kazi!

 • Shahada hii hata hivyo inatatanisha kutokana hasa na mfumo mzima wa elimu ambao umekaa kipiramidi. Katika shahada ya kwanza mtu unafundishwa mambo mengi kwa ujumla. Lengo hapa ni kupata maarifa ya juu juu tu juu ya mada mbalimbali katika masomo kadhaa unayosomea. Katika shahada ya uzamili (Masters), piramidi inaanza kufanya kazi yake na mtu unaanza sasa kujibana katika kaeneo kadogo tu katika taaluma yako. Halafu inakuja hii shahada ya uzamivu. Hapa mtu unachagua kaeneo kadogo zaidi na kukafanyia utafiti wa kina mpaka utoe mchango fulani mpya katika kaeneo hako. Tena ni lazima usimamiwe na magwiji katika kaeneo hako unakokashughulikia na wakiridhika kwamba kweli utafiti wako umetoa mchango fulani mpya basi Ph.D unaipata Ng'wanawane.
 • Kuna "wasomi" ambao mara wakiipata hii Ph.D basi wanajiona kuwa wamefika na kujifanya kwamba wanajua kila kitu. Ukweli hata hivyo ni kwamba Ph.D inapaswa kuonwa kama mwanzo tu wa safari ndefu ya kusaka maarifa ya kina - safari ambayo kusema kweli haina mwisho. Kwa mantiki hii hata wenye hizo Ph.D bado ni wanafunzi hata katika vile vieneo vyao vidogo walivyovisomea. Na kuwa na Ph.D siyo kuelimika!
 • Mimi ni mmoja wa wale wanaoamini kwamba haiwezekani kuwa na ujuzi timilifu na sisi binadamu ni wanafunzi wa kudumu hapa duniani. Kwa hivyo badala ya kukakawana na hiyo Ph.D na kujifungia katika kaeneo hako kadogo ambako mtu umesomea,bado ni lazima kuendelea kujisomea kwa bidii na kujifunza maarifa ya jumla katika taaluma zingine. Mimi kwa mfano ni mpenzi sana wa vitabu vya falsafa na fasihi ya Kilimwengu na huvutiwa sana na maandishi ya wanafalsafa na waandishi mbalimbali mashuhuri kama George Orwel, Pablo Neruda na wengineo. Maandishi haya ni yenye kufikirisha sana na kusema kweli yanapanua mawazo na hata uwezo wa kujenga hoja.
 • Kwa sasa nimeanza kusoma vitabu juu ya wanasayansi mbalimbali, maisha yao na vitu vilivyowafanya mpaka wakafanya ugunduzi muhimu wa Kisayansi. Nimeshangaa kugundua kwamba mara nyingi ugunduzi muhimu ni mkusanyiko wa mawazo ya watu wengi katika wakati maalumu na wanasayansi wengi walichofanya ni kuyachukua mawazo yale na kuyafanyia majaribio ili kuyathibitisha kisayansi na hatimaye kuyapanga vizuri, kuyaundia fomyula na kisha kuyachapisha. Ugunduzi wa bomu la Nyuklia hapa Marekani, kwa mfano, ulikuwa ni juhudi za wanasayansi wengi ambao walikusanya mawazo yao pamoja mpaka wakafanikiwa. Ni wanasayansi wachache sana (Albert Einstein ni mmoja wao) ambao walianzisha matapo mapya kabisa ya kinadharia bila kutegemea mawazo ya watu wengine kwa kiasi kikubwa.
 • Tuendelee kusaka maarifa kwa kujisomea kwa bidii na tukumbuke kwamba hata hawa wenye Ph.D, hawajui kila kitu na tuwe huru kuhojiana nao bila woga wala kujidogosha. Maarifa hayana mwenyewe wala ukomo na msomi wa kweli ni yule anayeheshimu na kuitambua kanuni hii. Na kusema kweli, HATUHITAJI KUWA NA Ph.D KUWA WASOMI!!! Wikiendi njema.

2 comments:

 1. labda ni kweli, hatahitaji pure head damages (PHDs) ila tunahitaji watu wanaoyaishi mawazo yale wanayoyaamini zaidi. na mwenye PHD ni yule anayejuza kidogo tu

  maarifa yapo kwa wingi japo sio lazima kuyasomea bali kuayishi

  naweza sema, tunahitaji MEDITATORS wengi zaidi ya PHDs, amini usiamini

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU