NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, September 29, 2010

MBUNGE WANGU (MZEE WA VIJISENTI) MAMBO "POA": MAHAKAMA YAFUTA HATI YA KUMKAMATA.


Mahakama yafuta hati ya kumkamata Chenge
29 Sep 2010, 7:08 am
Ummy Muya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Kinondoni imefuta hati yake ya kuruhusu kukamatwa kwa mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge iliyotolewa juzi kutokana na mshtakiwa huyo kushindwa kutokea mahakamani.

Hakimu Sundi Fimbo alitoa hati hiyo juzi wakati Chenge, ambaye anatetea kiti chake cha ubunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki akiwa kwenye mkutano wa kampeni ambako alipigiwa debe na mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa yuko mikoa ya Kanda ya Ziwa.
   
Lakini mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, David Mwafwimbo aliiambia Mwananchi jana kuwa mdhamini wa Chenge aliibuka juzi akiwa amechelewa na akamuomba hakimu afute hati hiyo na ombi lake likakubaliwa.

"Mdhamini wake anayeitwa Masanja alimrudisha Hakimu Fimbo mahakamani ili kuomba kufutwa kwa kibali cha kumkamata mshtakiwa... ingawa mdhamini huyo alifika mahakamani hapo akiwa amechelewa, alienda kumuomba hakimu afute  hati hiyo na akakubaliwa" alisema Mwafwimbo.

Mwafwimbo alisema baada ya mdhamini huyo kufika, hakimu aliitisha tena jalada hilo na kuifuta amri hiyo ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.

Chenge alitakiwa kuanza kujitetea jana katika kesi inayomkabili ya kuendesha gari kizembe na kufanya makosa mawili ya kusababisha vifo vya watu wawili na jingine la kuendesha gari bila bima halali.

Chenge anadaiwa kugonga pikipiki ya maguruduma matatu, maarufu kama Bajaj iliyowabeba wasichana wawili na kusababisha vifo vyao ambavyo kisheria huchukuliwa kama makosa mawili tofauti.

Kutokuwepo kwake kulimfanya Hakimu Fimbo kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5. Lakini Zulfa Mfinanga na Herman Meza wanaripoti kutoka Shinyanga kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo lilikuwa halijapokea hati ya kumkamata.

Afisa upelelezi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Adam Nyakipande alikiri kusikia habari hiyo, lakini akasema walishindwa kuitekeleza kwa kuwa hawakupata kibali cha mahakama hiyo.

"Ninachoweza kusema ni kwamba sisi tunasubiri hati ya kumtia nguvuni... kwa ufupi bado hatujapewa kibali cha kumkamata lakini tukipata tutalifanyia kazi," alisema.

Chanzo: Mwananchi (via Dada Subi)

4 comments:

 1. Wewe, sijui jaribuni muone...siasa hiyooo, ujue huyo ni mtu anayeijua sheria pia, na anajua nini anachokifanya!

  ReplyDelete
 2. Chenge ni shujaa lakini katika ufisadi si sheria.Angekuwa hata nusu ya shujaa katika sheria angejua sheria ya Mwl. Nyerere kuwa ufisadi haulipi. Kesi zake zote anaweza hata kushinda. Lakini ambacho hatashinda ni kurejesha heshima yake ikizingatiwa vyeo andamizi alivyowahi kutumikia akavitumia kuiba.

  ReplyDelete
 3. Wewe subiri ushindi wa kishindo hapo. Ndipo utakapojua watanzania hawana uchungu na nchi yao. Lakini ipo siku tu watu wataamka toka usinginzini.

  Ona kule Nzega watu walivyofanya vitu vyao kumpinga mgombea aliyebebwa na CCM kwenye kura ya maoni. Nimejufunza kuwa watanzania wanaanza kupata mwamko. Nimesoma kule Iringa mtoto wa Kikwete alivyopuuzwa na vijana. Taratibu ipo siku mambo yatakuwa mswano.

  ReplyDelete
 4. Kutishiana kifo ni utoto. Ni kushinda kujadili mambo na badala yake unajadili watu.
  Mugumo

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU