NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, September 19, 2010

KIBAKA AKIONA CHA MOTO, ABANIKWA KAMA NDAFU!

 • Hiki ni kichwa cha habari kuelezea tukio lililotokea Septemba 15, 2010 kule Singida ambapo kibaka mmoja aliuawa na wananchi wenye hasira na kisha kuchomwa moto. 
 • Ni kweli kwamba wananchi wameshachoshwa na vibaka lakini (kama nilivyowahi kusema hapa) siungi mkono unyama huu unaotokea katika jamii yetu inayojidai kuwa ya kidemokrasia na yenye amani, usawa, upendo huku ikiwa na vyombo vya dola vinavyopaswa kusimamia usalama wa raia na mali zao. 
 • Polisi na mahakama vina kazi gani basi kama watu wanajichukulia maamuzi wenyewe kiasi cha kutoa maisha ya watuhumiwa kwa ukatili namna hii?
 • Mimi pia siwapendi vibaka kwani walishawahi kunikwapulia laptop yangu mpya kabisa pale Kariakoo lakini kamwe sipendi unyama huu. Hali hii inasikitisha na kama jamii inabidi tufike mahali tutafute suluhisho mwafaka kwa tatizo hili. Vibaka hawa ni zao la mfumo mbovu wa elimu, matabaka na umasikini uliokithiri katika jamii yetu.
 • Kupambana na umasikini na kujitahidi kuboresha maisha ya Watanzania wote, kutokomeza ufisadi na rushwa, kupunguza matabaka na kuboresha mfumo wetu wa elimu ni baadhi ya hatua za msingi tunazobidi kuzichukua kama kweli tunataka kupunguza hii chuki ya ajabu inayotufanya tuwaue vijana wetu kwa makosa ya kukwapua simu, heleni, saa na vitu vingine vidogo vidogo. 
 • Pengine nimalizie kwa kuuliza swali lililowahi kugusiwa na Euphrase Kezilahabi katika diwani yake ya Karibu Ndani: Tukichomana moto sisi kwa sisi, safari ni lazima iendelee???
 • Kwa habari kamili kuhusu tukio hili tembelea blogu ya Full Shangwe.

9 comments:

 1. Sasa kweli dunia imekwisha kweli kumbanika binadamu mwenzako kama kitimoto hivyo??

  ReplyDelete
 2. Sasa imekuwa kama tamaduni vile,majuzi wazee walibanikwa wazi wazi kwenye moto nchini Kenya. Hili la ubanikaji wa vibaka si tu kwamba inatokea kwetu Tanzania bali pia nchi zenye majina makubwa kama Nigeria mwendo ni huu huu.

  Mimi bado nitawalaumi wanasiasa kwa kutojali kuondoa umasikini uliokithiri wa wananchi wao. Nimesoma kwenye gazeti wabunge wakisubiri milioni 400 kama pension ya miaka mitano, hapa kweli tutaendelea kuwalaumu vibaka? au hata kuwapa adhabu wasizostahili? ni jambo la kusikitisha kwa kweli.

  ReplyDelete
 3. HIZI NI DALILI ZA MWISHO WA DUNIA, SI RAHISI KUMFANYIA HIVYO BINADAMU MWENZAKO HATA KAMA NI MWIZI.

  ReplyDelete
 4. Hivi kuna mtu anayewajibishwa kwa vitendo kama hivi? Lawrence Masha anasemaje kuhusu unyama huu? Polisi wako wapi? This has to stop. The vigogoz steal all the big money and leave the poor bila kitu mpaka wanabakia kuchomana moto. Mpaka lini??? Fikiria huyu angekuwa ndugu yako - potelea mbali hata kama ni kibaka - ungefikiria nini??? Sitaki tena kusikia eti Tanzania ni nchi ya amani. No, it is not!!!

  ReplyDelete
 5. Watanzania wanashangaza. Ukiwa fisadi, hawana tatizo na wewe, kama nilivyowahi kudokeza. Bofya hapa.

  Hao ndio wa-Tanzania walivyo. Hata serikali yao inawajua vizuri. Inaweza kuwaambia mafisadi warudishe mabilioni waliyoiba, na mambo yakaisha kimya kimya.

  Lakini kibaka hana mwanya huo. Akithubutu kukwapua kioo cha gari la fisadi, wananchi, hata kama wana njaa kiasi gani, watamfukuza kibaka huyo hadi wamkamate na kumchoma moto. Hao ndio wa-Tanzania, walivyo tayari kufa katika kutetea maslahi ya fisadi.

  Sisi tulipokuwa wadogo, wazee walihakikisha kuwa hatuoni maiti. Ilikuwa ni mwiko. Siku hizi, kuua vibaka ni aina ya burudani humo mitaani. Wote wanahudhuria, kuanzia wazee hadi watoto wadogo. Ni "muvi" ya kusisimua. Ndipo tulipo kama Taifa, kwenye suala la maadili.

  Kwa maana hii, ingawa leo wengine tunashtuka kwa ukatili unaofanyika, tukae tukijua kuwa hali itakuwa mbaya zaidi miaka ijayo. Kutokana na malezi wanayopata watoto humo mitaani, Taifa la kesho litakuwa ni Taifa la hayawani wakubwa, na hawatajitambua kama ni hayawani. Watakuwa si binadamu wa kawaida.

  ReplyDelete
 6. Yasinta na Najua Wajua: kweli ni jambo la huzuni kabisa. Utafikiri wameandaa kitoweo!

  Matiya: Tatizo hili lipo hasa katika nchi zenye umasikini na elimu legelege kwa raia zake. Kwingineko linakemewa sana na wahusika hupata adhabu kali.

  Hizo 40,000,000 wanazogawana waheshimiwa bila shaka ni za kwenda kuwasaidia katika kampeni kwa wanaoogombea. Kwa waliochakachuliwa basi ni mshiko tu wa bure. Kazi gani nyingine itakupa marupurupu kama haya? Ndiyo sababu kila mtu anataka kuingia mjengoni Chimwaga kwenda kufaidi maziwa na asali.

  Anonymous @ September 19, 2010 9:31 PM: Sijui kama wananchi hawa wenye hasira huwa wanachukuliwa hatua zo zote. Pengine wahusika wana data kamili kuhusu suala hili. Kwa vile wanaochomana moto ni walala hoi kwa walala hoi, sitashangaa kusikia kwamba hakuna anayejali. Siku ikitokea fisadi akachomwa moto ndiyo utaona. Vijana wa kazi kila kona na mkong'oto wa nguvu kwa "wavunja amani"

  Prof. Mbele: Hata sisi ilikuwa marufuku kwa watoto kuona maiti. Nakumbuka mwaka 1981 nilipokuwa darasa la 4 maiti za Wamasai wezi wa ng'ombe zilikuja zikatupwa karibu na shule yetu ya msingi. Japo tulikuwa wadadisi na tulikimbia kwenda kuangalia, haraka haraka viboko vilitembea na shule nzima ilifungwa kwa siku hiyo na watoto wote tukatakiwa kurudi nyumbani. Hii ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kuona maiti na ni taswira ambayo ilinihangaisha kwa muda mrefu kwani wezi wale walikuwa wamepigwa na kuharibiwa vibaya. Baadaye wanakijiji walileta magunia na kuwahifadhi maiti wale mpaka polisi walipokuja.

  Lakini hapa unaweza kuona watoto wadogo wakiangalia maiti bila wasiwasi - tena iliyobanikwa! Sijui tunajenga jamii ya aina gani.

  Halafu jambo jingine linaloshangaza katika picha hii na zinginezo nilizoziona ni ule ukosefu wa ubinadamu. Katika jamii "zilizostaarabika" binadamu anaheshimiwa awe hai au amekufa na jambo la kwanza utaona kwamba maiti hufunikwa. Lakini hapa naona hakuna anayejali kuifunika na kuihifadhi maiti hii. Akina mama wanaangalia tu bila wasiwasi wakiwa na kanga zao. Inashangaza sana!!!

  ReplyDelete
 7. Kama wanafikiri ni ndafu, si wagawane basi kila mmoja apate kitoweo. Umasikini umekithiri na sitashangaa kama huyu kibaka aligawanwa watu wakaenda kupika ugali wao na kufaidi.

  Bongo kweli tambarare!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU