NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, September 20, 2010

SIASA ZA MAJI TAKA: NI DALILI YA KUKUA KWA DEMOKRASIA NCHINI MWETU?

Katuni ni kutoka kwa Fede
 ****    *****  ****
Uchaguzi huu unaonekana kuwa tofauti na chaguzi zilizotangulia.
 • Kwanza: Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia majina makubwa katika medani ya siasa za Tanzania yakianguka katika kura za maoni. Hili ni jambo jema!
 • Pili: Kwa mara ya kwanza kuna mgombea wa uraisi wa upinzani ambaye kidogo ni tofauti na wagombea wote waliotangulia. Huyu wa sasa ni msomi aliyebobea, bingwa wa kujenga hoja, mwenye bashasha; na mwenye rekodi nzuri sana ya kutetea maslahi ya wanyonge bungeni.
 • Tatu: Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia "kashfa" mbalimbali za wagombea na watu wengine wenye majina makubwa zikiibuliwa. Wapo wanaotuhumiwa kuyakimbia maisha ya utawa na kuanza kupora wake za watu. Wapo wanaotuhumiwa kubaka na kutia mimba wanafunzi wakati wakiwa bado walimu. Wapo wanaotuhumiwa kuwa na nyumba ndogo za siri n.k.
 • Siasa hizi za ki- Argumentum Ad Hominem ni jambo la kawaida katika nchi zilizoendelea hususan hapa Marekani. Hapa mtu huwezi kukurupuka tu leo na kusema kwamba unagombea cheo cho chote kwani watu watachimbua maisha yako tangu ulipozaliwa. Kwa mfano, katika kura za maoni za kuchagua mgombea wa useneta wa jimbo la Florida kupitia chama cha Democrat, mgombea mmoja mashuhuri aliangushwa baada ya kudaiwa kwamba boti yake ya bei mbaya iliwahi kwenda Cuba kinyume cha sheria huku ikiwa na wanawake watingishaji (strippers). Ilidaiwa pia kwamba Mike Tyson, mwanamasumbwi tishio wa zamani ambaye hana sifa nzuri hapa Marekani alikuwemo katika msafara ule.
 • Japo mgombea huyu alijitetea sana kwamba boti yake ilibidi iende Cuba baada ya kupata matatizo ya kiufundi; na kwamba yeye mwenyewe hakuwamo katika msafara ule (japo baadaye alikiri kuwamo) na kwamba hakukuwa na wanawake watingishaji wala Mike Tyson, tayari hii ilitosha kuwapa wasiwasi wapiga kura na aliangushwa.
 • Hivi sasa mgombea wa Useneta kule jimbo la Delaware kupitia chama cha Republican ambaye tu ndiyo amechaguliwa naye moto umemwakia baada ya video yake moja ya zamani wakati akiwa shule ya Sekondari kuanza kuzunguka mtandaoni. Katika video hiyo anaonekana akisema kwamba alishawahi kujaribu mambo ya uchawi japo hakupata kubobea sawasawa.
 • Je, kwa vile nasi tumeshaingia katika siasa hizi za maji taka badala ya kumakinikia sera, hii ni dalili kwamba demokrasia yetu inakua? Je, hili ni jambo jema?
*******************
Angalizo: Hii iikuwa ni Fikra ya Ijumaa ya wiki jana lakini kwa bahati mbaya nilikosea "nikaitegesha" katika siku na tarehe ndiyo-siyo. Kunradhi!

5 comments:

 1. kweli siasa zinaelekea uelekeo wa aina yake. nakumbuka wakati wa kampeni za 2005 hakukuwa na haya kuhusu maisha binafsi. sasa kumepamba moto.
  siwezi kusema moja kwa moja kuwa ni kukuwa kwa demokrasia. ila naweza kusema sasa watu wengi wamepata mwamko na wamekuwa wafuatiliaji sana.
  jimboni kwetu kule Njombe Magharibi, mbombea ubunge wa Chadema karusha makombora kama hayo hayo kwa mgombea ubunge na udiwani wa ccm.
  kwa kuwa kule ni kijijini, wananchi wanatafsiri kama matusi.
  ukija hapa mjini Dar, watu wanazishabikia sana habari hizo.
  angalau tunapata nafasi ya kuwajua wagombea kiundani kabla hajujaamua endapo tunaweza kuwaamini.

  ReplyDelete
 2. kinacholeta ukubwa wa demokrasia kama ilivyo TZ katika uchaguzi huu sio siasa za maji taka bali wa TZ kutokupelekwa na majitaka wakazikwepa na kuangalia hoja za wagombea

  mahali pazuri kuelekea ukomavu wa democracy

  ReplyDelete
 3. nadhani kila jambo lina wakati wake. pengine tutazame nani kaanza kuwamwagia wenzake haya maji taka. Pengine pia sera zimekuwa ni zilezile ndio maana watawala wamekuwa walewale kwa miaka 50. pengine ni wakati sasa tukageza kidogo huko zinakoanzia maawa wao wameendelea. Marekani imeendelea kwa namna nyingi tu, hata mbaya pia.

  jana nimesoma makala ya mzee lyimo kule the citizen. analeta hekaya ya kupendekeza incumbent politicians wasipige kampeni kwani wao wanatakiwa kuhukumi na wapiga kura kwa kile walichokifanya. eti chema kijiuze.

  nadhani mtaji wa upinzani kokote kuwako ni kukosoa kwanza waliopo madarakani. sera za elimu, aflya, miunsombinu, kodi, kilimo nk nk nk kila mmoja atazisema ingwaje kwa lugha tofauti. hivi mathalani watanzania wa leo tunahitaji kuambiwa hospitali za mikoa zitakuwa za rufaa ikiwa hatuna hata zahanati za kutosha. hivi tunahitaji kuambiwa kila mkoa unahitaji kiwanja cha ndege cha kimataifa? cha nini. tunahitaji kuambiwa kila palipo na mfereji kutaletewa limeli likubwa. kama kuongoza ni kufanya majaribio basi na wengine nao wajaribu

  ReplyDelete
 4. Nanukuu "...katika uchaguzi huu sio siasa za maji taka bali wa TZ kutokupelekwa na majitaka wakazikwepa na kuangalia hoja za wagombea"

  Kamala kwako nasema 'TAWIRE'.

  hapa ndipo tutakapotofautiana na siasa za 'ng'ambo'. wakati tunataka kichwa cha mgombea na kujiuliza kitatufanyia nini wananchi, tunakatiaa kujua akichoka huwa anapumzika na nani. hatutaki kujua ufupi ama urefu wa maungo yake. hatutaki kujua ana 'vodosho' wangapi

  hatuna shida ya kujua vitu hivi mosi kwa kuwa hakuna aliyemsafi 100%. lakini, pili havitahusiana na kazi ya kututumikia wananchi. tutavihoji tu endapo vitu hivi vina historia ya kumfananya mgombea asifanye kazi vema.

  sehemu kubwa ya watanzania imebumbuluka

  ReplyDelete
 5. Ni kudanganyana kwa kwenda mbele. Tatizo la wananachi hasa walioko wilayani na vijijini ni wajinga wasiotaka kuelewa ukweli. Anakuja mgombea anaahidi MAISHA BORA kwa kasi mpya na nguvu mpya! Baada ya Miaka 5 anarudi na kuwapa ahadi nyingine lukuki tena za anasa kama viwanja vya ndege vya kimataifa na hosipitali za rufaa, mishahara minono kwa wafanyakazi wote. Watu wote lukuki walioenda kumsikiliza (hawazuiwi kwenda) wanasima na kupiga makofi na kusema na kuimba nambari waniiiiiiiiiix2.
  Ukiwatizama kwenye hizo picha unaona wanaishi katika maisha yaliyokata tamaa, mazingira na sura choka mbaya sasa sijui hayo ndio maisha bora walioahidiwa. Kwanini wasihoji tu hapo kuwa maisha bora yamepelekwa wapi? Watoto wachanga na wajawazito wanapoteza maisha kila siku (Takwimu zisizo sahihi ni kama 20 kwa siku!), Maajali ya kila siku yanaongezeka barabarani na lawama zinapelekwa kwa madereva, ndio madereva wanamakosa, sasa wanafanywa nini ili kuwarekebisha? Au ndio kama mwendo wa kuomba kura (kula?) wakati wa uchaguzi. Elimu i nazidi shuka chini, watoto kibao wanafeli kidato cha nne (chukulia asilimia 20, ndio wanafaulu). Kilimo kinazidi kurudi nyuma ihali wachache wanakuwa makabaila(kwa kujilimbikizia mashamba) na kudai eti kilimo kwanza? Ukienda pale Meatu au Mpanda au Lushoto ukamwuliza mkulima maana ya kilimo kwanza hajui! DUH huu ni upumbavu mkubwa sana! Samahani

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU